Wednesday, April 13, 2011

MABASI YAGONGANA NA KUUA WANNE.


Julieth Ngarabali, Mkuranga


WATU wanne wamefariki dunia papo hapo na wengine 30 kujeruhiwa vibaya katika ajali iliyohusisha basi mali ya kampuni ya Sumry huko katika eneo la Kisemvule barabara kuu ya Kilwa wilayani Mkuranga.

Ajali hiyo ilitokea majira ya saa moja usiku wa kuamkia jumatatu wilayani humo na ilihusisha basi aina ya Nissan Diesel, mali ya Sumry iliyokuwa ikiendeshwa na Patrick Lenard (35) Mkazi wa Tabata ikitokea Mtwara kwenda Dar es Salaam.

Basi hilo liligongana uso kwa uso na Toyota Coaster mali ya kampuni ya Asif iliyokuwa ikiendeshwa mkazi wa Mbagala Dar es Salaam na ilikuwa ikitokea mjini humo kwenda Rufiji.Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Absaloom Mwakyoma alithibitisha jana kutokea kwa ajali hiyo ambapo alisema ilisababisha vifo vya watu wanne ambao majina yao bado hayajatambulika na miili yao imehifadhiwa katika chumba cha maiti Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga.

Mwakyoma alisema kati ya majeruhi 30 wa ajali hiyo,wanne wamelazwa Hospitali ya Temeke na 19 Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga.Alisema chanzo cha ajali hiyo ni gari nyingine Toyota Land Cruiser Hardtop iliyokuwa ikiendeshwa na Mkazi wa Mtwara kuegesha pembeni mwa barabara vibaya na mwendo kasi wa basi la Sumry na Coaster hiyo.

Kamanda huyo wa Polisi Pwani alisema watuhumiwa wa ajali hiyo ni madereva wote wa magari hayo na kwamba wameshakamatwa na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote.

MWANANCHI

No comments: