Thursday, April 7, 2011

KATIBA MPYA: WATANZANIA WANAJUA WANACHOKIHITAJI?Joyce Mmasi

“BIA moja inauzwa kwa Sh1,500, halafu kilo moja ya Maharage ni Sh1,700. Je, maharage ni anasa kuliko bia?
Je, tunang’ang’ana leo kudai katiba mpya sasa, badala ya kuangalia ahadi ya maisha mazuri kwa wananchi wetu wanaokosa chakula au kukipata kwa bei ambayo haiwezekani tena?
Je, katiba mpya ndilo tatizo la sasa la wananchi wa Tanzania? Wanaodai Katiba mpya ni watu ambao tayari wanayo maisha na hiyo katiba mpya ni kwa ajili ya kuwalinda na kuwasaidia.

Hizi ni baadhi ya hoja zilizoibuliwa wakati wa kongamano la katiba lililofanyika Jumamosi katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo kijana aliyejitambulisha kwa jina la Macdonald, ambaye ni mwanafunzi aliyedai amehitimu shahada ya sheria katika chuo hicho mwaka jana alipopewa nafasi ya kutoa mchango wake akiwa na jazba alionekana kuwashambulia wengi waliokuwamo katika ukumbi huo na kuonekana akiunga mkono harakati za kudai katiba mpya.

Kijana huyo aliyesababisha ukumbi wote kukaa kimya kwa muda kufuatia mchango wake, licha ya kujitambulisha kama mwana- CCM, alivishutumu vyama vyote vya siasa nchini akisema kuwa vinaacha kujadili masuala ya msingi, ikiwamo kuangalia jinsi ya kutatua matatizo yanayolikabili taifa na wananchi wake hasa umaskini ambao ndio unawasumbua walio wengi na badala yake wanatumia muda wao mwingi kupambana majukwaani wakidai katiba mpya, ambayo kijana huyo alisema haina umuhimu kama ilivyo kwa tatizo la ugumu wa maisha unaoendelea kukua na kuongezeka siku hadi siku.

“Vyama vyote vya siasa, iwe CCM, Chadema, CUF na hata wanaharakati, wote wanazunguka tu wakijifanya hawajui matatizo ya wananchi, lakini tatizo siyo katiba mpya, bali hali za maisha ya wananchi wa vijijini ambao hawana shida na hiyo katiba, tatizo ni rasilmali zilizopo kushindwa kutumiwa vyema kuwakomboa wananchi,” anaeleza kijana huyo.

“Leo mwanafunzi wa chuo kikuu anapewa fedha ya kujikimu ya Sh5,000 kwa siku, anapewa asilimia 50 ya mkopo anajikuta akisoma katika mazingira magumu yasiyomwezesha kufanya vizuri. Haya ni matatizo makubwa kuliko hilo la Katiba na jambo la kushangaza ni kuwa hakuna anayesimama na kuyazungumzia matatizo hayo, Watanzania wengi wanaishi maisha ya shida, jiulizeni wote mliokaa hapa, watu wa kijijini wanaishi maisha ya namna gani.

Je, rasilimali za nchi yetu zinamsaidiaje mkulima aliyeko kijijini, je, wananchi wa kijijini wanaitaka katiba mpya,” aliendelea kuhoji kijana huyo.Kijana huyo alitumia muda wake mfupi kutoa dukuduku lake hilo na kusababisha ukumbi wote kuwa kimya hali iliyoashiria kuwa licha ya ujumbe ule kutolewa kwa jazba tena na kijana aliyeonekana kuwa mdogo kiumri, lakini inaelekea uliwafikia watu wengi na kila aliyeusikia wakabaki wakinong’ona kuwa kijana yule anayo hoja ya msingi licha ya kuitoa kwa jazba au hasira.

Hata hivyo, mchango wa kijana huyo ulijibiwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Barnabas Samatta ambaye alikuwa mchokoza mada katika mjadala huo ambaye pamoja na kukiri kuwa kijana yule hakufanya lolote baya kutokana na kuwa alitimiza haki yake ya kikatiba ya kutoa maoni, lakini akambeza kwa kumwambia kuwa Katiba mpya inaweza kuja na vipengele vitakavyosababisha kubana matumizi na kuwezesha matumizi yatakayopatikana kumfikia mwananchi wa kijijini pamoja na rasilmali zilizopo kuweza kumfikia mwananchi.

“Namuuliza yule kijana, endapo Katiba mpya itasema tupunguze idadi ya wabunge wawe 100 na mawaziri wasizidi 19, fedha zitakazosalia kutokana na kupunguza matumizi namna hiyo si zitaelekezwa katika kisaidia kupunguza umasikini na hata gharama za maisha.” Kauli hizo na nyingine zilijitokeza wakati wadau mbalimbali walipokutana katika kongamano na kujadili suala la kuwapo kwa Katiba mpya Tanzania.

Mjadala huo uliokutanisha wasomi, wanasiasa, vijana na wafuasi wa vyama vya siasa katika ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam ulizungumzia hoja kuhusu haja ya kuandikwa Katiba mpya nchini Tanzania. Jaji Mstaafu, Barnabas Samata alikuwa mmoja wa wasemaji katika kongamano hilo na ndiye aliyekuwa kivutio katika mjadala ule ambapo licha ya kuzungumza mambo mengi, hoja yake juu ya mamlaka kubwa iliyopewa Bunge, moja kati ya mihimili mitatu mikuu ya dola.

Pamoja na mambo mengine, Jaji Samatta akaeleza kuwa Bunge limepewa mamlaka na madaraka makubwa mno kupita kiasi na kwamba hali hiyo inaweza kuzalisha mambo mengi yasiyofaa endapo mamlaka ya chombo hicho hayataangaliwa upya.
“ Mfano, bunge likitaka linaweza kufuta utawala wa rais na kuweka wa kifalme na hakuna wa kuhoji. Bunge linaweza kufanya hivyo bila ushauri wa wananchi, ndio maana nasema, katiba mpya iwe wazi, wananchi ndio wawe wenye maamuzi ya mwisho, wananchi wawe na uamuzi wa mwisho na siyo mahakama, bunge wala watawala,” anasema

Jaji Samatta akatoa mfano kusisitiza hoja yake ya mamlaka makubwa ya Bunge na kusema, “Mfano mwananchi mmoja alikwenda mahakamani na mahakama ambayo ni moja ya mhimili wa dola ikatoa hukumu, lakini Bunge likarudi likakaa kule Dodoma, likatunga kifungu na kufuta uamuzi ule wa mahakama…. napendekeza, Bunge liwe na mamlaka ya kutosha, lakini lisiwe juu ya wananchi, wananchi ndio wanaopaswa kuwa juu ya Bunge, rais na mahakama,” anasema Jaji Samatta.

Akashauri Katiba mpya itoe hamasa kwa wazalendo kupambana na magonjwa mbalimbali ya kitaifa.
Mapambano dhidi ya ufisadi, rushwa kutowajibika kwa umma, kununua na kuuza kura, mila za kijadi zilizopitwa na wakati ambazo zinapingana na haki za binadamu ili binadamu wasiendelee kufanywa watumwa wa utamaduni.

Ikashauriwa kwamba wafungwa na mahabusu washirikishwe katika kutunga katiba mpya. Watu wanaotumia bahasha za serikali, wale wanaotumia karatasi za serikali kuandika mambo yao binafsi, wanaotumia kalamu za serikali kuwapa watoto wao wakaandikie shuleni, wote ni wakosaji, na wanaweza kwenda jela, hivyo ni vyema tuwashirikishe waliopo huko ili nao waseme ni katiba ya namna gani inawafaa.

Kongamano lile limemalizika na hoja mbalimbali kuibuliwa, lakini kutokana na michango ya watu swali linabaki, nini mahitaji ya wananchi; katiba mpya au maisha bora. Mijadala ya Katiba inaendelea na bila shaka Watanzania wanajua wanachohitaji.

MWANANCHI

No comments: