Thursday, February 3, 2011

MASWALI 9 KWA DON. AZIZ KUHUSU DOWANS


M. M. Mwanakijiji (BGM)

KUNA mtu mmoja tu katika Tanzania hii anayeweza kulisaidia taifa kuamua vizuri juu ya malipo ya Dowans.

Yaani mtu huyo akiamua kuweka bayana yale anayoyajua kuhusu dili zima la Dowans basi atakuwa amesaidia kufanya wananchi wajue na waridhike ya kwanini Dowans wanalipwa.

Mtu huyo ni Mbunge wa Igunga Rostam Aziz. Kwa muda mrefu Aziz amekuwa akihusishwa na umiliki wa kampuni hii lakini pasipo kubanwa au hata kutakiwa kutoa maelezo ya kina ya kuhusika kwake na kampuni hii.

Taarifa ambazo amekuwa akizotoa yeye mwenyewe ni zile tu ambazo amekuwa akitaka watu wajue na akikwepa mambo mengine ambayo ni muhimu.

Lakini sasa kuna mambo ambayo yako wazi na yanatosha kutaka kupata majibu ya kina kwa sababu ukiondoa kivuli cha ufisadi ambacho kimetanda kwenye suala la Richmond/Dowans bado kuna masuala ambayo kisheria yanaonekana ni halali kufanyika.

Ninaamini itakuwa vizuri kwa vile Rostam Aziz amekiri kuhusika na kampuni hiyo (kwa kuwashawishi kuja kuwekeza nchini – maneno yake) ninaamini anaweza kusaidia katika kufunga mjadala huu akionesha uzalendo wake kwa kujazia pale ambapo taarifa zinakosekana.

Narudia tena mtu pekee anayeweza kutoa majibu ya maswali yafuatayo kwa kina na kwa usahihi ni Rostam Aziz Mbunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), chama ambacho serikali yake iko tayari kutoa malipo ambayo (japo ni fedha kidogo sana) yataongeza kidogo katika mfuko wake. Siamini kama ni kidogo kiasi cha kuweza kusamehe deni.

Ni katika kutafakari sana hoja nyingi za hivi karibuni najikuta nauliza maswali yafuatayo ambayo Rostam ndiye pekee anaweza kuyajibu kwa usahihi. Itasaidia vile vile katika kumsafisha yeye mwenyewe ili hatimaye malipo ya Dowans yatakapolipwa Watanzania wajue kwa uwazi nani ananufaika nayo n.k.

 1. Rostam Aziz ana uhusiano au ushirikiano gani wa kibiashara na Brig. Jen. (mstaafu) Suleiman Mohammed Al-Adawi wa Oman na Falme za Kiarabu ambaye ndiye mmojawapo wa wenye hisa katika Kampuni ya Dowans Tanzania Limited na Dowans S.A?

  Swali hili ni muhimu kidogo kwa sababu jawabu hili litatudokeza kwa kwa mfano maslahi ya kifedha ambayo Rostam anayo katika malipo ya Dowans. Kimsingi ninachouliza ni je kuna biashara yoyote au kampuni yoyote ambayo Rostam na Al-Adawi wana ushirika wowote (iwe wa kihisa, kikazi au kiushirika)?

 2. Wakati wa kampeni ya mgombea wa Urais kwa tiketi ya CCM, Rostam Aziz alikuwa ndiye Meneja wa kampeni hiyo. Jukumu lake mojawapo lilikuwa kutafuta fedha kwa ajili ya kampeni hiyo ikiwemo kupokea michango ya watu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

  Mmojawapo wa watu ambao inadaiwa kuchangia kampeni hiyo kiasi kikubwa ni Al Adawi. Je, Rostam anaweza kutuambia, Al-Adawi alichangia kiasi gani kwenye kampeni ya Rais Kikwete kuingia Ikulu 2005?

 3. Ukiondoa mchango wa Al-Adawi ambaye ni mtu wa karibu (na alikuwa mtu wa karibu) na watawala wa Oman na wale wa Falme za Kiarabu, ni mtu gani mwingine kutoka katika nyumba/familia hizo ambaye alitoa mchango kwenye kampeni ya Kikwete?

  Swali hili linataka kuelewa kama kwa kiasi chochote watu wafamilia hizo walikuwa wanatarajia kupata maslahi fulani baada ya Kikwete kuingia madarakani.

  Hili ni kweli vile vile kwani inafahamika baadhi yao walichangia kampeni ya CCM mara ya pili kumuingiza Mkapa madarakani mwaka 2000 na matokeo yake ni yale ya Yaeda Chini.

  Je, yawezekana watu wale wale ambao wameshaligusa taifa kwenye Loliondo, na Yaeda Chini ndio wale wale watu wa Dowans Holdings S.A?

 4. Rostam alipewa nguvu ya kisheria ya kufanya kazi kwa niaba ya Dowans Holdings S.A mwishoni mwa mwaka 2005. Kuanzia wakati ule hadi leo hii hatujaisikia kampuni ya Dowans ikifanya shughuli nyingine yoyote zaidi ya kuhangaika na haya majenereta.

  Je, Rostam Aziz tangu mwanzo alijua kuwa kampuni yake iliundwa ili kuingia mkataba wa kuleta majenereta ya nishati na imekuwa ni jukumu lake kuhakikisha kuwa Dowans ndio wanapewa mkataba huo tangu mwanzo?

  Na kuwa kitendo cha serikali (yakiwa ni maslahi ya kina Msabaha na wenzake) kutoa mradi huo kwa Richmond ilivuruga mpango wa awali wa kuipa Dowans tenda?

 5. Kutokana na hoja ya 4 hapo juu Rostam Aziz alipewa mamlaka hayo ya kuwa mwakilishi wa kisheria wa Dowans Holdings hapa Tanzania na Wakurugenzi wa kampuni ya Dowans Holdings S.A ya Costa Rica. Tunafahamu majina ya wakurungi hao kuwa ni Bernal Zamora Arce na Noemy del Carmen Cespedes Palma.

  Tunafahamu kuwa Arce na Palma ni watu wanaohusika na uanzishwaji wa makampuni mbalimbali kwa ajili ya kuficha wamiliki halisi huko wao wenyewe wakijipa Ukurugenzi. Wamefanya hivyo kwa makampuni ya Renalco Financial Services, Citigate Management Services Ltd, Westfield Finance Services na ASCN Information Technologies Ltd yote yakisajiliwa huko Uingereza.

  Tunafahamu Arce anaanuani ya makazi Uingereza na Costa Rica. Na tunafahamu kuwa Ukurugenzi wa kampuni siyo umiliki wa kampuni.

  Hivyo kwa kadiri tunavyojua Palma na Arce siyo wamiliki/pekee wa Dowans Holdings S.A. Wanatekeleza wajibu wa kisheria tu wa makampuni ya Costa Rica kuwa ni lazima yawe na angalau na maafisa watatu.

  Nyuma ya hawa wakurugenzi wapo wamiliki hasa wa Dowans S.A ambao walimchagua na kukubaliana na Rostam kuwa awakilishe maslahi yao je, Rostam yuko tayari kuwataja hadharani wamiliki halisi wa kampuni ya Dowans Holdings S.A ambao majina yao yako Costa Rica na ambao miongoni mwao ni watu wa karibu yake sana?

 6. Akiwa ndiye mwakilishi wa kampuni ya Dowans Holdings S.A hapa Tanzania na ambaye kutokana na maamuzi yake ndiye alisimamia uanzishwaji wa kampuni ya Dowans Tanzania Limited (iliyowapachika Ukurugenzi wale waliotajwa na Waziri Ngeleja mapema mwaka huu) alijua lini kuwa kampuni yake mama ya Dowans Holdings S.A ilikuwa imeshaingia mkataba na Richmond kuchukua mkataba wa TANESCO bila ya kuihusisha TANESCO kama mkataba ulivyotakiwa?

  Na tangu alipojua na akiwa ni Mbunge wa Jamhuri ya Muungano alifanya nini kutoa taarifa kwa vyombo husika kuwa utaratibu umekiukwa na hivyo ilikuwa sahihi kwa TANESCO ivunje mkataba?

  Je, yawezekana kutokana na mgongano wa maslahi ya kifedha Rostam alijua asingeweza kufanya hivyo wakati analipwa na wamiliki halisi wa Dowans Holdings S.A? Je, itakuwa makosa kwa Watanzania wengine kuhoji uzalendo wake hasa kwa nchi yetu hasa akikubali kuliachia taifa liingizwe kwenye mzigo mkubwa wakati yeye ndiye mtu pekee ambaye angeweza kuzuia jambo hilo akiwa ndiye mwakilishi halali wa Dowans Holdings S.A?

 7. Kwa vile Rostam alinukuliwa mapema mwaka huu akidai kuwa kuwa fedha ambazo Dowans inaidai TANESCO ni fedha “ndogo” sana kwake na anaweza kuzitengeneza kwa miezi michache tu kutokana na shughuli zake za ndani na nje ya nchi.

  Je, haoni kuwa baada ya kuliachilia taifa kuingizwa kwenye mkataba mbovu, na kwa kushiriki kwake anahusika moja kwa moja na deni la TANESCO?

  Je, itakuwa makosa kwa wananchi kudai kuwa kwa vile yeye ameshakiri kuwa anautajiri mkubwa hivyo ataonaje akiamua kulipa deni hilo la TANESCO yaani, ajilipe yeye mwenyewe na akishalipa asiuze majenereta hayo (kwani ndiye mtu pekee mwenye uwezo wa kuruhusu yauzwe) na badala yake ayatoe kama sadaka au msaada kwa TANESCO ili kusaidia upungufu wa nishati ya umeme nchini?

 8. Kwa vile tunajua kuanzia kwenye utangulizi wa mada huu na ufuatiliaji wa kisiasa nchini kuwa kuna uhusiano usivonjika kati ya Rostam na Rais Kikwete katika masuala mbalimbali (binafsi na ya kisiasa) na tunafahamu kuwa kuingia kwa Dowans nchini kuokoa jahazi lilioshinda TANESCO ilikuwa ni sehemu ya mpango uliopangwa mapema tangu wakati wa kampeni yaani hata kama isingetokea Richmond bado Dowans ingeweza kufanikiwa kupata tenda ya kuleta majenereta.

  Ni kwa kiasi gani Rais Kikwete anahusika na kampuni hiyo ya Dowans? Na ni kwa kiasi gani Andrew Chenge, Mwanyika, Lowassa n.k wanahusika na umiliki wa kampuni hiyo? Je, itakuwa siyo haki kudai kuwa Rais Kikwete naye ana hisa (kwa jina lake yeye mwenyewe au familia yake) kwenye kampuni ya Dowans S.A?

  Yawezekana hili ndilo linalofanya ulazima wa malipo ya Dowans uwe mkubwa hivi kiasi cha kumfanya hata Rais kushindwa kuchukua msimamo wa “kutokulipa” licha ya ushahidi wote uliopo mbele yetu wa jinsi gani mradi mzima ulisukwa ili kukinufaisha kikundi cha wanasiasa na wafanyabiashara wachache wa ndani na nje ya nchi?

 9. Ni kwanini yeye mwenyewe hajaweka majina yake kwenye makampuni mbalimbali yanayotajwa kuwa ni yake na kwa machache mengine amebadilisha badilisha majina kana kwamba ni watu tofauti?

  Kwa mfano taarifa ya Jarida la Africa Intelligence la mwaka 2009 ilidaiwa kuwa katika kampuni moja aliandikisha “wakurugenzi” (kama kina Bernal Zamora Arce) ambao walifanana majina na yeye mwenyewe - Rustom Aziz Sakarr, Rustam Sakarri, Rustam Sakaari, na Rostom A. Sakarr.

  Je, yawezekana alifanya hivyo kwa makusudi ya kutaka kuficha kuwa yeye ndiye mmiliki na mkurugenzi pekee wa makampuni hayo? Je, wananchi wamuone vipi? Kama amekuwa tayari kutumia uficho wa namna hiyo wakati anaanzisha makampuni hapa Tanzania yawezekana kweli kwake kushindwa kuanzisha makampuni nje ya nchi kwa kutumia majina ya watu wengine?

Ninaamini maswali haya ni maswali ya kuweka mambo sawa na kwa vile tunaamini kuwa Rostam ameonyesha uzalendo wa kuipenda nchi yake kwa kufungua biashara mbalimbali nchini na kujiingiza katika siasa na hata kutusaidia kupata Rais ambaye yeye alimuunga mkono.

Lakini katika mazingira ya sasa hivi nchini na pote duniani na hasa kutokana uelewa mpya wa wananchi wa Tanzania kuwa ufisadi umekithiri na kuwa wamechoka kuendelea kufanywa mazezeta ambao wanafuata tu kila wanachoambiwa.

Na hasa baada ya kuangalia jinsi gani mataifa mengine wananchi wameamka kudai haki zao, je itakuwa ni makosa kama Watanzania wakijua uzito wa suala la Dowans na wahusika wake kumtaka Rostam yeye mwenyewe akiongozwa na dhamira yake kuamua kujizulu ubunge wa Igunga na nafasi zake zote katika chama ili kuonesha kuwajibika kwake kwa kuliingiza taifa kwenye mkataba mbovu wa Dowans na zaidi ya yote kushiriki katika kudai shirika la walalahoi la umeme limlipe yeye na wenzake karibu bilioni 100 huku tayari wakiwa wameshapata karibu kiasi kama hicho kabla ya mkataba kuvunjika?

Kweli Rostam na walinzi wake serikalini wanataka wananchi wafanye nini ili wawajibike katika suala la Dowans?

Kwa ufupi ni kuwa Tuzo ya Dowans haipunguziki, hailipiki, hawalipwi na wakilipwa… Waangalie nchi nyingine zilizotengeneza, kulea, na kulipa mafisadi watawala wake wako wapi leo hii.

No comments: