Thursday, May 12, 2011

MJADALA WA BARABARA YA SERENGETIHoja Za Ndaskoi ni fikirishi lakini..............


Bipin Vishan

NIMESOMA kwa makini makala ya Bw. Nakaya ole Ndaskoi kuhusu sakata la barabara ya Serengeti na naomba nipate nafasi ya kuongeza kidogo kuhusu suala hili tata.

Lakini kwanza niwapongeze ninyi wa Raia Mwema kwa hazina ya makala zenu nyingi, na pia Bw. Ndaskoi kwa kuileta mada hii ya ‘Barabara ya Serengeti’ katika gazeti lenu. Kwa muda mrefu suala hili ambamo Tanzania na Watanzania ndiyo wadau wakuu tumeachwa tukijadiliwa kama vile jambo hili halituhusu sisi; bali dunia inayotuzunguka, na tena wao wa nje ndiyo wawe waamuzi wakuu kuhusu barabara hii.

Ingawa makala ya Bw. Ndaskoi inafundisha na kufunua mengi yaliyokuwa yamefichwa awali, kwa kiasi fulani ametumia mbinu ya kuwa ‘mchumi katika kutoa ukweli’ (being economical with the truth). Nitajaribu kudodosa kidogo kuongeza yale aliyoyaacha.

Ukurasa katika mtandao wa FaceBook anaoutaja Bw. Ndaskoi unaitwa savetheserengeti.org na pia wanaendesha ukurasa wa kampeni hiyo ya kupinga barabara kukatisha Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) unaoitwa Stop the Serengeti Highway – humo humo ndani ya FaceBook (na siyo kuipinga Serikali halali iliyopo madarakani).

Mpaka kufikia Mei mosi, 2011, ukurasa huu ulikuwa na zaidi ya mashabiki 40,000 na wanaendelea kuongezeka. Kinachosumbua akili yangu ni idadi ndogo ya Watanzania na Wakenya katika mashabiki wa kurasa hizo. Kingine ni jinsi zilivyojaa zaidi michango ya Kiingereza kuliko Kiswahili.

Ukienda katika mtandao wa Google, kuna zaidi ya wavuti (kama ni Kiswahili sahihi kwa uwingi wa tovuti) 14,300 ambazo zote zinapinga mpango huo wa Serikali kujenga barabara kwa kukatisha Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Michango hiyo imeandikwa kwa lugha mbalimbali; isipokuwa sijaona ya Kiswahili!

Hoja kwamba barabara zinahitajika kusogeza mbele gurudumu la maendeleo haipingiki; bali mtazamo wa savetheserengeti.org na wa Stop the Serengeti Highway (ninazitaja hizi mbili kwa sababu Bw. Ndaskoi amewatumia hawa kuhalalisha makala yake), ni kwamba; si lazima kuunganisha mikoa miwili inayopakana kwa barabara au reli au chombo kingine cha ardhini hata kama utaharibu mazingira.

Kwa mfano, hivi sasa tuna mkoa wa Iringa unaopakana na mikoa ya Rukwa na Katavi (mkoa mpya), lakini hakuna barabara ya moja kwa moja inayowaunganisha hadi sasa. Na mojawapo ya sababu kuu ni kuwepo kwa Hifadhi ya Taifa Ya Ruaha na Mbuga za Wanyamapori (Game Reserves) baina ya mikoa hii. Vile vile kwa Mashariki mwa mkoa huo kuna Selous Game Reserve ambayo inazuia ujenzi wa barabara kuunganisha na mikoa mingine.

Hawa ‘wahafidhina’(fanatics, zealots, fundamentalists nk) ambao Bw. Ndaskoi anawaita wapinzani wa Serikali, kwa maoni yangu, ni ‘wanaharakati’ na ‘wakereketwa’ wa uhifadhi na utunzaji wa maliasili, mazingira na uotoasili vikiwemo wanyamapori na misitu asili. Bw. Ndaskoi ana hasira na hawa, hivyo anatumia jazba kuwaita ‘wahafidhina’. Wanamtibulia agenda yake na zile za makundi yake (kama yapo).

Pamoja na mapendekezo ya Benki ya Dunia kudhamini (si kuikopesha Tanzania) na mapendekezo ya Serikali ya Ujerumani kudhamini (si kuikopesha Tanzania), hoja ya Serikali ya Ujerumani ndiyo inayopewa upendeleo mkubwa na savetheserengeti.org na Stop the Serengeti Highway.

Hoja hii, kwa kifupi, inasema kuwa Ujerumani watagharamia utafiti na baadaye ujenzi wa barabara zote za vijijini katika Wilaya ambazo zinapakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti – wakimaanisha rural road networks ili kurahisisha mawasiliano ya kimiundombinu kati ya kata na Wilaya zao; na kisha wilaya na mikoani mwao.

Kwa maana hiyo, mikoa itakayonufaika na msaada huu wa Ujerumani ni ile ya Arusha na Musoma. Na barabara hizi zitajengwa hadi kufikia hadhi ya ama kuwa zinapitika kipindi cho chote katika mwaka (all weather roads) au hadhi ya kuwekwa lami. Kwa njia hii, huduma muhimu zote zitapatikana katika mikoa husika bila kusababisha uharibifu wa mazingira na kuathiri uoto asili wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti – kwani suala la barabara kukatisha hapo ili kusogeza mbele gurudumu la maendeleo halitakuwa na mantiki yoyote tena.

Ingawa Ofisi ya Habari ya Ikulu ilisema kuwa mojawapo ya sababu tatu za msingi ni kusogeza huduma muhimu kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kuna hisia kwamba lengo hasa ni kuunganisha bandari ya Tanga na mji wa Musoma ili kusogeza urahisi wa kufikisha mizigo nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na DRC Mashariki – kama mbadala wa bandari ya Dar es Salaam. Hivyo, wananchi wa vijijini pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti hawakuwa walengwa, na ndiyo maana hata katika sababu zilizotolewa wao (walengwa) wamekuwa sababu ya tatu na ya mwisho!

Hivyo vikao vya hizo ‘kamati za madiwani’ anavyotaja Bw. Ndaskoi navyo ni tata. Ni kweli walikutana na kufanya kikao – lakini swali linakuja: Je, ni kawaida kuwepo na vikao vya ‘ujirani mwema’ kati ya wilaya hizo, mikoa hiyo au hata mikoa mingine nchini? Haiyumkiniki ‘kikao’ hicho kiliandaliwa na ‘dola. Mbona awali havikuwepo wakati changamoto zipo tangu enzi za ukoloni na si hili la barabara tu?

Hivi karibuni viongozi wa Wilaya ya Ngorongoro wamenukuliwa wakiisihi Serikali iiondoe Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kutoka katika hadhi ya Urithi wa Dunia (World Heritage Site) ya UNESCO, kwa sababu wananchi wao hawajaona mafanikio yoyote yatokanayo na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wala kutokana na kuwa na hadhi hiyo! Hawajaona yaliyofanywa na TANAPA katika kuchangia maendeleo ya vijijini huko huko kwao!

Hoja ya Profesa Parkipuny ina mantiki yake, lakini mapendekezo yake kuwa barabara ipite nchini Kenya bado kutaleta suala la Idara ya Uhamiaji, suala la thamani ya fedha (pamoja na kuwa mchakato wa kuwa na sarafu moja unaendelea). Pia kujenga barabara kutoka Lengijape-Kitumbeine-Meirungui-Gelai-Ol Doinyo Lengai-Ziwa Natron-Elojata-Bonde la Ufa-Masusu-Digodigo-Loliondo-Lemisigio na kuingiza Kenya; kisha iendelee hadi mji wa Mulat kukatisha Nyanda za Loita ndipo igeuke kuelekea kusini Magharibi hadi Sirari (Tanzania); labda nielekeze hoja yangu upande wa kwetu Tanzania.

Tayari makabila wenyeji yanayoishi katika maeneo yaliyopo pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wameonja ‘joto ya jiwe’ kwa kunyang’anywa ardhi kimabavu ili kupisha Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) na Mbuga za Hifadhi za Wanyamapori (Game Reserves) kama vile ile ya Loliondo na Ngorongoro Conservation Area mkoani Arusha na Maswa mkoani Shinyanga/Musoma. Kwa maana hiyo ardhi ambayo hivi sasa wamo ndani yake haiwatoshelezi kwa kukidhi kikamilifu mahitaji yao kwa ajili ya kilimo na ufugaji.

Hivyo, dhana ya kuwanyang’anya tena kipande cha upana wa takriban meta 50 (ukifikiria uwepo wa road reserve na mitandao ya nyaya za gridi za umeme (ambazo huwekwa jirani na barabara kwa ajili ya kurahisisha matunzo na ukarabati) na urefu unazofikia zaidi kidogo ya Kilometa 250 (meta 250,000) ina maana umewaondolea wananchi hao hao meta za mraba milioni 12.5 kutoka katika ardhi ambayo nayo ni finyu kwa mahitaji yao.

Ina maana kwamba hawatafuga tena wala kulima! Na hiyo ni kwa mkoa wa Arusha tu; tena labda wilaya moja tu. Pia ukichukulia kwamba tayari kuna eneo la ardhi limetengwa kwa ajili ya ranchi ya wananchi wilayani Ngorongoro, utaona jinsi ardhi ‘huru’ kwa wananchi itakavyopungua.

Ndiyo maana savetheserengeti.org na Stop the Serengeti Highway sasa wanaishauri (na siyo kuipinga) Serikali ya Tanzania kwamba Serikali hiyo ipitie upya mpango wa ujenzi uliopo hivi sasa (ujenzi unategemewa kuanza 2012; yaani mwakani kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 480 ambazo nchi yetu inaweza kuzitumia katika miradi mingine endelevu). Badala yake, Serikali inashauriwa ikubali mapendekezo ya Benki ya Dunia pamoja na yale ya Serikali ya Ujerumani ambayo si gharama kwa Taifa letu.

Kwa msingi huo, binafsi pia napendekeza yafuatayo:

Kwa kuwa Rais Kikwete ameshatangaza dhamira ya serikali yake kuboresha na kujenga mtandao wa reli kutoka Dar es Salaam hadi nchi jirani za Rwanda na Burundi, na kwa kuwa tayari tuna barabara ya lami kuunganisha nchi hizo kupitia bandari kavu ya Isaka (labda kuna vipande vifupi vifupi havijamalizika kuwekwa lami lakini ujenzi ukiendelea); hivyo dhana ya kutumika kwa bandari ya Tanga kama kiungo nchi hizo igeuzwe kuwa:

Kiungo njiapanda (connection junction) kutoka reli ya kati kituo cha Ruvu kuelekea Tanga – Moshi – Arusha kifufuliwe, na njia hiyo itumike zaidi kwa ajili ya mizigo.

Kiungo cha reli kati ya Moshi (Tanzania) na Mombasa (Kenya) kifufuliwe.

Serikali yetu na ya Kenya waanze utafiti wa kuunganisha Arusha na Nairobi kwa reli. Hii itafungua pia uwezekano wa Tanzania kununua mafuta yake kutoka ama Sudan Kusini au kutoka Uganda ambako machimbo ya mafuta na upatikanaji wake upo. Tayari Kenya wana barabara ya lami inayounganisha Nairobi na Juba (Sudan Kusini).

Serikali ifanye tathmini ya uwepo wa njia ya reli baina ya Mwanza-Musoma na kuelekea Kenya (ama Nakuru au Kisumu).

Serikali ipitie upya sera yake ya Utalii (Tourism Policy) na kuiboresha ili kudhibiti/kupunguza idadi ya mahoteli ya kitalii na kambi za aina hiyo (camps, lodges and resorts) katika hifadhi zote za taifa; hususan ile ya Serengeti na viwanja vya ndege vinavyoendeshwa/kumilikiwa na mahoteli/kambi hayo/hizo.

Ukichukulia hayo na misaada ya Benki ya Dunia, Serikali ya Ujerumani na matakwa ya wananchi, tutaweza kuua ndege wengi kwa jiwe moja. Yaani; Serengeti itaokolewa, miundombinu itaboreka, uchumi wa nchi utakua na vilevile wananchi watapata maendeleo nk.

Mwisho, naomba kwamba mjadala huu uendelezwe ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi; kwani wengi wetu hawana mitandao ya kompyuta ama ufahamu wa kutosha wa lugha za kigeni; hususan Kiingereza. Hapa ufunguo ni kuwafahamisha na kuwaelemisha wananchi; kwani ndio wadau wakuu wa mradi huu wa ujenzi wa barabara ya Serengeti uliogubikwa na utata.

bipinvishani@gmail.comRAIA MWEMA

No comments: