Thursday, March 17, 2011

KAULI YA MCHUNGAJI HATIMAYE YATIMIAKAULI iliyotolewa na Mchungaji Ambilikile Mwasapile kwamba tiba ya magonjwa sugu ya kansa, kisukari, pumu na Ukimwi anayotoa katika Kijiji cha Samunge, Tarafa ya Sale, Loliondo itawavuta watu kutoka kila pembe ya dunia imeanza kutimia na kuitisha Serikali.

Akizungumza na Mwananchi jana, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Raymund Mushi alisema kauli hiyo imeanza kuonyesha dalili za kutimia na ikiwa hivyo hali itakuwa ngumu.

"Tumeanza kuona watu kutoka Afrika Kusini wanafika Loliondo, kuna wengine wa nchi nyingine tunasikia wanakuja... sasa kama kweli hali hii itatokea kutakuwa na haja ya kuweka mazingira mazuri ya kufika katika Kijiji cha Samunge," alisema Mushi.Alisema kama watu wa mataifa mbalimbali watafika Samunge ni faraja katika uchumi wa Tanzania kwani wataingiza fedha za kigeni na kuitangaza.

"Jambo hili linaonekana kuendelea kuvutia wengi na watu wa mataifa mbalimbali wakifika nchini ni faraja kiuchumi lakini pia ni muhimu kujiandaa kuwapokea," alisema Mushi.Mchungaji Mwasapile aliwahi kukaririwa akisema kwamba itafika wakati mtu kupata kikombe cha tiba anayoitoa itamchukua mwezi mzima akiwa Samunge.
Mchungaji Mwasapile alisema watu wa mataifa mbalimbali watakuja Tanzania na kumfuata huko, akisema Mungu amemwonyesha ujio wa watu hao, jambo ambalo litahitaji maandalizi.

Hivi sasa changamoto kubwa inayotatiza upatikanaji wa tiba hiyo ni barabara ya kufika Samunge ambayo ni mbovu na mawasiliano ya simu.Barabara inayotumiwa na magari mengi kutoka eneo la Kigongoni wilayani Monduli, kupitia maeneo ya Selela, Engaruka hadi kufika katika kijiji hicho ni mbaya kiasi cha kusababisha magari mengi kukwama.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Samunge, Michael Lengume alisema kijiji hicho chenye Kaya zinazofikia 500, tayari kimeanza kujiandaa kupokea maelfu ya watu kwa kutenga maeneo ya maegesho ya magari, malazi na huduma nyingine muhimu.Kwa takriban mwezi mmoja sasa habari za Mchungaji Mwasapile kutibu magonjwa sugu zimesambaa maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi, hali ambayo imewavutia maelfu ya watu kufunga safari kwenda huko.

Wabunge wachangamkia kupeleka wapigakura
Baadhi ya wabunge na wanasiasa wamejitokeza kuwapeleka wapigakura wao huko Samunge kupata tiba hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Tarime (CCM), mkoani Mara, Nyambari Nyangwine amejitolea kugharamia wananchi 200 wa jimbo lake ambao wanataka kwenda kupata matibabu huko.

Nyambari aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa wananchi wa jimbo lake wanaotaka kwenda huko wajiorodheshe katika ofisi yake wilayani hapo. "Nimeamua kuwapeleka baadhi ya wapigakura wangu ambao wanajisikia kuumwa kupata tiba kwa Babu kama shukurani zangu kwao... "alisema.

Mbunge wa Rorya (CCM), Lameck Airo alisema hadi sasa watu zaidi ya 150 wamejiorodhesha tayari kwa safari ya Loliondo kupata kikombe kutoka kwa Mchungaji Ambilikile.Mwingine ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Vedastus Mathayo Manyinyi ambaye amewasafirisha watu 130 kutoka Musoma kwenda Loliondo. Mkoani Arusha, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amejitolea kusafirisha wagonjwa 100 kutoka katika jimbo kwenda Loliondo.

Akizungumza na mamia ya wakazi wa jimbo hilo ambao walifika kujiandikisha kwa ajili ya safari ya kuelekea Loliondo jana nje ya ofisi yake, alisema ameguswa na afya za wakazi wa Jimbo la Arusha na kuamua kuingia gharama za kuwasafirisha kwa awamu.“Nimeguswa na afya zenu na kwa kuanzia, nimejitolea gharama zangu binafsi kuwapeleka wagonjwa 100 Loliondo ili wakapatiwe matibabu,” alisema Lema.

Habari hii imeandaliwa na Samson Chacha, Tarime, Moses Mashalla Mussa Juma, Arusha na Shija Felician, Kahama


MWANANCHI

No comments: