Tuesday, March 15, 2011

HATUJARUDI KATIKA ZAMA ZA UTUMWA WA FIKRA TANZANIA?
Na Baraka Mfunguo


Katika tembea tembea yangu katika vyombo vya habari vya kimagharibi , nimekutana na chombo kimoja cha habari maarufu cha Marekani ambacho kimeanzisha mradi mahsusi ambao ni kwa ajili ya kupiga vita utumikishwaji wa watu isivyokuwa kihalali yaani Utumwa. Utumwa ni kitendo cha kumtumikisha binadamu pasipo hiyari na pasipo ujira binadamu anatumikishwa na kufanywa kama mnyama pasipo kuzingatia utu wake. Nchi ambazo bado inaelezwa kwamba zinaendelea na biashara ya utumwa ni Sudan. Kwa mujibu wa mtandao wa Free the Slave.net, inaelezwa kwamba binadamu anaweza akauzwa kwa kiasi kisichopungua dola 90. Katika historia ya nchi yetu tumepitia utumwa ambapo waafrika tulitembezwa kwa miguu kutoka maeneo ya ndani ya nchi yetu na kwenda mpaka pwani ya Hindi ambapo tulipigwa bei kama vile samaki wanavyouzwa kwa mnada na kupelekwa nchi za Uajemi. Wengine walipelekwa Zanzibar kulima Karafuu kwenye mashamba ya makabaila n.k. Watumwa wanaume walihasiwa wakiwa katika nchi hizo za Uajemi. Ilielezwa kwamba Mwafrika alikuwa kama nuksi fulani hakuthaminiwa, hakuwa chochote. Wadau wakubwa walikuwa Waarabu na baadhi ya madalali wa Kiafrika miongoni mwetu mmoja wao akijulikana kwa jina la Tipp Tippu. Watumwa waliswagwa kama ng'ombe wakibebeshwa pembe za ndovu pamoja na vito mbalimbali vya thamani. Waafrika waliweza kuswagwa umbali wa kutoka Kigoma kuelekea Dar es Salaam ambao wagonjwa waliuawa sambamba na wale walioonekana kuwa wadhaifu. Katika Pwani ya Afrika Magharibi Utumwa ulifanyika kwa kiasi cha miaka 400 hasa baada ya mzungu kuivumbua Amerika pamoja na mashamba ya pamba ambayo ilizalishwa kwa ajili ya viwanda vikubwa huko nchini Uingereza. Inaelezwa kwamba baada ya kuona udhaifu wa Mhindi mwekundu katika uchapaji kazi ikaamuliwa Waafrika ndio sahihi. Na wao walisafirishwa kwenye majahazi kama vile ng'ombe. Wapo waliokufa njiani, wapo waliotekwa na kuuawa na maharamia na vyombo vyao kuzamishwa baharini n.k n.k Kimsingi ilikuwa ni unyama yote hii ilifanywa na Mzungu. Baadae wakasema kwamba utumwa ni kitu kibaya kwa hiyo ni lazima kipigwe vita. Baaada ya kupata walichotaka, baada ya mapinduzi ya viwanda mtumwa akaonwa hafai. Hivi ndivyo mwafrika anavyochukuliwa na anavyofanywa. Hali hii inaendelea lakini inakwenda kwa namna nyingine kabisa hivi sasa.

Hata hivyo kuna aina mpya ya utumwa imejitokeza hivi sasa. Mojawapo ikiwa ni biashara ya kusafirisha watu. Katika biashara hii ya kusafirisha watu, watu wa mataifa yaliyoendelea kiuchumi huziendea familia maskini na kuwashawishi kwamba wanamhitaji mtoto kwa ajili ya kumsaidia kumuendeleza kimaisha na ahadi kedekede ambazo hazielezeki. Familia hushawishika na kuamua kumtoa mtoto wao ili aende ama nchi za Uingereza, Marekani ama Ujerumani kimsingi nchi zilizoendelea kiuchumi. Akifika huko hali huanza kumbadilikia kwani yule aliyemchukua na ahadi tele hugeuka dalali na kumuuza ama kumtumikisha kwa ajili ya wateja wa ngono na masuala mengine. Hali hii inaendelea na imeshika kasi kubwa sana katika mataifa yanayojiita tajiri. Hapa Tanzania upo utumwa wa kutumikisha vitoto vidogo na kuvifanya "housegirls" pamoja na sheria ya kazi kupinga utumikishwaji wa watoto mambo hayo yanafanyika dhahiri sasa hivi Dar es Salaam. Tena kuna madalali maalum ambao kazi yao ni kukutafutia na kisha wao kupata kamisheni yao. Kimsingi hapo ndipo tulipofikia. Pia yapo madanguro ya kifahari ambayo watu hufuga machangudoa kwa ajili ya watu kujifurahisha na haya yapo sehemu za kifahari ambazo wewe na mimi ukiambiwa hutaamini. Sehemu hizi zimejibatiza majina ya "Massage Parlor" kuhalalisha uharamia wao. Na wateja wao ni wewe na mimi na yule. Na yapo yale madanguro pori mfano yale ya wahaya (no offense) miaka ya 60 inaelezwa maeneo ya Kisutu yalikuwa yakisifika kwa biashara hiyo na maeneo mengine mengi ya Uswahilini, na ipo ile ya Uwanja wa fisi nk nk. Pia wapo wale ambao biashara yao ni kusafirisha watu hapa Tanzania ambao wamewapachika jina la wahamiaji haramu kutoka Somalia, Ethiopia pamoja na mataifa yaliyoathirika kivita wahamiaji hao husafirishwa kwenda Afrika ya kusini kutafuta maisha na hupakiwa kama mizigo kwenye malori makubwa. Huu ni mtandao wa watu fulani unaowapatia pesa nyingi sana na wadau wakuu wapo hapa Tanzania na tunawajua. Siku zote wakikamatwa wanaoonekana wenye kosa ni hao wahamiaji haramu lakini hatujawahi kumtafuta mchawi aliye miongoni mwetu. Kwa sababu wachawi wenyewe ni hao wanaowakamata na kutangaza kwenye vyombo vya habari baada ya kukosa mgao wao. Kimsingi tunaekea katika unyama hakuna utu ama ubinadamu tena katika mfumo huu wa ubepari.

Aina nyingine ya utumwa ambayo ndio ninaizungumzia leo ni ile ya kifikra ambayo viongozi wetu wamepandikizwa. Aina hii ya utumwa ni mbaya sana kwani ndiyo inayosababisha mambo mengi kuyumba katika nchi yetu. Hatusemi kwamba viongozi wetu hawajitahidi kwa upande wao, lakini kwa kiasi kikubwa wamefunikwa na kuzidiwa kabisa. Ni kama mtoto mdogo aliyefunikwa kwa blanketi gubigubi na akalala fofofo. Viongozi wa mataifa ya magharibi wametumia kigezo cha propaganda, mikutano mbalimbali ya kimataifa na kuwaita viongozi wetu na kuwaweka majukwaani na kutoa" lip-service" huku wakichekacheka na kuuza sura katika vyombo vya habari ilhali hali ni mbaya kiuchumi katika nchi zao, maisha magumu, urari wa usawa kati ya walionacho na wasionacho kuongezeka. Viongozi hao pia huonyeshwa katika Televisheni mbalimbali za kimagharibi huku vyombo hivyo vikiwasifia kinafiki na kuwapaka mafuta kwa mgongo wa chupa. Lakini ukweli ni kwamba viongozi hao wanakuwa wakijikaanga wenyewe. Ni wangapi wasiomfahamu Zine Abidine Ben Ali na wangapi wasiomfahamu Hosni Mubarak. Viongozi hawa waliweza kufunikwa na kusahau kabisa kinachoendelea mpaka walipokuja kuondolewa na nguvu ya umma. Hata hivyo kabla ya kuondolewa kwao waliwakimbilia wale waliowafunika kwa blanketi na kuwaomba mbeleko na kukuta jamaa wameshawageuka huo ndio unafiki wa kisiasa. Lakini wao walishatimiza malengo yao.

Utumwa wa kifikra una historia ndefu pengine tuseme kwamba utumwa huu ulianzia wakati wa ukoloni. Mkoloni alitengeneza mfumo wa elimu ambayo ulimfanya Mwafrika kumtumikia bwana mmoja tu na si mwingine mzungu. Kingine aliweza kujenga kasumba na dhana kwamba vitu vizuri vyote ni lazima vifanywe na bwana mmoja tu na si mwingine....Mzungu. Huo ndio uliokuwa mwanzo wa utumwa wa kifikra. Baada ya Uhuru na hasa pia mapinduzi ya Urusi yaliyoondoa utawala wa kifalme wa Tsar na kuzaliwa Jamhuri ya Kisovieti, mataifa ya magharibi yalikuja na mpango kabambe wa kukabiliana na Jamhuri ya kisovieti. Moja ya ajenda kuu ni kujenga Urafiki na nchi za mataifa maskini hasa ya Kiafrika, Kuwalaghai viongozi wake na kufuata mkumbo wao mfano Mobutu Sese seko Kuku Ngbendu wa Zabanga , kuanzisha klabu mbalimbali za nchi zilizotawaliwa na mkoloni husika yaani mahusiano yale hayaishi mfano Common Wealth na Francophone, Kuyatumia makampuni makubwa kwa kizungu huitwa "Multi National Corporation" Ni nani asiyejua kwamba kampuni ya Shell inahusika kwa kiasi kikubwa kwa kifo cha Ken Saro Wiwa nchini Nigeria. Matumizi ya vyombo vya habari kwa ajili ya propaganda na pia Elimu.

Mipango hii ilifikia kilele chake miaka ya 80 pale Marekani ilipoanzisha mpango wake kabambe wa "New World Order" mpango huu uliasisiwa na aliyekuwa mkurugenzi wa shirika la Ujasusi la C.I.A la Marekani na kwa wakati huo ni rais ambaye aliitwa George H. Bush. Katika mfumo huu wa New World Order, Marekani aliamua kuiteka dunia katika nyanja zote. Tukianzia masuala ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni. Hata aina ya mziki tulio nao leo hii aina ya Hip hop ni zao la Marekani la New World Order, Shilingi yetu kulinganishwa na Dola , masuala ya ulinzi shirikishi kwa Marekani kuweka Manowari zake katika pwani mbalimbali, Masuala ya dini ambapo uliibuka mfumo mpya wa Evangelism katika dini za kikristo na watu kuwa na msemo kwamba " Nimeokoka" , " Nimezaliwa upya" , "Mpendwa" nk Aina hii ya Evangelism iliasisiwa na Billy Graham kule Marekani na ndio utaratibu unaoendelea katika nchi mbalimbali hivi sasa. Siku hizi sidhani kama kuna vijana watakuwa wanamjua Andanenga Andanenga, Shaaban Robert ama waandishi wa vitabu wazuri na mashairi wazuri kama akina Mohamed Seif Khatib na wengineo wengi.

Tukielekea kwenye suala la mavazi na fasheni ndio usiseme kila kitu kinachofanyika lazima kifananie Marekani zote hizo ni dhana , Kasumba, mtazamo wa watu ulioathiriwa na utumwa wa kifikra. Inafikia wakati ukimuuliza mtu ambaye yuko kwenye fani ya filamu anataka kuja kuwa kama nani akipata mafanikio anakutajia muigizaji maarufu wa filamu kule marekani. Imefikia wakati mpaka majina unasikia "Bollywood", "Tollywood", Nollywood". Kwani kuna ubaya gani tukiita mfano "Mbekenyera", "Kinjekitile Ngware" Kuna ubaya. Unajua kasumba hii wakati fulani ilikuwa mbaya mpaka watu wanakataa majina ya baba zao. Ama jina lake la kuzaliwa unakuta mtu anaitwa Chausiku anataka aitwe " Chay" Bakari atataka aitwe "Baky ama Beka" au Jakaya atataka aitwe " Jack", "Jey Key". Mtu anaongea kiswahili lakini karibu maneno yote kwenye sentensi ameweka Kiingereza na ni kiongozi wa serikali huyo. Na hata bungeni watu wana tabia hiyo sasa sijui kuongea kwao Kiswahili na kuchanganya na Kimombo kutawafanya wao tuwaone wamesoma sana ama watafanana na wazungu.Watu wamefikia hatua mpaka wanajichubua ngozi zao ili zifanane na za wazungu, wanatengeneza nywele zao zifanane na za wazungu. Wazungu nao kwa upande mwingine wanatumia gharama kubwa kutengeneza matangazo ya biashara ya vipodozi kwa ajili ya kutupumbaza na kutufanya tujione kwamba Mungu alikosea kwa kutuumba Waafrika.Wengine wanaamini kwamba, kuolewa ama kuoa mzungu, ni kujikwamua kimaisha ingawa naamini wapo wengine wanaolewa na kuoa kwa mapenzi yao, lakini kwa asilimia nyingi ni kutafuta maisha bora. Yote hiyo ni dhana iliyojengwa na kasumba na baadaye kuzaa utumwa wa fikra. Kwa kweli tumefikia katika hali mbaya sana. Kwenye vyakula mtu anataka kula vyakula vinavyoonekana kwenye picha yaani "junk foods" Ma burger na masoda ambayo hayana rutuba yoyote mwilini. Ukimuuliza kwani ukila ugali wa dona na kipande cha nguru kwa mlenda utapata ugonjwa gani, anakuona kama wewe mtu wa kijijini kweli kweli Maendeleo ni kula chakula anachokula mzungu. Vyakula vinavyotengenezwa kiwandani na kusindikwa kwa kemikali kali. Na usione ajabu matangazo ya waganga wa jadi kuhusu matibabu ya nguvu za kiume hayaishi. Ndiyo hali tuliyoikubali.

Enzi za Mwalimu Nyerere (RIP) kulikuwa na mfumo mzuri wa elimu ya kujitegemea uliendana sanjari na maisha ya watanzania. Watanzania walijiandaa kwenda kutumikia taifa lao kwa moyo wote na kulikuwa na operesheni maalum za JKT kwa ajili ya kuwaandaa vijana kwa ajili ya taifa lao mahali popote nchini bila kujali mazingira yake. Siku hizi baada ya wazee wetu kuonjeshwa sumu ya "New World Order" wameweka mfumo kwanza wa watu kuajiriwa ofisini, kuamini kwamba Dar es Salaam ndio kwenye mambo yote na hakuna sehemu nyingine na ndio maana wamachinga hawaishi, kupelekea mifumo ya maji safi na maji taka kuharibika kutokana na mipango miji mibovu isiyoendana na ongezeko la watu mijini na wao wanasema" tutabanana hapahapa". Wabunge na wawakilishi wote makazi yao ni Dar es Salaam wanakwenda sehemu walizoomba kura baada ya miaka 5 ati akikaa kijijini anaogopa kulogwa- Huo ni utumwa wa kifikra. Asilimia karibu 50% ya bajeti ya nchi kutegemea wahisani nao ni utumwa wa kifikra. Vipi akisema leo sikupi utafanya nini? Kiongozi wa nchi analazimika kutumia karibu theluthi tatu ya utawala wake kusafiri kwenda kupeleka bakuli kuomba misaada kwa nchi wahisani. Ilhali rasilimali zetu zilizopo katika nchi yetu zinatutosha kama tukiwa makini katika utendaji wetu, tukilipa kodi tukikazania uadilifu na kuachana na anasa zisizokuwa za msingi. Mtu anaamini akitembea na Toyota Land Cruiser V8 -gari ya mamilioni atafika kwa uhakika kuliko akitembea na passat, Landrover n.k Utumwa wa Kifikra. Kuna haja gani mtu kutimiza majukumu yake ya kila siku akajitangaza kwenye kamera , blogs, TV, Vyombo vya habari na kadhalika wakati ni wajibu wake kufanya hivyo. Wanasiasa ni watu wa ajabu sana wao kwao umaarufu ni kitu kikubwa na chenye thamani na kwa kuliona hilo wanabuni kila njia na mkakati wa kununua baadhi ya waandishi wa habari ili wawaandike wao kwa ujira mkubwa. Mwanasiasa huyo hata kama angekuwa na sura mbaya na ya mkosi kama "Bundi" ataonekana malaika tu. Wanasiasa wanawafanya Watanzania kuwa watumwa wa fikra kwa kutumia vyombo vya habari kuupotosha ukweli. Wakati waandishi wanafanywa kuwa watumwa wa fikra kutokana na hali yao ya umaskini na kukosa fedha inayopelekea wao kukiuka maadili. Hii haiishii hapo ni mpaka kwenye vyombo vya habari binafsi ambavyo navyo ni lazima viandike habari vya kumtukuza bwana mkubwa aliyewaajiri na kuwalipa mshahara hata kama ukweli uko mezani dhidi ya bwana wako mwandishi ataupoteza mbele ya kadamnasi ya watu. Huo ni utumwa wa fikra! Kibaya zaidi imefikia hatua watu wanaamini kwamba ili waneemeke na maisha ni lazima wawe Wabunge hii ni dhana mpya ambayo mtu ambaye anakuwa ama alikuwa na dhamana kubwa katika shirika la umma ama kitu chochote anafanya ubadhirifu wake akijua kwamba akiba yake hiyo anakwenda kuichezea kamari kwenye siasa.Lakini hata viongozi wenyewe huwarithisha watoto wao vijukuu, vimada wao na vitukuu vyao kwa kuweka mfumo wao ndani ya Chama kimoja kilichoshikilia dola hapa nchini kwa karibu miaka 50. Wapo wanaopata na wapo wanaokosa.Lakini, niliona mfano dhahiri kwa wengine ambao baadhi nilikuwa nao wakati nikihangahikia elimu yangu pale Mlimani. Wao walishaona mbali wakawa wanajipendekeza kwa mtoto fulani wa mkubwa ambaye naye alikuwa pale anasomea sheria. Wakawa wanamlamba mpaka viatu. Matunda yake yanaonekana leo hii. Wamekuwa waheshimiwa sana wao wanaitwa VIP sasa na wengine kushikilia idara nyeti serikalini. Sina hakika sana kama huyo jamaa, ama baba yake, akitoka madarakani baada ya miaka yake 10 ya Kikatiba kuisha, hao jamaa watakuwa salama sana kisiasa. Lakini ni lazima niwape hongera zao. Dhana yangu hapa ni kuangalia jinsi utumwa wa fikra ulivyotawala katika maisha yetu.Unaweza ukawa unatembea na V8 ama Benzi unaishi katika nyumba nzuri , akaunti yenye mafedha tele, watoto wanasoma nje ya nchi , utajiri mkubwa kutokana na kodi za wananchi lakini ukweli ukabaki moyoni mwako kwamba wewe ni mbwa wa fulani na unatakiwa utekeleze matakwa ya fulani pasipo kujali vipaumbele vya nchi. Kwa kuwa hivyo unapoteza imani na heshima kwa umma wazungu hita "dignity and Intergrity". Watu wanafikiria kwamba katika maisha ni lazima upite njia ya mkato ili ufanikiwe. SI KWELI.

Lakini lingine ambalo ni baya zaidi ni kuwa mafisadi na makuwadi wa kuiuza nchi yetu pamoja na rasilimali zake. Yote hiyo imetokana na kukithiri kwa utumwa wa kifikra. Shule zetu sasa hivi za serikali ukianzia msingi,za kata na kuendelea zimegeuka kuwa mapagala ama madanguro na sehemu za vijana kuvutia bangi.Watu wamepoteza maadili, waalim na wanafunzi. Siku hizi Mwalimu haheshimiwi kwa sababu mwalimu huyo ndiyo anayefanya vitendo vya ngono na mwanafunzi wake na mambo mengine mengi ukiachana na kuwatumikisha wanafunzi kwa kuuza bajia, vitumbua Aishkrimu na visheti.Kwa sababu mfumo mbovu ulioanzia juu umeathiri mpaka ngazi za chini. Tukijaribu kuchambua kwa kifupi, mfumo wa elimu wakati wa Ujamaa, ni kwamba wakati ule kulikuwa na shule za msingi za kawaida za UPE, misheni na zile za kimataifa ambazo kwazo zipo pia mikoani.

Watoto wa makabwela na hata wa Mwalimu walisoma shule za UPE. Lakini ndani ya mfumo huo huo kulikuwa na vigogo ambao waliwapeleka watoto wao shule za kimataifa zilizopo mikoani. Tofauti iliyopo kati ya shule ya UPE na ile ya kimataifa ni kwamba huduma na vionjo vinaongezeka na kingine kilikuwa ni lugha ya kiingereza. Mtoto akijua kiingereza alikuwa anaonekana kama Mungu na wazazi hujisikia raha kweli kweli kuitwa Mummy na Daddy. Baada ya kuingia "mfumo wa ruksa" ndipo tulipoanza kuona rangi dhahiri watu walikuwa wakiwasomesha watoto wao Kenya, Uganda na wengine wenye uwezo wa juu nje ya nchi kigezo kikiwa ni lugha ya kiingereza na kujiendeleza kiujumla kuendana na hali halisi ya uchumi. Sasa tukaanza kuona utitiri wa shule, shule ambazo wengine tusingetarajia kwamba zinekuwa shule kimsingi biashara ikawa imechukua mkondo. Kwa upande mwingine zikajitokeza shule ambazo ni za kidini yaani Seminari ambazo nyingine zilikuwapo kabla ambazo zilikuwa kazi yake ni kuwaandaa vijana kuwa makasisi wa makanisani nk. Hizi zingine zikawa na ajenda tofauti kidogo, hizi ajenda yake ziliendana na misingi ya kidini na watu walipata elimu lakini walisoma na kufuata misingi ya dini pamoja na kwamba Mwalimu alihakikisha hakuna ubaguzi na watu wa dini zote waliruhusiwa kusoma lakini msingi wake ukawa ni madaraja na makundi. Naweza kuonekana mdini lakini naomba nitoe changamoto kidogo (food for thought) Uvaaji wa hijabb mashuleni unamsaidia vipi mwanafunzi kufaulu masomo yake zaidi ya kumweka katika kundi fulani? Je wakati ule watu walikuwa wakivaa Hijjab hata katika shule za serikali za umma ukiacha za seminari zilizoendeshwa kwa taasisi zilizotaka misingi yake ifuatwe? Hatuoni kwamba tunatengeneza madaraja kupitia elimu?

Dini na Elimu nayo ni utumwa mwingine wa kifikra.
Dini imewadumaza badala ya kutimiza wajibu wao kwa vitendo wanamsingizia MUNGU. Kila kitu MUNGU akipenda kiasi cha kuwafanya Watanzania kama watoto hivi. Dini zinawafanya watu wakae wamsubirie MUNGU atende miujiza badala ya kufanya kazi, wanamsubiri MUNGU ashushe utajiri wakati utajiri tumeukalia wengine wanachukua na kuambaa nao. Dini sasa hivi imekuwa biashara na viongozi wengi wa dini wanatumia mwanya wa kisaikolojia kucheza na imani za watu. Kimsingi Dini ni utumwa mkubwa wa fikra ambayo imeturudisha nyuma sana. Watu wanakosa umakini wanapoteza weledi kwa sababu ya dini na unapozungumzia dini unagusa hisia ya mtu na kwa kiasi kikubwa na hata maamuzi mengine katika maisha ya mtu yanatokana na misingi ya dini yake.Tusitegemee miujiza katika chochote kama hatufanyi kazi. Viongozi wetu sasa hivi wamekwisha onja sumu ya udini kulingana na misingi niliyoieleza. Wengine ni kutokana na masuala ya kihistoria lakini wengine ni kama kutafuta ufahari.

Katika upande wa elimu nao usiseme shule za serikali ambazo watu walikuwa wakijivunia kwamba kijana/binti yake amefalu shule ya serikali leo hii ni kinyume chake. Zamani serikali ilikuwa na utaratibu wa Warant kwa wanafunzi wote wawe wa Serikali ama sio wa serikali ili waweze kupata usafiri nafuu wa kuwarudisha makwao kwa basi,treni, meli mpaka ndege leo hii wapi. Kijana ilikuwa ukisafiri unapatiwa chakula kitakachokuwezesha kujikimu wakati wa safari. Kwa wale wengine waliovuka na kwenda elimu ya juu na kupata nafasi za masomo nchi za nje, walikuwa wanashonewa suti wanapewa nguo maalum za kujisitiri na hali ya hewa katika nchi wanayo kwenda, pesa ya kuanzia maisha,gharama za safari, posho ya safari pamoja na gharama zote za masomo na malazi awapo nje ya nchi. Mwanafunzi wa elimu ya juu atokapo mkoani alikuwa anafikia hoteli moja Dar ilikuwa inaitwa MOTEL AGIP na hoteli nyingine mbalimbali zenye hadhi ya juu. Huyo ni Nyerere aliyeweza kuwakirimu akijua kwamba watakuja kuilipa nchi yao leo hii hao ndio wanaoiua elimu ya nchi hii wamekosa shukrani na wamemsaliti Mwalimu.Leo hii vijana wanaopelekwa nje wanakosa mpaka pesa ya ada ambayo serikali inawajibika kuwalipia moja kwa moja huku viongozi wetu wakiwa wamekazania kununua mashangingi ya mabilioni. Yaani ni madudu juu ya madudu. Viongozi wanaobuni sera na mikakati ya kuinua elimu nchini wamekuwa wa kwanza kuzinyooshea vidole na kuzitoa kasoro shule za serikali wakati wao ndio chanzo.Yote katika yote shule binafsi sasa ndiozinazoongoza katika kusaili wanafunzi wengi ambao ni watoto wa mabwanyenye ambapo wateja wao wakuu ni watoto wa wale ambao wanabuni sera na mipango ya kumkwamua Mtanzania dhidi ya ujinga, maradhi na umaskini. Mtoto wa mkulima ama wa maskini hahusiki kabisa na mwisho wa siku utasikia "Saint" fulani inafaulisha sana wanafunzi mimi nampeleka mtoto wangu akasome huko lakini ukichunguza siri yenyewe, utakuta ni kwamba watoto wanakaririshwa mitihani na wamiliki ambao lengo lao liko kibiashara zaidi kuliko kumjenga kijana kielimu na pia dhana nzima ambayo tayari inatokana na niliyoyaeleza kwamba mtu sasa anasoma si kuelewa kitu na kikufahamu kiufasaha la! Anasoma ili afaulu mtihani. Na hayo ndio madudu tunayoyaona leo hii. Madudu yenyewe ni kuvuja kwa mitihani ya taifa, elimu kugeuzwa biashara badala ya huduma, Wizara kubadilisha mitaala ya elimu mara kwa mara pasipo kuwaandaa watendaji yaani waalimu wa shule za umma, Udhaifu wa wizara badala ya kusimamia masuala ya kiufundi inakuwa mtekelezaji wa ajenda za kisiasa na madai ya waalimu kutosikilizwa. Na hata shule zenyewe tunazojivunia za kata za umma zilizokuwepo chngamoto ni hizo hizo na wanaofaidi ni watoto wa wale wanaosomeshwa nje ya nchi ama shule zinazojiita za kimataifa nchini. Mtoto wa mkulima hafaidi.


Tupo katika utandawizi/utandawazi lakini lengo na ajenda ni ile ile na hii ya sasa hivi inafanyika kiufundi zaidi na mabepari ambao wameshadhamiria kwa dhati na wanatutawala kifikra. Na sasa hakuna kiongozi anayeweza kuamini kwamba rasilimali zetu wenyewe tungeweza kuzitumia sisi wenyewe kwa kutumia mitaji, wataalam wa kwetu ama hata wale wa nje ambao tungewaajiri tu na sisi kuwapa wao chao na wao wakachapa mwendo. HAKUNA nasema HAKUNA sana sana atakwambia " Hizo ni ndoto za Alinacha" Wao waliwezaje? Tayari ni Utumwa wa kifikra. Ni hawa hawa walioua kilimo chetu cha biashara, viwanda vyetu, mashirika yetu ya umma, reli zetu, taasisi zetu leo watabadilisha kiswahili hiki kesho Kiswahili kile. Hata haya majanga ambayo yanasababishwa na wao na wanajaribu kutengeneza mazingira kwamba hatuwezi mpaka fulani na fulani waje wao ndio wanaoweza kutufulia umeme ama matatizo mengine kwani sisi hatuwezi.Huo ni Utumwa wa fikra.

Kwa kuhitimisha nataka kusema, Watanzania tumekuwa pia watumwa wa fikra wa kuamini kwamba chama fulani ndio kinafaa kuongoza nchi kwa sababu kimetuletea amani nk nk.Viongozi waandamizi wa chama hicho wanataka kutufanya tuamini kwamba kumsafirisha mama mjamzito kwa pikipiki ya miguu mitatu ni halali. Huo ni upumbavu unaosababishwa pia na utumwa wa kifikra unaowafanya watu waamini kwamba bila chama fulani hakuna Tanzania/ Tanganyika . Ili kuweza kuleta maendeleo katika nchi yetu ambayo inatimiza jubilee ya miaka 50 baada ya kutwaa uhuru wake ni lazima tujikomboe kutokana na utumwa wa kifikra. Tuachane na fikra za kibambucha za "Chizika", "Kuwa mjanja", "Uhuru wa kuongea", "Pamoja Daima" tuzingatie namna tutakavyoweza kuliletea maendeleo taifa letu. Waliotufanya tuwe maskini wa fikra mnawajua na ni kazi yetu kuwaondoa.Mtatuita mavuvuzela lakini mtambue kwamba kila kitu kina mwanzo na mwisho wake.

TAFAKARI CHUKUA HATUA. KAMA HUWEZI UMIA KIMOYOMOYO!

No comments: