Tuesday, March 1, 2011

KONA YA UCHOCHEZI: NAWAOMBA WATANZANIA WAHIFADHI UCHOCHEZI HUU

Mohamed Bouazizi enzi za uhai wake

Mohamed Bouazizi ni chanzo cha serikali ya Tunisia kuangushwa.
Ukitaka kumjua zaidi kijana huyu ni kwamba alikuwa ni Mmachinga, aliyefanya biashara zake maeneo yaliyokatazwa na serikali. Kama ilivyo hapa kwetu Tanzania.

Bouazizi alikuwa muuza matunda, ‘kikaragosi,’ mtu ambaye serikali haikumjali hata kwa kumpa pole tu ya shida zilizomsonga kwenye maisha yake.

Wengi tunajua, Bouazizi aliamua kujilipua, akakubali kuwa kondoo wa sadaka ya kuteketezwa, iliyopokelewa vizuri na Mungu na kusababisha machafuko nchi nzima hadi utawala uliompuuza ulipong’oka madarakani.

Mazingira yalimuondoa Rais Zine al-Abidine Ben Ali wa Tunisia madarakani nayaona kwa Rais Jakaya Kikwete na serikali yake.

Tanzania anayoiongoza ina akina Bouazizi wengi ambao shida zao zinapuuzwa uso mkavu na serikali ya CCM.
Akina Bouazizi wa Bongo wanalia na ugumu wa maisha, huduma duni za jamii, mfumuko wa bei, ukosefu wa ajira, rushwa, ufisadi na unyanyasaji wa vyombo vya dola vinavyojaribu kwa makusudi kuzima harakati za wanyonge kujikomboa.

Kama ilivyokuwa kwa Rais wa Tunisia, ndivyo ilivyo kwa Kikwete, Ben Ali alikaa Ikulu kimya akiamini Bouazizi hawezi kuleta madhara. Kikwete naye katulia wakati wanyonge wanalia.

Serikali ya Kikwete inafahamu kabisa akina Bouazizi wa Bongo wanaumia na mgao na gharama kubwa ya umeme. Wananchi walalahoi sasa wananunua uniti 8 za nishati hiyo kwa shilingi elfu tano. Mawaziri wenye dhamana wako kimya, wanakula na kulala. Wameridhika na hali hii.

Pengine kuridhika huko ndiko kunakowafanya viongozi wetu waone fahari kutembelea mashangingi na baadhi yao waendelee kuwanyonya wanyonge kwa kuishi kwenye hoteli za kifahari kwa kisingizio cha kukosa nyumba za kuishi ambazo zilikuwepo na kuuzwa kwa bei poa na hao hao wakubwa.

Ya Tunisia hayatofautiani na ya Tanzania, ndiyo maana nimesema serikali ya Kikwete inaweza kuaangushwa na Mohamed Bouazizi kwa mfumo ule ule.

Ikiwa nitaitwa mchochezi au jina lolote ambalo wataona linanifaa sitishiki, lakini ni lazima niseme kuwa mwenendo ambao serikali ya awamu nne inakwenda nao hautaiacha salama.

Msingi wa kudharau vilio vya wanyonge na viongozi kujijengea heshima kwenye jamii inayoteseka na ugumu wa maisha, utaiangusha serikali ya CCM.

Nikitazama Watanzania wanavyohangaikia kula yao ya siku, wanavyodhulumiwa haki zao, wanavyosotea ajira, wanavyobaguliwa katika huduma za jamii na tofauti kubwa ya kimaisha kati ya masikini na tajiri wa nchi hii, namhurumia Kikwete.

Binafsi najiuliza, wananchi wapatwe na dhiki gani nyingine zaidi ya hizi walizonazo ili serikali yao iwajibike ipasavyo na viongozi wao waoneshe kujali?
Serikali inajua elimu bora ni kwa wenye uwezo, tiba nzuri ni gharama, chakula kinahitaji fedha nyingi, haki inanunuliwa na hata heshima pia. Katika mazingia haya Bouazizi atasaidiaje?

Nikitolea mfano, sura ya elimu kwa fedha imejionesha mwaka huu. Waliofaulu vizuri kidato cha nne ni wanafunzi waliokuwa wakisoma sekondari za gharama kubwa, lakini watoto wa akina Bouazizi wameambulia 0 za kumwaga na sasa wamerudi makwao wakiwa wamekata tamaa ya maisha. Hawa ni akina Bouazizi.

Umeme ambao unatumika kurahisisha maisha ya wanyonge kwa akina mama kujiuzia barafu na vinywaji baridi nao hauwezekani siku hizi. Gesi imepanda, mkaa haununuliki, yote haya ni mateso kwa walalahoi.

Kama mchochezi nilitegemea kuona viongozi wetu wakionesha kujali shida za wananchi kwa kufanya kila liwezekanalo kuyapatia ufumbuzi matatizo ya jamii ya kila siku; lakini wapiii?

Tatizo la umeme limeanza kuwa sugu tangu utawala wa Rais Benjamin Mkapa. Toka wakati huo wananchi wanaimbishwa ngojera tu, matokeo yake yamejitokeza madudu ya Dowans na malipo ya shilingi bilioni 94,tulipe na mtambo ung’oke.

Wazee wa Ikulu wapo na mambo yanakwenda kwa kula kuku kwa mrija, uswahilini giza. Akina Bouazizi wa Kariakoo wanapigwa virungu na kudhulumiwa nyanya wanazopanga barabarani. Mmm!

Nitaonekana nachochea nikisema akina Bouazizi wa Bongo wamebaki kidogo wajilipue na hali ya nchi iwe tete? Acha ionekane hivyo, lakini kwa ukimya huu wa watawala wetu unaofumbia macho matatizo ya msingi ya wananchi, nawajibika kuandika haya.

Maana katika maisha yangu, sijawahi kusikia watu wakilalamikia maisha magumu kama wakati huu. Ikiwa Rais Kikwete anaambiwa na wasaidizi wake kwamba mambo uswahilini ni shwari na wananchi wanafurahia uongozi wake anadanganywa kwa kiasi kikubwa.

Nimelazimika kurudia makala haya kwa sababu nashuhudiwa kutoka moyoni kwamba hali ya nchi yetu ni tete na wakati wa unabii wangu kutimia umesogea naomba kuhifadhi maandishi haya kwenye kumbukumbu.


GLOBAL PUBLISHERS

No comments: