Thursday, April 21, 2011

NAPE: VITA YA MAFISADI SASA INAHAMIA KWA VIGOGO SERIKALINI

Tumaini Msowoya, Iringa

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amesema vita dhidi ya ufisadi sasa inahamia kwa watendaji wa Serikali wakiwamo mawaziri ambao watashindwa kutekeleza Ilani ya chama hicho kwa vitendo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Nape alisema mkakati wa chama sasa ni hakuhakikisha kuwa mafisadi hawana nafasi tena kwenye chama hicho na Serikali yake.

"Tumekuwa tukisema kwamba vita ya ufisadi haitaishia kwa watendaji wa chama tu. Itakwenda hata kwa watekelezaji wa Ilani ya CCM. Tutahakikisha kila anayepewa jukumu la kutekeleza ilani yetu, anawajibika," alisema Nnauye.

Alipotakiwa kufafanua aina ya watendaji anaowalenga katika vita hiyo, Nape alijibu: " Nasema wote, hata kama ni mawaziri au wakuu wa mikoa kwa sababu tunapoingia kwenye uchaguzi, siyo wao wanaokinadi chama. Huu ni wajibu wa kuhakikisha ilani yake inatekelezeka ili tunapokuja kwenye chaguzi kisipate pingamizi."

Kauli hiyo ya Nape ni msisitizo wa kile alichokisema juzi kwenye mkutano uliofanyika katika Viwanja vya Ofisi za Chama hicho, mkoani Iringa.

Katika mkutano huo, Nape alisema baada ya kumaliza vita dhidi ya mafisadi walioko ndani ya CCM, hatua inayofuata ni kwa viongozi wa Serikali wa ngazi zote ambao wamekuwa wakikisaliti chama hicho kwa kujifanya miungu watu.

Nnauye alisema suala la kujivua magamba linapaswa kuanza kufanyiwa kazi katika ngazi za wilaya na kwamba, ikiwa viongozi hao hawataamua kujiondoa wenyewe, wataondolewa kwa nguvu.

“Hatua inayofuata ni ya viongozi wa Serikali ambao ni wasaliti, wale ambao badala ya kutekeleza ilani ya chama chetu wanatekeleza ilani za matumbo yao. Hatutakubaliana na jambo hilo na hili lazima lifanyika kabla ya mwaka 2015,” alisema Nnauye.

Alisema wanachama pia watapatiwa nafasi ya kuwataja watu ambao wamekuwa wakichangia kukiangamiza chama hicho, wakiwemo mafisadi na wala rushwa.

Aliwataka viongozi wa CCM, kuanzia ngazi za mikoa, wilaya, kata na matawi kujitathmini wenyewe na hatimaye kujivua madaraka ikiwa wamekuwa wakitajwa kuhusika katika kashfa mbalimbali za ufisadi ambazo ndizo zilizokibebesha chama hicho mzigo mkubwa.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), John Chiligati alisema chama hicho kimetambua kuwa kilifanya makosa na hivyo kimejirekebisha ili kurudisha hadhi yake kwa wananchama.

“Kuna watu wameibebesha CCM mzigo mkubwa ambao umekigharimu, sasa hivi tunarejesha chama kipya ambacho kigezo cha uongozi au ujumbe wa NEC hakitakuwa fedha tena....” alisema Chiligati.

Katika mkutano huo wa Iringa Mjini, zaidi ya wanafunzi 100 wa vyuo vikuu mbalimbali mkoani hapa walijiunga na CCM kwa madai ya kufurahishwa na hatua ya kukibadilisha chama hicho na baadhi ya viongozi wa juu kujivua gamba.

Wakizungumza baada ya kupokea kadi za chama hicho, wanafunzi hao walisema walikasirishwa na baadhi ya vitendo vilivyokuwa vikifanywa na watu wachache ndani ya chama hicho, ndiyo maana waliamua kupigia debe vyama vya upinzani.

Walisema wana uhakika kuwa Halmashauri Kuu ya Taifa ndiyo sababu kubwa ya kulipoteza Jimbo la Iringa Mjini ambalo hivi sasa linaongozwa na Mbunge kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
MWANANCHI

1 comment:

Anonymous said...

Suala kwamba vita vya ufisadi ndani ya CCM imeisha wakati hakuna aliyenyang'anywa kadi ya uachama kati ya wale wanaojulikana kulihujumu Taifa zima kwenye kesi za Richmind na Dowans ni uhuni. Nape ni kijana lakini tayari ameshaingia katika mkumbo wa kuteteana ulioliletea Taifa letu maendeleo duni hadi hii leo. Wenye kujihusisha na ufisadi waondolewe kutoka katika chama na wapelekwe mahakamani. Sioni anapamabana vipi na ufisadi wakati hajatoa tamko wala msimamo wo wote kuhusiana na watu kama Chenge, Rostram Aziz, Karamagi, Lowassa etc kuondolewa katika chama na kushitakiwa. Nape ni mnafiki na hajui anachoongea. I have lost faith in him that i had that he would have had sympathy for his country as a young Tanzanian with future propects lead the Nation.