Tuesday, February 15, 2011

WABUNGE WAJIZOLEA 90 MIL KWA AJILI YA KUJINUNULIA MAGARIJUMLA ya Sh3.24 bilioni zimelipwa kwa wabunge ili kuwawezesha kununua magari binafsi kwa ajili ya shughuli za kibunge, imeelezwa.


Kwa mujibu wa habari hizo kila mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amelipwa Sh90 kwa ajili ya kujinunulia gari.


Aidha, wabunge hao wapatao 360 wamekatiwa bima ya afya inayotarajiwa kuanza kutumika kabla ya mwezi Juni mwaka huu.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika uzinduzi wa Tawi la Chadema, Mipango Kata ya Miyuji mkoani Dodoma wabunge wa Chadema, walisema kuwa wanashangazwa na hatua ya Rais Kikwete kuweka pikipiki za matairi matatu (Bajaji) kama moja ya vipaumbele vyake ili zitumike kubeba wajawazito wakati wabunge wanalipwa mamilioni.


Katika hotuba yake ya kulizindua bunge Kikwete alieleza mpango wa serikali yake kununua pikipiki hizo 400 zitakazosambazwa maeneo mbalimbali hasa vijijini kwa ajili ya kuwabebea wajawazito kama njia ya kupunguza matatizo ya usafiri kwenye maeneo hayo.


"Ndugu zangu hali ni mbaya, siku moja tutafanya maandamano bungeni, sio kutoka nje ya ukumbi. Inashangaza, tumepewa Sh90 milioni za magari kwa wabunge wote, huku bungeni tunajadili bajaji kuwa 'ambulance'(gari ya kubebea wagonjwa),'" alisema mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema.


Alisema mbali na hilo katika hali inayoonyesha kuwa hospitali za serikali ni mbaya, katika semina iliyofanyika Dar es Salaam hivi karibuni, wabunge waliomba kuwekewa bima za afya, kutibiwa nje ya nchi na katika hospitali binafsi hapa nchini.


"..Wabunge tumeomba 'insurance' (Bima) kila mmoja amepewa na kabla ya Juni naamini zitaanza kutumika, tumeomba kutibiwa 'private hospital' (hospitali binafsi). Hii inaonyesha hospitali za serikali zilivyo mbaya na hao wenye uwezo wanazikimbia," alisema Lema.


Aliongeza kuwa: Ndoto ya kuiondoa CCM ni 'serious' (thabiti), lakini mkifanya noma ya kupata haki, hiyo imebarikiwa. Kama (CCM) wanafikiri wanaweza kuendesha nchi watakavyo, sasa hawawezi, ninyi vijana msipojitoa kwa sasa nchi itakufa."


Alikwenda mbali zaidi akisema anaomba wake za viongozi wapate ujauzito na kupakiwa katika bajaji hizo wakati wa uchungu kwenda kujifungua ili waone adha ya usafiri huo itakavyokuwa.


Akiongea katika mkutano huo naye mbunge Tundu Lissu aliwataka wananchi kutoogopa mabadiliko na kwamba historia haiheshimu watu wanaoogopa.


""Historia haiheshimu wanaoogopa, tusije kusahau bei ya mabadiliko, bei yake ni kupigwa, kufungwa hata bei kubwa zaidi ya kifo," alisema Lissu.


Naye John Mnyika alisema Chama chake kitaandaa kongamano maalumu la vijana wa vyuo vikuu ili wapate muda wa kuzungumza nao vizuri na kwamba maandamano ya kuishia viwanjani yametosha na sasa watakuwa wakifika kwa wahusika.


"..Maandamano ya kuishia viwanjani imetosha, sasa tutaenda maeneo ya wahusika, vyuo lazima mjenge mtandao
imara, lazima mpambane na umasikini," alisema Mnyika.

MWANANCHI

No comments: