Monday, May 23, 2011

SITTA: NINA WAKATI MGUMU

Rehema Matowo, Moshi

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samwel Sitta, amesema anapitia nyakati ngumu za kisiasa kutokana na uamuzi wake wa kusimamia misingi ya haki, usawa na uadilifu iliyoachiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere lakini akaapa kupambana na mafisadi hadi nchi itoke mikononi mwao.

Kauli hiyo ya Sitta inakuja kipindi ambacho joto la siasa nchini limekuwa likipanda siku hadi siku huku chama chake cha CCM kikiwa katika kipindi kigumu cha mpito kutekeleza mpango mkakati ujulikanao kama kujivua gamba.

Akizungumza katika kongamano la miaka 50 ya Uhuru na maisha ya Watanzania lililofanyika katika Chuo Kikuu kishiriki cha Ushirika na Stadi za Biashara Moshi (MUCCOBS) na kuwashirikisha wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali vya kanda ya kaskazini, Sitta alisema kamwe hawezi kubadilika na atabaki kwenye viwango.

“Nawahakikishia nitapigana vikali kuhakikisha CCM inakua safi na nitapambana na waliokiharibu chama hadi kupoteza mwelekeo,” alisema Sitta.

Waziri Sitta alirejea tambo zake akisema yeye ni mwanasiasa mwenye viwango na ndiyo maana, wengi wanamgombania, lakini akawataka watambue kuwa hawezi kuhama chama chake kwa sasa baada ya miaka 50.

Alisema kitendo cha kuhama chama kwa sasa hakipo na anachokifanya ni kupambana na maovu yote yaliyopo ndani ya CCM na kuhakikisha kinarejesha heshima aliyoiacha Mwalimu Nyerere.

Waziri Sitta alisema nyakati hizo ngumu hazitamfanya abadilike wala kurudi nyuma na kuwa atapambana kuhakikisha nchi inakua safi na kutoka mikononi mwa mafisadi.

Aliitaja misingi iliyoachwa na Mwalimu kuwa ni usawa wa binadamu, kutobaguana kwa kabila wala namna yoyote, uadilifu na umoja ambayo alisema kwa sasa Watanzania wameiacha na ndiyo maana nchi ipo kama ilivyo leo.

Akizungumzia Tanzania ijayo baada ya miaka 50 ya uhuru, Waziri Sitta alisema wananchi wanategemea nchi yenye kujitambua na isiyo maskini na kuweka bayana, hiyo itawezekana endapo rasilimali zilizopo zitasimamiwa vizuri.

Aliwataka vijana kuepuka kuwa mawakala wa wanasiasa ambao wamefilisika kiakili na wanaojali matumbo yao na kuendelea kuliingiza taifa katika giza la umaskini.

Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki, alisema kinachoendelea nchini kwa sasa ni siasa za malumbano zisizo na tija kwa mwananchi wa kawaida hivyo vijana wasomi wanayo nafasi kubwa ya kuwaelimisha wananchi jinsi ya kuwatambua.

Akizungumza katika kongamano hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Harisson Mwakyembe alisema vijana wengi wamekuwa bendera fuata upepo na kushabikia mambo ambayo hawajayafanyia utafiti kujua ukweli wake.

Dk Mwakyembe aliwataka kutoa mwongozo katika mchakato wa uundwaji wa Katiba mpya na kuwataka kuondoa woga katika kuijadili kwa manufaa yao na kizazi kijacho.

Alisema tatizo kubwa la Watanzania ni woga kusema na wana hulka ya kulalamika. Alisema nyakati zimebadilika na wanapaswa kuwa jasiri katika kudai haki zao.


MWANANCHI

No comments: