Friday, April 29, 2011

BARABARA YA SERENGETI YAITISHIA TANZANIANa Navaya Ole Ndaskoy

MPANGO wa Serikali ya Tanzania kujenga barabara ya lami kuanzia Mto-wa-Mbu kupitia Engaruka, Ziwa Natron, Loliondo, Mugumu hadi Musoma unazidi kugonga vichwa vya habari kutoka pande zote za dunia.

Kwa mujibu wa Serikali lengo la barabara hii ni kuunganisha Mikoa ya Arusha na Mara kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Ni muhimu kueleza, japo kwa muhtasari, historia ya mgogoro huu unaoichafua Tanzania. Miaka ya 1980 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipendekeza kujenga barabara kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuunganisha Arusha na Mara.

Ikapeleka pendekezo hilo Benki ya Dunia kuomba ufadhili wa mradi huo. Benki ya Dunia ikafanya uchunguzi na kutupilia mbali pendekezo lenyewe kwa madai kwamba mradi ungeathiri kwa kiasi kikubwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Mwaka 2005, Serikali ya Rais Jakaya Kikwete iliingia madarakani. Kikwete akamteua Edward Lowassa, kuwa Waziri Mkuu. Serikali ikaanza upya, tena kwa madaha, mkakati wa ujenzi wa barabara hii iliyokosa ufadhili wa Benki ya Dunia.

Julai 2, 2007 Lucy Owenya, Mbunge wa Viti Maalumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alisimama Bungeni na kumuuliza Waziri Mkuu maswali kadhaa kuhusu mpango huu. Owenya aliitaka Serikali ifafanue, kwa kinagaubaga, kuhusu mipango yake ya kujenga (1) mahoteli katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (2) uwanja wa ndege wa kimataifa kilomita 16 tu Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (3) barabara ya lami kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na (4) mpango wa kuchimba magadi katika Ziwa Natron.

Waziri Mkuu, Lowassa, kama mwenye ghadhabu vile, na akishangiliwa sana na wabunge, alisimama na kusisitiza kwamba Serikali lazima itajenga vyote alivyoulizia Owenya. Lowassa alisema ni lazima barabara ya lami itajengwa kuanzia Mto-wa-Mbu kupitia Engaruka, Loliondo, Hifadhi ya Taifa Serengeti hadi Musoma.

Wakati huo, kama ilivyo sasa, mashirika mengi ya uhifadhi ya wanyamapori yalikuwa Tanzania. Hata hivyo yalitulia kama vile maji kwenye mtungi.

Hata hivyo, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ikampata mtetezi wa aina yake. Lowassa alilazimika kujiuzulu mwezi Februari 2008 wadhifa wa Waziri Mkuu baada ya Kamati Teule ya Bunge kufanya uchunguzi wa kina kuhusu ufisadi katika sekta ya umeme.

Mwaka jana mradi huu wenye thamani ya dola za Marekani milioni 480 unaopangwa kuanza 2012 uliibuka tena. Ni muhimu kukumbusha kuwa, baada ya Serikali ya Kikwete kupoteza ule umaarufu wa mwaka 2005, wahafidhina wa mazingira waliokuwa kimya sasa wakaibuka.

Wakati fulani kabla ya mwezi Juni mwaka jana Shirika la Kijerumani la Uhifadhi wa Wanyamapori, Frankfurt Zoological Society, lilichapisha ripoti dhidi ya barabara hiyo kwenye ukurasa wake wa tovuti. Ripoti hii iliandikwa na Profesa Anthony Sinclair wa Chuo Kikuu cha British Columbia, Kanada, Dk. Markus Borner, Mkugenzi wa FZS-Afrika, Gerald Begurube, aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa ambaye baada ya kuondoka TANAPA aliajiriwa na FZS. Ripoti hiyo yenye kichwa cha habari "The Serengeti North Road Project" imekuwa ndiyo msingi wa upinzani dhidi ya barabara hii.

Jambo la ajabu kabisa ni kwamba ripoti yao ilipendekeza kujengwa barabara kupitia kusini mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Walichora ramani pia kwenye ripoti hiyo kuelezea wazi wazi pendekezo hilo la barabara Kusini mwa Serengeti. Kwa mujibu wa ramani hiyo barabara ijengwe kuanzia Karatu kupitia Ziwa Eyasi hadi Lamadi ambapo ingekutana na barabara ya lami inayotoka Mwanza kwenda Musoma.

Ukurasa katika mtandao wa facebook ulianzishwa baada ya Boyd Norton kurudi kutoka Tanzania aliposikia habari za barabara hii, na sasa karibu una mashabiki zaidi ya 38,000. Miongoni mwao ni karibu wahafidhina wote wakubwa wa uhifadhi wa wanyamapori. Wanatumia jukwaa hili kuendesha kampeni za kibabe dhidi ya Tanzania.

Mbali na Boyd Norton na Dave Blanton viongozi wengi wa upinzani huu wameamua kujificha kwa kutotaja majina yao. Ni muhimu kusema kwamba FZS na AWF ndiyo vyanzo vya taarifa zao.

Juni 16, 2010 African Wildlife Foundation, shirika la uhifadhi wa wanyamapori la Marekani linalojidai ni la Afrika, lilitoa tamko kuhusu barabara na kusema, kama lile la Ujerumani, Serikali ijenge barabara kupitia Kusini mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Julai 31, 2010 Rais Jakaya Kikwete, bila shaka akiwa ameshtushwa na vitisho vya wahafidhina hawa wa mazingira, alihutubia Taifa mwisho wa mwezi, alisema Serikali yake itajenga barabara hiyo pamoja na kelele za wana mazingira.

Profesa Brian Wood, Mmarekani aliyepata kufanya utafiti katika ardhi ya kabila dogo kuliko yote Tanzania la Hadza alijitokeza kwenye ukurasa ule wa FB kupambana vikali na wahafidhina wale wa mazingira kupinga kupitisha barabara kwenye ardhi ya Hadza.

Hoja za Wood zikawalemea wahafidhina hawa. Hivyo wakajidai kubadili nia. Wakatoa msimamo kuwa ni kweli barabara waliyopendekeza awali ingewaathiri kwa kiwango cha kutisha waHadza. Sasa wakatangaza kuwa wanapendekeza barabara kutoka Arusha kwenda Babati, Singida, Shinyanga, Mwanza na hatimaye Musoma. Hii ni sawa na kumlazimisha mtu anayetaka kusafiri kwenda Arusha akitokea Dar es Salaam kusafiri kupitia Morogoro, Iringa, Dodoma, Babati na hatimaye Arusha. Mzungoko wa kutisha.

Takriban mwaka mzima sasa mashirika ya uhifafadhi wa wanyamapori ya ndani na nje ya Tanzania yamekuwa yakipinga kwa kila mbinu mpango huu.

Mashirika haya yamekuwa yakitumia vibaya vyombo vya habari kuendesha kampeni za uzengeaji, yaani lobbying, kupinga ujenzi wa barabara hii. Vyombo vingi vikubwa sana vya habari vya nje pia vimenasa katika mtego huu wa wahafidhina wa mazingira. Hapa ninamaanisha BBC, CNN, MSNBC, CBS, New York Times, Washington Post, Forbes, US Today, Guardian na Observer [ya London], Herald de Paris, National Geographic Magazine na hata Scienceline kutaja machache yenye majina makubwa.

Hata hivyo, ni jarida lenye hadhi sana, linalochapiswa nchini Uingereza, lijulikanalo kwa jina ka Nature Journal lililovunja rekodi. Septemba 16, 2010 lilichapisha habari iliyoandikwa na “wanasayansi” 27 dhidi ya barabara hii. Wote 27 walikurupuka tu kunyofoa na kunyofeka yale yale yaliyosemwa na akina Borner wa FZS tena bila kukiri.

Jarida la Nature lilisema “wanasayansi” hao 27 ni Andrew P. Dobson, Markus Borner, Anthony R. E. Sinclair, Peter J. Hudson, T. Michael Anderson, Gerald Bigurube, Tim B. B. Davenport, James Deutsch, Sarah M. Durant, Richard D. Estes, Anna B. Estes, John Fryxell, Charles Foley, Michelle E. Gadd, Dan Haydon, Ricardo Holdo, Robert D. Holt, Katherine Homewood, J. Grant C. Hopcraft na Ray Hilborn kwa mpangilio huo.

Wengine ni George L. K. Jambiya, M. Karen Laurenson, Lota Melamari, Alais ole Morindat, Joseph O. Ogutu, George Schaller na Eric Wolanski; kwa mpangilio huo.

Wako wapi waTanzania? Kama majina ni kielelezo, ukiwaondoa Bigurube, Jambiya, Melamari, Morindat na Ogutu genge zima hili ni Wamerekani na binamu zao toka Ulaya. Ajabu ni kwamba siku chache baadaye wanasayansi 290 walijiunga nao.

Wahafidhina hawa 27 wa mazingira walidiriki kutumia takwimu za utalii kuhalalisha madai yao. Walidai kuwa mwaka 2005 sekta ya utalii iliingizia Tanzania dola za Marekani milioni 824. Hata hivyo, imepata kurekodiwa kwamba kampuni za kigeni za kitalii zipatazo 34, kati ya kampuni 281 za kitalii zenye leseni, ndizo zinanufaika kwa kuleta karibu asilimia 80 ya watalii wanaokuja Tanzania. Wahafidhina hawa walikwepa kukiri wizi huu unaofanywa na makampuni mchana kweupe. Wangediriki kukiri hili bila shaka hoja yao dhidi ya barabara ingekosa mashiko.

Lakini pia “wanasayansi” 27 hawa hawakujali kabisa vilio na haki za wananchi wanaoishi Mashariki na Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Wakinyofoa na kunyofeka yale yaliyosemwa na FSZ walisema barabara ikijengwa Kusini mwa Serengeti itahudumia watu milioni 2.3 tofauti na watu 431,000 kama barabara ikipita hifadhini. Hoja hizi hazina mashiko kwani wananchi wanaoishi jirani na hifadhi hii waliondolewa kimabavu ili kupisha uanzishwaji wa hifadhi yenyewe miaka ya 1950.

Lakini kila jambo jema lina mwisho wake. Lowassa amejikuta akichukua jukumu la kuwa msemaji wa barabara hii yenye utata.

Kikwete amejiapiza mara kadhaa tena hadharani kuwa ni lazima Serikali yake itajenga barabara kukatiza Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kilomita 54 hivi.

Alipobanwa na wakubwa wa dunia hii jijini Davos Uswisis Kikwete alilazimika kujitetea. Januari 28, 2011 Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kutetea msimamo wa Kikwete. Katika taarifa ile Ikulu ilitoa madai matatu kuwa ndiyo sababu Serikali inataka kujenga barabara kupitia Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Madai hayo ni, kwanza, kupunguza idadi ya magari yanayopita hifadhini, pili, kufunga barabara inayokatiza kwenye hifadhi kwa kilomita 220 na kuifupisha kuwa kilomita 54 tu na, tatu, kujenga barabara kwa ajili ya jamii zilizopo pembezoni mwa hifadhi.

Wananchi wanaoishi jirani na hifadhi ni kipaumbele cha mwisho cha Kikwete. Hata vipaumbele vyake viwili vya awali vinatia shaka sana. Nini kinamsukuma Kikwete?

Mwaka 2002 Paul Tudor Jones II alinunua Pori Tengefu la Grumeti Magharibi mwa Serengeti. Akajenga hoteli tatu za kifahari Farufaru, Sasakwa na Sabora. Chumba kimoja kwenye hoteli hizi ni dola za Marekani 10,000; karibu Shilingi 15 milioni kwa usiku mmoja tu. Wateja wake ni matajiri haswa; kama vile Roman Abramovich yule tajiri mmiliki wa timu ya Chelsea, Uingereza. Paul na wateja wake hawataki mafukara karibu.

Paul amehamisha shule ya msingi ili kupisha ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa kilomita 16 hivi Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti. Endapo uwanja huu utajengwa mabilionea wenzake watatua moja kwa moja jirani na hifadhi yake ya Grumeti. Itakumbukwa kuwa mwaka 2009 Abramovich aliacha dege lake Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro maana lisingeweza kutua viwanja vilivyoko Serengeti.

Paul alishajaribu, bila mafanikio, kuhamisha Kijiji cha Robanda kilichoko jirani na hoteli yake pale Sasakwa. Mtu huyu huyu hataki kuiona ile barabara ya kilomita 220 ambayo Kikwete naye anasema lazima ataifunga.

Je, Paul Tudor Jones II ni nani hadi afanyiwe kazi ya kufunga barabara? Huyu ni tajiri wa kutupwa. Kwa mujibu wa jarida la Forbes Paul Tudor Jones II ni mmiliki wa dola za Marekani bilioni 6.3 mwaka 2009. Fedha hizi ni nyingi mno. Ni zaidi ya bajeti nzima ya Serikali ya Tanzania kwa mwaka. Zinatisha.

Kule kwao Marekani Paul Tudor Jones II hafurukuti hata kidogo. Miaka ya 1990 aliponea chupuchupu kutupwa jela baada ya kuharibu mazingira ya ardhi oevu Chesapeake. Alilazimika kulipa faini ya zaidi ya dola za Marekani milioni mbili.

Ili kukwepa sheria kali za Marekeni pamoja na vyombo vya habari Paul amekimbilia Zimbabwe na Tanzania. Katika nchi hizi bilionea huyu hufanya kila atakalo bila kuguswa na mtu sembuse kitisho cha kutupwa jela. Mashirika ya kihafidhina ya uhifadhi wa wanyamapori yanajifanya kutofahamu kuwa Paul Tudor Jones II ndicho chanzo cha barabara hii. Hawathubuti kumsema. Huchangia fedha nyingi kwenye miradi yao.

Novemba 1, 2010 baada ya mapambano makali kwenye FB wahafidhina wanasalimu amri na sasa kupendekeza barabara ya Arusha-Babati-Singida-Shinyanga-Mwanza-Musoma. Awali walipendekeza barabara ijengwe kuanzia Karatu-Eyasi-Lamadi-Musoma kupitia ardhi ya Hadza. Wabunge kadhaa wa Bunge lililopita kutoka ukanda huo walishabikia sana mpango huu maana ni muhimu kwao kwa kura.

Mbali na kumpigia chapuo tajiri, Paul Tudor Jones II, endapo barabara ile ingejengwa kuanzia Mto-wa-Mbu kupitia Engaruka hadi Loliondo na baadaye Musoma kwa kiasi kikubwa barabara hii ingepitia jimbo la Monduli.

Mustapha Akunaai, Mbunge wa Mbulu (CHADEMA), ni Katibu wa TATO, umoja wa makampuni ya biashara ya utalii Tanzania. Hivi karibuni TATO ilitangaza kupendekeza barabara ijengwa kuanzia Karatu-Mbulu-Haydom-Shinyanga-Singida hadi Musoma.

TATO haikusema barabara hii itawasaidia vipi wananchi waishio Mashariki na Magharibi mwa Serengeti ambao Serikali inadai kuwa ndio walengwa wa barabara inayojadiliwa. Wananchi wa Wilaya za Mbulu na Karatu wameifanyia Serengeti jambo gani jema hata wazawadiwe barabara iliyokusudiwa kujengwa kwa ajili ya wananchi wa Wilaya za Ngorongoro na Serengeti waliokuwa wamefukuzwa kimabavu ili kupisha hifadhi? Akunaai anafahamu kuwa barabara hii itapita katika jimbo lake la Mbulu.

Sasa tuendelee kutaza matukio muhimu yanayozunguka mjadala wa barabara hii. Mapema Novemba mwaka jana Serengeti Watch, Shirika Lisilo la Kiserikali, lilitanganzwa kuwa limeanzishwa na akina Dave Blanton na Boyd Norton pamoja na wahafidhina wengine saba. SW lilisajiliwa chini ya Sheria 501(c)3, maana yake inaweza kuchangisha fedha bila kodi, ya Marekani. Hii nayo ni taasisi nyingine ya Marekani.

Desemba 10, 2010 ANAW, taasisi ya kutetea haki za wanyama Kenya, ilifungua kesi dhidi ya Serikali ya Tanzania katika Mahakama Haki ya Afrika ya Mashariki.

Kwa mujibu wa Saitabao ole Kanchory, Wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya, anayeiwakilisha ANAW, mteja wake anaiomba Mahakama kuipiga marufuku Serikali ya Tanzania kujenga barabara hii sasa na hata milele; isitokee tena Serikali ikataka kujenga barabara.

Januari 27, 2011 Rais Jakaya Kikwete akutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia, Ms. Ngozi Ikonjo-Iweala, Davos, Uswiss, na kumhakikishia kuwa Serikali ya Tanzania haitajenga barabara kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kiwango cha lami. Na kwamba zile kilomita 54 ndani ya hifadhi hazitatiwa lami.

Februari 8, 2011 Mabaraza ya Madiwani kutoka Wilaya nane za Mikoa ya Arusha na Mara yalitoa tamko la pamoja kuunga mkono mpango wa Serikali kujenga barabara kuanzia Mto-wa-Mbu kupitia Loliondo na Mugumu hadi Musoma. Wilaya hizo ni Monduli, Ngorongoro, Serengeti, Tarime, Bunda, Musoma, Rorya na Musoma Vijijini.

Februari 9, 2011 Mwakilishi wa Benki ya Dunia Tanzania, John McIntire, pamoja na wasaidizi wake walikutana na Rais Kikwete Ikulu Dar es Salaam na kuahidi kuipa Serikali fedha kwa ajili ya kujenga barabara kupitia Kusini mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti. Rais aliwashukuru na kurudia kusema kuwa wananchi waishio Mashariki na Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti wanahitaji maendeleo ikiwemo barabara.

Februari 18, 2011 Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani, Dirk Niebel, ajiunga na wanaopinga barabara kupitia Hifadhi ya Taifa Serengeti. Niebel alisema Ujerumani, kama Benki ya Dunia, itatoa fedha kufadhili ujenzi wa barabara kusini mwa Serengeti. Niebel amiminia sifa Frankfurt Zoological Society eti kwa kazi nzuri inayofanya.

Tukio kubwa la hivi karibuni kabisa ni yale maandamano yaliyofanyika jijini Nairobi, Kenya, Machi 19, 2011 kupinga barabara hii. Hii ilikuwa tarehe maalumu iliyopangwa kwa miezi kadhaa kabla na wahafidhina wa uhifadhi wa wanyamapori.

Ubabe, ubinafsi, ufisadi na kiburi cha utajiri na mamlaka hukwamisha mawazo mbadala. Mbunge wa Ngorongoro, 1980 hadi 1990, Moringe Parkipuny, alipendekeza barabara ijengwe kwa ajili ya kuunganisha miji ya Arusha na Musoma kupita nchini Kenya.

Barabara mbadala anayopendekeza Parkipuny inaanzia Lengijape kutoka barabara ya sasa ya Arusha-Nairobi na kupitia Ketumbeine, Meirugoi, Gelai na Mlima Lengai hadi Ziwa Natron. Ingepitia Elojata kutoka kwenye Bonde la Ufa na kuelekea Masusu, Digodigo, Loliondo na kuvuka mpaka pale Lemisigio kuingia Kenya na kuzunguka Pori la Taifa la Maasai Mara na kurudi Tanzania kupitia Sirari. Kutoka hapo inaendelea hadi Musoma. Barabara hii ni fupi kuliko ile ya Kusini ya wahafidhina wa uhifadhi.

Lakini pia inaleta huduma muhimu kwa mamia ya maelfu ya wananchi waishio katika wilaya jirani kama vile Monduli, Ngorongoro, Serengeti, Tarime, Bunda, Musoma, Rorya na Musoma bila kuathiri Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Pori la Taifa la Maasai Mara. Wenyeji wa wilaya hizi walifukuzwa kimabavu ili kupisha Serengeti miaka ya 1950.

Barabara hii ingeilazimisha Kenya kubeba mzigo wake wa uhifadhi wa wanyamapori. Serengeti imeungana na Maasai Mara. Jukumu la kuhifadhi linapaswa kubebwa na nchi zote mbili. Kiutendaji ni rahisi hasa zama hizi za Muungano wa Afrika ya Mashariki.

RAIA MWEMA0754 453 192

No comments: