Wednesday, March 9, 2011

MUUGUZI WA HOSPITALI YA TMJ AJITOLEA DAMU KUOKOA MAISHA YA MGONJWAJUZI na jana katika vyombo vya habari viliripoti habari inayohusu muuguzi wa Hosptitali ya TMJ ya jijini Dar es Salaam, Beatrice Mwaibanji (39), kufanya kitendo cha kizalendo cha kuokoa maisha ya mwanamke aliyepata tatizo la kuvuja damu kwa mfululizo baada ya kujifungua mtoto.

Muuguzi huyu ambaye ni wa aina yake alifanya kitendo hicho cha kijasiri na cha kiungwana cha kutoa damu yake na kumwekea mama aliyejifungua baada ya kutokuwako na damu ya kumwekea katika hospitali hiyo.

Taarifa zinadai kwamba muuguzi huyo alifikia uamuzi huo baada ya kuona mama aliyejifungua ameishiwa nguvu kwa kutoa damu nyingi na kwamba kulikuwa hakuna njia nyingine ya kuokoa maisha yake zaidi yeye kujitosa kwenye maabara ya hospitali hiyo kutoa damu na kisha kumwekea mama mzazi huyo.

Hivyo baada ya muuguzi huyo kumwekea damu mama huyo ambaye alikuwa amejifungua salama mtoto wa kiume aliweza kupata nguvu na hadi sasa anendelea vema kumlea mwanaye.

Sisi wa Mwananchi tumezipokea taarifa hizi za muuguzi huyu kwa faraja na tunaona kitendo hicho alichoonyesha si tu kinajenga imani ambayo imeanza kupotea kwa wauguzi bali kinaonyesha bado kwenye tasnia ya uuguzi kunao wazalendo wachache ambao wanaweza kusimama kifua mbele na kusema kwamba wao ni waadilifu kitaaluma. Hakika muuguzi wa TMJ ni mmoja wao.

Tunasema hivi kwasababu katika miaka ya karibuni kina mama wamekuwa wakitoa lawama chungu nzima kwa wauguzi kwamba wamekuwa wakiwanyanyasa kwa maneno na vitendo wakati wakienda kupata huduma mbalimbali hospitalini ikiwamo ya kujifungua.

Tabia hii ya wauguzi imekuwa ikilalamikiwa na wananchi, lakini hakuna ufumbuzi ambao umepatikana kwenye hospitali hasa zile za Serikali. Hivyo basi ni maoni yetu kwamba mfano huu mwema wa muuguzi wa hospitali ya TMJ, utaigwa na wengine katika kutoa huduma zao kwa wagonjwa.

Vilevile, tumefarijika kwamba uongozi wa TMJ umeamua kumpa cheti cha damu salama na kwamba unaangalia aina ya motisha wa kumpa kwa kazi nzuri aliyoifanya. Nasi tunampa hongera kwa kuonyesha uzalendo wake kwa vitendo.


MWANANCHI

No comments: