Saturday, February 12, 2011

SIR. GEORGE KAHAMA: CCM HAIKO SALAMAHALI ya kutokukubaliana na mwenendo wa mambo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inazidi kujipambanua, kada wa mkongwe wa TANU na CCM, Sir George Kahama, naye ameibuka akitaka kauli za viongozi na matamko ya chama hicho yaegemee zaidi tafiti badala ya utashi wa viongozi, ili kubeba uzito unaostahili.

Mwenendo wa sasa wa CCM unabainisha kuwa hata vikao nyeti, ikiwamo Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu NEC) vimeanza kupoteza mvuto, vikiibua misimamo inayopingana na sehemu kubwa ya jamii.

Kati ya masuala ambayo yanatajwa kuitenga Kamati Kuu na Halmashauri Kuu, vyombo muhimu vya CCM ni kutothubutu kuwachukulia hatua za kinidhamu viongozi wa CCM, wasio na maadili.

Kutokana na hali hiyo, Sir George Kahama anasema; “Chama sasa kinahitaji Idara nzito ya utafiti, yenye wataalamu waliobobea. Lazima chama kiwe na watafiti wa kisiasa, kisaikolojia na kiuchumi,” alisema Kahama katika mazungumzo yake na Raia Mwema, kabla ya mazishi ya Kada mwanzilishi wa TANU, Chifu George Patrick Kunambi, Ubungo-Msewe, jijini Dar es Salaam.

“Hali si nzuri kwa sasa CCM, leo nadhani ukiuliza sababu kitafiti kwa nini KANU (kilichokuwa chama tawala Kenya) kimeondolewa madarakani au UNIP (chama kilichodai uhuru Zambia), sidhani kama utapata sababu za kitafiti, utapata sababu kwa mujibu wa maoni ya unayemuuliza,” alisema Sir George.

Alisema viongozi wa chama hicho wanahitajika sasa kuongoza kwa kuzingatia mwenendo wa kitafiti huku wakiheshimu misingi na imani ya chama chao.

“Haiwezekani kiongozi wa chama anaibuka na kuzungumzia suala analodai ni la chama huku akitambua kuwa haliwiani na misingi na imani ya chama. Lazima chama kijirudishe karibu na wananchi zaidi, wazidi kukiamini na hii itafanikiwa kama kutakuwa na Idara imara ya utafiti,” alisema.

“Wakati ule wa Mwalimu Nyerere chama kilikuwa kikizingatia taarifa za utafiti. Kaulimbiu zilizoibuliwa zilitokana na utafiti kwamba watu wamechoshwa na nini, wanahitaji nini na kwa wakati gani.

“Kwa mfano, Mwalimu aliibua kaulimbiu ya Tujisahihishe...hii ilizingatia mwenendo wa dunia kwa wakati ule, baadhi ya viongozi waliwasahau wananchi na wananchi walianza kuchoshwa na hali hiyo.

“Wakati ule Obote anapinduliwa utafiti ulibainisha hatua za kufanya, tuliibua mwongozo maalumu. Kwamba viongozi wasiwe wanyapara...Mwalimu Nyerere alisimamia hili ingawa baadhi ya wenzake walimpinga wakisema bila unyapara kazi hazifanyiki ni kulea uzembe.

“Unajua kuna jambo jingine ambalo watu hawajui na wengine wanapotosha. Kwa nini Mwalimu Nyerere alijiuzulu serikalini kwenda kuimarisha chama?

“Watu wasichokijua ni kwamba alifanya hivyo baada ya kuona dalili za wazi kwamba viongozi baada ya kupigania Uhuru walianza kujisahau, wakaona ndiyo mwanzo wa kufaidi nchi, ndani ya TANU walijisahau, wakaanza kutafuta fedha za mitaji kwa waasia na watu wengine, wakaanza kuwasahau wananchi wadogo waliohangaikia Uhuru.

“Hali hii Mwalimu aliiona na ndipo alipojiuzulu serikali kwenda kuimarisha chama, kiwe chama cha wananchi wote, kisichotelekeza nguvu za wanyonge waliopigania Uhuru. Pili, alitaka kuweka mipaka ya kiutendaji kati ya chama na serikali, isionekane makosa ya chama ndiyo makosa ya serikali,” alisema Kahama aliyepata kuwa Waziri na mbunge kwa awamu tofauti, ikiwamo Awamu ya Kwanza.

Hata hivyo, katika hatua nyingine Sir George Kahama alivutiwa na hatua ya wananchi pamoja na baadhi ya viongozi kutoa maoni yao bila woga, wakikosoa na kupendekeza hatua za kuchukuliwa.

“Navutiwa na maoni ya watu mbalimbali ni kama vile wakati wananchi wana maoni mazuri kuliko baadhi ya viongozi, ingawa ndiyo mnasema sisi tumepitwa na wakati, mawazo mazuri hayawezi kupitwa na wakati, yanafaa kutumika wakati wote,” alisema.

Wakati Kahama akiwa na maoni hayo, wiki kadhaa zilizopita, vijana wa CCM waliozungumza na waandishi wa habari wakitoa kauli zinazoashiria kutoridhika na mwenendo wa mambo ndani ya chama chao na serikalini, kiasi cha kutoa maazimio ya hatua za kutekelezwa na chama hicho pamoja na serikali.


RAIA MWEMA.

No comments: