Thursday, March 17, 2011

MADAI YA UCHOCHEZI NA MASALIO YA FIKRA ZA KIKOLONI NDANI YA WATAWALA NA WATAWALIWA


M.M Mwanakijiji

WATAWALA wanadai maandamano yaliyokuwa yakifanywa na CHADEMA huko Kanda ya Ziwa kuwa ni ‘uchochezi’ na yana lengo la kupandikiza ‘chuki dhidi ya serikali’ na walitaka yakomeshwe mara moja.Wengine wakitumia kisingizio hicho hicho cha ‘uchochezi’ walifika mahali pa kudai kuwa kinachofanywa ni ‘uhaini wa wazi’ na mmoja wao akiwa anayumba yumba kwa ugimbi wa madaraka akadai kuwa angeweza hata kukisimamisha chama hicho na akatishia kuwa kinaweza kufutwa.

Wote hawa wanaamini kabisa kuwa kinachofanyika ni ‘uchochezi’ na hivyo wamebakia kuwatisha wananchi kuhusu masuala ya umwagikaji damu, vita, vurugu n.k kwa sababu tu hoja zinazopelekwa kwa wananchi zinaweza kuwafanya wananchi waichukie serikali yao. Hili kwao ni uchochezi.

Fikra hizi za kuogopa wananchi kwamba wanaweza kuichukia serikali iliyoko madarakani hazikuanzishwa na kina Tendwa, Pinda, Chiligati au Kikwete mwenyewe.

Hawa wamekutana tu na hofu hii kwa sababu ya nafasi zao za kihistoria. Watawala kuogopa wananchi wao haikuanza leo katika nchi yetu na katika eneo letu la Afrika ya Mashariki na kwa kweli katika jamii zote ambazo zimewahi kutawaliwa.

Utawala wa Mwingereza uliochukua eneo la Tanganyika toka kwa Mjerumani (kufuatia kushindwa kwake kwenye vita ya kwanza ya dunia) ulianza toka mwanzo kabisa kudhibiti habari na uhuru wa maoni kwenye eneo hili. Gazeti la kwanza huru katika Tanganyika la Tanga Post and East Coast Advertiser lilimwa barua ya kutaka uchapishaji wake upitiwe na mpitiaji wa serikali. Hiyo ilikuwa ni 1919.

Japo hakukuwa na sheria ya magazeti moja kwa moja lakini kulikuwa na kifungu katika Sheria ya Kanuni za Adhabu ya 1920 Kifungu cha 63 ambayo iliweka wazi kuwa ilikuwa ni kosa kuchapisha habari ya uongo ambayo ingeweza kusababisha hofu kwa jamii.

Kulikuwa na vifungu pia vilivyozuia uingizwaji wa machapisho nchini (vitabu n.k) ambavyo vingekuwa ni kinyume na masilahi ya umma. Sheria hizo zilionekana kuwa hazikutosha kuhakikisha hakuna upinzani au ukosoaji mkali wa serikali au maneno ambayo yangeonekana kuwachukiza watu. Katika kitabu chake cha Historia ya Vyombo vya Habari vya Tanzania (The Media History of Tanzania) cha mwaka 1998 kilichochapishwa na Ndanda Press mwandishi Martin Sturmer anasema kuwa “punde ilionekana kwa serikali (ya kikoloni) kuwa vyombo huru vya habari vya wakazi wenyewe vilihatarisha maslahi yake”.

Sturmer anatusimulia kuwa mwaka 1928 ilipitishwa sheria ya magazeti namba 22 ambayo ilikuwa na lengo la kusimamia uchapishwaji na ufanyaji kazi wa magazeti katika Tanganyika. Baadhi ya watu wa kwanza kuona makali ya sheria hiyo ni kijarida cha Al Muslim ambacho muanzilishi wake alishindwa kuweka dhamana ya kiasi cha fedha na kujikuta anashindwa kuchapisha. Mchapishaji huyo alitaka kuanzisha kijarida hicho ili kiwe sauti ya Waislamu na kiweze kuwa na mtazamo tofauti kulinganisha na machapisho yaliyotolewa na Wahindu. Hata hivyo mchapishaji wa gazeti la The Ismaili Voice hakutakiwa kuweka dhamana yoyote miaka minne baadaye licha ya kuwa naye alikuwa anataka kuchapisha gazeti la kila wiki.

Sababu kubwa ambayo ilisababisha tofauti hiyo (kati ya gazeti la Al Muslim na The Ismaili Voice) ni kuwa serikali ilikuwa na uvumilivu mkubwa kwa magazeti ambayo yanaonyesha kuandika mazuri ya serikali (ya kikoloni) kuliko yaliyokuwa yakiandika habari ambazo zilionekana kuionyesha serikali hiyo katika mwanga mbaya.

Mwaka 1955 yakafanyika mabadiliko katika kile kifungu cha 63 cha sheria ile ya Kanuni za Adhabu na hapo kwa mara ya kwanza yakiangizwa kwa uwazi kabisa mambo yanayohusiana na uchochezi.

Tukumbuke haya yalifanywa na utawala wa kikoloni na siyo wa Nyerere! Kipengele cha 63B kikafanya kuwa ni kosa “kuandika, kuchapisha au kutoa kauli” ambayo ingeweza kusababisha vurugu, chuki na hata hisia mbaya kati ya jamii za watu. Na hapo ndipo suala la sheria za uchochezi zilipoanza kujitokeza sana na sana.

Wa kwanza kukiona cha moto kwa kuandika habari ambayo watawala wa wakati huo (wakoloni) waliona kuwa ni ya “kichochezi” lilikuwa ni gazeti maarufu la Mwafrika. Wahariri wake, Kheri Rashid na Robert Makange, walishitakiwa kwa uchochezi hasa baada ya gazeti lao kuandika maneno yafuatayo:

Sisi wote tunajua kuwa Mwingereza yupo hapa kwetu kwa sababu ya kutunyonya damu na kujipatia manufaa yake mwenyewe, na wala asitudanganye kwamba yupo hapa kwakuwa anatuonea huruma na kutaka kutufundisha ustaarabu au kuleta maendeleo ya nchi. Maneno haya ni kigeugeu cha kutaka kutufunika macho; na kwa kadri atakavyo zidi kuwa hapa ndivyo madini na fedha zitakavyo zidi kutolewa katika nchi hii 75 kupelekwa kwao, ambako bila ya sisi hawawezi kuishi sawasawa (Toleo la 19 Juni 1, 1958, Uk. 5).

Ninapoyasoma maneno hayo mwili wangu unanisisimka kwani miaka zaidi ya hamsini baadaye baadhi ya hisia za Watanzania zinarandana na kukumbatiana na hisia za wazee wetu hawa. Labda ambacho mtu anaweza asiwe amekiona ni kuwa hawa wahariri mmoja alikuwa ni Mkristu na mwingine Muislamu na wote wawili waliupinga utawala ambao waliuona kuwa hauna maslahi kwa watu wetu. Hawakukubali kugawanywa kwa misingi ya dini, mahali, au ukabila.

Kwa ufupi, wazee hao walihukumiwa kifungo cha miezi sita jela kwa uchochezi. Hii ilikuwa ni kabla ya utawala wa Nyerere. Hata Mhariri aliyewafuata, Joel Mgogo, naye alijikuta anashtakiwa kwa uchochezi vile vile na kulipa faini.

Mojawapo ya wahanga wengine wa sheria hizi za kuzuia uchochezi hakuwa mwingine isipokuwa Baba wa Taifa wa ukweli mwenyewe Mwl. Julius Nyerere (kiongozi wetu mmoja siku hizi anamuita Mzee Nyerere, wakati mwingine anamuita kiongozi wa leo Baba wa Taifa- go figure!). Nyerere licha ya kuwa alikuwa ni kiongozi wa TANU (Mwenyekiti) alikuwa pia ni Mhariri wa gazeti la “Sauti ya TANU” na alijikuta wakati mmoja anaingia kwenye matatizo pale alipoandika kwenye gazeti hilo kauli ifuatayo ambayo watawala wa kikoloni waliiona kuwa ni ya kichochezi:


Maafisa hawa hawa ambao wako tayari watu waseme uongo mahakamani ili kuikomoa TANU; maafisa hawahawa ambao wanatishia na kuadhibu wasio na hatia; wanaotukuza na kuzawadia ulaghai eti wana ujasiri wa kudai utawala wa sheria. Eh Mwenyezi Mungu utuepushe na kufuru hii isiyo kifani. Utawala wa sheria ni kitu kitakatifu. Wale wenye kuheshimu utawala wa sheria ndio wakiitie…Sababu pekee hawa wendawazimu wanajitahidi kuwachokoza watu wafanye vurugu ni ukweli kwamba hawawezi kutugusa kama tukibakia tunafuata sheria (Toleo la 29, Sauti ya Tanu Mei 27 1958).

Tafrisi ya kutoka Kiingereza kuja Kiswahili ya kwangu lakini inaondoa utamu wa lugha ya Kiingereza ilivyotumika. Naomba niweke kauli hiyo katika Kiingereza kwani najua nina uhakika sijatendea haki kilichosema:

These same officials who would have the people commit perjury in court if only to help them to vilify TANU; these same people who intimidate and punish innocence, cajole and reward crookery have the temerity to invoke law and order. Lord Almighty deliver us from this vile blasphemy. Law and order is a sacred thing. Let only the law-abiding invoke it. (...) The reason why lunatics have been trying to provoke the people into violence is the fact that they know we are virtually invincible if we remain a law-abiding Organization.

Nyerere alikutwa na hatia ya kufanya uchochezi dhidi ya maafisa wa serikali kinyume cha sheria. Alihukumiwa naye miezi sita jela au kulipa faini. Nyerere alikubali kulipa faini na kama ambavyo inanukuliwa sehemu mbalimbali ilikuwa ni vigumu kuchagua kwenda jela au kulipa faini kwani ulikuwa ni mwaka wa uchaguzi vile vile. Baada ya kuzaliwa kwa taifa jipya la Tanganyika Nyerere alijikuta anakabiliwa na changamoto kubwa ya uhuru wa habari na maoni na utawala wa serikali yake. Je, katika miaka hiyo michanga ya mwanzo ya taifa, ni vyema kuacha vyombo vya habari viwe huru kuliko wakati wa mkoloni? Yaani, viwe huru kukosoa uongozi na watendaji mbalimbali.

Nyerere aliona kuwa kuachia vyombo vya habari kuwa huru kiasi hicho lilikuwa ni kosa katika “miaka hii muhimu” ya mwanzo wa taifa. Kazi kubwa ilikuja baada ya Uasi wa Jeshi, Muungano na baadaye kutangazwa kwa Azimio la Arusha. Mabadiliko ya kisiasa yalitoa changamoto kubwa kwa nchi kwenye suala la vyomo vya habari. Hata gazeti la “The Standard” lilipotaifishwa ilibidi mhariri wake ahakikishiwe mapema kabisa kuwa vyombo vya serikali havitaliingilia katika utendaji wake na mhariri huyo mpya alitaka Nyerere mwenyewe atoe uhakikisho huo hadharani badala ya kumuhamikikishai katika mazungumzo ya wao wawili.

Siku lilipotaifishwa Nyerere aliandika tahariri ndefu kidogo akihakikishia uhuru wa gazeti hilo na kile ambacho kilikuja kuonekana kama ni uhuru wa magazeti mengine yote nchini. Hilo hata hivyo halikuwa kweli kabisa kwani pamoja na kuwa Nyerere mwenyewe alikuwa ni mhanga wa sheria za kikoloni lakini alikubali kuendelea nazo. Hata baada ya mgogoro wa Kambona ilikuwa wazi kwake kuwa nchi isingeweza kutawalika vizuri chini ya uhuru usio na mipaka wa vyombo vya habari na matokeo yake akakumbatia wazo kuwa vyombo vya habari vinahitaji kudhibitiwa na maoni kuangaliwa kama yanahatarisha masilahi ya umma.

Hivyo, mwaka 1968 yakafanyiwa mabadiliko ya ile sheria ya magazeti ya 1928 ya kikoloni ambapo sasa ilimpa madaraka rais ya kusitisha gazeti lolote ambalo lilionekana kuandika vitu ambavyo vilikuwa kinyume na masilahi ya taifa.

Mwaka 1970 Sheria ya Usalama waTaifa ikapitishwa ambayo pamoja na mambo mengine ikawabana waandishi kuandika habari za mambo ya usalama na ulinzi habari ambazo zingeweza kuwa za manufaa kwa adui.

Mabadiliko hayo yakasababisha Mhariri wa gazeti la Kikatoliki la Kiongozi kukamatwa kwa kuandika habari za mabinti waliokuwa wakipata uja uzito katika kambi za JKT.

Hitimisho la hayo yote (katika historia hii fupi niliyosimulia) ni kuwa hatimaye mwaka 1976 ilipitishwa sheria mpya ambayo iliunganisha Sheria ya Magazeti ya 1928 na vifungu vya kanuni ya adhabu na hivyo kuweka mahali pamoja vifungu vikali kabisa vya kuzuia maoni.

Kimsingi tulichukua hofu za mtawala mkoloni tukazikumbatia na kuziweka kuwa hofu za mtawala mwananchi. Lakini sisi tukaenda mbali zaidi kwa kumpa rais na waziri madaraka makubwa sana kuhusu uhuru wa maoni. Si tu kuwa tulitengenezewa sheria mbovu kabisa ya kusimamia utendaji wa vyombo vya habari lakini vile vile tulifanya kuwa ni vigumu kabisa kutafuta haki mahakamani kwa mtu au chombo kinachoonekana kimekosewa.

Ndiyo maana leo hii Waziri anaweza kulifungia gazeti kwa muda au daima bila gazeti hilo kuweza kutafuta unafuu mahakamani. Tukaweka madaraka makubwa kwa chombo cha kusimamia usajili wa magazeti n.k Na ndio ndani ya sheria hii vifungu vinavyotajwa tajwa kuhusu “uchochezi” vimejificha na vinatisha kweli!

Ni kwa sababu hiyo Tume ya Nyalali ilipendekeza kuwa Sheria hiyo ya Magazeti ibadilishwe/ifutwe kwani ilikuwa inakinzana na Ibara ya 18 ya Katiba ya Muungano iliyotambua uhuru wa maoni wa wananchi.

Tume yake ilitoa mapendekezo mengine ikiwemo kuundwa kwa baraza la habari. Baraza la Habari limeundwa lakini sheria ya magazeti ipo na ndiyo inayotumiwa na kina Kikwete, Chiligati, Tendwa na wengine kuwatishia Watanzania! Hivyo leo hii tunapowasikia watawala wetu wanaanza kulia “uchochezi uchochezi” sisi wengine tunakumbuka tulikotoka. Watawala wetu wa leo hii wanataka watawale kwa raha mustarehe.

Hawataki wasumbuliwe kwa maandamano, kwa hoja, na kwa maandishi. Wanajua wanayo silaha mikononi mwao na sitoshangaa kuwa wako tayari kuitumia kwani wameshaitumia mara kadhaa.

Ndugu zangu, tulichonacho katika sheria zetu ni masalio ya ukoloni. Lakini siyo tu ni masalio ya ukoloni katika sheria zetu bali kuna masalio ya ukoloni katika fikra zetu. Ninapowaangalia na kuwasikiliza watu wazima ambao wanajua historia yetu wanaposimama na kudai ati maandamano ya CHADEMA “ni uchochezi” ninashangaa.

Ninashangaa na kutatizwa na fikra hizo. Kwani hakuna jukumu la kisheria au la kikatiba na kwa hakika hakuna jukumu la kidhamira la kutaka watu waseme maneno mazuri na kuipamba serikali. Hakuna matakwa ya kikatiba ambayo Mtanzania anatakiwa kuipenda serikali yake hata ikifanya madudu.

Tukiwakubalia hawa wanaotaka tusisababishe hisia mbaya au chuki dhidi ya uongozi mbovu ina maana wanatutaka tuwe wanafiki wa dhamira zetu. Kwamba, wao washindwe kushughulikia tatizo la nishati nchini na sisi tukae kimya tusinung’unike wala kujisikia vibaya! Kwamba taifa zima lichezewe akili na kina Rostam na Al Adawi na Watanzania wote ndani na nje ya Tanzania tubaki tunakenua meno tusikasirike au kuwa na hisia mbaya dhidi ya watendaji walioshindwa kuwashughulikia watu hawa.

Tukikubali kuwa wananchi kukasirika, kukerwa, kupinga na kuwakataa viongozi na utawala mbovu kama ule uliokataliwa na kina Nyerere, Rashid na Makange ni kosa la jinai, na kuwa ni uchochezi ambao watawala walioshindwa sasa wanataka kutumia nguvu ya sheria mbovu; basi wengi tutakuwa na hatia na wengine tunakiri tuna hatia!

Tuko tayari kulipa gharama yoyote na wengine tayari tunalipa gharama ya kukataa kuwa kasuku wa uongozi uliolifikisha taifa letu katika kona ya kukata tamaa, na kutulazimisha kupiga magoti kwenye mawe ya ufisadi.

Kinachofanywa na CHADEMA siyo uchochezi na hakiwezi kuwa uchochezi hata kama Kamati Kuu ya CCM na Jeshi zima la Tanzania litaita hivyo. Kinachofanywa ni kuliamsha Taifa na kuwaamsha Watanzania ili watambue kuwa matatizo yao yanahusiana moja kwa moja na serikali iliyoko madarakani, naam yanahusiana na utekelezwaji wa sera mbovu zilizoshindwa za Chama Cha Mapinduzi.

Kinyume na watetezi wa serikali hii ambao wanafikiri suala hili ni la dini, kabila au udugu ukweli utabakia kuwa ukweli kwamba uongozi mbovu na sera mbovu zinahitaji kupingwa si kupepewa kama mtu aliyepandisha maruhani ambaye anaulizwa swali yeye “kiti anataka nini”.

Wanaotaka kutetea yanayofanywa na viongozi wabovu ana haki hiyo! Anayetaka kutuambia Dowans ndio mwokozi anayo haki hiyo; anayetaka kusema kuwa kinachoendelea Tanzania siyo ufisadi kweli bali ni chuki dhidi ya kiongozi Mwislamu au kuendelezwa kwa mfumo “Kristu” ana haki hiyo. Anayetaka kutafuta udhuru wa matatizo yetu bila kuhusisha CCM na sera zake afanye hivyo.

Lakini, wanapofanya hivyo wasifikiri wanaondoa haki yetu kuwapinga. Na sisi tuna haki na tuna wajibu kwa dhamira zetu (kama wao walivyo kwa za kwao) kukataa uongo, kubeza ubovu, kufichua ulaghai wa kisiasa na kwa hakika tunao wajibu wa Kikatiba kabisa kuwafahamisha wananchi ubovu wa seriakali na ugoigoi wa viongozi wao. Huu si uchochezi, si uchokozi, bali ni uelezi unaohitaji pongezi!

Uchochezi wa kweli unafanywa na wanasiasa walioliingiza taifa letu kwenye mikataba mibovu, unafanywa na watendaji ambao wameshindwa kuwawajibisha viongozi wazembe, unafanywa na vyombo vya usalama ambavyo vimekaa pembeni huku ulaghai unahubiriwa hadharani kama imani, na unafanywa na wale wote ambao kutokana na nafasi zao wameshindwa kuongoza kwa hekima na uthubutu na kusababisha wananchi wawachukie.

Inashangaza kinachoonekana ni hofu ya watawala dhidi ya taifa la wananchi walioamka. Wanaogopa kwamba Watanzania Wakristu na Waislamu kama wazazi wao miaka zaidi ya hamsini iliyopita wataunganika pamoja kuwapinga watawala. Wanaogopa kuona vijana wa Kiislamu na wa Kikristu, Wahindu na wenye imani za jadi watakaposimama pamoja kama wale wa kule Misri kupinga uongozi wa muda mrefu uliojikita madarakani. Hili linawatisha kama nini.

Bahati nzuri kampeni ya CHADEMA na ya wanaharakati wengine imezidi kuwauanganisha vijana hao na vijana hao kama wenzao sehemu nyingine duniani wamezidi kutambua kuwa maisha yao yanaathiriwa na uongozi ulio madarakani bila kujali dini, matabaka, rangi au makabila yao. Kwani vijana hao wanajiuliza kwani mabomu ya Gongo la Mboto yaliwaangukia Waislamu peke yao? Kwani mabomu ya Mbagala yalitua kwenye nyumba za Wakristu peke yao?

Je, kipindupindu kikija Temeke kitaanza kuchagua nyumba ya Mchagga na Mzaramo? Je, mvua ikinya Dar na mafurikko uchwara yanapotokea ubovu huo unaonekana kwa macho ya wasomi tu na wale ambao si wasomi wanaona “bongo tambarare”?

Watanzania wameamshwa na sasa hata madai ya udini yanaanza kupotea kwani hata Hosni Mubarak alijaribu gia hiyo lakini Wamisri hawakudanganyika. Sasa hivi, CCM imejaribu suala la ukabila, sasa iko kwenye suala la udini, na hili kwa vile linaanza kutoweka kwa sababu watu wamekubali mabadiliko zaidi wameamua kuanza kutumia madai ya “uchochezi”.

Ndugu zangu, hata hilo nalo litafikia mwisho. Na wakati umefika wa kuzifuta mbali sheria hizo ambazo nimezizungumzia kwani ni kinyume na jamii inayotaka kujenga demokrasia ya kweli.

Wenzetu Uganda mahakama imefutulia mbali sheria za namna hiyo (ambazo zilikuwa zinafanana na za kwetu); Wamarekani wenyewe waliwahi kuwa na sheria kama hiyo ya mwaka 1918 lakini waliifuta miaka miwili baadaye. New Zealand walikuwa na vifungu hivyo vya uchochezi lakini walivifuta mwaka 2007; Uingereza ilikuwa na sheria hizo na mwaka 2009 hatimaye ilifutilia mbali (isipokuwa inapohusisha wahamiaji); na nchi nyingine zimefanyia mabadiliko sheria zao ili kuweza kuzifanya ziandane na mawazo mamboleo juu ya suala la demokrasia na haki za raia.

Ninachotaka kusema kwa kifupi ni kuwa hakuna uchochezi na kama hakuna uchochezi hakuna uhaini kwani uhaini ni kusimama kinyume cha taifa lako na kutaka kuliangamiza. Ukiniuliza mimi, mafisadi ndio wahaini wa kwanza kabisa. Cha kushangaza si Tendwa wala Chiligati mwenye ujasiri wa kuwaita mafisadi wahaini. – go figure!

No comments: