Tuesday, February 15, 2011

MBOWE AMTOSA SHIBUDA UWAZIRI KIVULIIsrael Mgussi, Dodoma


KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe jana alitangaza Baraza la Mawaziri Kivuli likiwa na mawaziri 29 wote kutoka Chadema, huku akimtosa Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda.Shibuda ambaye aliyehamia Chadema baada ya kutoswa kwenye kura za maoni ndani ya CCM, ameonekana kuwa na toifauti za kimtizamo dhidi ya chama chake cha sasa hali inayoweza kuwa ndiyo imechangia kutokuwamo kwenye Baraza la Mawaziri Kivuli.

Katika Baraza hilo, Mbowe amewateua Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kuwa Waziri Kivuli wa Fedha, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika kuwa Waziri Kivuli wa Nishati na Madini na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee kuwa Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Wizara ya Fedha na Uchumi inayoongozwa na Waziri Mustapha Mkullo, ndiyo muhimili wa uchumi wa nchi, ikishughulikia masuala yote yanayohusu mipango na bajeti, wakati Wizara ya Nishati na Madini inayoongozwa na Waziri William Ngeleja inabeba uzito mkubwa kwa sasa kutokana na kuwapo kasoro kadhaa za kiuendeshaji ambazo zimekuwa zikigusa sekta zote muhimu za uchumi wa nchi na maendeleo.

Changamoto kubwa katika wizara hiyo ni matatizo makubwa ya uhaba wa nishati ya umeme, ambayo kwa sasa yamesababisha kuwapo kwa mgawo wa umeme wa muda mrefu, huku sekta ya madini ikilaumiwa kwa kutowanufaisha Watanzania na badala yake kuwanufaisha wageni kutokana na udhaifu wa sheria pia mikataba baina ya Serikali na wawekezaji.

Kwa upande wa Mdee, atakuwa ana kwa ana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye alianza kutekeleza wajibu wake katika wizara hiyo kwa kasi baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete.

Katika Bunge la Tisa, Mdee alikuwa miongoni mwa wabunge waliopigia kelele uozo katika sekta ya ardhi, kiasi cha kuwataja majina ya baadhi ya viongozi katika Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam kuwa ni mafisadi kutokana na tuhuma zilizokuwa zikiwakabili.

Mbowe akitangaza Baraza lake Kivuli jana alisema, anaweza kulifanyia mabadiliko na kuhusisha wabunge wa
vyama vingine vya upinzani wakati wowote na kwamba mabadiliko yatafanyika baada ya wao (wapinzani) kuzungumza na kufikia muafaka.

Katika baraza hilo lililotangazwa baada kipindi cha maswali na majibu, Mbowe mwenyewe anakuwa Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi huku naibu wake akiwa Silinde David Ernest.

Idadi ya Mawaziri Kivuli
Mbowe alisema baraza lake halina mawaziri wengi ili kuonyesha mfano wa kukwepa matumizi yasiyokuwa ya lazima kwa vitendo."Pamoja na idadi ya mawaziri na naibu mawaziri wa Serikali kuwa 50, uteuzi wangu umeteua wasemaji wakuu na manaibu wasiozidi 29 ili kuonyesha kwa kivitendo, kilio chetu cha muda mrefu cha kuwa na baraza dogo la mawaziri.

Aliwataka viongozi wa Serikali kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wasemaji hao wa Kambi ya Upinzani kwa lengo kujenga nchi na demokrasia ya kweli.

"Ikumbukwe kwamba watendaji wa Serikali hawana vyama na wanahudumia Serikali iliyopo na kuwa tayari kuhudumia Serikali ijayo bila kujali inaundwa na chama gani cha siasa. Uzoefu unaonyesha kuwa wasemaji wa upinzani wamekuwa wakionekana wanoko, vizabinazabina na wasio na uzalendo pindi wanapohoji au kukosoa, ni rai yetu kuwa muundo huo uondoke kwani lengo letu ni kujenga nchi," alisema Mbowe.

Mawaziri wengine kivuli
Kwa mujibu wa Mbowe, Waziri Kivuli katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), amekuwa Raya Ibrahim Khamis, Waziri wa Uwekezaji na Uwezeshaji amekuwa Esther Matiko huku naibu wake akiwa Vicent Nyerere.

Mbowe alimteua Said Amour Arfi kuwa Waziri katika Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Mchungaji Israel Natse kuwa Waziri wa Mahusiano na Uratibu, huku Susan Lyimo akiteuliwa kuwa Waziri katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Pauline Gekul ameteuliwa kuwa Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Leticia Nyerere Waziri wa Ofisi hiyo akishughulikia mazingira ambapo Zitto Kabwe amekuwa Waziri wa Fedha huku naibu wake akiwa Christina Mughwai.

Godbless Lema amekuwa Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, Tundu Lissu, Katiba na Sheria, Ezekia Wenje akienda Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Joseph Selasini alipewa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Silvester Kasulumbai akiteuliwa kuongoza Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

Wengine walioteuliwa na wizara zao katika mabano ni Profesa Kulikoyela Kahigi (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Halima Mdee (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) na Mchungaji Peter Msigwa (Maliasili na Utalii).

Mhandisi Salvatory Machemuli ataongoza Wizara ya Ujenzi, Mhonga Ruhwanya (Wizara ya Uchukuzi), Lucy Owenya (Viwanda na Biashara), Christowaja Mtinda (Elimu na Mafunzo ya Ufundi) na Dk Gervas Mbasa (Afya na Ustawi wa Jamii).

Pia wamo Regia Mtema (Kazi na Ajira), Naomi Kaihula (Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto), Joseph Mbilinyi (Habari,Vijana na Michezo), Mustapha Akunaay (Ushirikiano wa Afrika Mashariki), Meshack Opulukwa (Kilimo, Chakula na Ushirika) na Highness Kiwia amekuwa Waziri Kivuli wa Maji.

Shibuda akabwa koo
Wakati Shibuda akitoswa katika Baraza Kivuli, wanachama wa Chadema walio katika Vyuo Vikuu mkoani Dodoma, wamepanga kwenda Ofisi za Bunge leo kwa lengo la kumzuia mbunge huyo kuingia bungeni wakidai ni msaliti.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika sanjari na uzinduzi wa tawi la chama hicho, Mipango, Kata ya Miyuji mkoani Dodoma, walisema kuwa awali walipanga kufanya hivyo jana, lakini kutokana na tukio la Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kutakiwa kutoa uthibitisho wa madai yake kuwa Waziri Mkuu kuidanganya jamii.

Mwenyekiti wa Tawi la Chadema Mipango, Leonard Toja alisema kuwa mbunge wao Shibuda amewasaliti kwa kuonyesha kuwa bado ana mapenzi na CCM huku akiutaka uongozi wa juu wa Chadema kumwajibisha.

"Tunalaani kauli za Shibuda, ni mamluki anayetimiza malengo yake kwa
kukivuruga chama, viongozi wa Chadema chukueni maamuzi magumu," alisema Toja ambaye pia ni kiongozi wa Baraza la Vijana wa Chadema katika Vyuo Vikuu vya Kanda ya Kati aliposoma risala yao.

Akichangia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete wiki iliyopita, Shibuda pamoja na
mambo mengine alinukuliwa akizungumzia kuhusu malezi ya vijana akisema vijana wa sasa wanahitaji mwongozo mzuri zaidi wa malezi na kwamba yeye atabaki na maadili aliyojifunza ndani ya CCM aliyosema pia atayapeleka Chadema.

Akizungumza baada ya mkutano wa uzinduzi wa Tawi la Chadema Mipango Kata ya Miyuji, Dodoma, Toju ambaye ni mwenyekiti wa tawi hilo alisema wao kama vijana wa Chadema hawana haja ya malezi anayotaka Shibuda kuyapeleka kwao.

"Yeye allisema anataka kuleta malezi aliyoyapata CCM alete Chadema, malezi ya CCM ayalete Chadema!, hapa hatutaki na sisi tutaandamana Jumanne(leo)
kwenda kumzuia Shibuda asiingie bungeni, " alisema Toju.

Hata hivyo, wakizungumza katika mkutano huo, Lema na Halima Mdee walionyesha mtazamo tofauti kuhusu Shibuda.Wakati Lema akisema kuwa suala hilo lipo ndani ya uwezo wa viongozi wa chama chao, Mdee alisema hakuna haja ya kumfuatilia mbunge huyo na kwamba kama hukumu atahukumiwa na jamii husika.

Hata hivyo, Shibuda mwenyewe hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo.


MWANANCHI

No comments: