Saturday, April 30, 2011

KUPOROMOKA KWA UTAWALA WAO: MWANZO WA MWISHO?

Na. M. M. Mwanakijiji

Huwezi kutawala wananchi bila maono. Huwezi kuwatawala watu bila kuwapa mwelekeo wa wapi unataka kuwapeleka nawe badoukajiita "kiongozi mzuri". Naam, utawala usio na maono ya pamoja yenye kushirikisha matamanio na njozi za wananchi hugeuka na kuwa utawala wa kuburuzana, kutishana, kubishana na kubabaishana. Ni utawale wa kibabe.

Utawala ambao msingi wake ni vitisho, hadaa, matumizi ya dola au vyombo vya usalama ni utawala ambao umetengeneza ndani yake mbegu za kuvunjika kwake. Jamii zote za watu duniani ambazo zimewahi kujaribu kujenga tawala zisizo na maono ya pamoja zimeishia kuparaganyika. Zilijaribu kudumu kwa muda lakini kwa vile mbegu za kuparaganyika zinapandwa na kumwagiwa maji na ukosefu wa maono basi tawala hizo hufika mahali huanza kujivunjavunja zenyewe kama biskuti zilizomwagiwa maji.

Hili ni kweli kuanzia utawala wa enzi za Waajemi na Wakaldayo kama ilivyokuwa katika utawala wa Warumi na Wagiriki na kama ilivyokuwa katika tawala za Wamisri wa kale na tawala nyingine nyingi duniani. Tawala zinapofikia mahali pa kufanikiwa huanza kutengeneza ndani yake chembechembe za ukosefu wa maono kwani kila mmoja anaanza kutenda kwa manufaa yake mwenyewe na baada ya muda wanajikuta kundi kubwa la watu wao likiwa limetupwa nje ya baraza la mafanikio.

Hili ndilo lililosababisha Mapinduzi ya Ufaransa na baadaye kuvunjavunja nguvu za Mfalme kule Uingereza na hata kuchochea kwa kiasi kikubwa mapinduzi adhimu ya Marekani ambayo yalibainisha uwezo na haki ya wananchi kuikamata nchi na utawala wao mikononi mwao.

Katika taifa letu watawala wetu wameanza kuparaganyika. Sababu kubwa inayokoleza na kuharakisha kuvunjika vunjika kwa utawala wao siyo ufisadi tu - kwani ufisadi hasa ni dalili ya sababu yenyewe bali hasa ni Uroho. Wenzetu wanaita "greed"

Uroho kama nitakavyokuja kuonesha huko mbeleni tukijaaliwa ndio msingi wa kuvunjika na kumeguka kwa watawala kwani kila mmoja wao anataka kukusanya zaidi kwake na kwa familia yake na kwa jamaa yake. Uroho siyo wa madaraka tu - kwani huo upo na wote tunauona bali uroho mali na vitu. Kwa kadiri ambavyo waroho hawa wanazidi kujikusanyia pasi wenyewe kujua wanajikuta wanawanyangánya wananchi wao vitu vyao vingi kwa kutumia "sheria na taratibu".

Hata hivyo huwezi kuwanyangánya wananchi kila kitu. Unaweza kuwanyangánya ardhi, unaweza kuwanyangánya nafasi za kufanikiwa, unaweza kuwapora hata nguvukazi yao lakini kuna vitu viwili huwezi kuwapora na ni vitu hivyo ambavyo huwezi kuwapora ndivyo ambavyo tumeviona vikisababisha mabadiliko makubwa huko Afrika ya Kaskazini na Mashariki ya kati. Vitu hivyo ni Utu na Uhuru.

Mwanadamu ni kama paka ambaye umemuweka kwenye kona na kuanza kumpiga au kumnyanyasa. Utaweza kufanya hivyo kwa muda fulani lakini anapofikia mahali ambapo kizingiti cha woga kinapaswa kuvukwa mwanadamu hana cha kuogopa kwani nini kitaweza kumtokea zaidi ambacho tayari hakimtokei? Ndio utaona kuwa wanadamu katika mazingira hayo hawaogopi kifo wala mateso kwani hivyo vyote vinaweza kuhimiliwa isipokuwa ukosefu wa Utu na uhuru.

Ni hili ndilo liliwafanya kina Mandela kwenda kifungoni, Martin Luther King Jr. kutembea kule Selma, Alabama na hata kina Nyerere kukubali kufikishwa mahakamani kwa makosa ya uchochezi. Ni hili la kutambua tunu isiyo kifani ya utu na uhuru wa mwanadamu vilivyowafanya wananchi wa Zanzibari kuinuka dhidi ya utawala dhalimu wa Sultani na vibaraka wake na hatimaye kuweka utawala wa wananchi na kurudisha utu na uhuru wao.

Ni hili ndilo tunaloliona Syria leo hii ambako vikosi vya Bashar vinajitahidi sana kuzima maasi. Tatizo ni kuwa Bashar na wengine wenye kutegemea dola wanasahau kuwa mwanadamu akishavuka kizingiti cha woga hakuna risasi, pingu, wala jela inayoweza kuzima fikra zake zinazolia "mabadiliko mabadiliko". Wamisri baada ya kumfunga Khaled kwa wiki mbili wakati wa vuguvugu la mabadiliko lililomuondoa Mubarak miezi michache tu iliyopita walidhania kuwa kwa kufanya hivyo basi kijana yule angeweka manyanga chini na kwenda kujificha na familia yake.

Hawakutarajia kumuoja Khaled akizungumza kwenye TV na kusema kuwa yuko tayari kupoteza vyote alivyokuwa navyo - pamoja na familia yake - kama kwa kufanya hivyo kungempatia hadhi na utu na uhuru wake kama mwanadamu. Hii dhana watawala waliolewa madaraka hawaielewi. Sote tunakumbuka kilichotokea masaa machache baadaye kwani wale Wamisri ambao tayari walishaanza kukata tamaa walipata nguvu mpya na hatima kufanya kile kinachoitwa "the final push" iliyomtoa Mubarak madarakani.

Ndugu zangu, utawala wa CCM nchini umeparaganyika. Hawana maono ya pamoja na hawana mwelekeo wa pamoja - wanatuongoza kutoka katika hulka na siyo kutoka katika mtima wa kiakili. Wanaongozwa kama na hisia na wamepoteza uwezo wa kushika gidamu ya farasi wa mabadiliko na sasa mabadiliko yanaanza kuwaperekesha puta. Wameparaganyika kiasi kwamba sasa wanaanza kuumana na kutafunana wenyewe kwa wenyewe huku wakijiaminisha kuwa wanaongoza!

Naam, tunachoshuhudia ni mwanzo wa mwisho wa utawala ambao zamani uliwahi kuwapa wananchi wetu tumaini; tunashuhudia mwisho wa kizazi ambacho kilipewa nafasi ya kutuongoza kikashindwa na hata jaribio la kupitisha mikoba yao kwenda kizazi kingine linaonekana kushindwa vile vile kwa sababu badfo wanaamini ni wao pekee ndio wenye kustahili kutawala. Siyo hivyo tu wanaamini wanatakiwa kutawala bila kuulizwa, wafuje bila kukatazwa, wale bila kunyangánywa na wagawane bila watu wengine kusema kwanini.

Watanzania wameshavuka kizingiti cha woga; wanadai mabadiliko. Mabadiliko ambayo msingi wake ni Uhuru na Utu. Huko ndiko tulikoanzia kama taifa. Naam huko ndiko tunarudia. Nje ya hapo ni uadui wa kudumu kati yetu na wao. Wanyakyusa wanasema "tukufumusya ubulughu, bwitu naabene". Yaani tunatangaza ugomvi kati yetu na wao. Ni ugomvi wa kudumu. Mpaka wao wasalimu amri.

No comments: