Tuesday, March 29, 2011

UVCCM -ARUSHA NAO WATOA TAMKO LAO

MAAZIMIO YA BARAZA LA UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM)


MKOA WA ARUSHA – LONGIDO

UTANGULIZI
Kikao cha baraza la vijana la mkoa wa Arusha kilichokaa leo tarehe 28 Machi 2011, wilayani Longido kama ambavyo taratibu na kanuni za UVCCM zinavyoelekeza. Hili likiwa ni baraza la kwanza kufanyika baada ya uchaguzi mkuu wa 2010, tunapenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Jakaya Mrisho Kikwete kwa ushindi alioupata na pia kuwapongeza wabunge na madiwani wote wa Chama Cha Mapinduzi na kuwahakikishia kwamba kama vijana tupo tayari kukabiliana na changamoto zote tulizokutana nazo kwenye uchaguzi na tutafanya kazi bega kwa bega kuhakikisha tunafanikisha vizuri zaidi chaguzi zijazo.

Hili lililikuwa ni baraza la kawaida la kazi na agenda kadhaa zilijadiliwa. Kufuata majadialiano yaliyoendelea kwenye kikao, Baraza la Mkoa wa Arusha limeazimia yafuatayo:

MAAZIMIO

  1. Baraza limesikitishwa sana na kauli zilizotolewa na baadhi ya vijana wa UVCCM wakianza kuhubiri siasa ya kibaguzi wa makabila kwa kutoa matamko kwambaRais 2015 asitoke kanda ya kaskazini,Baraza linachukua fursa hii kuwaonya vijana wenzetu hao wanaopotoka, na labda kama ambavyo wamekumbushwa juzi, tuwaambie tena kwamba Rais wa awamu ya kwanza Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitokea mkoa wa Mara (KANDA YA ZIWA), Rais wa awamu ya pili Mhe. Ally Hassan Mwinyi alitokea Zanzibar (VISIWANI), Rais awamu ya tatu Mhe. Benjamin William Mkapa alitokea Mtwara (KANDA YA KUSINI) NA Rais wetu wa sasa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete anatokea mkoa wa Pwani (KANDA YA PWANI), sasa kama hawa vijana wenzetu wangetaka watanzania wafanye uchaguzi kwa kuangalia maeneo ambayo viongozi hao wanatoka, basi tungetegemea waseme sasa kwamba 2015 ni zamu ya Rais kutokea KANDA YA KASKAZINI AU, NYANDA ZA JUU KUSINI, na tunaamini kote huku kuna viongozi mahiri na makini wenye uwezo wa kuongoza nchi vizuri kabisa, lakini sisi kama vijana weledi wa CCM na tuliolelewa vizuri kwenye misingi thabiti ya nchi yetu ya UMOJA na AMANI, hatuamini hata siku moja kwenye kuchagua viongozi kwa kuangalia Rangi, Dini au kabila, Baba wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alishaonya kwa ukali sana kuhusu ubaguzi wa aina yoyote, sisi tunaamini kila Raia wa Tanzania kutokea upande wowote ule wa nchi anayo haki ya kikatiba ya kuwania nafasi ya URAIS na wananchi wa Tanzania watampima kwa rekodi yake ya uongozi na uwezo wake wa kutatua matatizo ya wananchi, hii ndiyo Tanzania tunayoifahamu sisi kama vijana wa Chama Cha Mapinduzi.
  2. Mkoa wetu wa Arusha ni mkoa uliobarikiwa kwa kuwa na rasilimali nyingi sana na tunamshukuru Mwenyezi Mungu, na mojawapo ya rasilimali hizo ni pamoja na madini ya tanzanite na vivutio vingi vya utalii, na hivi vyote vinahitaji Tanzania kama nchi iweze kutangazwa vizuri KIMATAIFA ili mkoa wetu na taifa tuweze kupata manufaa zaidi kwa rasilimali tulizonazo na moja ya nyenzo muhimu katika kutangaza nchi ni pamoja kuwa na “National Carrier” yako, ambayo inakuwa ni shirika la ndege ambazo serikali ina hisa na shirika hilo linabeba jina la nchi na linapeperusha bendera ya taifa popote pale linapokwenda duniani. Kwa masikitiko makubwa sana na kwa kipindi kirefu, nchi yetu Tanzania tumekuwa na Shirika letu la ATC, ambalo kipindi fulani lilikuwa linarusha ndege mpaka Heathrow, London – Uingereza, lakini shirika hilo leo limekuwa kama mtoto yatima. Sisi vijana tunajiuliza, kama mjasiriamali mzawa amefanikiwa kuendesha shirika lake la PRECISIONAIR kwa mafanikio makubwa, serikali inashindwaje kuendesha ATC? Kama vijana wa mkoa wa Arusha tunaungana na kamati za Bunge na tunaitaka serikali kusimamia hili jambo kwa makini, nasiyo kwa kuinyima ATCL ruzuku tu, bali kuanza kwa kuvunja Bodi ya wakurugenzi na menejimenti yote, hivi sasa ni AIBU KUBWA kwa nchi, tunaomba watuondolee aibu hii haraka iwezekanavyo. Haiingii akilini kama nchi ndogo na tena ambazo zimetoka vitani hivi majuzi kama Rwanda, Burundi na Comoro, wao waweze kuendesha mashirika yao ya ndege zilizobeba majina ya Mataifa yao na sisi kama nchi yenye rasilimali nyingi kiasi hicho tushindwe kuendesha shirika letu la ATCL.
  3. Agenda mojawapo ya kikao chetu ilikuwa ni tathmini ya uchaguzi, na kama baraza tunapenda kuchukua fursa hii kuwapongeza viongozi wote wa wilaya za mkoa wa Arusha kwa kufanikisha uchaguzi mkuu vizuri sana na kufanikiwa kushinda majimbo ya uchaguzi matano kati ya saba, tunawapongeza sana. Na pia kusimamia kura za Mwenyekiti wetu wa Chama, Jakaya Mrisho Kikwete kushinda vizuri mkoani kwetu Arusha, tukiongozwa na wenyeji wetu wa kikao chetu wa jimbo la Longido ambaye Rais alipata 85% na tukifuatiwa jimbo la Monduli ambapo Rais alipata asilimia 84%, lakini pamoja na kuwapongeza viongozi waliosaidia kufanikisha uchaguzi mkuu, lazima pia kulaani viongozi wa chama waliotumika kukihujumu chama wakati wa uchaguzi na kutusababishia kushindwa vibaya kwenye majimbo mengine na kumpunguzia sana kura Mhe. Rais wetu, na sisi kama vijana tunasema hatutavumilia viongozi wa namna hiyo, na kwa kuonyesha mfano, na kwa kutekeleza maazimio ya baraza kuu la UVCCM lililokaa wiki iliyopita, baraza limeamua kumsimamisha Ndg. Gambo Mrisho kwa kushiriki kukihujumu chama katika jimbo la Arusha mjini na kuendelea kutoa maneno ya kashfa kuhusu Chama na aliyekuwa mgombea wa Chama chetu Jimbo la Arusha Mjini Dr. Batilda Buriani kwenye maeneneo mbalimbali na hata kwenye ofisi ya UVCCM mkoa mbele ya viongozi wengine wengi, hii ni dhambi ambayo haisameheki na kwasababu hiyo, Baraza limeazimia kuwa kijana huyu siyo mwenzetu na tunamuomba Mwenyekiti wa CCM Taifa kulivalia njuga suala hili kwa maeneo mengine ya nchi ili viongozi wote waliokihujumu chama watupishe mapema, twende tukijiandaa na uchaguzi wa 2015 na wanachama ambao tunaamini wapo tayari kufa kwa kutetea imani za Chama Cha Mapinduzi. Tunaamini kama isingekuwa kwasababu ya viongozi wasaliti kama hawa, Mhe Rais Jakaya Mrisho Kikwete angepata ushindi mkubwa zaidi kuliko ushindi alioupata wa asilimia 61% kwenye uchaguzi mkuu 2010.
  4. LOLIONDO – ‘KWA BABU’, hii imekuwa moja ya vivutio vikubwa sana hapa mkoani kwetu Arusha kwa wananchi kutoka mikoa mbalimbali na hata nje ya nchi kwenda kupata ‘kikombe’ kwa babu Loliondo. Tunaelewa na kuheshimu kwamba hili ni suala la imani ya mtu binafsi kwenda Loliondo kwa babu, lakini sasa inapotokea kwamba inaweza kugeuka kuwa janga la kitaifa, sisi kama viongozi hatupaswi kuendelea kukaa kimya tena. Kuna taarifa zinazosema kuwa watu 10-15 wanafariki kila siku wakiwa wanaelekea kwa babu, na tumeona taarifa za mikutano ya wakuu wa mikoa tofauti wakikaa kutafuta suluhisho, na sisi kama vijana wa mkoa wa Arusha tunaitaka Wizara ya Afya kupitia halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro kutoa suluhisho haraka iwezekanavyo kwa kusimamia kuboresha miundombinu na siyo kuwaachia KANISA na watumishi wa Babu au kama sivyo kusitisha huduma mpaka miundombinu itakapokuwa tayari na wagonjwa wote warudishwe mahospitalini. Hii ni hali ya hatari ambayo inapaswa sasa kufanyiwa maamuzi magumu.
  5. BARABARA YA ARUSHA – NAMANGA, tunapenda pia kutoa pongezi sana kwa Serikali ya CCM kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi, leo vijana wote walioshiriki baraza hili na kusafiri kutokea Arusha mjini wamejionea kazi nzuri inayoendelea ya barabara ya Arusha-Nairobi na kama siyo taratibu za watu wa uhamiaji mpakani, tunaamini sasa unaweza kufika Nairobi kwa masaa mawili tu, na hii tunaamini ndiyo itawasaidia watanzania kuweza kunufaika zaidi na fursa za shirikisho la Afrika Mashariki. Kwa mafanikio kama haya na mengi mengine, tunaamini kabisa wananchi wataendelea kuwa na imani na Chama Cha Mapinduzi na tutashinda uchaguzi mkuu wa 2015 kwa kishindo zaidi.


KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI


JAMES OLE MILLYA
MWENYEKITI UVCCM - MKOA WA ARUSHA


KWA HISANI YA JAMII FORUMS

No comments: