Tuesday, March 22, 2011

ZIARA HIZI ZA JK WIZARANI ZIFANYIWE TATHMINI

Tunalazimika leo kuuliza sababu za Rais Jakaya Kikwete kufanya mzunguko wa pili wa ziara zake katika wizara mbalimbali hapa jijini Dar es Salaam. Tumeambiwa kuwa ziara za Rais katika raundi hii ya pili katika wizara hizo ni kueleza viongozi na watumishi kuhusu dira ya serikali yake kuelekea mwaka 2015.

Itakumbukwa kuwa mara baada ya kuingia madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Rais Kikwete alifanya ziara katika wizara zote na kukutana na watumishi wa wizara hizo. Hakika ziara hizo ziliwapa wafanyakazi wa Serikali na wananchi wote kwa ujumla hamasa na matumaini makubwa, kwani Rais Kikwete si tu alionyesha nia ya kuyaelewa mazingira ambayo wafanyakazi hao walikuwa wanafanyia kazi, bali pia aliwapa changamoto na kuweka malengo ambayo yalipaswa kufikiwa na watumishi hao na kuahidi kufuatilia utekelezaji wa maagizo yake muda si mrefu.

Ziara hizo za Rais Kikwete katika wizara zote ziliibua msisimko, faraja na bashasha kubwa, kwani ujio wake katika wizara hizo ulionekana kwa wananchi kama fursa maalumu kwao kukutana na kiongozi ambaye alionekana kugusa hisia zao na kuwapa matumaini ya maisha bora, kwani kaulimbiu ya kampeni zake ilikuwa “Maisha Bora kwa Kila Mtanzania”.

Ziara hizo zilifuatiwa na Semina Elekezi za mawaziri na makatibu wakuu ambazo zilijulikana kama “Semina za Ngurudoto” ambazo, ingawa ziliendeshwa kwa gharama kubwa za fedha za walipa kodi, zilikuwa na tija kwa sababu ziliwapa viongozi hao mwelekeo na dira ya Serikali ya Awamu ya Nne kuelekea mwaka 2010. Viongozi walengwa walizisifia semina hizo kwamba ziliwapa uelewa wa mfumo wa utawala na hali ya kufanya kazi kwa kujiamini. Hakika, Taifa lilionekana kuzaliwa upya.

Lakini mwaka mmoja baada ya ziara za Rais Kikwete katika wizara zote na “Semina Elekezi za Ngurudoto”, moto uliokuwa umewashwa na hamasa na matumaini yaliyokuwa yamesimikwa na Rais huyo katika mitima ya watumishi wa Serikali na wananchi kwa ujumla, yalianza kufifia taratibu siku hadi siku na hatimaye yakazimika kabisa mwaka 2007 baada ya kashfa ya Richmond. Hii ilitokana na ukweli kuwa Rais hakufuatilia utekelezaji wa maagizo na maelekezo yake kwa viongozi wa wizara hizo na taasisi zake kama alivyokuwa ameahidi awali.

Ni katika muktadha huo ziara za hivi sasa za kiongozi huyo katika wizara na taasisi zilizo chini ya wizara hizo zinapaswa kutazamwa. Kwamba ziara hizo sasa hazionyeshi kuwa na jipya, hamasa wala msisimko ni jambo lisilohitaji kufanyiwa utafiti wala uchunguzi, zaidi ya maelezo kuwa kwa kuwa ziara za awali za kiongozi huyo hazikuonekana kuleta tija, ziara za hivi sasa hazitarajiwi kuleta tija pia.

Ni kwa misingi hiyo tunamshauri Rais Kikwete kuwa pengine ingekuwa vyema iwapo angetafuta utaratibu mwingine wa kukutana na watendaji wa wizara na taasisi zake na kuwapa dira ya serikali yake kuelekea mwaka 2015. Tunadhani kuwa badala ya kuzifanya ziara hizo zionekane kama sarakasi au matamasha kiasi cha kusababisha msongamano wa magari kutokana na kufunga barabara kupisha misafara yake, ingetosha tu iwapo angewaita viongozi wa kila wizara Ikulu na kuwapa maelekezo husika.

Ziara katika kila wizara zimeonekana kupunguza tija na kusababisha gharama kubwa, kwani wizara zinasemekana kutumia zaidi ya wiki moja kufanya maandalizi ya kumpokea kiongozi huyo katika sehemu zao kwa risala na hotuba ndefu. Bila shaka pia ziara hizo zinasababisha kiongozi huyo aweke pembeni shughuli nyingi muhimu za Serikali.

Tunadhani pia kwamba kwa kufanya ziara hizo za kueleza mawaziri na wasaidizi wao kuhusu nini la kufanya, Rais anafanya kazi na majukumu ya Waziri Mkuu na Katibu Mkuu Kiongozi. Tunapendekeza kuwa Rais ajikite katika masuala nyeti na muhimu yanayolisibu Taifa na awaachie wasaidizi wake kazi ambazo wameajiriwa kufanya.


MWANANCHI

No comments: