Wednesday, May 18, 2011

REFLECTION YA SAFARI KUSINI MWA TANZANIA


HAJA YA KUTAMBUA ‘MKUFU’ WA MAENDELEO


Na Beda Msimbe,

UTANGULIZI


Niliandika mradi wa kwenda Kusini mwa Tanzania kuandika habari baada ya uchaguzi.
Nilieleza nia yangu na baada ya nenda rudi ya majibu na maswali nilienda Safari hii ambayo hakika ilinifunza mambo mengi kuanzia ukweli wa mambo miongoni mwa wananchi,viongozi, matumaini na balaa linalokabili upungufu wa mkufu katika kutekeleza mradi mkubwa ambao unaunganisha mikoa mitatu na nchi jirani tatu.

Mradi huu ambao niliamua kufuatilia ni wa mabilioni ya shilingi ni ufunguo wa maisha ya watanzania na huenda ndio mradi pekee unaosuasua ambao hauna muunganiko na kueleweka vyema kwa watendaji wa serikali na wanasiasa sembuse wananchi.

Hoja ya msingi katika hili ni uchumi na kauli za chama tawala za kuinua mazingira ya Tanzania.


MRADI WENYEWE

Niliandika kuomba nafasi ya kuangalia mambo mawili ambayo ama hakika ni miradi miwili ambayo mimi niliona inafanana: nayo ni korido la Mtwara na makaa ya mawe na chuma.Katika miaka 20 ijayo mwenendo wa Tanzania katika uchumi unategemea sana ufanisi wa miradi hiyo ambayo ukiigawa ni mitatu na yote ipo Kusini mwa Tanzania. Yaani korido, mawe na chuma.

Huwezi kuamini kabisa kwamba eneo ambalo limebaki kuwa maskini sana kwa kipato ndilo hasa lenye ufunguo wa maisha bora nchini Tanzania.

Ili kuwa na viwanda mama kama ilivyonadiwa na vyama vingi kikiwemo chama tawala cha CCM, chuma cha Liganga lazima kitoke kuwezesha utengenezaji wa nondo na bidhaa mbalimbali za chuma na uyeyushaji wa chuma wenye uhakika unahitaji umeme wa uhakika ndipo makaa ya mawe yanapotakiwa kutoka.

Chuma na makaa hayo yanahitaji miundombinu inayofaa kwa namna yoyote ile na hapa ndipo unapoangalia korido la Mtwara ambalo limelenga kujenga miundombinu na pia kuweka viwanda karibuni mwa Bandari.

Nilitarajia kuperemba sana mambo yanayohusu miradi hiyo kwa kuzingatia ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya kuwa na msingi wa kutengeneza uchumi wa kati kwa kuwa na viwanda mama na umeme wa uhakika.

SAFARI ILIKUWAJE

HOJA iliandikwa na kuwasilisha katika kitengo husika Desemba 31 mwaka 2010 ikapitishwa Januari 11 na tarehe 15 /1/2011 nilianza safari ambayo ilimalizika Januari 29,2011.Nililazimika kupanga namna ya kuanza kazi hiyo na haikuwa rahisi.
Nilianzia safari yangu Mtwara mahali ambapo kinadharia nilidhani ni kichwa cha miradi yote.

Nilifika huko lakini kutokana na mazingira halisi badala ya kutumia barabara ya Kusini Mtwara, Nachingwea, Masasi kuelekea Ruvuma katika katika legi ya pili ya safari nililazimika kurejea tena Dar es salaam na kuchukua safari ya kwenda Ruvuma kabla ya kurejea Iringa na kuingia Ludewa kupitia Njombe katika legi ya tatu.

Mvua upande wa Kusini zilikuwa zinanyesha kipindi hicho na hilo ndilo hasa lililonifanya nisipitie njia ya kusini kutokana na ukweli kuwa siku zilikuwa chache na kutoka eneo moja la kazi hadi jingine ni siku nzima kutokana na miundo mbinu dhaifu, nilikwama siku moja kufika katika eneo la biashara la boda Mtwara,nilikwama siku mbili Songea na nililazimika kulala siku mbili zaidi Njombe kutokana na mvua kubwa iliyokuwa inanyesha njia nzima kuelekea Ludewa.
NILICHOJIFUNZA

Wilaya ya Ludewa ambapo wakati mvua pamoja na barabara yake kuhudumiwa kila mara inakuchukua siku mbili kutoka Njombe wa basi kufika huko ni eneo tajiri sana kijiolojia. Na Mtwara yenye bandari bomba kabisa inafaa kabisa kuwa gateway ya Tanzania na majirani zake.

Eneo la Ludewa linahifadhi mamilioni ya tani ya makaa ya mawe na chuma vitu muhimu vinavyoweza kufanya taifa lotelote lile duniani kujiamini kwamba linaweza kufanya kitu Fulani.

Mwaka 2004 wakati Rais Jakaya Kikwete akiomba kura alikuwa anaelewa thamani halisi ya eneo hili kwa taifa la Tanzania miaka 100 ijayo kwa kutengeneza thamani halisi ya utajiri wake wa kijiolojia ambapo makaa ya mawe na chuma yapo nje nje; ni hapa alipowaambia wananchi kwamba kazi ya kuyathamanisha (kuyafanyiakazi) madini hayo ilikuwa ianze katika awamu yake ya kwanza.

Imechukua miaka mingine mitano tangu ahadi itolewe kuanza kuona dalili ya kupambazuka hata baada ya miaka 40 ya kujua ukweli na kutoutekeleza. Hapa si madini ya mawe na chuma pekee, eneo hili la kusini lina miamba mingi yenye madini ya aina anuai.

Ingawa mwelekeo wa sasa ni kufua umeme kwa kutumia makaa ya mawe yaliyopo Mchuchuma kuwapo kwa hisani ya Mungu ya kuweka chuma karibu na makaa kunatoa taswira ya wazi kwamba ni sisi wenye matatizo na si Mungu na inawezekana kabisa kuwa moja ya mataifa yenye viwanda vikubwa vya chuma kama tukianza kukiyeshusha chuma kwa wastani unaostahiki.

Kuwapo kwa shughuli za uchimbaji mawe na chuma kunatakiwa kusaidiwe kutengenezwa kwa miundombinu ambayo ni muhimu kwa ajili ya kusafirisha makaa ya mawe na pia chuma na katika hili barabara na treni ni muhimu.Kuna mazungumzo ya miaka nenda rudi,hakuna ufumbuzi unaonekana karibu.

Ingawa taarifa ya awali ilikuwa kujengwa kwa njia ya reli kuelekea bandari ya Mtwara ambapo kiuchumi ni sawasawa ikiwa ni pamoja na kutumbukiza mradi huo kama sehemu ya mradi mkubwa wa korido la Mtwara , utengenezaji wa miundombinu hii ya kusafirisha madini kunaweza kununufaisha pia wananchi wa wa kawaida wa eneo hilo ambao kwa sasa wanakuwa na dhiki kubwa mvua inapochanganya, kwa kuwaandaa tayari kutumia nyenzo husika kwa maendeleo.

Pamoja na kuonekana kwamba safari hii serikali ya Chama cha mapinduzi imedhamiria kupiga hatua moja kubwa mbele hasa ya kurekebisha upatikanaji wa umeme kwa kufungua maeneo ya Kusini ili pia kuvuna mali asili nyingine ambazo zinapatikana kama madini ya atomiki bado kunashida kubwa ya maunganiko kisekta na hasa uelewa wa Wananchi viongozi walio na Wananchi na katika safari hii nimebaini Wananchi hawajui kitu na viongozi wao sawia, wataalamu yao yamo katika makabrasha na katika mikutano ya kuomba fedha na mbaya zaidi yamo katika mioyo yao wakisubiri wanasiasa.

Miradi katika mikoa inayoandaliwa haina uhusiano wa karibu wa kubebana na miradi mikubwa iliyopo sasa na huenda itakapoanza kutekelezwa basi wananchi wataiona si sehemu yao.


JE SAFARI HII INA MANUFAA?

Ni dhahiri kwa makala nilizoandika katika hili wenye akili na wanazuoni wanaweza kuelewa nini hoja za wananchi na nini nilichokuwa nakifikiri baada ya mazungumzo marefu na umma.
Pengine kama si mradi huu nisingejua kwamba wananchi hawajui kuwa mradi wa korido la Mtwara upo rasmi toka miaka ya 2004 ilipotiwa saini na Rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa huko Malawi, na mbaya zaidi hatutumii nafasi ya kibiashara kati yetu na majirani zetu huku itifaki ya forodha ikiwa kikwazo kikubwa.
Pia kwa mradi huu nimejenga maarifa mapya ya kiuandishi na kuweka taarifa mpya za mradi huu ambao unaweza kuwa na maana kama utakuwa kama mkufu kwa Wananchi na kutekelezwa kwa namna hiyo.

Nimeweza kujua kwamba makaa ya mawe yalijulikana toka ukoloni yakafanyiwa hesabu tukashindwa kujipanga wenyewe tukabaki ombaomba wa kimataifa wakati katani ingeliweza kututoa kwa kuweka msingi wa uchimbaji wa madini haya kwa kutumia nyenzo zilizopo na hasa umma.

MATATIZO

Pamoja na kujidai kuwa nimekuwa na muda wa kuona mambo, nilikacha kuenda maeneo mengine ya mbali kwani kukodisha pikipiki bei kubwa na magari hayafiki.Njia ya kwenda Ludewa kupitia Mbambay ina vitu vingi lakini sikuweza kwasababu lojistiki kuwa mbaya ingawa kijiolojia ni njia bora zaidi kuifuatilia.

Viongozi na wataalamu wamekuwa na msaada mdogo kutokana na woga na kutokuwa tayari kuwa wazi katika fikira, utoaji takwimu kutokana na kile wanachokiona na wanachoshughulika nacho katika viongozi wote aliyekuwa mkweli ni mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali mstafu Anatory Tarimo.

Mtwara wana shida ya biashara na Msumbiji hawana cha kuzungumza zaidi ya kulalamika, Ruvuma hivyo hivyo na Iringa vivyo hivyo.Maeneo mengi hayafikiki kirahisi na wale wenyeji wanataka kulipwa kama watu wa skauti. Lakini pia muda uliopangwa kwa kuzingatia fedha zilizopo si kitu sahihi sana kwani muda mwingi unatumika katika kusafiri kutokana na ubaya wa miundombinu na muda mdogo wa field hasa unapolazimika kutaka kusahihisha au kuwa na takwimu halisi.

Wanasiasa wamebaki kusema siasa, wataalamu nao wanakatisha tamaa na Wananchi wamebaki mbumbumbu na kufikiria kwamba wanageuzwa watumwa katika nchi yao:kuona wanasiasa wanazungumza tu wajapoambiwa wasukume kupatikane uwezo wa kukabiliana na mambo mapya.KWA HISANI YA LUKWANGULE ENT. BLOG

No comments: