Sunday, March 13, 2011

TIBA YA LOLIONDO UTATA MTUPU

  • Mchungaji Ambilikile agoma dawa yake kupimwa
  • Viongozi wa serikali, CCM wamiminika
  • Ushuhuda wa ‘waliopona’ utata mtupu

NI majira ya saa ya tano asubuhi. Nawasili nyumbani kwa Mchungaji Mstaafu Ambilikile Nasapila (76) “Babu” iliyopo katika kijiji cha Samunge, tarafa ya Sale, Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha, umbali wa Kilometa kama 400 kutoka mjini Arusha baada ya safari ndefu ya saa zaidi ya nane.

Kwa hakika, kijiji hiki kwa sasa ndicho kijiji kinachotajwa sana na watu kuliko kijiji kingine chochote mkoani Arusha kama si Tanzania baada ya mchungaji huyo ‘kugundua’ kinachoitwa kuwa ni “dawa ya ajabu” inayotibu maradhi sugu matano.

Safari yetu ilianza saa usiku wa Alhamisi ya Machi 3 kwa gari aina ya Landcruiser lenye namba za usajili T 612 AGP likiendeshwa na dereva Victor Leons, na kwa hakika safari hiyo imeacha kumbukumbu ya aina yake kwa kuwa moja ya safari ngumu sana baada ya gari letu kupata hitilafu ya kupasuka kwa rejeta kabla ya kufika kijiji cha Engaruka wilayani Monduli.

Wakati gari linapata hitilafu ilikuwa imetimu saa 10 za alfajiri na mimi na abiria wengine wanane niliokuwa nasafiri nao, tulilazimika kusubiri usiku huo katikati ya pori ambalo linaelezwa kuwa na wanyama wakali hadi tulipopata msaada wa msamaria mwema mmoja aliyekuwa akipita barabara hiyo ambaye alitusaidia majani ya chai na maji kiasi cha lita 5 ambayo tuliyatumia kuyaweka katika rejeta hiyo kuziba sehemu iliyotoboka.

Wahenga walisema msafiri kafiri. Ni baada ya “sayansi” hiyo isiyo rasmi ya ‘kutibu’ gari ndipo tulipoendelea na safari na kufika kijiji cha Engaruka ambako tulinunua madumu yenye maji na majani ya chai ya kutosha na kuendelea na safari ambapo tulilazimika kusimama na kuongeza majani ya chai na maji kila baada ya Kilometa 20 ili kupoza Injini ya gari iliyokuwa ikipata joto kutokana na kupasuka kwa rejeta. Na hiyo ndiyo iliyokuwa sababu kubwa ya kuchelewa kufika kwa “Babu”; tofauti na matarajio yetu.

Akitumia uzoefu wa kusafirisha watalii katika barabara za hifadhi za Taifa, dereva aliyekuwa akituendesha alitumia "ushujaa" mkubwa kuhakikisha kuwa tunafanikiwa kufika kijijini hapo pamoja na kuharibikiwa gari.

Sehemu kubwa ya barabara ya kwenda katika kijiji hicho ni mbovu sana na iliyojaa mashimo na vumbi jingi. Njiani tulikuta magari mengi yakiwa yameharibika na kushindwa kuendelea na safari ya kwenda Samunge.

Nyumbani kwa Mchungaji

Na hali ninayoikuta nyumbani kwa Mchungaji Ambilikile inanistua kidogo. Ni hali ya kelele na majibizano makali baina ya watu ambao kwa haraka naelezwa kuwa ni watu waliofuata matibabu kwa mchungaji huyo na watumishi wa mchungaji.

Watumishi kadhaa wakiwa na fimbo na vipande vya miti wanajaribu kuzuia umati mkubwa wa watu nje ya nyumba ya Mchungaji; huku baadhi ya watu ambao ni wagonjwa wakiwa wamelala mbele ya nyumba ndogo sana iliyojengwa kwa miti na udongo.

Nje ya kijumba hicho cha Mchungaji, kuna wagonjwa waliolala hapo ambao hawajiwezi. Hali zao ni mbaya sana kutokana na kudhoofika kwa maradhi kiasi kwamba hawezi hata kujisogeza ukichanganya na uchovu wa safari ndefu ya kufika hapo na muda walionekana kuzungukwa na ndugu na jamaa zao waliokuwa wanawahudumia.

Kwa ujumla, hali ni ya kusikitisha mno na kuogofya; kwani pamoja na vurugu za kusukumana baina ya watumishi na watu wanaotaka kuingia nyumbani kwa mchungaji, wagonjwa waliolala wanaonekana wazi kuwa na maumivu makali kutokana maradhi, uchovu na kelele za watu wanaotaka kuingia eneo hilo.

Na wakati mwingine ilikuwa vigumu kuamini kwani watu niliowakuta hapa wengi ni kutoka mjini Arusha ambao nafahamiana nao vizuri kikazi kama maofisa wa ngazi za juu wa idara mbalimbali za serikali, wabunge wa Bunge la Jamhuri na viongozi, viongozi wa vyama vya siasa, wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite na wafanyabiashara wengine maarufu wenye asili ya Kiasia.

Wafanyabiashara hawa wengi wamefika hapa kwa kutumia usafiri wa ndege za kukodi hadi uwanja wa ndege wa Wasso uliopo Loliondo umbali wa Kilometa 60 kutoka kijiji hicho, na baadaye husafirishwa kwa magari ya kukodi hadi kijijini hapo.

Wako pia watoto wenye umri wa kuanzia miezi mitatu hadi miaka 15, na wote walionekana kuambatana na wazazi ama walezi wao na watoto hawa kimsingi walipaswa kuwa mashuleni kuendelea na masomo yao; kwani kipindi hiki si cha likizo.

Pia hapa wapo maafisa wa Mahakama ya Mauaji ya Rwanda (ICTR), maafisa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na vijana maarufu wa kiume na kike ambao hufahamika zaidi kama “masista du” wanaofanya kazi katika makampuni mbalimbali ya mjini Arusha.

Naambiwa kuwa kila moja hapa anataka kupata kikombe cha dawa ya maajabu, na ingawa Mchungaji huyo ametoa mwongozo kuwa anatibu magonjwa matano sugu, lakini wengine wanaotaka dawa hii ya maajabu kila moja ana matatizo nje ya hayo magonjwa sugu.

Kwa mujibu wa maelezo ya baadhi ya wagonjwa, matatizo hayo yaliyo nje ya mwongozo wa Mchungaji ni pamoja na nguvu za kiume kwa wanaume na hata wale wenye matatizo ya uzazi; huku wengine wakionekana ni watu wanaofuata mkumbo tu ilimradi wapate dawa hiyo.

Kila mmoja alionekana akikwepa kamera ya mwandishi, na wengine walikuwa wanatoa vitisho vya hapa na pale kupigwa picha; hasa maafisa wa serikali ambao inaonekana wengi wameondoka katika maeneo ya kazi bila idhini za wakubwa wao.

“Sitaki kupigwa picha hapa. Unajua hii ni sehemu ya tiba kwa hiyo lazima uheshimu ‘praivesi’ zetu (faragha). Tuko hapa kwa sababu tuna matatizo. Si kwa kupenda”, alisema ofisa moja wa Serikali mwenye cheo cha juu.

Sababu za vurugu, naelezwa kuwa ni Mchungaji huyo kusitisha kutoa huduma ya kugawa dawa kwa wagonjwa baada ya baadhi ya wagonjwa hao kuvuruga utaratibu uliokwepo wa kupanga foleni ili kupata “kikombe cha dawa ya maajabu”.

Nje ya nyumba hiyo na barabara inayopita mbele ya nyumba ya Mchungaji, kuna msururu wa magari na kwa haraka nakadiria kuwa msururu huo una urefu wa Kilomita kama tano na magari yanayozidi 1000 huku magari yenye usaji wa namba za serikali za STK, Mashirika ya Umma (SU) na namba za ubalozi yakitamalaki.

Mmoja wa watumishi hao, Sediay Berere, anaeleza kuwa Mchungaji amegoma kutoa huduma kutokana na watu kuvuruga utaratibu uliopangwa ambao huwa watu wanaofika hapo kupata dawa kuunga foleni ambapo kila moja hupewa kikombe kimoja cha dawa hiyo, na baada ya kunywa humpisha mwenzake.

“Kama unavyoona idadi ya watu imeongezeka sana leo. Sasa kuna watu wanataka wapatiwe dawa bila ya kupanga foleni na hiyo tunaona ni ukiukwaji wa taratibu zetu kwasababu kuna watu wengi ambao wako hapa tangu juzi, na bado hawajapata huduma”, anaeleza mtumishi huyo.

“Watu wanafanya vurugu na kusababisha kiasi kikubwa cha dawa kumwagika kama unavyoona hapa, na hii ni hasara kubwa; kwani dawa hii pia inapatikana kwa gharama kubwa”, anasema mtumishi huyo.

Mtumishi huyo anaongeza:”Na watu hapa wanaofanya vurugu ni wale ambao wanatoka Arusha. Wengi wanataka kupata huduma wakidhani hapa tunajali umaarufu wao….hapana hapa hakuna mfanyabiashara maarufu, afisa wala kiongozi wa serikali. Watu wanatakiwa kupanga foleni kulingana na muda kila moja aliowasili”.

“Mchungaji hana muda wa kutaka kufahamu anayepata huduma ana cheo, umaarufu au ukwasi kiasi gani. Hapa watu wote ni sawa, na kila mmoja atakunywa dawa inayotolewa kwa utaratibu ulio sawa”, anaongeza.

Baada ya mazungumzo ya hapa na pale hadi inapotimu majira ya saa 8, napewa fursa ya kuzungumza ana kwa ana na Mchungaji Ambilikile kupata ufahamu kuhusu tiba yake hiyo ya ajabu.

Ana kwa ana na Mchungaji Ambilikile

Tofauti na matarajio yangu, Mchungaji Ambikile anaonekana kuwa mzee wa kawaida kama walivyo wazee wengi wa maeneo ya vijiji vya Tanzania. Ni mcheshi kiasi; huku akizungumza kwa uangalifu mkubwa kwa kuchagua maneno. Na anaanza kwa kunitahadharisha kuwa muda wake ni mdogo sana hivyo niulize maswali ya msingi tu kuhusu tiba anayotoa.

“Kijana wangu, kama unavyoona, nimezungukwa na idadi kubwa ya watu wanaohitaji huduma; hivyo utanisamehe sana sitakuwa na muda wa kutosha wa kuzungumza na wewe. Nakuomba uniulize kwa kifupi mambo ya msingi kuhusu dawa yangu, nami nitakupa majibu”, anaeleza.
Hata hivyo, anaanza kwa kunieleza kuwa yeye ni mzaliwa wa Rungwe, mkoani Mbeya, na kwamba alizaliwa miaka 76 iliyopita (1935), na ni Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Sonjo, mtaa wa Samunge.

“Na kama nilivyokueleza, mimi ni Mchungaji mstaafu lakini pia ni “Nabii” ambaye naweza kuona maono au ndoto na kuzungumza na Mungu mara kwa mara na Mungu. Na yote ninayoyatekeleza kama unavyoona ni maagizo ya Mwenyezi Mungu.”

“Nimefanya kazi za uchungaji tangu mwaka 1967 katika sehemu kadhaa nchini hadi mwaka 1989 nilipohamishiwa katika eneo hilo. Na nimefanya kazi za uchungaji hapa hadi nilipostaafu mwaka 2002”, anaeleza.

‘Nilianza kuota maono na kusikia sauti ya Mungu tangu mwaka 1991 ikinieleza kuwa nibaki kuishi eneo hili; kwani Mungu alikuwa anataka kunipa kazi maalumu ambayo kwa wakati huo sikuifahamu”, alisema.

Mchungaji Ambilikile anaongeza kuwa kwa muda wote huo aliendelea kuwa na maono hayo hadi mwaka 2009 alipoota kuwa Mungu anamhitaji awape dawa watu wanaougua maradhi ya ukimwi ambao ni moja ya magonjwa yaliyoteketeza maisha ya watu; hasa katika nchi za Kiafrika.

Dawa hiyo inatokana na mizizi na magamba ya mti unaoitwa “Muugamuryaga” kwa lugha ya kabila la Kisonjo ambalo ndilo wenyeji au wakazi wa tarafa ya Sale yenye vijiji zaidi ya 10.

Jina la kitaalamu la mti huo kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza bado halijafahamika. Utengenezaji wa dawa hiyo ni kuchemsha kwa maji mizizi, na baadaye wagonjwa hunywa kikombe kimoja cha maji yake kama dawa. Mchungaji huyo ameupanda mti huo mbele ya nyumba yake ili watu wanaofika hapo wapate kuuona.

“Nilimwuliza Mungu je baada ya kunionyesha dawa nimtibu nani?.....Mungu alijibu kuna mwanamke atakuja kuchota maji katika bomba la maji lililo jirani na nyumbani kwako ambaye anaishi na virusi vya ukimwi na umtibu huyo”, alisema Mchungaji huyo.

Mchungaji Ambikile anaongeza: “Kweli baada ya siku chache alikuja mwanamke huyo ambaye ni mkazi wa kijiji hiki na kila mmoja alikuwa anamfahamu kuwa anaishi na virusi vya ugonjwa wa ukimwi na alikuwa katika utaratibu wa kupewa madawa ya kupunguza makali ya ukimwi (ARV). Nilimpatia dawa kwa mara ya kwanza”

Alisema baada ya kupata dawa hiyo, mwanamke huyo aliacha kutumia dawa za kupunguza makali (ARVs) na baada ya kupimwa aligundulika kuwa hana virusi hivyo, na ndipo alipokuja kutoa ushuhuda kanisani na kijiji kizima na habari zake kusambaa.

Hata hivyo, mwanamke huyo ambaye hata hivyo jina lake halitajwi hakupatikana. Raia Mwema ilipomwuliza Mwenyekiti wa kijiji hicho, Jonas Ngirobei, kuhusu mwanamke huyo alijibu kuwa si rahisi kumpata; kwani anaishi upande wa pili wa kijiji hicho ambao si rahisi kufika kwa wakati huo.

Mchungaji Abilikile aliendelea kueleza kuwa baada ya muda huo kidogo kidogo wagonjwa waliendelea kujitokeza na aliendelea kuwatibu, na ndipo habari za mafanikio ya dawa yake zilisambaa katika vijiji vya Wilaya ya Ngorongoro na hadi wilaya jirani za mkoa wa Arusha na baadaye nje ya mkoa huo.

“Baadaye Mungu aliniotesha tena kuwa watu wake wanaumia kwa maradhi sugu mengine zaidi ya ukimwi, na mimi nikaitikia kwa kuwapatia dawa hiyo wagonjwa wenye maradhi hayo”, alisema.

Alisema kwa sasa dawa hiyo inatibu maradhi sugu kama kisukari, pumu, kifafa, ukimwi na kansa, na anadai kuwa tayari kuna wagonjwa wengi ambao wamepona maradhi hayo baada ya kutumia dawa yake.

Alisema hakuwahi kuitangaza tiba hiyo mahala popote, lakini amekuwa anapokea wagonjwa kutoka mikoa mbalimbali nje ya Arusha kama Manyara, Dodoma, Singida, Mara, Kilimanjaro, Mwanza, Dar es Salaam, Morogoro, Iringa na Mbeya.

“Pia nimeshawapokea wagonjwa kutoka nchi jirani kama Kenya, Uganda na mataifa mengine ya nje kama Oman, Ujerumani, Norway na Uingereza…..na wote dawa hii imewasadia sana”, anadai Mchungaji huyo.

“Nimeota maono mengine kuwa watu kutoka mataifa mengine watakuja kwa wingi kufuata dawa hapa na watapata tiba kwa bei ile ile ambayo Mungu ameipanga ambayo ni Shilingi mia tano”, aliongeza.

Kuhusu dawa hiyo kufanyiwa utafiti na wataalamu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii ili kufahamu uwezo wake wa kutibu maradhi anayoyataja, Mchungaji Ambilikile anakataa katakata dawa yake kuchunguzwa na wataalamu kwa madai kuwa dawa hiyo ni kutoka kwa Mungu, na kwamba hata ikichunguzwa, wataalamu hao hawawezi kugundua chochote.

“Sitaki kuhusisha dawa hii na wataalamu unaowataja…..Hii si kazi yangu; bali ni kazi ya Mungu, na hata wanaopona ni wale ambao wameweka imani yao mbele ya Mungu kuwa wataponyeshwa na dawa hii”, anaeleza.

Tofauti na wagunduzi wengine, Mchungaji Ambilikile anaweka wazi mti anaotumia, jinsi anavyoandaa dawa hiyo kwa uwazi, lakini sharti kubwa ni kuwa ni lazima ampe mgonjwa dawa hiyo kwa mkono wake mwenyewe, na mgonjwa lazima ainywe hapo hapo mbele yake na si kuondoka nayo.

“Dawa hii lazima nikupe mwenye kwa mkono wangu, na pia lazima mgonjwa ainywe hapa hapa…..Hairuhusiwi kumpelekea mgonjwa aliye nyumbani au hata nje ya eneo hili. Iwapo dawa itatolewa bila idhini yangu, haitakuwa na manufaa yoyote. Itakuwa sawa na mtu aliyekunywa maji ya bomba”, alisema.

Kuhusu taarifa kuwa atasitisha utoaji dawa hiyo wakati wa kipindi cha Kwaresma ambacho ni wakati wa mfungo kwa waumini wa madhehebu ya Kikristo, Mchungaji huyo anaeleza kuwa wataendelea kutoa huduma hiyo isipokuwa siku ya Ijumaa Kuu na siku ya Sikukuu ya Pasaka.

“Tuatendelea kutoa huduma ya dawa kama kawaida ispokuwa siku ya Ijumaa Kuu na siku ya Sikukuu ya Pasaka tutapumzika, na baada ya hapo tutaendelea kama kawaida”, anaongeza kusema.

Mchungaji huyo anatoa tahadhari kwa wagonjwa wanaotumia dawa hiyo; hasa wale wanaoishi na virusi vya ukimwi kuwa dawa hiyo si kinga ya kutokuambukizwa tena virusi vya ugonjwa huo iwapo mgonjwa atapona baada ya kutumia dawa.

“Ni lazima mgonjwa abadilishe mwenenendo wake kwa kuacha tabia ya ngono baada ya kupona….Akiambukizwa tena hawezi kupona kwa dawa hii. Mgonjwa anatumia mara moja tu na hairuhusiwi kurudiwa”, anaongeza.

Mchungaji Ambilikile anakiri kuwa kutokana na kuongezeka kwa wingi wa watu katika eneo hilo, sasa anakabiliwa na changamoto mpya ambayo ni pamoja na kuongeza kiasi cha dawa, kuni za kuchemshia na miundo mbinu ya eneo hilo kama vyoo na sehemu za kupumzikia wagonjwa.

“Hapa ndipo ninapohitaji msaada wa Serikali; hasa wa kupatiwa gari ambalo litasadia kubeba kuni za kuchemshia dawa. Na pia kutengeneza hapa ili kupata eneo la kuegeshea magari pamoja na wagonjwa kupumzikia”, anaeleza.

Baada ya kumaliza mahojiano hayo, mchungaji hana muda wa kupoteza. Anaendelea na kazi ya kutoa dawa yake baada ya kupangwa utaratibu mpya ambao ni kugawa dawa kwa watu walioko ndani ya magari.

Katika utaratibu huo mpya, Mchungaji na watumishi wake husimama pembeni mwa barabara na gari moja baada ya lingine hupita hapo ambapo watu walioko ndani hupewa vikombe na kunywa dawa na kuondoka eneo hilo kupisha gari lingine.

Katika utaratibu huo mpya linazuka tatizo lingine ambapo madereva wa magari waliokodishwa na wagonjwa walianza mtindo wa kuwatoza watu fedha kuanzia Shilingi 10,000 hadi Sh. 50,000 kwa mtu mmoja ili waingie katika magari yao na wapate nafasi ya kupata dawa hiyo.

Utaratibu huo pia ulizua malalamiko; kwani kuna wagonjwa ambao wamefika eneo hilo bila magari; hivyo hukaa kwa muda mrefu bila kuhudumiwa na hivyo kuendelea kuwepo kwa msongamano wa watu.

Kutokana na msongamano wa watu, hali ya upatikanaji wa huduma za kijamii katika kijiji hicho ni mdogo sana, kuanzia huduma ya vyoo, vyakula, maji na huduma nyingine muhimu kama mawasiliano ya simu.

Wakati eneo linakuwa na watu zaidi ya 2,000 kwa wakati mmoja, choo kilichopo hapo ni kimoja tu na wakati mwingi wagonjwa wanaofika hujisitiri katika vichaka vinavyozunguka eneo hilo na kusababisha vinyesi vya binadamu kutapakaa kila mahali.

Hali hiyo, inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa mengine kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kijiji hicho, Jonas Ngirobei ambaye aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo waliitisha kikao cha kamati ya Maendeleo ya kata ambayo imependekeza kamati ya watu watano kusaidiana na mchungaji huyo katika masuala kadhaa kama kuongeza idadi ya vyoo na pia kupanga utaratibu mzuri wa watu kupata huduma hiyo ya dawa.

“Kamati hiyo ya watu watano itaangalia maeneo muhimu yanayohitaji marekebisho pamoja na jinsi ya kulinda usalama wa watu na mali zao; maana ni wazi kuwa vitendo vya uhalifu vitaanza kutokea”, alisema.


Maisha ya kawaida katika kijiji hicho yamebadilika sana bei ya vyakula ni ya kutisha na wagonjwa wengi wanaofika hapa wameshindwa kumudu gharama za kununua vyakula hivyo.

Kwa mfano, mama lishe wanaouza vyakula vingi vikiwa katika mazingira yasiyoridhisha kwa usafi wanauza sahani moja ya wali na maharage kati ya Shilingi 3,000 na Sh. 4,000, kikombe kimoja cha chai Shilingi 500, na nyama ya mbuzi huuzwa kati ya Shilingi 12,000 hadi 15,000 kwa kilo moja.

Ushuhuda wa waliotumia dawa

Kuna taarifa nyingi na za kutatanisha kuhusu watu waliotibiwa na Mchungaji huyo na kupona maradhi yaliyokuwa yanawasumbua, lakini wengi wanatoa ushuhuda kuwa wamepona maradhi sugu kutokana na dawa hiyo ya maajabu.

Mmoja wa watu hao (mwenye asili ya Kiasia ) aliyezungumza na Raia Mwema kwa sharti la kutotajwa jina, ambaye alikuwa katika kijiji cha Samunge, alieleza kuwa ana mtoto wa kaka yake mwenye umri miaka 12 aliyezaliwa na virusi vya ukimwi na baada ya kutumia dawa hiyo mwezi uliopita amepimwa, na kiasi cha virusi vilivyobaki mwilini ni kidogo sana.

“Mimi mwenye ndiye nilimleta mtoto huyo hapa kwa Babu kunywa dawa mwezi Januari, na baada ya kumpima mwezi uliopita vipimo vinaoonyesha kuwa CD4 zake ziko juu sana na kiasi cha virusi ni kidogo; hivyo tunasubiri tena mwezi huu tukampime tena na matokeo hayo ndiyo yaliyonifanya mimi kurudi hapa kunywa hiyo dawa”, alieleza.

Aidha, baadhi ya watu wenye ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu wanatoa ushuhuda kuwa wamepata nafuu, lakini kwa baadhi ya wagonjwa hali zao zimezidi kuwa mbaya.

Raia Mwema imeelezwa kuwa tayari mmoja wa watu waliokwenda kupata dawa hiyo wiki tatu zilizopita alifariki dunia Jumatano iliyopita huko Ngaramtoni wilayani Arumeru wakati mwingine ambaye anaishi na virusi vya ukimwi yuko mahututi katika hospitali moja iliyopo Usa River wilayani Arumeru pia.

“Ndugu yangu alikwenda na mwenzake kupata dawa; kwani wote walikuwa wanaishi na virusi na baada ya kurejea hali zao zikabadilika tayari mwenzake ameshafariki na amezikwa wiki iliyopita wakati ndugu yangu amelazwa na ana hali mbaya”alisema.

Kauli za viongozi wa serikali na dini

Akizungumzia tiba hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali, alieleza kuwa kwa sasa serikali inachofanya ni kuweka mazingira mazuri ya utoaji huduma katika eneo hilo na kumsaidia Mchungaji huyo kukabiliana na changamoto ya kukabiliana na idadi kubwa ya watu.

“Kwa kweli idadi ya watu ni kubwa sana hapa wilayani. Nimemwagiza OCD aongeze idadi ya askari wa kikosi cha kutuliza ghasia katika eneo hilo ili walinde usalama na kusaidia kupanga watu, lakini tufanye mipango ya kujenga vyoo vya dharura ili watu waweze kujisitiri kwa ustaarabu”, alisema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isidori Shirima, ambaye pia ni Mwenyeiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Arusha, alieleza kuwa Serikali haina mpango wowote wa kuzuia au kupiga marufuku utoaji dawa hiyo iwapo watu wanaotumia wanatoa ushuhuda kuwa wamepona maradhi yanayowasumbua.

“Kama wanaamini kuwa wanapona, sisi kama Serikali hatuwezi kuwazuia; kwani kufanya hivyo ni sawa na kuwanyima haki wananchi kwa yale ambayo wanayaamini”, alisema.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk.Salash Toure hakupatikana jana kuelezea mtazamo wake kuhusu tiba hiyo, lakini mmoja wa madaktari wa Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, kitengo cha Ukimwi, aliliambia Raia Mwema kuwa ni mapema mno kwa wananchi wanaokwenda kupata tiba hiyo kuamini kuwa wamepona. Alisema ni lazima dawa hiyo ithibitishwe kwanza kisayansi kwamba inaponya magonjwa hayo.

“Kwa ufahamu wangu, magonjwa yote yanayodaiwa yanatibiwa na Mchungaji huyo ni magonjwa sugu ambayo yamekuwa yakiwapasua vichwa wataalamu wa afya duniani. Sasa watu wawe makini na dawa hizo kabla hazijathibitishwa na wataalamu wa afya; vinginevyo watakuwa wanapoteza muda wao na kuingia gharama za bure”, alitahadharisha.

Hadi tunakwenda mitamboni, idadi kubwa ya wananchi kutoka mikoa mbalimbali ilikuwa bado inamiminika kwenda katika kijiji hicho kupata tiba ya dawa hiyo ya “Babu”; huku wengi wakiwa wamekwama mjini Arusha kwa siku kadhaa kutokana na kukosa usafiri wa kwenda huko ambapo sasa wanalazimika kulipa nauli ya Shilingi 120,000 kwa mtu mmoja kwa magari aina ya Landcruiser yanayotumika kusafirisha watalii na kwa mabasi ni Shilingi 80,000 kwa mtu mmoja.


RAIA MWEMA

No comments: