Thursday, February 10, 2011

WANAFUNZI 1200 UDSM WARUDISHWA MAKWAO


ZAIDI ya wanafunzi 1,200 wa shahada ya kwanza katika Koleji ya Uhandisi na Teknolojia (COET) ya chuo kikuu cha Dar es Salaam, wamesimamishwa masomo kwa muda usiojulikana baada ya kugoma kwa siku tano mfululizo na kufanya vurugu chuoni hapo.

Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Rwekaza Mukandala, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari chuoni hapo.

Kwa mujibu wa mukandara, kuanzia Februari 4, waka huu, kikundi cha wanafunzi wa koleji hiyo, wamekuwa wakivuruga madarasa, kuwatisha wahadhiri na kuwazuia wenzao kufanya mitihani.

Alisema chanzo cha vurugu hizo, ni kushinikiza uongozi wa chuo, usimsimamishe masomo mwanafunzi mwenzao wa mwaka wa tatu Jamson Babala, ambaye Novemba 12 mwaka jana wakati wa mtihani wa marudio, alikutwa na karatasi kwenye chumba cha mtihani, na alipotakiwa kuitoa mwanafunzi huyo aliitafuna na kuimeza.

“Kufuatana na taratibu za mtihani, msimamizi wa mtihani alimtaka mtahiniwa andike na kutia saini tamko kwenye kijitabu chake cha kujibia maswali kuthibitisha yaliyotokea, na mtahiniwa akafanya hivyo, kisha akaruhusiwa kuendelea na mtihani wake wa mwisho,” alisema Profesa Mukandala.

Profesa Mukandala alisema suala hilo, lilifikishwa katika kikao cha kamati ya masomo ya shahada za awali.
Alisema kamati hiyo, ilimuhoji mwanafunzi huyo pamoja na wasimamizi wa mitihani, na ilijiridhisha kuwa mwanafunzi huyo ana hatia na ilipendekeza kwa seneti ya chuo hicho, mwanafunzi huyo, achishwe masomo.

Kwa mujibu wa Profesa Mukandala, baada ya mwanafunzi huyo kufahamishwa juu ya hatua hiyo, aliiandika barua kwa makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Mukandala kutaka kupunguziwa adhabu, lakini suala hilo lilikataliwa na wanafunzi wenzao baada ya kuanza mgomo, walisema hawawezi kusoma bila kuwa na mwenzao huyo.

“Kitu walichokifanya hakikubaliki, hatuwezi kuendesha chuo kwa kushinikizwa,” alisema Profesa Mukandala.
Alisema kutokana na hali hiyo, wanafunzi hao watarudi majumbani kwao kwa muda usiojulikana wakati taratibu za kubaini vinara wa vurugu hizo, zikiendelea.

“Masharti ya kurudi na lini watarudi tutasema baadaye, sasa hivi kwanza tunataka amani irudi chuoni, watu waweze kuendelea na masomo yao, hatuwezi kuendesha chuo kwa kulindwa na polisi,” alisema Profesa Mukandala.
Mara baada ya kupokea taarifa ya kufungwa kwa chuo, wanafunzi hao walikubaliana na uamuzi huo, na waliondoka katika chuo hicho kwa utulivu.

Juzi Mwananchi ilishuhudia wanafunzi ha, wakifanya mandamano ndani ya chuo hicho huku wakikmba nyimbo za kejeli dhidi ya uamzi wa kumufukuza mwanafunzi huyo na kutishia kuwa wasingekuwa tayari kurudi darsanani hadi hapo atakaporudishwa.

Pamoja na kufanyamaandamano hayo ya ndani pia badhi yao waliweka ulinzi mkali getini na kuzuia mtu yeyeto asiyehusika kuingia ndani ya Chuo hicho wakiwemo waliokuwa wakiingia kwa lengo la kujisomea.

“Angusha kitambulisho chako hapa,eleza unataka kwenda wapi kufanya nini kama huna kitambulisho hakuna kuingia ndani na wale wanaokwenda kwenye kipindi leo hakuna masomo”alisikika mwanafunzi mmoja akipaza sauti getini hapo.

Juzi Mwananchi ilishuhudia idadi kubwa ya wanafunzi ambao walionekana kutokubaliana na mgomo huo na kwamba wanafunzi hao walilazimika kwenda kukaa kwenye miti iliyoko nje ya geti la Chuo hicho na kujisomea.
Habari hii imeandaliwa na Fredy Azzah,Geofrey Nyangóro na Edom Mwasamya

MWANANCHI

No comments: