Friday, April 1, 2011

CCM NA UFALME ULIOGAWANYIKA WATASIMAMA VIPI?


Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela

MSEMO huu wa kale unasimama kuwa ni kweli. Kwamba, ufalme wowote ambao umegawanyika hauwezi kusimama.

Hoja ya msemo huu si kwamba ufalme usiokuwa na “tofauti za ndani” la hasha bali ufalme ambao tofauti zake zimesababisha ugawanyike hauwezi kusimama. Katika nadharia ya vita (war theory) majeshi yanapotoka kwenda kupigana ni lazima yawe katika umoja wa lengo na umoja wa mikakati ili kuweza kumshinda adui.

Jeshi ambalo wapiganaji wake na makamanda hawako katika lengo moja au ambao hawaelewani haliwezi kumshinda adui. Hili linathibitishwa na historia mahali pote duniani.

Kwa mfano, siku za karibuni tumeona jinsi jeshi la Libya lilivyoanza kugawanyika siku za mwanzo za mapinduzi ambapo baadhi ya wanaanga wake walitoroka na ndege zao baada ya kukataa kutii amri za kuwashambulia raia wenzao.

Haikuwa katika viongozi wa chini tu bali hata baadhi ya makamanda waliasi serikali na kwenda upande wa waandamanaji. Hili la kugawanyika tumeliona pia Yemen ambapo baadhi ya makamanda wa ngazi za juu waliamua kuchukua upande wa waandamanaji.

Nadharia hii ya umoja katika vita huenda mbali zaidi hata katika maisha yetu ya kawaida. Familia ambayo imegawanyika yenyewe ndani kwa ndani haiwezi kusimama.

Ni jambo moja kuwa na tofauti kati ya kaka na dada au baba, kaka zake na dada zake au mama na kakaze na dadaze. Lakini inapofikia kwamba tofauti hizo huzaa mpasuko wa familia kiasi kwamba hata watoto wa ndugu hao hawazungumzi maana yake ni kuwa familia hiyo imegawanyika.

Na ukiikuta familia ambayo imegawanyika kwelikweli utaona kuwa hata upande mmoja wa familia (damu ile ile) unaweza kuwa katika mafanikio makubwa lakini upande mwingine wa familia (uliotengwa) ukiwa katika hali ya umasikini wa kutupwa. Na cha kushangaza ni kuwa wakati mwingine unahitajika ujasiri wa upendo tu ambapo upatano wa familia unapatikana. Bila ya shaka kuna masimulizi mengi tu ya familia ambazo baada ya kutengana kwa muda mrefu ziliamua kupatana na kurejesha nguvu yao kama familia.

Hili nalo ni kweli hata kwenye siasa na uongozi. Ukikutana na kundi la kisiasa ambalo tofauti zake zimesababisha mgawanyiko/mpasuko basi ujue kundi hilo liko katika wembamba wa udhaifu wake na kama wasemavyo wahenga “kamba hukatikia pabovu” basi ndivyo kundi hilo linapokuwa katika hatihati ya kuvunjika. Kundi la kisiasa ambalo limefikia kugawanyika si kwa misingi ya maslahi tu bali hata kwa misingi ya kiitikadi na mtazamo ni vigumu sana kupatana.

Mgogoro unaoendelea ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) umefikia kiwango cha mgawanyiko. Ni mpasuko ambao hauwezi kuondolewa kwa vikao wala hauwezi kukoma kwa kutishiana na kupigana mikwara kwenye vyombo vya habari.

Mgawanyiko huu ni mgawanyiko wa msingi mno ambao unatishia kabisa ushindi wa CCM na tayari kwa kiasi kikubwa tunaona jinsi ulivyoigharimu CCM katika Uchaguzi Mkuu uliopita. Ni mgawanyiko wa msingi ambao kama ni vitani ni sawasawa na wanajeshi ambao mbele ya adui yao wanageukiana wenyewe na kuanza kutwangana risasi. Katika mazingira hayo adui anachohitaji kufanya ni kuokoa silaha zinazoangushwa na kuteka mateka; adui hahitaji kupigana; anasubiri ushindi usio na jasho.

Tofauti zilizopo ndani ya CCM ni kubwa kuliko tunavyofikiria na ni wazi haziwezi kumalizwa kwa kutolewa matamko juu ya matamko, kauli juu ya kauli na maelezo juu ya maelezo. Tunapoangalia kauli za Vijana Pwani, Taifa, Kilimanjaro na Tabora na muda si mrefu tutasikia wa Mwanza na mikoa mingine. Tunajikuta tunaamini kabisa kuwa vita ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015 itapiganwa kwa kiasi kikubwa ndani ya CCM.

Vijana wa CCM wataendelea kuumizana wenyewe na wakati huo huo wakongwe wa CCM nao wataendelea kuumizana wenyewe na kujeruhiana na hata wakati mwingine kuchukuana mateka. Hata kauli kama za Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa wanaolumbana walete malumbano yao kwenye vikao vya chama zinavutia masikio lakini zina walakini mkubwa.

Hao wanaolumbana ndio hao hao walioko kwenye vikao hivyo hivyo! Hivi, Rostam Aziz, kwa mfano, ataenda kulalamika wapi? Samuel Sitta aende kulalamika wapi? Dk. Harrison Mwakyembe aende kwenye kikao gani akalalamike? Kina Beno Malisa na Hussein Bashe au kina Ridhiwani na hata Mwenyekiti Kikwete mwenyewe watalalamika wapi? Ni vikao gani vya CCM ambavyo ndani yake wamo watu wasiolalamika au kulalamikiwa? Leo hii CCM kimejawa na makundi yanayopingana kiasi kwamba hata kikiitishwa kikao kimoja tu kuna uwezekano wa watu kufikia kuchapana ngumi!

Ni mgawanyiko ambao unaweza kuhitimishwa kwa hatua kuchukuliwa. Kama nilivyosema mwanzoni hapo juu kuwa mgawanyiko katika vita wakati mwingine unasababisha majemedari kuhama kambi kabisa lakini wakifanya hivyo wajue wawe tayari kushambuliwa na waliokuwa marafiki zao. Wale wanaopingana ndani ya CCM hawawezi wote kubakia ndani ya CCM. Hawawezi kubakia kwa sababu wanakipotezea chama hicho muda na nguvu ya kupambana na changamoto za kiuongozi na kisiasa.

Hivyo, vile vinavyoitwa “vikao vya chama” vinatakiwa kufanya maamuzi ya haraka na ya kuthubutu; maamuzi ya kuwatimua kutoka ndani ya chama viongozi ambao ni tatizo kwa CCM na ambao wamekuwa ni kichocheo cha migogoro.

Katika kufikia uamuzi huo CCM itahitajika kufanya uamuzi wa kanuni ya kuwatimua viongozi hao. Kwa mfano, je iwakumbatie viongozi wenye kuhusishwa na ufisadi na kuwatimua wanaolalamikia ufisadi ndani ya Chama? CCM ikienda huko maana yake ni kuwa wananchi wa kawaida wataona kuwa hatimaye chama hicho kimeamua kuchukua rasmi upande wa mafisadi.

Lakini kikiamua kuwatimua wale wanaotuhumiwa na ufisadi au wanaoonekana kuwatetea mafisadi CCM kinaweza kujikuta kinapoteza wafadhili wake wakubwa na wakati mwingine hata baadhi ya viongozi wake watarajiwa.

Baadhi ya watu wenye nguvu sana ndani ya CCM ndio wale wale ambao wanatajwa katika ufisadi wa kila aina na ndio wale wale ambao kwa kutumia nguvu zao wamewezesha kuchaguliwa kwa viongozi mbalimbali ndani ya CCM. Hawa si rahisi kuwang’oa pasipo kujisababishia madhara ndani ya chama.

Hii ndiyo sababu kubwa ni kwanini hakuna kiongozi mwenye ujasiri wala uthubutu wa kusimamia kanuni za CCM na nidhamu ya chama. Hakuna mwenye uwezo wa kunyoosha kidole kutaka fulani na fulani wawajibishwe bila ya yeye mwenyewe kunyoshewa kidole. Matokeo yake ni kuwa CCM iko katika udhaifu mkubwa kuliko wakati mwingine wowote ule.

Na kama ambavyo tulivyowahi kuandika mara kadhaa huko nyuma ukweli ni kuwa CCM haiwezi kudumu na kuwa imara ikiwa katika udhaifu kama uliopo sasa. Mgawanyiko mkubwa uliopo ndani yake ni ishara wazi kuwa hata serikali inajikuta ni dhaifu.

Sababu ni ile ile, wapo watendaji ndani ya serikali ambao na wenyewe wamejipanga kufuatana na makundi yaliyomo ndani ya CCM. Wapo ambao wamejipanga na Mwenyekiti wa Taifa na wapo waliojipanga na upande wa watetezi wa mafisadi – kwani nao wananufaika na ufisadi huo na wapo ambao na wenyewe wamejipanga na wale wanaojipambanua kuwa ni wapiganaji – japo na wenyewe waweza kuwa ni mafisadi watarajiwa.

Katika mazingira haya ni wazi hatuna budi kujiuliza upinzani unatumia nafasi hii vipi katika kujijenga na kujiimarisha na kuchukua “mateka” wa CCM? Mtu yeyote aliyefuatilia maandamano ya CHADEMA Kanda ya Ziwa anaweza kuona upungufu mmoja mkubwa sana, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hakikujizolea wanachama wengi wapya au kufungua matawi mengi mapya na kusimika uongozi mpya mahali ambapo hakukuwa na viongozi. Na kuwa baada ya maandamano nini kimefuatia nyuma yake? Je kuna semina za viongozi zimefanyika au kuandaa makada wa chama huko ambapo viongozi wa taifa walipita?

Vinginevyo CHADEMA itapita na kushangiliwa na watu kupita na mabango kulalamika lakini hakuna matokeo zaidi. Na hakuna kitu ambacho kinahakikisha matokeo zaidi kama kupata wanachama wapya – si mashabiki wa zamani. Katika udhaifu wa sasa ambao pia umechangiwa na mahusiano ya karibu kati ya CCM na CUF CHADEMA inajikuta imeachiwa uwanja huru wa kujijenga na kuwa chama chenye nguvu zaidi cha upinzani nchini.

Hata hivyo, nalo hilo litakuwa na matatizo kidogo; itakuwaje kama ndani ya CHADEMA nako wamegawanyika? Je, kama ufalme wa CCM uliogawanyika ndani yake hauwezi kusimama, itakuwaje ufalme wa CHADEMA ukigawanyika wenyewe utaweza vipi kusimama au kuweza kushika madaraka ya kutawala nchi? – isipokuwa kama baadhi ya watu wanadai kuwa CHADEMA haijagawanyika.

Dai hili haliwezi kuonekana kwa kauli mbele ya vyombo vya habari au kwenye vikao tu bali kwa kuonyesha umoja wa nia, mikakati, ushiriki na mipango ya pamoja. Nje ya hapo, CCM hata katika udhaifu wake bado itaonekana ina nguvu.- fikiria ufalme huo ukija kupatana!

RAIA MWEMA

Barua-pepe:


No comments: