Monday, March 7, 2011

AWAOMBEA WATU KWA KUWAVUTISHA BANGI,SIGARA NA POMBE


Florence Majani


HATIMAYE watu ambao walikuwa wakiishi nyumbani kwa mwombezi anayejulikana kwa kama Maalim, wakidaiwa kutibiwa kwa sigara, bangi na pombe kali wameondolea kwenye nyumba hiyo, katika kazi iliyowashirikisha viongozi wa serikali, polisi na ndugu wa mwombezi huyo.

Yahya Tibe Shogosha (Maalim) asmbaye ni mkazi wa Tabata, Uwanja wa Twiga, jijini Dar es Salaam anatuhumiwa kuwalaghai watu kadha wa familia moja kwa maelezo kwamba anawatibu na badala yake kuwagombanisha, kuwafanya watumwa wa ngono na kuwanywesha vileo akidai ni moja ya tiba.

Hata hivyo Maalim Shogosha huyo ambaye hivi sasa yuko katika kijiji cha Bugabo, mkoani Kagera ambako alikwenda kuhudhuria msiba wa wazazi wake amekanusha tuhuma dhidi yake kwa kusema kwamba "wanaonituhumu walikuwa na melengo yao binafsi na wala tuhuma zao si za kweli".

Nazungumza na mdogo wa Maalim huyo, Milton Tibe Shogosha, ambaye anasema kuwa aibu kubwa imeikumba familia yao kutokana na madai yaliyotolewa dhidi ya kaka yao.

“Huyu ni kaka yangu, amenilea tangu nikiwa mdogo hapa mjini, nayajua mema yake na mabaya yake, lakini miaka ya hivi karibuni ni kama amebadilika na mabadiliko yake kwa kweli si mazuri,” anasema Tibe.

Anasema, baada ya kubadili dini kutoka ukristo na kuanza kufanya maombi, kaka yao alibadili jina na kuitwa Yahya Tibe Shogosha, badala ya jina la awali la Rugakingira Tibe Shogosha.

Ndugu huyo aliongeza kuwa Maalim Yahya ni msomi ambaye alikuwa na cheo kikubwa serikalini, lakini ghafla alibadili dini na kujiunga na dhehebu moja la kiislam linaloitwa ‘Tabligh’ na baadaye aliacha kazi akidai kuwa kazini kuna mashatani ambao watamuua.

“Tulimshangaa kwa kitendo chake cha kuacha kazi, unajua kaka alikuwa na cheo kikubwa serikalini, alikuwa ni Mwenyekiti wa Asasi za Kiraia za Afrika Mashariki, aliwahi kufanya kazi UNDP, na alikuwa anamiliki nyumba na magari kadhaa, si hivyo tu bali alikuwa kiungo anayetegemewa sana ofisini kwake na alipoacha kazi walimbembeleza sana,” anasema Tibe.

Maombezi na tiba

Ndugu huyo anaendelea na kusema, baada ya kaka yao kuacha kazi walimsikia akitangaza ya kuwa ni mwombezi aliyetumwa na Mungu kuwaokoa watu, lakini kilichowashangaza ni taratibu za maombezi yake.

“Kwanza hakuwa akisali msikitini kama wafanyavyo wengine, bali alikuwa na chumba maalum ndani ya nyumba yake alichokiita msikiti, ambacho kina godoro(tazama picha), gusati na meza ndogo yenye quoran, mkuki, na fimbo ya mkwaju, lakini cha ajabu zaidi ni kuwa hujifungia chumbani na watu kwa muda mrefu akidai anawaombea," anasimulia mdogo wake huyo.

Kingine ni jinsi anavyokaa nao nyumbani kwake na kuwafungia ndani tu bila kutoka, anasema na kuongeza kuwa:

“Humu ndani anaishi na familia zaidi ya tatu, anadai anawaombea lakini matendo yenyewe yanayofanyika wakati wa maombezi yanatushangaza, hujifungia na huyo mama(anamnyooshea kidole Mwidina Nuru mwanamke aliyeishi kwa Maalim kwa miaka zaidi ya kumi) wanadai wanasali.”

'Wagonjwa' watoka kwa maalim

Ndugu huyo wa Maalim anaongeza kuwa, baada ya waandishi wa habari kufika mapema mwezi huu na kufichua mambo ambayo baadhi hata wao walikuwa hawayajui walidhalilika kiasi kikubwa na kuazimia kulimaliza tatizo hilo kwa kuwahamisha watu wote waliokuwa wanatibiwa na Maalim katika nyumba hiyo.

“Tumetoka kuzika, tumemuacha Tibei Shogosha Bukoba, lakini nia ni kumaliza dhalilisho hili kwani matendo yanayodaiwa kufanywa na kaka yetu hatuyaelewi hata kidogo, kwa hiyo tumewaita majirani, polisi na mashuhuda ili waone jinsi ambavyo tunamtoa mama huyu(Mwidina Nuru) katika nyumba hii,” Anasema.

Mdogo huyo wa Maalim aliwaita polisi, pamoja watoto wa Mwidina ambaye habari zake ziliwahi kuandikwa katika gazeti hili, Februari mwaka huu, ili wafike kumchukua mama yao.

“Baadhi ya watu waliokuwa wakiishi humu wameondoka na tunataka tusafishe kabisa hii nyumba na tuchome kila kitu kibaya lakini kuhusu huyu mama, tumeamua tuwaite polisi pamoja watoto wake kwani amekuwa mbishi kutoka,” anasema Tibe.

Mjumbe wa serikali za mitaa wa Tabata Twiga, Joakim Julaya, anazungumza na kusema, anashangazwa na tabia za Maalim huyo kwani si mzungumzaji na hana ushirikiano na wenzake.

“Kwa kweli mimi sura yake nimeiona mara chache sana, naingia nyumbani kwake kwa sababu ni mjumbe na ninatakiwa kufikisha baadhi ya taarifa lakini majirani wengine hawamjui kabisa”, anasema Julaya.

Mjumbe huyo anakanusha kufahamu kama Maalim ni mwombezi lakini alidhihirisha kustaajabishwa kwake na namna anavyosihi na kusema kuwa ni nadra sana kuona mlango wa nyumba yake ukiwa umefunguliwa na hana ushirikiano na majirani si katika msiba wala sherehe.

Majirani zake

Kijana mmoja aliyekuwa shahidi katika kesi ya kuhamishwa kwa Mwidina Nuru kutoka katika nyumba ya Maalim, Michael Zakaria, anasema kuwa imekuwa afadhali kwa mama huyo kuondoka kwani mambo yaliyokuwa yakifanyika ndani ya nyumba hiyo ni ya ajabu na ya aibu.

Jirani mwingine ambaye anaonekana kumfahamu kwa karibu na kwa muda mrefu Maalim, Rhoida Mwangoka anasema, anamfahamu vizuri Maalim kwani walihamia mwaka mmoja huko Tabata.

“Namfahamu, anaitwa Rugakingira, ni msomi wenye digrii, alikuwa anafanya kazi yake nzuri akiishi na familia yake vizuri lakini ghafla alibadilika akaanza kuvaa mavazi ya nusu kanzu, mara tukasikia ameacha kazi, akadai anaombea wenye matatizo,” anasema na kuongeza:

“Baada ya hapo maisha yake yakawa ya ajabu sana, hakuna mtu anayeingia ndani kwake, mimi mwenyewe leo ndiyo nimetia mguu, haji misibani licha ya hiyo harusi lakini baya zaidi ni tabia yake ya kuwaharibu vijana wa kiume na wake za watu akidai kuwaombea.”

Rhoida anasema, ni bora Mwidina Nuru aondoke katika nyumba hiyo kwani wamemuona hapo muda mrefu na maisha yake si mazuri kabisa.

Baada ya Tibe, kufanikisha zoezi la kuwatoa watu wanaoishi nyumbani kwa Maalim akiwemo Mwidina Nuru, nazungumza na mtoto wa kiume wa mama huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.

“Kwa kweli hatuamini kama mama yetu ametoka katika mikono ya Maalim, tulifunga na kuomba Mungu atutetee katika hili na kweli ametusikia, sasa hivi nampeleka mama nyumbani kwangu na tutaanza maisha mapya,” anasema kijana huyo akilia kwa furaha.

Maelezo ya Mwidina Nuru

Mwidina Nuru ni mwanamama ambaye amesihi nyumbani kwa Maalim kwa zaidi ya miaka kumi 'akitibiwa', hali ambayo ilisababisha mtafaruku pale watoto wake walipokuwa wakijaribu kumtoa mikononi mwa mwombezi huyo. Katika mazungumzo yake Mwidina anasema:

“Mimi sio kwamba sitaki kuondoka hapa, bali sitaki kuondoka kwa fujo kama wanangu walivyokuja kunichukua mwanzoni,(anasema huku akikusanya mabegi yake) sing’ang’anii kwa watu ingawa wamenihifadhi kwa miaka kumi sasa”.

Anasema, habari za yeye na Maalim kujifungia chumbani kwa muda mrefu wakifanya maombezi ni za kweli ingawa anadai hakuna lolote baya linalofanyika zaidi ya maombi.


Maelezo ya Maalim

Rugakingira Tibe Shogosha hivi sasa yuko kijijini Bugabo mkoani Kagera ambako alikwenda kuhudhuria matukio ya misiba ya wazazi wake. Katika mazungumzo yake na Mwananchi anakiri kwamba kweli yeye ni mwombezi na amekuwa akifanya hivyo kwa muda mrefu lakini akasema hajawahi kufanya maovu kama inavyodaiwa.

"Mimi naishi na familia yangu na nina mke na mtoto wako hapo hapo, sasa hata wwe fikiria ninawezaje kufanya hayo mambo wanayodai wakati familia yangu ipo na hata ukimuuliza mke wangu, siku zote tumesihi kwa amani sana," anasema Shogosha na kuongeza:

"Nimewasaidia watu wengi sana, mwingine alikuja kwangu na mkewe wakakaa kwangu hadi matatizo yao yalipoisha wakaodoka, kwahiyo hayo mambo mengine yanayosemwa si ya kweli ni uzushi mtupu lakini mimi ninaendelea kuwaombea kwa Mungu hao wanaonichafua".

Kuhusu kuhamishwa kutoka nyumbani kwake kwa Mwidina Nuru na wagonjwa wengine, Maalim Shogosha anasema "Nimeridhia hao watu waliokuwepo kwangu waondoke, tulijadili kama familia ikaonekana kama hawa watu nawasaidia halafu ndugu zao hawataki basi waondoke, kwahiyo kuondoka kwao mimi nakufahamu si jambo geni kwangu".

Anakiri kwamba suala la Mwidina kuishi kwake lilisababisha mvutano mkali miongoni mwa watoto wa mama huyo, kwani kaka yao mkubwa alikuwa akitaka waendelee kuishi kwake (kwa maalim) lakini watoto wengine wawili walikuwa wakitaka mama yao aondoke.

"Hawa watoto awali walikuwa wakikaa kwangu ila ni kama miaka miwili sijawaona, sasa haya mambo wanayozua leo yanatoka wapi? alihoji Maalim Shogosha na kuongeza kuwa, walitumia mwanya wakati yeye akiwa safarini kumchafua.

Alipohojiwa kuhusu godoro kuwepo ndani ya 'msikiti' anakofanyia maombezi, Maalum alisema "inawezekana wakati msiba vitu vikawekwa sehemu yoyote, kwahiyo siwezi kujua nilipoondoka vitu vingine viiwekwa wapi, kwahiyo pengine hilo godoro liliingizwa huko baada ya mimi kuondoka".

Maalum Shogosha alilithibitishia Mwananchi kwamba alikuwa muumini wa dini ya kikristo lakini akakanusha kwamba hakubadili dini hiyo. "Siwezi kusema nilibadili dini, ni hali ya kuombea tu, si uanafahamu mtu akiwa anaombea, huwezi kusema amebadili dini,"alisema.

Shogosha anakiri kwamba aliwahi kufanya kazi serikali katika taasisi ya Washirika lakini akakanusha kufanya kazi UNDP. Alisema baada ya kuondoka washirika alijiunga na ubalozi wa Marekani akiwa ofisa katika kitengo cha kusadia mashirika yasiyokuwa ya kiserikali.


MWANANCHIMy Take

Bongo siku hizi kila kitu kinafanyika mradi walioko madarakani wanafanya bila haya na watu wanajifanyia upuuzi wao tu!

No comments: