Thursday, May 5, 2011

DK. KASHILILA UMENENA

KATIBU wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, kwa mara nyingine amewashutumu wabunge kwamba wamekuwa ‘wakiuza sura’ zaidi bungeni badala ya kutimiza wajibu wao kama wawakilishi.

Dk. Kashilila amekwenda mbali zaidi na kusema wabunge wengi ni wavivu wasiopenda kusoma wala kudurusu nyaraka mbalimbali hatua inayowafanya washindwe kuibua hoja nzito zenye maslahi kwa umma.

Kauli hiyo imekuja siku mbili baada ya mtendaji huyo mkuu wa Bunge kujitokeza hadharani kumkingia kifua Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuhusu utendaji wake na kuwataja wabunge wapya kuwa ni mbumbu wa kanuni.

Akizungumza na Mtanzania katika mahojiano maalumu ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Dk. Kashilila alionyesha kushangazwa na utendaji wa wabunge wa sasa aliosema umejaa mbwembwe zaidi badala ya ufanisi wa kazi za uwakilishi.

Katika eneo la kusoma, Dk. Kashilila alisema. “Tunawapa vitabu na nyaraka mbalimbali lakini hawasomi, kipindi fulani wakaleta hoja kwamba vitabu inakuwa mzigo hivyo wanahitaji nyaraka ziwekwe kwenye CD.

“Tukajiuliza ni wabunge wangapi wanamiliki laptop (kompyuta ya mkononi). Tuliamua kutoa laptop 20 kwa wabunge kwa ajili ya majaribio, ili tuone wanatumia kwa kiasi gani, tulipozikusanya tulikuta hazijatumiwa na nyingine zimemwagiwa chai na bia,” alisema.

Akizungumzia utendaji, Dk. Kashilila alisema wabunge wengi wameshindwa kutambua na kuzitumia kanuni za Bunge katika kutimiza wajibu wao na badala yake wamebaki kurushiana vijembe bungeni na wakati mwingine kulumbana na spika au mawaziri.

“Katika nchi ya kidemokrasia inayoongozwa kwa utawala wa sheria wabunge ni watu muhimu sana katika kuleta mageuzi ya kimaendeleo, wana kazi na majukumu mengi sana ya kufanya lakini hawafanyi.

“Kazi yao imebaki kupiga makofi, kuchoma nyama, kula na kunywa basi. Kazi ya mbunge ni kuibua hoja za msingi na kufuatilia mipango ya Serikali,” alisema.

Dk. Kashilila alisema kwa kutumia kanuni za Bunge, wabunge wanaweza kuleta mageuzi ya maendeleo na kutatua kero za wananchi kwa haraka zaidi badala ya kusubiria ahadi za Serikali kupitia majibu ya mawaziri wake bungeni.

Dk. Kashilila alitolea mfano wa kanuni ya 30 inayoruhusu wananchi kuandaa waraka unaoelezea kero zao kisha kuwasilisha bungeni ambao mwisho wake ni Serikali kutekeleza azimio la Bunge kwa kutatua kero hiyo.

“Kanuni ya 30 inaruhusu wananchi kupeleka bungeni petition (maombi). Kanuni inasema, kama kuna tatizo ambalo limekuwa kero kwa wananchi na Serikali hailitatui, wananchi wa eneo husika wanatakiwa kuandika waraka.

“Wakishaandika na kuorodhesha majina yao, wanachotakiwa kufanya ni kumtafuta mbunge asiyekuwa wa jimbo husika. Yule mbunge anapeleka ile petition bungeni.

“Kwa mujibu wa kanuni hii, Spika atamruhusu yule mbunge kusoma maombi ya wananchi ya kutaka kero ile iondolewe. Spika ataagiza Kamati ya Bunge ichunguze haraka suala hilo na kisha baada ya hapo, Spika atatoa azimio la Bunge la kuitaka Serikali kutatua kero hiyo.

“Huu ni mwaka wa 30 kanuni ii ipo, sijaona mbunge akitumia kanuni hii… wananchi wana matatizo mengi, hawa wabunge wanashindwa vipi kuwaandaa wananchi wao na kufuata maelekezo ya kanuni hii kutatua kero za watu?” alihoji.

Dk. Kashilila aliendelea kusema: “Mbunge makini huwezi kumwona akihangaika na maswali bungeni, kule ni kupoteza muda, maana waziri anaweza kutoa majibu mule bungeni ikawa hivyo swali limejibiwa halafu hakuna kitu kinachoendelea,” alisema.

Kauli hiyo ilikuwa majibu kwa mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) ambaye hivi karibuni alimwandikia barua Spika wa Bunge, Anne Makinda, akilalamikia swali lake la Wizara ya Maji kutojibiwa kikamilifu bungeni.

“Hiyo haikuwa njia sahihi, sasa anamwandikia barua Spika ili iweje? Spika hajibu maswali. Ndiyo maana nasema wabunge hawasomi na hawataki kujishughulisha na suala zima la kudurusu,” alisema.

Hata hivyo Dk. Kashilila alimsifu Mbunge wa Moshi Mjini, Phillemon Ndesamburo (CHADEMA): “Wewe uliwahi wapi kumwona Ndesamburo akiuliza swali bungeni? Na wala hatoi hela zake mfukoni, yule mzee ni mjanja anacheza na kanuni na kufuatilia ahadi za Serikali.

“Anachokifanya yeye, anafuatilia ahadi na mipango ya Serikali anakwenda kwa DAS (Ofisa Tawala wa Wilaya) anawaeleza kuwa kuna fedha zilizotolewa, wale jamaa wakiona vile wanajua mbunge amejua mpango mzima wanajipanga kutekeleza.

“Baada ya hapo, anapanda jukwani anawaeleza wananchi barabara ya kuanzia mahala fulani hadi Kibololoni kuanzia wiki ijayo itaanza kujengwa. Kweli ikifika siku hiyo watu wanaona magreda,” alisema.

Akitolea mfano wa mabunge mengine alivyoshughulikia maombi ya wananchi, Dk Kashilila alisema: “Kule India, Serikali iliwahi kuwazuia wanawake wanaojiuza. Wale wanawake wakaandika petition (maombi) wakampa mbunge akawasilisha bungeni.

“Katika malalamiko yao, wanawake hao walihoji sababu za Serikali kuwaingilia na kuwazuia wasifanye kazi ile, wakati Katiba ya nchi yao inasema kila raia anapaswa kuwa na ajira na Serikali haijawapa ajira.

“Bunge lilichunguza likaona Serikali imefanya makosa likatoa azimio Serikali iliwalipa wale wanawake kila mmoja fedha inayolingana na Sh milioni 30 kila mmoja na eneo jingine wakatafutiwa kazi. Hiyo ndiyo nguvu ya petition (maombi),” alisisitiza.

Katika hatua nyingine Dk. Kashilila aliwaponda wabunge wa viti maalumu akisema kundi hilo ni mzigo kwa taifa kwa kuwa hawana kazi wanayoifanya zaidi ya kukidhi maslahi ya kisiasa.

Dk. Kashilila alisema ni Tanzania pekee ndiyo yenye wabunge wa aina hiyo ikilinganishwa na nchi nyingine zinazofuata mfumo wa mabunge ya jumuiya ya madola (Commonwealth).

Mtendaji huyo wa Bunge alihoji sababu za kuwepo kwa kundi hilo la wabunge, wakati wabunge wa majimbo wapo. Wabunge 102 kati ya wabunge 350 waliopo bungeni hivi sasa ni wabunge wa viti maalumu.

“Wabunge wa majimbo wapo 239, ndiyo kusema kwamba katika eneo lote la Tanzania hakuna eneo lisilokuwa na uwakilishi bungeni. Ukisema kila mbunge wa jimbo aende jimboni kwake, utakuta nchi yote ipo covered (ina wabunge).

“Sasa unajiuliza kama hivyo ndivyo hawa wabunge wa viti maalumu wa kazi gani? Wanafanya kazi ipi special (maalumu) ambayo haifanywi na mbunge wa jimbo?” alihoji.

Alipoulizwa iwapo hoja yake hiyo inalenga kushauri wabunge wa viti maalumu wafutwe, Dk Kashilila alisema: “ Mimi siwezi kushauri moja kwa moja kwamba wabunge hawa wafutwe, ila tunaweza kufanya marekebisho tukaiga affirmative policy ya Uingereza.

“Tukatenga maeneo, kwamba katika kila majimbo kumi ya uchaguzi majimbo manne yawe kwa ajili ya wanawake kama hoja ni kuwa na wanawake bungeni. Hapo vyama visisimamishe wagombea wanaume katika majimbo hayo.

“Kwa kufanya hivyo tutajikuta tumewaondoa hawa wabunge wa viti maalumu ambao kimsingi mimi sioni kazi wanayofanya na badala yake tutakuwa na wanawake bungeni, lakini wanaotokana na majimbo,” alisema.

Wakizungumza na Mtanzania kwa nyakati tofauti, baadhi ya wabunge walitoa maoni tofauti kuhusiana na kauli hiyo, huku baadhi yao wakiipinga wazi wazi kauli hiyo.

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) alimtaka Dk. Kashilila kwenda mbali zaidi kwa kutaja takwimu za wabunge wavivu wa kusoma ikiwezekana hata na vyama vyao, badala ya kutoa kauli ya jumla.

“Mimi sitaki kuzungumzia sana kauli hiyo ya Dk. Kashilila. Wewe Mkotya unanijua mimi napenda kusoma na wala huwa sipendi kutoa kauli za kukurupuka, ndiyo maana huwa napenda kusoma.

“Lakini ninachotaka kusema ni kwamba Dk. Kashilila asiishie tu hapo kusema wabunge ni wavivu wa kusoma, kwa kauli hiyo inawahukumu hata wale wabunge wanaotimiza wajibu kikamilifu.

“Yeye ni mtendaji wa Bunge, ataje takwimu za wabunge wavivu pamoja na vyama vyao, ili wabunge hawa waweze kubadilika kabla ya 2015. Kauli hii ya Dk.Kashilila inathibitisha aina ya wabunge waliopo bungeni.

“Mwaka jana wakati wa kampeni CHADEMA tuliwatahadharisha sana wananchi na kuwataka wasipige kura kwa ushabiki, wachague wabunge makini wenye uwezo. Uwezo wa mbunge ni pamoja na kusoma nyaraka mbalimbali ili uweze kuisimamia vizuri Serikali,” alisema.

Kwa upande wake Mbunge wa Ilala, Musa Azan Zungu (CCM), alisema: “Wabunge hatusomi sehemu moja na wala hatutoki sehemu moja, hivyo siwezi kusema habari ya kusoma kwa wabunge ambao sikai nao.

“Lakini kwa upande wetu Ilala tunaendelea vizuri, tunaboresha huduma katika Hospitali yetu ya Amana pamoja na miundombinu mbalimbali, nimemaliza au unajambo jingine unataka?” alihoji.

Alipotakiwa kufafanua zaidi, alisema:“Wabunge wanapatiwa mafunzo na semina mbalimbali, sasa utasemaje watu hawasomi? Wabunge tunasoma na kudurusu ispokuwa pale bungeni hatupati muda wa kutosha wa kuchangia na muda ni mdogo,” alisema.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM) alimshangaa Dk. Kashilila kwa kutoa mashambulizi makali dhidi ya wabunge wa viti maalumu, huku akisema wabunge hao ni watu wenye mchango mkubwa kwa jamii.

“Hayo ni maoni yake, lakini kusema wabunge wa viti maalumu ni mzigo kwa taifa mimi nadhani siyo sahihi. Wabunge wa viti maalumu wana mchango mkubwa kwa jamii na hata hao walioweka mfumo huu walijua wabunge wa viti maalumu wana mchango.

“Tunafanya shughuli nyingi za kijamii, tumekuwa tukisaidiana na wabunge wa majimbo katika mambo mbalimbali. Pale ambapo wabunge wa majimbo hawatimizi sisi tumekuwa tukiziba mapengo. Kwa hiyo si kweli kusema wabunge wa viti maalumu hawana kazi ya kufanya,” alisema.


MTANZANIA

No comments: