Friday, May 20, 2011

MJADALA WA UCHAGGA NA UISLAM WAENDELEA

Imetolewa Jamii Forums

Nitaomba radhi kwa kuanzisha thread mpya ili niweze kupata fursa ya kujibu hoja za ndugu yangu Mimi Mwanakijiji au kama anavyojiita sauti ya kijijini inayoelezea iliyoandikwa kwenye gazeti la
Tanzania Daima: Kama CHADEMA ni Wachagga, CCM ya Waislamu?

Napende niwaeleze wale wote walioshabikia historia ya TANU kuwa wamelishwa "tango pori" na mheshimiwa sana Mwanakijiji japo sijaelewa amefanya kwa makusudi au kwa kutokufahamu kwakuwa tunae humu jamvini ni imani yangu atatueleza na kututanabaisha mapenzi yake juu ya vyama alivyovizungumzia, ila ningependa kumshauri awe mzalendo zaidi na apendelee kuwaelimisha watu kwa historia ya ukweli japo kwa kiwango cha asilimia 80 kama si mia kwa mia.


Pengine ni vyema tuangalie mtiririko wa kupigania uhuru wa nchi hii ili tuone mchango wa Mwanakijiji juu ya hoja yake na tupate kumuenzi kwa kutupa elimu na historia adhimu tusioijua:


1929: TAA yaundwa ikiwa na wajumbe wafuatao:


1. Kleist Sykes, 2. Mzee bin Sudi, 3. Ibrahim Hamis, 4. Zibe Kidasi, 5. Ali Said Mpima, 6. Suleiman Majisu, 7. Raikes Kusi, 8. Rawson Watts, 9. Cecil Matola.


1950: TAA yawasiliana na KAU; Abdulwahid alikwenda Nairobi kukutana na Jomo Kenyatta ili kujenga mawasiliano na chama cha Kenya African Union (KAU).


1951: Kuundwa kwa tawi la siasa la TAA; likiwa na wajumbe wafuatao:


1. Abdulwahid Sykes (Secretary)
2. Sheikh Hassan bin Amir
3. Hamza Kibwana Mwapachu.
4. Said Chaurembo
5. Dk. Kyaruzi.
6. John Rupia.
7. Stephen Mhando


1951: Kenyatta akutana tena na viongozi wa TAA. Safari hii mkutano huo ulifanyika Arusha. Wajumbe wa TAA walikuwa Abdulwahid Kleist Sykes, Dossa Aziz na Stephen Mhando.


1952: Abdulwahid alichaguliwa kuwa Rais wa TAA.


1952: Mwalimu Nyerere atambulishwa kwa Abdulwahid na Bwana Kasela Bantu. Baada ya utambulisho huo ikawa kila Jumamosi Mwalimu Nyerere akawa anakutana na akina Dossa Azizi, Bw. Ally Sykes, Abdulwahid Sykes, Dustan Omar na Mhando kujadili mustakbali wa nchi ya Tanganyika.


Mikutano hiyo ama ilikuwa ikifanyika nyumbani kwa Dossa Azizi mtaa wa Congo au mtaa wa Stanley nyumbani kwa Abdulwahid.


Alikuwa ni Dossa Azizi ambaye mara nyingi alikuwa akimrudisha Mwalimu Nyerere kwa gari lake Pugu (St. Francis College) baada ya mkutano.


1953: Mwalimu achaguliwa kuwa Rais wa TAA. Wazee waliompa nguvu ya kisiasa Mwalimu mara baada ya kuingia katika TAA/TANU.


Sheikh Hassan bin Amir, Sheikh Suleiman Takadir, Mzee Mohammed Jumbe Tambaza, Mshume Kiyate na Mwinjuma Mwinyikambi. Wengine walikuwa Rajab Diwani, Makisi Mbwana, Sheikh Haidar Mwinyimvua na Idd Faiz Mafongo. Aidha walikuwepo Idd Tosiri, Sheikh Mohamed Ramia na Mashado Ramadhani Plantan.


Oktoba 10, 1953 Mwalimu Nyerere, Abdulwahid Sykes, Ally Sykes, Dossa Aziz na John Rupia walikutana kujadili namna ya kuibadili TAA kuwa chama kamili cha siasa.


1954: TANU yaanzishwa. Wajumbe wa mkutano uliojadili kuibadili katiba ya TAA kuwa TANU walikuwa Abdulwahid Sykes, Julius Nyerere, Tewa Said Tewa, Dossa Aziz, Ally Sykes, Kasela Bantu, ,Abubakar Ilanga na Saadan Abdu Kandoro. Wengine walikuwa S.M. Kitwana, C.O. Milinga, Patrick Kunambi, Gerimano Pacha, Japhet Kirilo na L.M. Makaranga. Walikuwa pia Joseph Kimalando na John Rupia.

Mkutano wa kuizindua rasmi TANU ulihudhuriwa na wajumbe wafuatao: Julius Nyerere, Abdulwahid Sykes, Ally Sykes, Dossa Aziz, John Rupia na Mshume Kiyate. Wengine walikuwa Makisi Mbwana, Jumbe Tambaza, Juma Waziri, Clement Mtamila, Rajab Diwani, Schneider Plantan na Marsha Bilali. Walikuwepo pia Rashid Ally Meli, Frederick Njiliwa, Idd Faiz Mafongo, Idd Tulio, Denis Phombeah na wengine.

Napenda kumfahamisha ndugu yangu Mwanakijiji kuwa pia ndani ya TAA na TANU kulikuwa na kina
Dr Michael Lugazia, Dr Vedasto Kyaruzi, Dr Luciano Tsere, Dome Budohi, Zuberi Mtemvu, Ali Mwinyi Tambwe, Tatu bint Mzee, Mwinyijuma Mwinyikambi, Sheikh Mohamed Ramia wa Bagamoyo


Julius Nyerere alipewa kadi ya TANU Na. 1, kadi Na. 2 ikaenda kwa Ally Sykes na Abdulwahid akachukua kadi ya TANU Na. 3, Dossa Azizi alichukua kadi Na. 4, kadi Na. 5 ikaenda kwa Phombeah. Dome Okochi alipata kadi Na. 6, John Rupia Na. 7, Bibi Titi Mohamed kadi Na. 16 na Idd Tosiri kadi Na. 25.

Ndugu yangu kwa Mwanakijiji.

Kwa watu makini makala yako ni moja ya utumiaji kalamu kupotosha jamii makala yako imebaka historia ya kweli ya TAA/TANU na sasa CCM kama nilivyoeleza mwanzo pengine mapenzi ya chama kimoja wapo ndio mapenzi hayo yamekusukuma kuinanga historia ya kweli.


Ni matumaini yangu ipo siku utaungana na Joseph Mihagwa utajitolea kuuvunjaa mwiko wa kuuzungumzia muungano inavyostahili.


Mwisho kabisa ninapenda kutoa rai kuwa si vema kuufananisha kabila na dini unless uwe una chuki dhidi ya dini unayoihusisha na kabila unalokusudia. Ningeona umetenda haki ukaelezea Ukristo/Uislam wa CCM na CDM kuliko kufananisha uchagga na uislam kwa hilo ndugu yangu hukuwatendea haki waislam mimi nikiwa miongoni mwao.

Wangapi wanajua historia ya madaktari watano – Dr. Vedasto Kyaruzi, Dr Joseph Mutahangarwa, Dr Wlibard Mwanjisi, Dr Michael Lugazia na Dr Luciano Tsere na mchango wao katika kusukuma mbele harakati za TAA kati ya 1948 – 1950?

Shukrani sana na nakutakia siku njema wewe na jamaa wote wa JF.


Mohammed Shossi.JAMII FORUMS

2 comments:

mzalendo #1 said...

Kazi nzuri ya uchambuzi wa historia yetu. Tafadhali endelea kutuelimisha.

mzalendo #1 said...

Kazi nzuri ya uchambuzi wa historia yetu. Tafadhali endelea kutuelimisha.