Monday, April 4, 2011

UVCCM YATAKA MAFISADI WAFUKUZWE UANACHAMA CCM


Geofrey Nyangóro


KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UV-CCM), Martine Shigela amepokea mapendekezo ya vijana wa Tawi la Matangini, Kimara jijini Dar es Salaam kwamba wtuhumiwa kwa ufisadi akiwamo waliokuwa mawaziri na wabunge wa sasa, kufukuzwa uanachama ili kurejesha imani ya chama hicho kwa wananchi.

Akizungumza baada ya kusomewa risala hiyo Shigela alisema anaungana na vijana hao kwa asilimia mia moja na kwamba viongozi wasio na maadili ni mafisadi na mwisho wao umekaribia.

Shigela alisema chama hicho hivi sasa kina mafisadi na wamekuwa wakikiuka maadili kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa na kwamba kinachofanyika sasa ni kuangalia namna ya kukisafisha chama hicho kuanzia ngazi ya chini.

Kuhusu maandamano ya Chadema alisema umoja huo haupaswi kukaa kimya na wao wana haki ya kuandaa maandamano kupinga Chadema isifanye maandamano kushinikiza uchaguzi wa Meya Arusha, urudiwe.

Awali akisoma taarifa hiyo yenye kurasa 11 katika mkutano wa tawi, uliofanyika juzi Kimara Matangini, Katibu wa UV-CCM wa tawi hilo Asenga Abubakar alisema vigogo hao wamechangia kuiweka CCM katika hali mbaya kutokana na tuhuma za ufisadi.
“Kama tunakipenda chama, lazima tuseme ukweli na chama kijivue gamba kama alivyosema Mwenyekiti Rais wetu Dk Jakaya Kikwete kwenye mkutano wa kusherehekea miaka 34 ya CCM.

“Tunashauri uchunguzi wa kina ufanyike katika ushiriki wao katika mikataba ya kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond, Dowans, mkataba wa madini wa Buzwagi, ununuzi wa Rada na Ndege ya rais kwani ni aibu kubwa kwa baadhi ya watu hawa kuendelea kuwa wajumbe wa kamati kuu na ile ya maadili, achilia mbali uanachama wa CCM,”alisema.

Vijana hao walishauri chama kuunda kitengo cha uchunguzi juu ya mwenendo wa wanachama wao na vigogo na kusema kweli juu ya majibu na matatizo yanayoikabili CCM.

Alisema idadi ya watu wanaokichukia chama imezidi kuongozeka na hilo ni kutokana na wananchi kutoridhishwa na mambo yanayotokea katika uongozi wa juu wa chama hicho.

Kuhusu uongozi wa juu vijana hao waliwatupia lawama kuwa kitendo chao cha kubadili majina ya wagombea na kuwaacha wagombea wanaokubalika kwa wananchi ni chanzo cha wananchi kuichukia CCM.

Akizungumzia hali ya kisiasa Abubakari alisema ni mbaya na imevurugwa wakati wa kura za maoni.


MWANANCHI

No comments: