Sunday, March 27, 2011

VIONGOZI WETU WANAFURAHIA MATANUZINa Evarist Chahali

NIANZE kwa kuungana na Watanzania wenzangu kuwapa pole ndugu zetu wa Japan waliokumbwa na janga la tetemeko kubwa la ardhi ambalo limesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha.

Athari za janga hilo zitaikumba Tanzania kwa vile Japan ni miongoni mwa wafadhili wakuu wa nchi yetu. Ni wazi kwamba kipaumbele kwa nchi hiyo baada ya janga hili kitakuwa katika masuala ya ndani, kama vile kutengeneza miundombinu iliyaharibiwa vibaya, badala ya kutusaidia sie tunaotegemea kudra za wafadhili.

Pengine tukio hili linaweza kutupa fursa ya kuangalia kwa undani michango ya wafadhili wetu katika sura tofauti kidogo. Mara nyingi huwa najiuliza inawezekanaje kwa wafadhili wetu kumwaga misaada yenye thamani ya mabilioni ya shilingi kila mwaka lakini hawajali sana kufuatilia namna misaada hiyo inavyotumika.

Nilipofika hapa Uingereza kwa mara ya kwanza nilishangazwa na namna hawa wenzetu-tunaowategemea sana kwa misaada ya hali na mali-wanavyoendesha mambo yao.

Mifano ni mingi, lakini mmoja ulionigusa zaidi ni namna wanavyojitahidi kubana matumizi. Kwa mfano, msafara wa waziri mkuu wa hapa unakuwa na magari machache tu, huku gari za thamani zaidi zikiwa Range Rover ambazo zinatengenezwa hapahapa Uingereza.

Magari yanayotumiwa na mawaziri na wabunge ni ya kawaida sana. Ni aina ya usafiri unaolenga kumwezesha kiongozi kutoka sehemu moja kwenda nyingine na wala si ishara ya kumtofautisha na watu wa kawaida.

Na ni jambo la kawaida kwa waziri mkuu wa nchi hii kusafiri kutoka mji mmoja kwenda mwingine kwa kutumia treni. Kutumia usafiri wa kawaida hakumfanyi kiongozi kupungukiwa chochote bali kunamwezesha kutekeleza majukumu yake kama wananchi wengine.

Ni muhimu pia kufahamu kuwa wanasiasa wengi hapa Uingereza wanaojimudu kiuchumi. Baadhi yao, kama Waziri Mkuu wa sasa, David Cameron, ni watu waliokulia katika familia za kitajiri. Kwa lugha nyingine,ni watu “waliozoea raha”. Na kwa vile uchumi wa nchi unaruhusu, isingekuwa vigumu kwao kutamani na kumudu vitu vyenye thamani kubwa wakati wa uongozi wao.

Labda utasema ni vigumu kwa waziri wa Tanzania kupanda treni ya Reli ya Kati kwa vile ni usafiri usiofaa kwa jinsi treni katika reli hiyo zilivyo. Lakini laiti kama usafiri huo ungekuwa na umuhimu kwa viongozi wetu-kwa maana kama wangekuwa wanautegemea kwa safari zao-ni dhahiri wasingeipuuza sekta ya usafiri wa reli.

Nirudi tena kwenye mifano ya hapa nilipo. Usafiri wa kawaida wa Waziri Mkuu wa Uingereza anapokwenda nje ya nchi ni kwa kutumia ndege za Shirika la Ndege la hapa, British Airways (BA). Hadhi ya Waziri Mkuu haishuki kwa kutumia usafiri huo “wa umma” bali wanachojali Waingereza ni umuhimu wa safari husika ya kiongozi wao.

Akina sie tunaoendesha nchi kwa kutembeza bakuli la kugombea misaada tunataka rais wetu awe na ndege yake. Na walipakodi wanapohoji gharama za ununuzi na uendeshaji wa ndege hiyo, waziri mwenye dhamana anawakaripia kwa kuhoji “wanataka rais asafiri kwa punda”?!

Si siri kuwa laiti safari za mara kwa mara za Rais Jakaya Kikwete nje ya nchi zingekuwa zinategemea “Air Tanzania”, shirika hilo lililogeuzwa uwanja wa mazoezi ya kufisadi, lingeshawezeshwa kuhudumia umma na safari za mkuu wa nchi.

Wakati wafadhili wetu wanazitumia vizuri balozi zao kuwawakilisha nchi za nje, na hivyo kupunguza safari zisizo za lazima za viongozi, akina sisi tunashuhudia viongozi wetu wakitumia muda mwingi safarini nje ya nchi kana kwamba walioteuliwa kutuwakilisha huko wana mapungufu ya kiutendaji. Kibaya zaidi, safari hizo zinazoligharimu Taifa kiasi kikubwa cha fedha zetu “za ngama” zinajumuisha mlolongo wa watu.

Watetezi wa safari za mara kwa mara za Rais Kikwete wanadai kuwa safari hizo ni muhimu sana kwa Taifa, hususan katika kuwabembeleza wafadhili watupatie misaada. Kichekesho ni kwamba ukichanganya idadi ya waliomo kwenye msafara husika na posho wanazolipwa, hata tukifanikiwa kupata msaada uliofuatwa huko nje inakuwa sawa na “kuuza ng’ombe ili kumudu gharama ya kesi ya kuku”.

Japo mfumo wetu wa utawala umerithiwa kutoka nchi za Magharibi, watawala wetu wameamua kwa makusudi kuukongoroa na kuiga lifestyles za wafanyabishara matajiri duniani. Wanachopuuza ni ukweli kwamba wakati wengi wa wafanyabiashara hao wanaendesha maisha ya kifahari kutokana na jasho lao binafsi, gharama za maisha ya “kitajiri” ya watawala wetu inabebwa na walipakodi, wengi wao wakiwa masikini wa kutupwa.

Kwa vile “ligi ya kuangamiza fedha ya mlipakodi” inaanzia ngazi za juu serikalini, hali hiyo imesambaa mpaka ngazi za chini za mfumo wa utawala wa umma. Bajeti za halmashauri za wilaya, miji na majiji zinamezwa kwa kiwango kikubwa na gharama binafsi za wanaoongoza halmashauri hizo.

Sijui vigogo hawa wanajisikiaje wanapoelezwa kuwa usafiri mkuu wa Meya wa Jiji la London, Boris Johnson, kwenda na kutoka ofisini kwake ni baiskeli. Mwanasiasa huyo tajiri amekuwa akihamasisha kwa vitendo matumizi ya baiskeli badala ya magari ili, pamoja na mambo mengine, kupunguza msongamano katika jiji hilo na kutunza mazingira (kwa kupunguza carbon emissions).

Sasa kwa jinsi tulivyozoea kuwaona viongozi wetu wapenda maisha ya ufahari wakiwa kwenye “mashangingi” yao, si ajabu siku diwani tu (achilia mbali mkuu wa wilaya) akionekana anaenda ofisini kwa baiskeli kuna watakaohisi amerukwa na akili!

Majuzi, baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari jijini Dar es Salaam waliandaa maandamano kwenda Ikulu kuwasilisha kilio chao kwa Rais Kikwete kuhusu ongezeko la nauli. Kwa vile watawala wetu ni kama wana “allergy” na maandamano, waliamuru askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kusambaratisha maandamano hayo.Who knows,huenda intelijensia ya Jeshi la Polisi ilionyesha kuwa maandamano ya wanafunzi hao yana uhusiano na “uhaini wa CHADEMA” kutumia haki yao ya kikatiba kuandamana.

Lakini hata kama maandamano hayo yangeruhusiwa na wanafunzi wakafika Ikulu, huenda wangejikuta kama wanaongea Kindamba kwa Mchina. Wamiliki wengi wa daladala ni vigogo haohao wanaoliliwa na wanafunzi kuhusu ongezeko la nauli, wengi wa watoto wa viongozi wetu ni wanafunzi wa international schools au shule za ng’ambo na hawajahi kupanda daladala maishani mwao.

Tunaongozwa na watu wasioelewa kabisa kinachoendelea katika dunia halisi (ya watu wa kawaida). Hawaguswi na vilio vya wananchi kuhusu uhaba wa maji, mgao wa umeme, ugumu wa maisha, nk, kwa vile hawajawahi kukumbwa na kero hizo. Laiti mgao wa umeme ungesababisha vigogo kukaa vitambi wazi maofisini kwa vile mgao wa umeme umesababisha viyoyozi kutofanya kazi wangeendelea kupiga danadana kuhusu tatizo la umeme?

Kigogo ambaye akiumwa kichwa tu anakimbilia ughaibuni kupata matibabu hawezi kuona mzaha kwenye “mpango kabambe” wa huduma ya kusafirishia wagonjwa kwa pikipiki.

Lakini kwa namna fulani wafadhili wetu nao wanapaswa kubebeshwa lawama kwa kumwaga misaada yao pasipo kufuatilia kwa karibu namna misaada hiyo inavyotumika.

Ni wazi kuwa iwapo wafadhili wangefuatilia kila shilingi wanayotupatia kama msaada, na hivyo misaada hiyo yote kuelekezwa inakostahili, watawala wetu wasingemudu kuendesha maisha ya kifahari kana kwamba ni wafanyabiashara wakubwa.

Lakini hata kama wafadhili wataendelea “kuzembea” katika ufuatiliaji wa jinsi misaada wanayotoa inavyotumika, kuyumba kwa uchumi wa dunia kunaweza kuwalazimisha kuwa makini zaidi.

Na wafadhili wetu wanaweza kuwa na msaada zaidi kwa nchi yetu kwa kuzibana taasisi zao za fedha zinazohifadhi “vijisenti” vya watawala wetu ambao chanzo pekee cha utajiri wao ni “biashara” ya kuongoza wananchi masikini.

Sitaki kuamini kuwa upole wa wafadhili katika ufuatiliaji wa matumizi mabovu ya misaada yao unatokana na madai kuwa at the end of the day fedha wanazotupatia zinarejea kwao kupitia “vijisenti” vya vigogo vinavyotunzwa kwenye taasisi za fedha katika nchi za wafadhili hao.

Barua-pepe:RAIA MWEMA

No comments: