Friday, March 4, 2011

UDIKTETA WA CHAMA KIMOJA NA HATIMA YA TANZANIANa. Lula wa Ndali Mwananzela

MADIKTETA pote duniani wanafanana. Wanafanana kwa tabia, mitazamo yao, malengo yao na wanafanana hata makosa yao. Na wanafanana vile vile kwa kitu kingine cha kutufanya tufikirie, hakuna dikteta ambaye amewahi kukubali kuwa yeye ni dikteta na kuvaa sifa hiyo kwa heshima. Madikteta wote wamejizunguka na wingu la kutisha kiasi kwamba, raia wanalazimika kuonesha hofu mbele zao kwa kukiri kuwa wanawapenda.

Nimesema madikteta sehemu zote duniani wanafanana. Wanaamini kuwa wao ndio pekee wenye uwezo na haki ya kutawala. Hakuna dikteta duniani ambaye anaamini kuna mtu mwingine anayeweza kutawala vizuri zaidi kuliko yeye. Hii ndiyo asili ya fikra za kidikteta. Madikteta duniani hujiona kuwa wao pekee ndiyo wenye sera “safi” na mbinu “bora” za kutawala hata kama sera na mbinu hizo zimejionesha miaka nenda rudi kuwa haziwezi kuyainua maisha ya watu wake wengi. Huwezi kumwambia dikteta kuwa anatawala vibaya au utawala wake ni mbaya. Utaishia selo!

Wanaamini kuwa bila ya wao nchi haiwezi kutawalika. Kwa muda mrefu na sehemu mbalimbali duniani, watawala wenye mrengo wa kidikteta huwajaza watu hofu kuwa wao wakiondoka madarakani nchi yaweza kuvurugika na machafuko makubwa. Kwa vile ndio wameshikilia madaraka, hueneza uongo huu na kuwapata mamilioni ya watu ambao huamini kuwa bila ya watawala wao kweli nchi itavurugika. Wakati mwingine wenye kuamini imani hii isiyo na msingi wowote ni watu ambao wanaonekana kuwa na dalili ya usomi. Katika mfumo wenye udikteta, utaona watu wasomi kabisa wanaimba wimbo kuwa bila dikteta fulani nchi haiendi.

Madikteta wote duniani hupenda kusifiwa. Madikteta wasiposifiwa wanaanza kuona kuwa wanachukiwa na wanaanza kutenda kidikteta zaidi na kufanya mambo ya kutafuta sifa. kama hakuna watu wa kuwasifia hujisikia wapweke sana na wanaanza kuwa nawasiwasi kuwa yawezekana watu wameanza kuamka. Hivyo hujikuta huanza kuhamasisha sifa. Sehemu nyingine duniani, wameanzisha hata bendi au vikundi vya sanaa vya watawala ili viimbe sifa zao.

Tunaowaita “madikteta” kimsingi tunazungumzia ni watawala wa amri au kiimla. Watawala ambao hutumia maneno na kauli kutawala, maneno na kauli ambazo husindikizwa mara zote na tishio la nguvu. Madikteta hawawezi kutawala kwa kushawishi ambao ndio msingi wa demokrasia yeyote duniani. Madikteta wana haraka sana ya kutumia nguvu dhidi ya upinzani wanaoupata au wanaohisi wataupata.

Lakini kuna kufanana kwingine kwa madikteta duniani ambako hatuna budi kukufikiria kwa sekunde. Madikteta hawawezi kuachia madaraka kirahisi! Hii ndiyo sababu wanaitwa madikteta. Wako tayari kutumia mbinu mbalimbali ili kuendelea kukaa madarakani. Watatumia ujanja, watapinda sheria, watunga uongo, na ikibidi wanaweza hata kufanya mazingaombwe yenye kufanana na demokrasia (kama uchaguzi ambao wao hushindwa kwa asilimia 90!) ilimradi tu wananchi wasiweze kuamka na kuwakataa.

Hata hivyo, madikteta wote duniani hukabiliwa na tatizo moja kubwa ambalo tangu enzi na enzi hawajaweza kulipatia dawa. Tatizo ambalo huwa kama kivuli kikiwafuata kila waendako na kama jinamizi lisilowaachia kila wakilala. Kuanzia kina Musolini, Lenin, Idi Amin, na hata tawala zenye mlengo wa kidikteta kama ule wa kikaburu vyote vimekabiliwa na tatizo moja kubwa ambalo ndio huuangusha utawala wa kidikteta. Fikra huru.

Madikteta duniani hawajawahi pata dawa ya kuzima na kuzuia mawazo huru. Wameweza kuwafunga watu pingu na kuwaweka magerezani na wakati mwingine kwa muda mrefu, lakini hawakuweza kufunga fikra zao. Wameweza kuwapiga watu risasi na kuhakikisha kabisa wamekufa, lakini bila kusababisha fikra zao kufa. Fikra huru hudumu na hupitishwa toka kizazi kimoja kwenda kingine.

Tukielewa hayo tutaelewa kuwa utawala wa kidikteta si lazima uwe ni utawala wa mtu mmoja. Mtu mmoja mmoja anaweza asiwe dikteta kwa namna hiyo, lakini upo udikteta mwingine wa hatari zaidi. Nao ni udikteta wa chama kimoja. Chama ambacho kina nguvu kuliko mfalme na makali kuliko ya sime. Udikteta wa chama kimoja unawezwa kusemwa kuwa ni utawala mbaya zaidi na ambao kuangushwa kwake ni vigumu zaidi kuliko udikteta wa mtu mmoja! Ni rahisi kumuangusha mtu mmoja ambaye ni dikteta kuliko kukiangusha chama ambacho ni cha dikteta.

Ingawa Tanzania imerudi kwenye mfumo wa vyama vingi, lakini bado chama kimoja tawala kinahodhi nguvu kubwa sana ya madaraka kiasi kwamba, kina uwezo wa kufuta haki ya mwananchi kama mwalimu anavyofuta maandishi ubaoni na hakuna mtu wa kulalamika au kuidai zaidi ya kufanya makongamano ya kujadiliana jinsi gani serikali imeweza hivyo. Katika taifa letu leo hii unapofikia kuwa Mahakama inashiriki katika uvunjaji huu mkubwa wa haki za wananchi na majaji saba wote wanaunga mkono kurudisha jambo ambalo Katiba inasema halitakiwa kurudishwa bungeni, siyo tu kwamba utawala wa kiimla unaanza kukua, bali unathibitika tu.

Lakini utawala wa kidikteta hupata nguvu zaidi kutoka katika mafuta mabaya kabisa ambayo hayakomi, yaani mafuta ya ufisadi. Sifa kubwa ya tawala zote za kidikteta duniani (uwe wa mtu mmoja au chama kimoja) ni kutamalaki kwa ufisadi katika maeneo na nyanja zote na kuwa watu hatimaye hujifunza kuishi, kuzalisha, kufanikiwa na kuendelea katika mfumo huo wa kifisadi. Huwezi kamwe kutenga utawala wa kidikteta kutoka mfumo wa utawala wa kifisadi. Ni shilingi ile ile yenye pande mbili.

Lakini haijalishi vinaangukaje, la maana ni kutambua kwanza kwamba madikteta wote duniani hufanana. Wawe ni mtu mmoja au wa chama kimoja cha siasa kinachotawala. Sifa zao ni zile zile, mitazamo yao ni ile ile, mweleko wao ni ule ule na matokeo ya utawala wao ni yale yale! Na wapo ambao hawawezi kufikifiria kuishi nje ya mfumo huo. Na wapo wenye fikra huru.

Niandikie: Lulawanzela@yahoo.co.uk


MWANANCHI

No comments: