Monday, March 21, 2011

BARAZA KUU LA UVCCM WAWASHIANA MOTO

KATIKA kile kinachoonyesha kuwa hali ni tete ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), jana mkutano wa umoja huo ulitawaliwa na jazba huku, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba na Mjumbe Shy Rose Bhanj wakitupiana maneno makali.

Habari zilizopatika kutoka ndani ya mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa White House mjini hapa, zinaeleza mvutano wa Makamba na mjumbe huyo uliibuka wakati Shy Rose alipokuwa akichangia mada kuhusu hali ya kisiasa na kusema viongozi ndani ya CCM ndiyo chanzo cha CCM kunyang'anywa baadhi ya majimbo katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Hali hiyo ilionekana kumkera Makamba ambaye alisisimama bila kufuata utaratibu wa kikao hicho na kumkatiza Shy Rose akisema kauli hiyo haina ukweli.

Naye Shy- Rose naye akitoa maneno ya kumpinga Makamba kabla katibu mkuu huyo wa CCM naye kuendelea kuzuia kuwatupia lawama viongozi.

Kuona hivyo, Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM, Beno Malisa aliingilia kati na kuyazima huku kila mmoja akionekana kuwa na hamu ya kuendeleza ubishi baina yao, hata hivyo kikao kikaendelea na utaratibu wake.

Katika hatua nyingine wajumbe wa mkutano huo wamepinga hatua ya Halmashauri Kuu ya CCM kumrejeshea uanachama Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Nape Mnauye, aliyevuliwa uanachama wa UVCCM mwaka uliopita.

Kabla ya mkutano huo wa jana, juzi wajumbe wa Baraza Kuu la umoja huo walikesha Mjini Dodoma, katika vikao visivyo rasmi kupanga mikakati ya kufanya mageuzi makubwa ndani ya umoja huo.

Nape alivuliwa uanachama kutokana na kuwa na umri kupita wa miaka 35. Vile vile, wajumbe wa mkutano huo wamemchagua kada wa mkongwe wa chama hicho Kingunge Ngombare Mwiru kuwa Kamanda mkuu wa umoja huo kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Marehemu Rashid Kawawa.

Hata hivyo, mkutao huo umetawaliwa na mgawanyiko wa makundi mawili miongoni mwa wajumbe. Kundi la kwanza ni lile ambalo linamuunga mkono uongozi wa uliopo mdarakani na lingine likitaka kufanya mapinduzi ya kuung'oa viongozi.

Hadi jana jioni wajumbe hao walikuwa wakijadili ajenda ya umuhimu wa kuendelea na sekretarieti ya umoja huo au iondoke. Wajumbe walisema uongozi wa sasa wa umoja huo umeshindwa kazi na kwamba hauna budi kuondoka.

Sekretarieti ya umoja huo inaundwa viongozi mbalimbali akiwamo Katibu Mkuu, Martin Shigela. Hata hivyo, wachumbuzi wa mambo ya siasa ndani ya chama hicho wanasema kuwa mgawanyiko ndani ya chama umoja huo ni joto la urais wa mwaka 2015.

Mgawanyiko huo ulioanza kujionyesha tangu juzi baada ya wenyeviti wa UVCCM wa baadhi ya mikoa ya Tanzania Bara kufanya mkutano mzito katika Hotel ya New Dodoma unaoelezwa kuitishwa na mmoja wa wajumbe wa Baraza Kuu la umoja huo kuweka msimamo wao.

Hata hivyo, hali hiyo ilimpa wakati mgumu Kaimu Mwenyekiti wa Umoja huo, Benno Malisa ambaye alikuwa akihaha kutafuta baadhi ya wajumbe wenye ushawishi mkubwa kwa ajili ya kunusuru ajenda zake, wakati wajumbe hao wakikutana New Dodoma Hotel.

Baadhi ya waliohudhuria kikao hicho hotelini hapo walidokeza kwamba, pamoja na mambo mengine kikao hicho kilikusudia kuwa na maamuzi magumu ndani ya mkutano Baraza Kuu la UVCCM, waliyodai kuwa hayajawahi kutokea.

“Naomba muamini kuwa tumechoka kupelekwa kama watu wasiokuwa na msimamo. Hivyo kama sio leo katika Baraza, lakini muda wowote tutafanya mapinduzi makubwa ambayo yatawashangaza wengi,” alisema mmoja wa wenyeviti kutoka Kanda ya Ziwa.

Licha ya kueleza kwa undani zaidi juu ya matarajio yao, mwenyekiti huyo alidokeza kuwepo mgawanyiko mkubwa wa kimakundi ndani ya UVCCM.

Alifafanua kuwa lipo kundi la vijana linaloandaa mikakati ya urais 2015 ambalo kwa sehemu kubwa linapingana na kundi linalotetea uongozi ulipo madarakani hivi sasa.

Aliweka wazi kuwa kundi jingine ni lile linalojiita la haki na ambalo linasimamia maadili, lakini kwa sehemu kubwa linaonekana kupandikizwa na baadhi ya vigogo ndani ya CCM.

Hata hivyo, akizungumzia kilichoelezwa kuwa ni mikakati ya wazi ya mageuzi UVCCM, mmoja wa makatibu wa vijana wa mikoa ya Kusini alisema kila mmoja kati yao anakusudia kuonyesha makucha yake na kwamba hawatakubalina hali iliyotokea katika Baraza Kuu la Mjini Iringa mwaka jana ijirudie.

“Kwa ujumla mapinduzi yapo, tutayafanya, lakini sio kwa kukandamizwa kama ilivyokuwa Iringa Mei mwaka jana, ambapo kwa sehemu kubwa tulikuwa tunapelekeshwa. Safari hii tutafanya mapinduzi ya maslahi, hata mimi nipo tayari. Lakini nasema kama ni mapinduzi ya kushinikizwa sipo tayari, wengine tunalinda vibarua,” alisema Katibu huyo.

Ufunguzi wa Mkutano
Akifungua Kikao cha Baraza ndani ya ukumbi wa White House, Kaimu Mwenyekiti wa Umoja huom, Benno Malisa, alisema Baraza hilo kwa mara ya kwanza linategemea kufanya mambo makubwa ikiwamo kutengeneza muundo wa umoja huo.

Malisa alisema tangu Umoja huo ulipoanzishwa mwaka 1978 una muundo ule ule ambao unaonekana kupitwa na wakati na haukidhi mahitaji ya vijana wa sasa.

“Tangu Umoja huu ulipoanzishwa mwaka 1978 bado tupo katika muundo ule ule, hivi kweli vijana wa mwaka 2010 wanaweza kuwa na mahitaji sawa na ya vijana wa mwaka ule (1978), inabidi kuangalia kwa mapana,” alisema Malisa.

Alisema pamoja na mambo mengine pia watajadili hotuba ya Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa mjini Dodoma katika kilele cha Siku Kuu ya Kuzaliwa kwa CCM Februari 5 mwaka huu.

Kaimu Mwenyekiti huyo wa UVCCM alisema sehemu kubwa watakayoiangalia ni kipengele alichosema, "lazima CCM ijivue gamba lake", na kufafanua kuwa vijana watazama zaidi katika ajenda hiyo na kuangalia mustakabali wa kisiasa nchini.

Mbunge amwaga mamilioni
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mbunge wa Viti Maalumu kundi la Vijana, Catherine Magige, jana alimwaga mamilioni ya fedha akitoa Sh50,000 kwa kila mjumbe wa Baraza hilo, akisema kuwa ilikuwa ni ya kuwapa chakula cha mchana.

“Waheshimiwa wajumbe wa Baraza Kuu, Mheshimiwa Mbunge mmoja alileta ujumbe wake hapa akitaka tuwajulishe kuwa amewaalika katika chakula cha pamoja leo hii. Lakini kwa kuwa anajua kila mtu anapenda kula chakula chake nimeombwa nimwambie Mwenyekiti kuwa anatoa Sh50,000 kwa kila mjumbe kwa ajili ya chakula hicho sasa hivi,” alisema Naibu Katibu UVCCM Bara.

Baada ya maelezo hayo Magige ambaye aliingia bungeni kupitia mkoa wa Arusha alisimama na bahasha yenye rangi la kaki mkononi mwake na kueleka meza kuu, ambapo alimkabidhi Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM Beno Malisa na haikujulikana mara moja fedha hizo zilikuwa ni kiasi gani.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa UVCCM, wajumbe waliotakiwa kuhudhuria katika mkutano huo walikuwa 135 (ibara 89) ya kanuni za UVCCM, lakini waliohudhuria jana walikuwa 107.

Kimahesabu kutokana na idadi hiyo ikiwa Magige alitoa fedha hizo kwa idadi ya vijana walikuwepo ndani ya ukumbi atakuwa alitoa Sh5,350,000.

Wahisi mkono wa mtu

Baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, jana walishukuru kupewa fedha hizo na kueleza kuwa wamekumbukwa, lakini wakasema kuwa nyuma ya pazia la fedha hizo kulikuwa na mkono wa mtu.

“Ni kweli amefanya vizuri sana huyu Mheshimiwa kutupatia kiasi hicho, lakini kwa maoni yangu najua kuwa, lazima nyuma ya fedha hizo kuna kitu, naomba mfuatilie," alisema mmoja wa wajumbe akiwaambia waandishi wa habari.

Agenda zawa siri

Katika hatua nyingine, jana waandishi wa habari waligonga ukuta walipotaka kujua ajenda za mkutano huo baada ya kuelezwa kuwa uongozi hautaweza kuwapa ajenda hizo, badala yake wanawaweza kupewa vitu vingine ikiwemo ratiba.

MWANANCHI

No comments: