Monday, May 9, 2011

YA OBAMA, KIKWETE NA USALAMA WA TAIFANa Evarist Chahali

VUGUVUGU la kuwania nafasi ya urais wa Marekani katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani limenza kupamba moto.Wakati hadi sasa hakuna majina yanayotajwa kuchuana na Rais Barack Obama katika kinyang’anyiro cha kupitishwa kuwa mgombea kwa tiketi ya chama cha Democrats, hali ni tofauti kwa chama cha Republicans.

Wana-Republicans wanaotajwa kuwania kuchuana na Rais Obama (ambaye ameshatangaza nia ya kugombea tena) ni pamoja na aliyekuwa mgombea mwenza wa chama hicho katika uchaguzi mkuu uliopita, Sarah Palin.

Wengine wanaotajwa ni Spika wa zamani wa “bunge dogo” (Congress) Newt Gingrich, Gavana wa zamani wa jimbo la Minnesota, Tim Pawlenty, “Mbunge” (congresswoman) wa Minnesota, Michelle Bachmann, Gavana wa zamani wa jimbo la Massachusetts, Mitt Romney, Seneta wa zamani wa jimbo la Pennsylvania, Rick Santorum na Gavana wa zamani wa jimbo la Arkansas, Mike Huckabee.

Lakini mtu anayeonekana kuzua tashwishwi kubwa ni tajiri wa uwekezaji kwenye majengo, Donald Trump. Hadi sasa tajiri huyu, ambaye pia ni maarufu kwa kipindi chake maarufu katika luninga kiitwacho Apprentince hajatamka rasmi iwapo ataomba kupitishwa na chama cha Republicans kuwania urais hapo mwakani.

Hata hivyo, Trump amekuwa akivuma sana kwenye vyombo vya habari baada ya kujiweka karibu na kundi linalojulikana kama Birther ambalo limekuwa likihoji uraia wa Rais Obama, likidai kuwa si mzaliwa wa Marekani; bali alizaliwa Kenya. Trump alidakia hoja hiyo kwa nguvu kubwa na kupita huku na kule akisisitiza kuwa kama kweli Obama alizaliwa Marekani basi aonyeshe cheti chake cha kuzaliwa.

Hoja hiyo kuhusu uraia wa Rais Obama haijaanza majuzi; bali tangu wakati wa mchakato wa uchaguzi uliopita wa kumpata mgombea urais kwa tiketi ya Democrats. Kambi ya mpinzani mkuu wa Obama katika mchakato huo, Hillary Clinton, ilijaribu kuibua suala hilo bila mafanikio. Lakini pengine kilichofanikiwa ni ukweli kwamba hoja hiyo haijafa tangu wakati huo.

Tafiti mbalimbali za maoni zimeonyesha kuwa angalau theluthi moja ya Wamarekani (hususan wafuasi wa Chama cha Republicans) wanaamini kuwa Obama sio Mmarekani halisi; bali ni Mkenya. Mtandao wa intaneti umefurika conspirancy theories kuhusu uraia wa Obama, na tajiri Trump alifanikiwa kwa kiwango kikubwa kueneza “fitna” hiyo.

Lakini katika hali isiyotarajiwa, wiki iliyopita, Rais Obama aliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kutangaza kuwa ameamua kuweka hadharani cheti chake cha kuzaliwa. Katika mkutano huo, Obama alitanabaisha kuwa “ana mambo ya muhimu zaidi ya kushughulikia kuliko kuendekeza upuuzi unaoenezwa kuhusu uraia wake”.

Ungetaraji kuwa uamuzi huo wa busara wa Obama ungemnyamazisha Trump. Lakini katika kile kinachotafsiriwa kama kutapatapa, licha ya kujimwagia sifa kuwa “amempelekesha” Obama hadi akaamua kuthibitisha uraia wake, tajiri huyo mwingi wa vituko ameibuka na madai mengine mapya kuhusu elimu ya Rais huyo wa Marekani.

Trump anadai kuwa ana mashaka jinsi Obama alivyomudu kujiunga (na hatimaye kuhitimu) vyuo vikuu vyenye hadhi kubwa vya Columbia na Shule ya Sheria ya Harvard (Harvard Law School). Tajiri huyo anadai kuwa “vyanzo” vyake vimemfahamisha kwamba Obama alikuwa “kilaza” (mwanafunzi asiye na uwezo kitaaluma) na haingewezekana kujiunga na vyuo hivyo vinavyofahamika kama Ivy League kutokana na ubora wake wa hali ya juu kitaaluma.

Madai haya mapya ya Trump yamepelekea baadhi ya watu kumtuhumu kuwa ni mbaguzi wa rangi.Hoja yao inaelemea kwenye tafsiri kuwa tajiri huyo anaamini kuwa Wamarekani Weusi (kama Obama) hawana uwezo wa kitaaluma kustahili kujiunga na vyuo vyenye hadhi ya juu.

Lengo la makala hii, hata hivyo, si kujadili siasa za Marekani; bali mwenendo wa mambo huko nyumbani Tanzania; hususan jitihada za chama tawala CCM kuwatenga baadhi ya viongozi wake wanaotuhumiwa kwa ufisadi (“kujivua gamba”).

Kwa kutumia mfano wa namna Rais Obama alivyokuwa akiandamwa kuhusu uraia wake, kwa nini isifike mahala Rais Jakaya Kikwete akaamua “kujivua gamba” kwa kuweka hadharani mambo kadhaa ambayo kwa kiasi kikubwa yanasababisha mkanganyiko usiostahili katika utekelezaji wa azma ya CCM ya “kujivua gamba”?

Kwa mfano, kwa nini Rais Kikwete ameendelea kupuuza kelele za Watanzania wanaotaka kumfahamu mmiliki wa kampuni ya Kagoda ambayo kimsingi ndiyo iliyonufaika zaidi na ujambazi wa EPA? Ni wazi kuwa Kikwete anafahamishwa na wasaidizi wake kuhusu maneno “ya mtaani” kwamba wananchi wanaamini kuwa fedha za EPA ndizo zilimwezesha kuingia Ikulu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Tukiweka kando namna Kikwete amekuwa “akisuasua” kuchukua hatua thabiti dhidi ya majambazi wa EPA, skandali hiyo pia imesababisha “magamba” mengine makubwa yanayochafua dhana ya utawala bora nchini Tanzania.

Miongoni mwa makampuni yaliyotajwa kunufaika na fedha za EPA ni kampuni mbili zinazodaiwa kumilikiwa na afisa mmoja mwandamizi wa Idara ya Usalama wa Taifa. Kampuni hizo ni Clayton Marketing Ltd na Excellent Services Ltd ambazo ni miongoni mwa kampuni 22 zilizotumiwa kuchota kifisadi Sh. bilioni 133 za BoT kupitia Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).

Hadi sasa Serikali ya Kikwete haijafanya jitihada zozote za kuufahamisha umma iwapo kampuni hizo zilikuwa ni miliki binafsi ya afisa huyo au zilikuwa “fronts” za taasisi hiyo nyeti. Madhara ya kuchelea kwa serikali na vyombo vyake kuchukua hatua stahili ni kuichafua Idara ya Usalama wa Taifa kiasi cha kuibua hisia kuwa huenda ilihusika katika ujambazi wa EPA.

Hisia hizo zinazoweza kuwa potofu zinapewa nguvu na ukweli kwamba hadi leo taasisi hiyo haijafanya jitihada zozote za kujisafisha katika utata huo, hali inayoweza kujenga hisia au imani kuwa kampuni hizo za afisa huyo zilikuwa ni sehemu tu ya ‘utendaji’ wake wa kazi kama mtumishi wa idara hiyo muhimu na nyeti.

Kama uongozi wa juu wa Idara ya Usalama wa Taifa ulidiriki kuitisha mikutano na waandishi wa habari kukanusha tuhuma za mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA, Dk. Willibroad Slaa, kuwa taasisi hiyo ilishiriki “kuchakachua” kura katika uchaguzi mkuu uliopita, iweje basi hadi leo ipo kimya kuhusu afisa wake mwandamizi kutajwa kuwa mnufaika wa ujambazi wa EPA?

Na katika hili, Rais Kikwete hawezi kukwepa maswali; kwani kikatiba yeye ndiye mkuu “halisi” wa idara hiyo. Kama kweli angekuwa anakerwa na “gamba” hilo asingeshindwa kuchukua hatua stahili.

Lakini pia katika harakati za Kikwete kuiwezesha CCM kujivua magamba kuna suala la msingi linaloihusu Idara ya Usalama wa Taifa. Kuna madai kuwa taasisi hiyo inafuatilia kwa karibu nyendo za wanasiasa “magamba” wanaodaiwa kuwa na mkakati wa “kulipa kisasi” kwa kuendesha harakati zitakazowezesha kuvuliwa kwake uenyekiti wa Taifa wa CCM.

Swali la msingi ni hili: Je, idara hiyo inafanya hivyo kama sehemu ya wajibu wake kuhakikisha usalama wa Rais au inamfanyia kazi binafsi kama Mwenyekiti wa CCM? Ni muhimu pia kutambua kuwa operesheni za kufuatilia nyendo za “wanasiasa magamba” zinaendeshwa kwa fedha za walipakodi wa Kitanzania pasipo kuangalia kama ni wana-CCM au la.

Kama madai hayo ni kweli, basi, nikumbushe hapa kwamba Watanzania hawastahili kubebeshwa mzigo wa gharama za kudhibiti mgongano wa kimaslahi kati ya Kikwete na “maswahiba” zake ambao leo hii wanaitwa “magamba”; licha ya ukweli kuwa walikuwa “damu moja” mwaka 2005 kuhakikisha anaingia Ikulu.

Wito wangu kwa Idara ya Usalama wa Taifa ni kuwasihi warejee skandali ya Watergate ya nchi ya Marekani ambapo Rais Richard Nixon alilazimika kujiuzulu kufuatia, pamoja na makosa mengine, kuelekeza ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia na kuzitumia dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa.

Nimalizie kwa kumsihi Kikwete kutambua kuwa wanachohitaji Watanzania sio tu kukabiliana na ufisadi ndani ya chama chake; bali pia kuanza kuwashughulikia mafisadi wanaozidi kuigeuza nchi yetu kuwa “shamba la bibi”.

Nikumbushe pia hapa kwamba huko nyuma Kikwete alishatuambia kuwa anawafahamu kwa majina ila anawapa muda wajirekebishe. Sote tunajua kwamba hawajajirekebisha, kwa hiyo aanze sasa kuwashughulikia wote kisheria.

Kadhalika, kLinkama alivyofanya Obama baada ya kuandamwa na tuhuma kuwa sio Mmarekani, ni muhimu kwa Kikwete kufanya kila analoweza kuwathibitishia Watanzania kuwa kuwepo kwake kwenye “List of Shame” iliyotolewa na CHADEMA pale Mwembeyanga, mwaka 2007, ni uzushi tu.

Vinginevyo, anaweza kuyadhibiti “magamba” kwa kutumia taasisi za umma lakini hatoweza kudhibiti hisia kuwa “ameamua kuwatosa maswahiba zake baada ya kuona hawahitaji tena”.


RAIA MWEMA

No comments: