Wednesday, April 20, 2011

JAMIIFORUMS YAKANUSHA TUHUMA ZA CCM
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mawasiliano:

Bw. Maxence Melo

Kitalu 1258, Mtaa wa Mibega

| S.L.P 4203, Dar es Salaam

| Simu: 0222843510

| Baruapepe: info@jamiimedia.com

Mtandao wa JamiiForums.com unakanusha vikali

madai yasiyo na msingi ya Chama cha Mapinduzi kuhusu umiliki, malengo na nafasi ya JF katika medani ya vyombo vya habari nchini na mchango wake katika mijadala ya kisiasa nchini.

Aprili 19, 2011, DaresSalaam, TANZANIA

JamiiForums.com ni mtandao wa kijamii (Social Network) ulioanzishwa rasmi mapema mwaka 2006 ukijulikana kama JamboForums.com na upo chini ya kampuni ya Jamii Media. Mtandao huu hutembelewa na wastani wa watu 20,000 kwa siku ambapo kila mtumiaji hutumia wastani wa dakika 17 akiperuzi tovuti hii na huperuzi walau kurasa 11. Tovuti hii inakua kwa kiwango cha asilimia 25 kila mwezi. Sasa hivi kuna wanachama waliojisajili wanaokaribia 40,000.

Hii inaifanya JamiiForums (JF) kuwa ni miongoni mwa mitandao mashuhuri zaidi na inayokusanya na kutembelewa na Watanzania wengi zaidi na ambayo inamilikiwa na kuendeshwa na Watanzania. JF inawafikia na kugusa maisha ya Watanzania wengi kila siku na kila mahali ambapo mtandao wa intaneti umefika.

Tunapenda kuufahamisha umma kuwa madai yaliyotolewa karibuni na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (Tanzania Bara) Bw. Pius Msekwa [tarehe 14, Aprili 2011] huko Dodoma kwenye kutambulisha uongozi mpya wa Chama hicho yenye kuhusisha mtandao wa JamiiForums (JF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo hayana msingi wala ukweli, ni ya kubuni na yenye lengo la kuwatisha Watanzania kutoa maoni yao huru kupitia mitandao mbalimbali katika zama hizi za TEKNOHAMA.

Madai hayo kwa mara ya kwanza tuliyasoma yakiwa yameripotiwa kwenye gazeti la Nipashe la Aprili 12, 2011 pamoja na gazeti la Mtanzania la siku hiyohiyo ambayo yote yalinukuu taarifa ya ‘Kikosi Kazi’ kilichoundwa na Chama hicho kutafuta sababu ya kufanya vibaya kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Taarifa hiyo ya Kikosi kazi ambayo JamiiForums.com imeona nakala yake maudhui yake yalirudiwa na Bw. Msekwa katika hotuba ambayo sehemu yake ilirushwa na Televisheni ya Shirika la Taifa la Utangazaji (TBC) na gazeti la serikali la Daily News la siku iliyofuata.

Sehemu ya taarifa hiyo inasema:

Midia za kijamii (social media) kama vile simu za mikononi, blogs, twitter na utubes; ni vyombo vyenye nguvu kubwa ya kuhamasisha watu. Ongezeko la wasomi kutokana na kupanuliwa kwa elimu ya sekondari na ya vyuo vya elimu ya juu, kumeongeza idadi kubwa ya watu, hasa vijana, wanaoingia katika mtandao wa teknolojia ya mawasiliano na kupashana habari. Mfano hai ni “JamiiForum(s)” iliyoundwa na vijana wa CHADEMA, ambao wanafanya kazi hatarishi kwa chama chetu na serikali yake kwa kutoa taarifa nyingi za upotoshaji ambazo zinasomwa na watu wengi sana duniani.

Madai hayo kwamba JamiiForums, inafanya kazi hatarishi dhidi ya CCM na serikali ni madai ambayo yana lengo la kuchafua mtandao huu, kuuvunjia hadhi ambayo JF imejijengea kwa gharama kubwa na kwa muda mrefu; na yana lengo la kuwatisha Watanzania ambao aidha ni wanachama au wasomaji wa mtandao wetu na mitandao mingine ya kijamii kama Twitter, Facebook na Youtube ili waweze kujiona kuwa wanafanya kitu kinyume cha sheria. Ni jaribio dhaifu la Chama Cha Mapinduzi kuubebesha lawama mitandao ya intaneti kwa mapungufu na migongano iliyojitokeza ndani ya chama chao katika miaka michache iliyopita na siku za karibuni.

Tunapenda kuwahakikishia watumiaji wa mitandao yote ya kijamii na hasa wanachama wa JamiiForums na wale wanaoutembelea mtandao wetu kila siku ili kupata habari, kushiriki mijadala mbalimbali na hata kukutana na marafiki mbalimbali ya kuwa mtandao wa JamiiForums haujaanzishwa na CHADEMA, haujawahi kufadhiliwa na chama hicho na ni mtandao huru zaidi katika Tanzania ambao Mtanzania yeyote bila kujali dini, kabila, chama au lugha ana uwezo wa kujiunga nao bure kabisa.

Tangu kuasisiwa kwake JF imekuwa ikiendeshwa kwa gharama za michango ya hiari ya wanachama wake pamoja na matangazo ya kibiashara kutoka makampuni yanayoheshimika nchini pamoja na taasisi za kimataifa kama Tanzania Media Fund ambao ni wadau wakubwa wa habari nchini. Yote haya yanafanyika bila kupoteza nafasi yetu kama jukwaa huru ambapo Watanzania “wanathubutu kuzungumza kwa uhuru”.

Tunaamini kuwa mtandao wetu umelengwa na Chama cha Mapinduzi kwa sababu katika miaka mitano iliyopita JF imeshiriki vilivyo katika kufichua karibu kashfa zote ambazo

zimerindima nchini na hatimaye kusababisha Chama tawala kuamua kujivua gamba. Tulitarajia kuwa badala ya kulaumiwa kuwa tunafanya kazi “hatarishi” kwa CCM na serikali yake, chama hicho kingetoa tuzo kwa mtandao huu kwa ujasiri dhidi ya ufisadi kwani ni kutokana na kazi yetu hiyo tumeweza hata kuonyesha kuwa kulikuwa na gamba lisilotakiwa ndani ya chama hicho kikongwe.

Tulitarajia kama chama tawala chenye vyombo vya kuweza kuufanya utafiti kujua ukweli usio shaka kuhusu taasisi ama chombo kama JamiiForums ikiwa ni pamoja na kujua wahusika na vyanzo vyake vya mapato kabla ya kutoa taarifa ya kupotosha kwa umma. Aidha tulitarajia chama hiki kutumia fursa ya mitandao ya kijamii kukusanya maoni ya wananchi lakini ajabu ni kuwa bado kinaonekana kupuuza nguvu ya mitandao hii na kuiona mahasimu kwa uhai wa chama. Tulitarajia pia CCM kuwashukuru wahisani kwa kuvisaidia vyombo vya habari ambavyo havijiwezi badala ya kuwabeza na kuwaita ‘wakoloni mamboleo’.

Madai haya ambayo yamesomwa na kusikiwa na watu wengi nchini yametusababishia usumbufu mkubwa kama taasisi inayomiliki mtandao huu na kwa vile madai haya pia yamesababisha wasiwasi usio wa lazima kwa wanachama wetu takribani 40,000 na ambao wametawanyika pote nchini na katika kila kona ya dunia. Tunaamini kuacha madai haya yasimame bila kupewa changamoto tutakuwa tumetoa kibali kwa CCM na serikali yake kuanzisha au kuendeleza sera ya vitisho na unyanyasaji kwa watu na vyombo ambavyo wakuu wa chama hicho wanaona kuwa havikubali kukaa kwenye mstari wa kutouliza na kushangilia.

Mwisho, tunapenda kuwahakikishia wanachama na wananchi wote kuwa JamiiForums itaendelea kuwa mtandao huru usiofungamana na chama chochote, dini yoyote au mrengo wowote wa kisiasa. Na ya kuwa tutaendelea kuwa jukwaa huru ambalo linaweka nafasi kwa Watanzania kuzungumza, kubishana, kubadilishana mawazo na kupeana habari mbalimbali kuhusiana na taifa lao bila woga, upendeleo, husuda au kujipendekeza kwa mtu au chombo chochote.

MWISHONo comments: