Thursday, March 3, 2011

MAKALA YA MBWAMBO
PALE ZAWADI INAPOPELEKWA KIBAHA KWA HELIKOPTA


MARAFIKI zangu wanapokuwa na muda wa kunisikiliza, huwa napenda kuwakumbusha kwamba Watanzania tumepanda ufisadi, na sasa tunavuna ufisadi. Mara nyingi huwa nawaambia hivyo wakati wanapolalamikia kutamalaki kwa ufisadi nchini.

Na kila mara nawakumbusha kwamba ufisadi ulianza kulelewa katika ngazi za juu za uongozi nchini, ukashuka hadi ngazi za mikoa na wilaya kabla ya kushuka zaidi hadi ngazi za vijiji, kata, mitaa na ndani ya familia.

Kama tungechukua hatua mapema ya kuuzika wakati ulipokuwa ngazi za juu; pengine tusingefikia hatua tuliyofikia sasa. Lakini hatukufanya hivyo, na sasa ufisadi umekuwa sehemu ya utamaduni wetu; maana hakuna asasi, sekta au taaluma iliyosalimika. Kwa wana taaluma ; katika kumi labda unaweza kupata wanne tu walio safi kabisa! Wengi tumeathiriwa kwa namna moja au nyingine na utamaduni huu mpya.

Na ndiyo maana wiki iliyopita sikushangaa kusoma mtandaoni na kwenye ujumbe wa simu (sms) malumbano ya waandishi wa habari kuhusu ujio wa huyo tuliyeelezwa kuwa ndiye mmiliki wa Dowans, Mohamed Yahya Al Adawi (wengine wamempachika jina la utani la Ali Hadaiwi!).

Katika malumbano hayo, baadhi ya waandishi wa habari wanawashutumu wenzao kwamba wamechukua jukumu la kuwa maofisa uhusiano wa mwekezaji huyo kutoka Uarabuni. Na kwa kuwa suala zima la Dowans limegubikwa na hisia za ufisadi, waandishi hao wanahisi wenzao wamepewa ‘bahasha’ kumpigia chapuo Mwarabu huyo na mitambo yake ya Dowans.

Waandishi wanaoshutumiwa nao wamekuja juu na wanawashutumu wenzao kwa kushindwa kuonyesha kwa Watanzania pande zote za tatizo; yaani kumpa pia Mwarabu huyo fursa ya kusikilizwa ikiwa ni pamoja na haki ya yeye kuamua kupigwa au kutopigwa picha katika mkutano wake na waandishi wa habari!

Nachelea kutoa hukumu kwa upande wowote kati ya hizo mbili za waandishi wa habari zinazozozana, kwa kuwa sina ukweli wote kuhusu jambo hilo. Hata hivyo, malumbano yao yanadhihirisha kitu kimoja; nacho ni kwamba, kwa sababu ya ufisadi kutamalaki nchini, hata waandishi wa habari nao sasa hawaaminiani tena katika kutekeleza majukumu yao.

Na si tu kwamba hawaaminiani tena wenyewe kwa wenyewe, lakini hata wananchi nao wameanza kupoteza imani nao kwa kasi. Na huwezi kuwalaumu. Utawalaumu vipi wakati magazeti (kwa mfano) yanaibuka na vichwa vya habari vinavyopingana kwa tukio linalofanana kama vile press conference? Unaweza kusoma magazeti mawili hadi matano, na bado usielewe ukweli wa nini hasa kilizungumzwa au kuulizwa kwenye press conference.

Vyovyote vile; ninachotaka kueleza hapa ni kwamba uandishi wa habari, kama zilivyo taaluma nyingine nchini, nayo imeathiriwa mno na kutamalaki kwa ufisadi nchini. Lakini haishangazi. Kama hata wanasheria, wahandisi, madaktari, wanasiasa, mashehe na maaskofu wote wamekumbwa na upepo wa ufisadi, waandishi wao ni nani wasikumbwe na upepo huo?

Ndugu zangu, tumepanda ufisadi na sasa tunavuna ufisadi. Na penye mavuno ya ufisadi hakuna haki, hakuna kuaminiana, hakuna ufanisi wa kazi, hakuna uzalendo na wala hakuna utawala bora.

Penye mavuno ya ufisadi kuna kiburi, majivuno, jeuri na ubabe wa fedha – tena za utajiri wa kupindukia; lakini zaidi ya yote kwenye mavuno ya ufisadi kuna umasikini uliokithiri na utumiaji mbaya wa madaraka - iwe ni kwenye asasi binafsi, iwe ni serikalini au hata jeshini.

Ndiyo, hata jeshini. Nasema hivyo kwa sababu katika miaka ya karibuni tangu ufisadi uanze kutamba nchini, hata jeshi letu la ulinzi (JWTZ) nalo pia limepata shea yake ya mavuno ya ufisadi.

Sitaki kuingia ndani katika suala hili kwa sababu ya unyeti wa chombo chenyewe, lakini ni nani asiyejua kwamba sambamba na ufisadi huo, nidhamu kwa wanajeshi wetu nayo pia imekuwa ikidorora kwa kasi?

Ni nani ambaye hakusoma magazetini tukio la wiki iliyopita huko Gongo la Mboto ambako wanajeshi walitoka kambini mwao usiku na kwenda mitaani kuwacharaza mikanda raia hadi kuwaumiza vibaya, eti tu kwa sababu mwenzao mmoja alipigwa na raia mtaani?

Ni nani ambaye hakupata kusoma huko nyuma habari za wapiganaji wa JWTZ walioshuka kutoka kwenye gari lao na kumchapa vibao trafiki kwa kuwa hawakuridhika na namna alivyokuwa akiongoza magari barabarani?

Sambamba na utovu huo wa nidhamu, yapo pia matumizi mabaya ya madaraka ndani ya jeshi hilo. Na hili linanikumbusha ujumbe mmoja wa sms niliotumiwa na msomaji wangu mmoja, wiki iliyopita, akimlalamikia mkubwa mmoja jeshini kwa kutumia vibaya madaraka yake; ikiwa ni pamoja na kutozijali fedha za walipakodi wa nchi hii. Alilalamika hivi msomaji wangu huyo:

“Hebu sikia upuuzi huu wa kamanda mmoja wa Airforce (anamtaja jina). Siku ya Ijumaa, tarehe 25 Februari alikwenda Ngerengere kwa gari lake la JW aina ya VX (Shangingi) kufuatilia mafunzo ya marubani. Mafunzo yalipomalizika, akaamuru ndege mbili za kijeshi za mafunzo zimrudishe Dar huku yeye akiwa ndege ya mbele na nyingine nyuma ikimsindikiza.

“Gari lake akaliacha lirudi tupu Dar likiwa na dereva tu. Maofisa wengine walijitahidi kumshauri sana kuwa taratibu za flight zinaandaliwa saa 24 kabla ya ndege kuruka. Isitoshe, akaambiwa kuwa yeye si rubani wala rubani mwanafunzi na kwamba kanuni haziruhusu; kwani ndege inabeba watu wawili tu. Yaani nyuma ni mwalimu (mkufunzi) na mbele mwanafunzi. Hata mafundi ndege hawaruhusiwi kupanda labda kwa dharura tu. Aliambiwa pia kuwa maandalizi ya checking ya ndege kabla ya safari yana dril zake, na kikubwa ni kwamba kuomba kutua Dar inahitaji muda kwa mamlaka husika.

“Lakini cha kushangaza, afande huyo hakusikia ushauri, na akalazimisha apelekwe Dar kwa ndege hizo. Matokeo yake ni kwamba ndege aliyopakia ilipotua Dar tu ikapata breakdown ya tairi moja kutoka lock, na hitilafu hiyo ikaivuta ndege nje barabara na kuzua tafrani kubwa kwa rubani, Meja...(anamtaja jina) aliyekuwa akimwendesha.

“Na kama si uhodari wa rubani huyo, tungempoteza kibosile huyo mzembe wa JWTZ, lakini pia tungempoteza rubani na ndege yenyewe! Kitendo cha kulazimisha safari hiyo kingeweza kuleta ajali hata kwa watumiaji wengine wa uwanja wa ndege wa Dar na kuleta usumbufu kwa waongoza ndege.”

Ndivyo alivyoandika msomaji wangu huyo katika sms yake kwangu. Kwa hakika, hakuishia hapo tu; bali alitoa pia mfano mwingine wa matumizi mabaya ya madaraka ya ofisa huyo wa jeshi ambapo aliwahi kuamuru helkopta ya jeshi (JWTZ) imsafirishe kutoka Dar hadi Kibaha Msangani ili kumpelekea zawadi bosi mwenziwe jeshini ambaye ni rafiki yake!

Hebu fikiria mpenzi msomaji: Ofisa wa jeshi amepewa na serikali gari la kifahari aina ya Landcruiser VX (Shangingi) ili alitumie kwa safari zake, na bado anaona hiyo haitoshi, na badala yake analazimisha kusafirishwa kwa ndege ya jeshi au helkopta ya jeshi hata kwa umbali mfupi wa Dar – Kibaha! Utaliitaje hili kama sio matumizi mabaya ya madaraka ambayo asili yake ni kutamalaki kwa ufisadi nchini?

Hivi kama pesa za umma za mafuta ya ndege yaliyotumika kumrusha afande yule toka Ngerengere hadi Dar na yale ya helkopta aliyoitumia kupeleka zawadi Kibaha zingeokolewa, zingeweza kutumika kutatua matatizo mangapi nchini hata ndani ya jeshi lenyewe? Nadhani ni mengi, hasa katika kipindi hiki ambacho serikali yenyewe inalia ukata.

Na hapo tumezungumzia safari mbili tu; maana yawezekana katika kipindi cha mwaka mmoja afande huyo hufanya safari nyingi za kifahari za namna hiyo. Isitoshe, huo ni mfano wa afande mmoja tu. Yawezekana pia kwamba wapo wengi wa sampuli yake ndani ya jeshi letu.

Ndugu zangu, ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba tumetumbukia katika tope la ufisadi kiasi kwamba hata vyombo vyetu nyeti kama vile JWTZ, Usalama wa Taifa na Polisi navyo havijasalimika. Katika hali kama hiyo, ni nani atatuvuta tutoke katika tope hilo kama sote (na asasi zetu nyeti) tumetumbukia?

Ndiyo maana nilikuwa (binafsi) nausubiri kwa hamu kubwa mwezi Machi (2011); maana ndiyo mwezi ambao Rais Kikwete aliwaahidi Watanzania kwamba ataongoza mabadiliko makubwa ya kukisuka upya chama tawala CCM ikiwa ni pamoja na kuwatosa baadhi ya wanachama na viongozi wake waliokichafua kwa kuhusishwa na ufisadi; jambo lililofanya chama hicho kichukiwe na mamilioni ya Watanzania.

Niliusubiri kwa hamu mwezi huu kwa sababu, kama nilivyopata kueleza huko nyuma, siamini kwamba Rais wetu ana ubavu wa kupambana na mafisadi papa ndani ya chama hicho ambao si tu wamekifanya kichukiwe na wananchi, lakini pia wamekuwa chanzo kikuu cha mtikisiko wa serikali yake.

Imani yangu hiyo kwamba Kikwete hana ubavu wa kupambananao au kuwatosa ilizidi kuimarishwa na tukio lile la Bungeni la hivi karibuni ambapo baadhi yao walifanikiwa kutwaa uongozi wa kamati nyeti za bunge.

Nina hakika “ushindi” wao wa kishindo wa Dodoma wa hivi karibuni (uliotokana na wabunge wa CCM) ulilenga katika kutuma ujumbe mahususi kwa Kikwete kwamba “hawawezi”, na kwamba licha ya yote yanayozungumzwa juu yao, bado wataendelea kuwa na nguvu kubwa ndani ya chama tawala CCM.

Tafakari.

Barua-pepe:
RAIA MWEMA

No comments: