Thursday, May 26, 2011

UVCCM -ARUSHA WATOA TAMKO LA KUMKANA MWENYEKITI WAO
TAMKO LA VIJANA WA CCM MKOA WA ARUSHA
Tarehe 25/05/2011

Ndugu zangu waandishi wa habari leo tumeona tuwaite hapa ili tuweze kutoa maoni yetu kuhusiana na mustakabali wa chama chetu cha Mapinduzi na Jumuiya yetu ya Umoja wa vijana wa CCM mkoa wa Arusha.

Tumewaita hapa kwa malengo makuu Sita:-

1.
Kuunga mkono Halimashauri kuu ya CCM Taifa kwa kuona umuhimu wa kuifanyia kazi kwa vitendo falsafa ya kujivua gamba. Tunaipongeza na kuiunga mkono Halmashauri kuu ya CCM Taifa kwa kutambua kwamba mafisadi wamechangia sana kukidhoofisha na kukipotezea mvuto chama chetu mbele ya umma wa watanzania. Kwa mantiki hiyo tunatamka kwa kauli moja kwamba mapacha hao watatu wa kifisadi ambao ni Edward Lowasa, Rostam Azizi na Andrew Chenge na vibaraka wao wafukuzwe mara moja kwa maslahi ya CCM na Watanzania. Pia tunasisitiza kuwa Andrew Chenge aondolewe kwenye kamati ya maadili ya CCM mara moja na wakati huohuo Edward afukuzwe kwenye kwenye ya uwenyekiti wa Bodi ya udhamini ya umoja wa vijana wa CCM Taifa haraka iwezekanavyo.

2.
Sisi vijana wa CCM kutoka sehemu mbalimbali za Mkoa wa Arusha tunamtaka kuwa James Millya ambaye ni kibaraka mkuu wa mafisadi mkoa wa Arusha ajiuzulu mara moja na tunatamka rasmi kumfukuza kwenye UVCCM mkoa wa Arusha ili apate fursa ya kwenda kuwa tumikia mafisadi. Tunamtaka James Millya aache kufikiria kwa kutumia tumbo na badala yake atumie kichwa. Pia tumeshaandika barua yenye kumbukumbu namba kumb. Ars/Malalamiko/01 kwenye Chama kuelezea namna alivyo mnafiki, mfitini,mwongo na namna asivyo jali maslahi ya vijana wa UVCCM mkoa wa Arusha. Vilevile tunapenda kuujulisha umma wa Tanzania kuwa Ally Bananga anaetumiwa na Millya pamoja na mafisadi hana nafasi yoyote ndani ya Umoja wa vijana wa CCM kuanzia kwenye tawi hadi Taifa. Kwa mantiki hiyo Ally Bananga aache mara moja kuganga njaa kwa kutumia jina la UVCCM. Pia tunampa onyo kali Catherine Magige aache mara moja kutumia fedha za mafisadi kuwagawa vijana wa Arusha kabla hatujatumia haki yetu ya kikanuni ya kumsimamisha Ubunge. Tunajua kuwa amepata ubunge kwa nguvu za kifisadi kupitia UVCCM.

3.
Sisi vijana wa CCM kutoka sehemu mbalimbali za Mkoa wa Arusha tunakiomba chama cha cha mapinduzi kiwafukuze mara moja makatibu wa UVCCM kutoka wilaya za Monduli, Arumeru, Longido na Karatu kwa kushiriki mandalizi ya maandamo haramu na kwa kukataa wito wa chama wa kwenda kutoa ushahidi wa malamiko yao kuhusu mjumbe wa Baraza kuu la UVCCM Taifa. Kitendo hicho cha kukataa wito wa Chama ni dharau na ukosefu wa maadili.

4.
Sisi vijana wa CCM kutoka sehemu mbalimbali za Mkoa wa Arusha tunatamka kwamba ili kulinda hadhi ya CCM mkoa wa Arusha tunamtaka Onesmo Nangole ajiuzulu mara moja kwa kuwa anafanya kazi ya Fisadi Edward Lowasa na si ya CCM. Kitendo chake yeye cha kufanya kazi ya mafisadi na si ya CCM kimetupelekea kupoteza majimbo mawili kwenye uchaguzi mkuu wa 2010.

5.
Sisi vijana wa CCM kutoka sehemu mbalimbali za Mkoa wa Arusha tunatamka kwamba Mhe. Mary Chatanda (MB) ambaye ni katibu wa CCM Mkoa wa Arusha ni mpiganaji na ni lulu ya CCM mkoa wa Arusha. Amefanya mengi ya maana na wa-CCM makini, wazalendo na wanaojali maslahi ya chama chetu wanatambua hilo. Pia tunawaomba CCM Taifa waendelee kumwacha hapa Arusha ili aendelee kukijenga chama na kukomesha mafisadi pamoja na dagaa wao.

6.
Sisi vijana wa CCM kutoka sehemu mbalimbali za Mkoa wa Arusha tunatamka rasmi kumtambua Ndugu. Mrisho Gambo kuwa ni mjumbe halali wa baraza kuu la UVCCM Taifa kuwakilisha mkoa wa Arusha. Tunamuunga mkono kwa ujasiri wake, umahiri wake na uzalendo wake wa kupambana na ufisadi ndani ya chama na Tanzania kwa ujumla. Na huo ndiyo msimamo wetu kwa kuwa una tija kwa vijana wa Tanzania. Tunashauri CCM Taifa kuwaita rasmi mapacha watatu wa kifisadi (Edward Lowasa, Rostam Azizi na Andrew Chenge) kwenye kamati ya maadili ya CCM Taifa na kisha kuwafukuza mara moja kama kweli tuna nia ya kuendelea kuwa chama tawala katika nchi hii.

TUTASEMA KWELI DAIMA FITINA KWETU MWIKO
KAULI YETU: KULINDA NA KUJENGA UJAMAA
KITADUMU CHAMA CHAMAPINDUZI BILA MAFISADI

No comments: