Thursday, April 14, 2011

MJADALA WA KATIBA: KILA MTU ANA UHURU WA MAONI NA KUSIKILIZWA

Joyce Mmasi

MJADALA wa wazi wa muswada wa marejeo ya katiba, unaotarajiwa kuwasilishwa katika kikao cha Bunge kinachoendelea mjini Dodoma, umekumbwa na dhoruba kali huku kati ya vituo vitatu vilivyotengwa kwa ajili ya kupokelea maoni, viwili vikikumbwa na vurugu mbaya zilizosababisha umwagaji wa damu na kingine kikiukataa muswada na kupinga hata kuujadili.

Dosari mbalimbali zimeonekana kutawala katika zoezi hilo la ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusiana na madai ya kuandikwa katiba mpya ambapo licha ya kupingwa na wananchi walio wengi, lakini umesababisha vurugu zisizokoma.

Bila kupindisha maneno, chama kinachoonekana na hata kulalamikiwa kuleta vurugu hizo kwa namna moja ama nyingine ni Chadema ambapo katika maeneo yote ya Dar es Salaam na Dodoma kimetajwa kuhusika na vurugu.

Hali hiyo imeleta mitazamo tofauti ambapo baadhi ya watu wameeleza kuwa hali hiyo ikiachwa iendelee upo wasiwasi wa maoni yanayotafutwa na kisha kufanikiwa kukusanywa kuwa yenye sura ya chama kimoja tu cha siasa.

Hatua ya viongozi wa Chadema wakiongozwa na mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kupita katika chuo kikuu cha Dodoma na kukusanya wanafunzi kwa maelezo ya kuwahamasisha wausome muswada na kisha wajitokeze kwa wingi katika ukumbi ulioandaliwa kwa ajili ya maoni ili kwenda kutoa maoni yao ndio chanzo cha kukihusisha chama hicho na vurugu hizo za Dodoma.

Vurugu hizo za wanafunzi waliolazimisha kuingia katika ukumbi ulioandaliwa kwa ajili ya shughuli hiyo licha ya kuelezwa kuwa kutokana na idadi yao kuwa kubwa kuliko uwezo wa ukumbi, wasingeruhusiwa kuingia wote waliozidi 2,000, agizo ambalo wanafunzi ho walilikataa na askari wa kutuliza ghasia kufika eneo la viwanja vya Bunge na kuwatawanya wanafunzi hao kwa mabomu ya machozi hali iliyosababisha zoezi hilo kusimama kwa muda kutokana na vurugu hizo.

Mbunge wa Arusha mjini, Lema amekuwa akitamka wazi kwa nyakati tofauti kuwa yeye na chama chake wamefikia hatua ya kuwahamasisha wanafunzi kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao juu ya muswada huo kwa kuwa wanafunzi hao ni wasomi wenye uwezo wa kuusoma na kuuelewa muswada huo ulioandikwa kwa lugha ya Kiingereza.

“Nimemwambia mkuu wa mkoa wa Dodoma aliponiuliza, kuwa nitazunguka katika vyuo vyote nchini, nitaenda kuwahamasisha wanafunzi kujitokeza kwa wingi kuusoma na kuleta maoni yao kuhusu muswada wa marejeo ya Katiba, nimeamua kuanza na wasomi maana ndio wenye uwezo wa kusoma na kuelewa lugha ya Kiingereza iliyotumiwa makusudi huku ikijulikana wazi kuwa lugha inayoeleweka kwa urahisi na Watanzania wengi ni ile ya Kiswahili,” alisema Lema alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Chuo kikuu cha Dodoma mwishoni mwa wiki iliyokwisha.

Ingawa Chadema kupitia viongozi wake wanakataa kuhusika na vurugu hizo, lakini ukweli halisi ni kuwa chanzo cha vurugu za Dodoma ni msimamo wa wanafunzi wa UDOM kuamua kujazana kwa maelfu katika ukumbi wa Pius Msekwa uliopo viwanja vya Bunge, huku wakishinikiza kuingia wote kwa wingi wao licha ya ukumbi huo kuonekana wazi kuwa hauna uwezo wa kubeba idadi kubwa ya watu.

Kwa maelezo ya watendaji wa ofisi za Bunge, ukumbi huo unao uwezo wa kubeba watu 500 tu, hali iliyowalazimu wahusika katika zoezi hilo kuwataka wanafunzi waliojitokeza kwa ajili ya kutoa maoni yao kuingia kwa mafungu ili waweze kupata nafasi ya kutoa maoni.

Uhusiano wa Chadema na vurugu hizo za Dodoma unadhihirika pale wanafunzi wa UDOM walipolalamika kusumbuliwa na Chama hicho kwa kuitwa na wanapoitikia wito kuletewa usumbufu tena wa kutakiwa kuondoka eneo hilo huku wakiwa wamefika hapo kwa maelekezo yao.
“Hatuondoki ng’oo, tuende wapi wakati ni nyinyi mliotufuata Chuoni na kututaka tufike hapa kwa wingi, iweje sasa tumeitikia wito halafu mtuambie tuondoke? Hatuondoki hapa mpaka kieleweke,” baadhi ya wanafunzi wa UDOM walisikika wakimjibu Lema.

Wakati vurugu za namna hiyo zikitokea mkoani Dodoma, hali ya namna hiyo ilijitokeza pia jijini Dar es Salaam kwa wajumbe wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chadema kuzomea wajumbe waliotoka katika Chama tawala hali iliyosababisha mwenyekiti wa mjadala huo kulazimika kusimamisha zoezi hilo kwa saa mbili.

Chanzo cha vurugu za Dar es Salaam ni tabia ya zomea zomea iliyofanywa na washiriki wa semina wakati mwakilishi wa CCM Tambwe Hiza alipokuwa akitoa mchango wake juu ya muswada huo, alishindwa kumaliza kile alichokuwa akisema kutokana na kuzomewa na kutakiwa asiendelee huku wachangiaji kama Dk. Slaa na wengine wakishangiliwa hata kabla ya kuanza kuongea.

Lakini hali ya vurugu na kutokuelewana ilionekana kutowafurahisha baadhi ya viongozi wa idara mbalimbali za serikali ambao walitoa maoni yao kuhusiana na vurugu hizo.

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju anasema ni jambo la kusikitisha kuona watu wameandaliwa kuleta vurugu badala ya kutoa hoja zitakazosaidia kuondoa dosari zinazolalamikiwa ili ziweze kurekebishwa.

Anasema lipo tatizo la baadhi ya watu ambao hawataki kuruhusu wala kusikiliza maoni na mawazo ya watu wengine na badala yake wanataka watu fulani tena wa upande mmoja tu ndiyo watoe maoni yao na ndio yasikilizwe na kuchukuliwa kama mawazo yanayotakiwa.

“Hata kama wanatoa maoni mazuri kiasi gani lazima wasikilize na maoni ya watu wengine, lakini tatizo lililopo ni kuwa watu wamejiandaa au kuandaliwa kutaka maoni ya upande mmoja tu ndio yapewe nafasi na kusikilizwa huku wengine wakinyimwa nafasi,” anasema Masaju.

Spika wa Bunge, Anne Makinda naye alitoa angalizo kwa kuwataka wananchi wote wanaofika katika vituo vya kukusanyia maoni wasikilize mawazo ya wengine na kwamba kamati itayapokea maoni yote na kuyafanyia kazi.

“Tabia ya kuzomea na kushangilia haikubaliki. Kinachohitajiwa ni maoni, sikiliza mwenzio anasema nini na wewe toa ya kwako, kamati zitayachukua mawazo na maoni yako na kuyafikisha kunapohusika. Ni lazima mawazo ya kila mtu yaheshimiwe.

Kwa upande wake Msajili wa vyama vya siasa, John Tendwa anasema ni hatari kubwa kuona kuwa wapo watu ambao hawataki kabisa kusikiliza wala kuwaona watu wengine wakitoa maoni yao na kusema hali hiyo ni ya hatari kubwa kwani huenda ikasababisha zoezi kuwa la watu fulani na sio la Watanzania wote.

Tendwa anasema “watu wameandaliwa kufanya vurugu, lakini ushauri wangu ni kuwa watu wajadili hoja, na kila mtu asikilize na kuheshimu mawazo ya mwenzake hata kama hakubaliani nayo, huo ndio ustaarabu na ndio tabia ya wasomi kusikiliza na kuheshimu mchango wa wenzako,” anasema .


MWANANCHI

No comments: