Thursday, June 2, 2011

KAMBI YA UPINZANI YATAJA VIPAUMBELE VYA BAJETI

YAPENDEKEZA POSHO ZA VIKAO VYA WABUNGE, SERIKALINI ZIFUTWE


Boniface Meena

KAMBI ya Upinzani bungeni imetaja vipaumbele sita vya bajeti yake mbadala ya mwaka wa fedha 2011/2012, ikitaka kufutwa kwa posho (sitting allowance), za vikao vyote vya serikali na wabunge.Vipaumbele hivyo vimetangazwa jana, ikiwa ni wiki moja kabla ya serikali kuwasilisha bungeni, Bajeti yake ya mwaka 2011/2012 itakayotangazwa Jumatano ijayo. Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo ameshatangaza vipaumbele 12 vya Bajeti ya Serikali ambavyo ni mara mbili ya vile vya kambi ya upinzani.

Kambi hiyo ya upinzani bungeni imeeleza kuwa katika vipaumbele vyake itaweka msisitizo katika miundombinu, umeme, kuwezesha ukuaji wa sekta za uzalishaji na hasa ukuaji wa uchumi vijijini na kuimarisha utawala bora.

Imetaja kuimarisha usimamizi wa mashirika ya umma na kuboresha maendeleo ya rasilimali watu kwa kuwekeza kwenye ubora wa elimu nchini.

Akitaja vipaumbele hivyo mbele ya waandishi wa habari jana, Naibu Waziri Kivuli, Wizara Fedha na Uchumi, Christina Mughwai alisema dhamira ya bajeti hiyo mbadala ni kutoa unafuu wa kodi kwa wananchi maskini na kuhakikisha kuwa anayepaswa kuilipa anafanya hivyo kwelikweli.

Mughwai ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), alisema bajeti hiyo itasomwa bungeni na Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe.

Kuhusu miundombinu
Alisema kuwa bajeti hiyo itaweka msisitizo kwa barabara zote muhimu ambazo hazijaanza kujengwa, ili zianze kuanzia mwaka huu wa fedha wa 2011/2012.

Mughwai alisema pia wataweka msisitizo katika upanuzi wa bandari kwa kutumia ushirikiano wa Sekta Binafsi na Serikali (Public Private Partnership- PPP) pamoja na kuimarisha Bandari ya Mtwara.

Alisema katika eneo hilo, watasisitiza pia uboreshwaji wa Reli ya Kati ili iweze kufanya kazi ya kusafirisha mizigo na abiria kwa kiwango cha kuridhisha hadi hapo fedha za kujenga reli mpya zitakapopatikana: "Pia Shirika la Ndege la Taifa liongezewe mtaji wa kulifufua, ili liweze kujiendesha kibiashara na kwa ufanisi."

Tatizo la umeme
Kuhusu umeme, Mughwai alisema bajeti ya kambi ya upinzani itapendekeza fedha zipelekwe kwenye miradi mitatu mikubwa na kwamba miradi hiyo ianze mara moja.

"Miradi hiyo ni umeme wa makaa ya mawe megawati 1,500 katika Migodi ya Mchuchuma, Ngaka na Kiwira, pia umeme wa gesi (Mtwara Gas Pipeline) megawati 300 kutoka Mtwara, Dar es Salaam hadi Mwanza," alisema Mughwai.

Alisema kambi hiyo pia itapendekeza mradi kabambe wa kusafirisha na kusambaza umeme mijini na vijijini chini ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) ufanye kazi kwa nguvu zaidi.

Sekta ya uzalishaji
Katika eneola uzalishaji, Naibu Waziri huyo Kivuli wa Fedha na Uchumi alisema wanasisitiza kuboresha miundombinu, upatikanaji wa majisafi na salama ikiwa ni pamoja na kuongeza ubora wa bidhaa za kilimo: "Tutaelekeza rasilimali za kutosha kwenye kukuza uchumi vijijini."

Utawala Bora
Katika kuimarisha utawala bora, alisema kambi yake inataka serikali itenge fedha za kutosha kuwezesha mchakato wa kuandika Katiba Mpya ili Watanzania wote waweze kushiriki katika mchakato huo.

Pia alisema wanataka kuanzishwe kitengo maalumu kwa ufisadi mkubwa (Serious Fraud Office) ndani ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) ili kuimarisha utawala bora.Mughwai alisema kuwa wanataka pia mfumo mpya wa kudhibiti mgongano wa maslahi, hasa kwa wanasiasa kutenganisha mgongano wa maslahi katika biashara zao.

Alisema wanataka kuanzishwa kwa ofisi ya bajeti ya Bunge ili kuweka uwazi zaidi kwenye Bajeti ya Serikali kwa kuwa hivi sasa wabunge hawahusishwi katika kuipanga: "Tunapendekeza itungwe Sheria ya Bajeti itakayowezesha kuanzishwa kwa Ofisi ya Bajeti."

Maendeleo ya rasilimali watu
Waziri huyo Kivuli wa Fedha na Uchumi alisema katika maendeleo ya rasilimali watu, kambi yake inataka kuhakikisha watoto wanaomaliza kidato cha nne, wanapata mafunzo ya ufundi ili waweze kujiajiri wanaporudi vijijini.

"Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu inapata fedha za kutosha kutoka kodi ya uendeshaji ujuzi, robo tatu ya kodi hii ambayo inakwenda Hazina ibaki kwenye bodi ili kukidhi mahitaji ya mikopo. Kimsingi lengo la bajeti yetu katika elimu ni kupata elimu bora na si wingi wa majengo ya shule ama wanafunzi wanaomaliza shule."

Naibu msemaji huyo alisema kuwa wapinzani wanataka kuanzishwa pensheni kwa wazee wote wenye umri zaidi ya miaka 60 na kuanzishwa kwa bima ya afya kwa wananchi wote."Bima hii iwe ni ya lazima kwa watu wote, wafanyakazi na wasio wafanyakazi na ichangiwe na wananchi wenyewe pamoja na serikali," alisema.

Usimamizi wa mashirika ya umma

Kuhusu usimamizi wa mashirika ya umma, alisema kambi ya upinzani inataka uanzishwe Mfuko wa Taifa wa Uwekezaji (National Investment Fund) kwa ajili ya kutoa mitaji kwa mashirika ya umma na mapato yake yatokane na asilimia ya faida za mashirika inayokwenda kwenye bajeti sasa.

Alisema kambi hiyo pia inataka kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mafuta na kulibadili Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuwa shirika la kibiashara la mafuta.Pia kambi hiyo inataka kupunguzwa bei ya mafuta kwa asilimia 40 na kupanua wigo wa kodi kwa kuweka lengo la kukusanya mapato ya ndani sawa na asilimia 20 ya pato la taifa.

Mughwai alisema kambi ya upinzani pia inataka pia kuangaliwa upya kwa mfumo wa utawala wa kodi akitolea mfano kampuni zinazofanya kazi nchini, lakini zimesajiliwa nje hali inayosababisha zilipe kodi katika nchi zilikosajiliwa na taifa kukosa mapato.

"Tunataka kodi inayoitwa 'Presamptive Tax' ifutwe kwa sababu inasababisha kampuni ndogo zisijisajili, hii husababisha ukwepaji wa kodi hasa katika sekta isiyo
Linkrasmi.Alisema mashirika ambayo serikali ina hisa yajisajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ili ziweze kuuzwa.

Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012 itaelekezwa katika sekta za nishati, elimu, kilimo na mifugo. Sekta nyingine zitakuwa ni za miundombinu,Uvuvi, maendeleo ya viwanda, afya, maji, ardhi, nyumba na makazi, rasilimali watu, sayansi na teknolojia, huduma ya fedha na masuala mtambuka.MWANANCHI

No comments: