Friday, June 10, 2011

CHUKI DHIDI YA SERIKALI HUPANDIKIZWA NA SERIKALI YENYEWE
Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela

KATIKA mazingira ya kawaida chuki dhidi ya serikali yoyote duniani haitokei hivi hivi tu bila sababu. Wananchi hawawezi kuamka asubuhi na kuanza kuichukia serikali yao. Watu hawawezi kuwa na sababu ya kumchukia mtawala kama mtawala hawapi wananchi sababu ya kumchukia. Kwa kawaida kuna sababu kadhaa zinazoweza kuwafanya raia kuichukia serikali iliyoko madarakani.

1.Kutawaliwa na watu wasiochaguliwa au kuridhiwa na wananchi

Mojawapo ya sababu zinazowafanya raia wa nchi fulani kuwa na chuki dhidi ya watawala ni kuweko madarakani kwa serikali isiyotokana na wananchi hao au isiyoridhiwa na wananchi hao. Hii ndio sababu ya wananchi kumchukia mkoloni au utawala wa kidikteta (uwe wa mtu mmoja au wa chama kimoja).

Wanadamu tunapenda kuwa huru kutawaliwa, na siyo kulazimishwa kutawaliwa. Utu wetu unaita uhuru huo. Pale ambapo wananchi wanakuta watawala ambao aidha wamejilazimisha juu ya wananchi au wamejipandikiza kiujanja, basi, chuki huanza kujengeka kati yao.

2. Kutawaliwa pasipo haki

Wakati mwingine watawala wanaingia madarakani wakitokana na wananchi hao lakini wanapoingia madarakani wanatawala watu pasipo haki; wakiwanyanyasa na kuwakandamiza na kuwafanya wananchi wawe kama wanyama waliowekwa kwenye zizi huku wanachapwa viboko bila kukoma.

Haki ndio msingi wa amani na mahusiano mazuri kati ya watawala na watawaliwa. Utawala ambao hauzingatii haki - na hapa sizungumzii uwepo wa mahakama au polisi - nazungumzia tunu ya kupata kile ambacho mtu anastahili kutokana na utu wake au uraia wake.

Utawala usio wa haki na hasa wa kipolisi, husababisha chuki kati yake na wananchi wake. Wananchi wanaiona serikali ni ya kikandamizaji na serikali inawaona wananchi wake kama wagomvi. Utawala wa kikoloni ulikuwa na mambo yote hayo. Hakuna haki ya msingi kama haki ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wako kama mwanadamu mwingine.

3. Kutawaliwa na ufisadi

Hakuna utawala mbaya kama utawala wa kifisadi (corrupt regime). Utawala wa kifisadi unatukuza madili, na mitkasi ya kiujanja ujanja. Utawala wa aina hiyo hudumu kwa kuvunja sheria au kuzipinda bila kumjali yeyote kwani kuanzia usalama, polisi, mahakama na wanasiasa wote wako kwenye chungu kimoja; huku kila mmoja akinufaika na uzembe wa mwingine na kila mmoja akilinda ubovu wa mwingine.

Utawala wa kifisadi husababisha chuki dhidi ya wananchi; kwani chini ya mfumo wa utawala wa kifisadi kikundi cha watu wachache, hasa walio karibu na walio madarakani, kinazidi kufanikiwa huku mamilioni ya wananchi wengine wakiwa kama watazamaji katika uwanja wa mpira.

Katika mfumo wa namna hiyo wananchi hujenga chuki dhidi ya serikali yao kwa sababu wanatambua kuwa serikali yao imewekwa kwenye mikono ya mafisadi na hakuna mwenye uwezo wa kutoka humo. Serikali inakuwa imefungwa nira isiyovunjika na shingo za wahalifu wa kimataifa. Wananchi hutambua kuwa serikali yao haina uwezo wa kupambana na uhalifu wa namna hiyo.

Kwa muda mrefu nchi kama Marekani zilijikuta zinalazimika kupambana na wahalifu wa namna hiyo na kuleta kile kinachoitwa “law and order” kwani maeneo yake mengi yalianza kutawaliwa kwa sheria za msituni.

Katika nchi kama za kwetu, sheria za msituni bado hutumika ambapo wenye nguvu hutembea kwa uhuru wakati maskini hunyanyasika na kuumizwa, na hata kidogo walichonacho inabidi watumie nguvu nyingi kweli kukilinda.

4. Serikali kutosikiliza kilio cha wananchi wake

Mojawapo ya sababu za mgongano kati ya Wamarekani na Ufalme wa Mwingireza ambao Marekani ilikuwa ni mojawapo ya makoloni yake, ni kuwa Mfalme alikuwa hataki kusikiliza malalamiko ya wananchi wake wa Marekani. Wamarekani wa wakati ule walijaribu mbinu nyingi na njia nyingi kumshawishi Mfalme abadili sera zake dhidi ya koloni hilo na kulipatia uhuru zaidi wa kujiendesha, lakini Mfalme George akakataa kabisa.

Matokeo yake kikundi cha waasisi kikaamua kupanga njama za kutangaza uhuru wa makoloni ya kwanza 13 ya Marekani kuwa yatakuwa nchi huru. Na sababu za kujitenga zikaanishwa vyema katika Azimio la Uhuru la Marekani la mwaka 1776.

Serikali yoyote isiyosikiliza wananchi wake inawapa sababu wananchi kuichukia. Ninapozungumzia kusikiliza sina maana ya kutoa ahadi au kwenda mitaani na kukusanya maoni; nina maana ya kushughulikia kero na matatizo mbalimbali ya wananchi yakaondoka - siyo kupunguka au kuahidi kuyapunguza.

Wananchi wanapolalamikia matatizo mbalimbali ambayo hayawezi kuondolewa bila ya kuhusishwa na serikali; na kama matatizo hayo ni ya msingi mno na yenye kukandamiza na kuwanyima uhuru wao, wanategemea kuwa serikali itafanya jambo. Lakini kama serikali haifanyi kitu au kile kinachofanyika ni geresha ya wazi au kukosa umakini, wananchi wataanza kuichukia serikali hiyo.

Wananchi wanachukia serikali yao na hata kutaka kuiondoa madarakani pale wananchi hao wanapojikuta wamekata tamaa. Wananchi wakikata tamaa huichukia serikali.

Yote ninayasema hapa kwa sababu kuna watu wanataka watu waamini kuwa CHADEMA, wapinzani, au waandishi fulani fulani wa habari “wanapandikiza chuki” dhidi ya serikali. Maofisa wa Jeshi la Polisi (kina Chagonja na wenzake) wanataka kulitisha taifa zima likubali kuwa chuki iliyopo nchini dhidi ya serikali imepandikizwa na wanasiasa.

Ndugu zanguni, polisi hawawezi kuua wananchi kiholela bila hata kuchunguzwa; halafu wananchi wachekelee! Ndugu zangu, haiwezekani serikali ishindwe kuwakamata mafisadi wa Meremeta na Kagoda, lakini ikaweza hadi kukodisha ndege kumtia nguvuni Mbowe; halafu wananchi wachekelee tu!

Serikali haiwezi kukimbilia kukamata vibaka wa hapa na pale, lakini wanaotumia mabenki yetu kufanya uhalifu wa kimataifa wakiendelea kupita na suti zao halafu wananchi washangilie.

Ndugu zangu, kama umwagikaji wa damu nchini mwetu hasa kwenye mazingira ya kisiasa umekuwa ukifanywa na serikali (kupitia polisi), basi, hata chuki ambayo tunaona inazidi kukolea taratibu haisababishwi na kina Mbowe au na Slaa. Ooh hapana! Chuki ambayo inazidi kukolea miongoni mwa vijana wetu haitokani na kina Zitto na Mnyika - tutawaonea tu.

Chuki hiyo, inasababishwa na watawala walioshindwa na inasababisha wananchi kuona kuwa katika nchi yao wao wamekuwa vibarua. Inasababishwa na hisia ya kwamba taifa lililokataa kujenga matabaka sasa limejenga matabaka, kuyabariki na kuyalinda.

Chuki iliyopo sasa haisababishwi na kina Lipumba au vyombo vya habari - wanavisingizia. Inasababishwa na viongozi wazembe wenye kufikiri wao ni zawadi ya Mungu kwa Tanzania na hivyo hutawala kwa kunyanyasa watu bila kujali lolote.

Ndugu zangu, chuki ambayo tunaishuhudia ikijaa pole pole na kuanza kutengeneza mapovu kama bia iliyotikiswa, lazima itafute mahali pa kutokea.

Nasikitika kusema vitendo vya hivi karibuni vya kukosa hekima kwa baadhi ya watendaji wa serikali, kunatafuta njia ya kuwafanya wananchi watolee hii chuki na hasira ambayo imeanza kugandamana na damu zao.

Ndugu zangu, kama serikali na chama tawala; hasa huko Bungeni wanakoanza wataendelea kuonekana wanawanyanyasa wapinzani au kuwafanyia vitendo vya kiudhalilishaji, nitakuwa mtu wa mwisho kushtuka nikisikia kile ambacho wote tunajua chaweza kutokea Tanzania kikitokea.

Naomba mnisome kwa makini sana; kwa kadri chuki hii inazidi kuongezwa na serikali, na hasa kauli za kidini, kibaguzi na hata za kibabe; ndivyo hivyo hivyo wananchi wanazidi kuwa sugu.

Jamani, Assad wa Syria aliweza kuwatisha watu wake kwa muda mrefu na sasa hivi pamoja na risasi nyingi, hajalazimisha mapenzi kwake tena. Kina Chagonja na IGP Saidi Mwema na wenzao wasifikirie virungu na risasi zinaweza kuzima fikra huru za hawa Watanzania.

Hakuna nchi iliyofanikiwa kuzima fikra huru kwa nguvu - hili somo watawala wetu wakilielewa hawatoshangaa siku moja wakajikuta mikononi mwao kuna damu nyingi ya Watanzania, lakini huku Watanzania wakiendelea kusimama dhidi yao.

Njia pekee ya kutagua mgogoro ambao watawala wameujenga ni kuanza kutawala kwa haki, kutonyanyasa watu, kuheshimu haki za wananchi na raia; kwani hawa watu wanaoagizwa watu wakamatwe au kupigwa risasi wasishangae na wao wakajikuta tunawapeleka kwenye mahakama za kimataifa na kuanza kampeni ya kuzuia misaada Tanzania hadi watakaposalimishwa kwenye mahakama hizo.

Msifikiri Watanzania wataendelea kuburuzwa; kwani tayari wameshaonesha kuwa hawako tayari kuburuzwa milele. Isije siku wakasema na kuonesha kuwa hawatoburuzwa tena. Ole wetu tukiiona siku hiyo!

Barua-pepe:
RAIA MWEMA

No comments: