Sunday, February 20, 2011

MAFISADI WETU NA NYERERE KUSUSIA CHAKULA LONDONGodfrey Dilunga

WAZIRI Mkuu wa 48 wa Uingereza (1976 hadi 1979), James Callaghan, aliyefariki Machi 26, mwaka 2005 akiwa mzee wa miaka 93, angeielezea vyema Tanzania na alivyomfahamu Julius Nyerere.

Callaghan, kwa jina la utani Gentleman Jim au Big Jim, alitambua uthabiti wa Tanzania kusimamia inachokiamini bila woga kwa vigezo vyovyote. Iwe kigezo cha maslahi ya taifa, rafiki au wafadhili.

Pengine hadi anakufa, Gentleman Jim alikuwa akiikumbuka zaidi Tanzania katika tukio lililomfedhehesha katika ulimwengu wa wanadiplomasia.

Mwalimu Nyerere alimsusia chakula cha mchana alichokiandaa kwa heshima zote za kiitifaki. Kususa huko msingi wake si ugomvi kati ya viongozi hao.

Msingi ulikuwa ni kuendeleza uthabiti wa Tanzania kuendelea kusimamia harakati za ki-utu na ki-maadili. Balozi wa Tanzania nchini Uingereza mwaka 1977, Amon Nsekela, ni shahidi wa tukio hilo.

Tanzania ya Nyerere iliamini na kupigania ukweli kuwa; utu na maadili si masuala ya kuhodhiwa kimahakama.

Si wigo wa kisheria pekee unaostahili kutumika ili kufikia kilele cha utawala bora wenye misingi ya utu na maadili.

Katika harakati za kufikia kilele cha utu na maadili hakuna ulazima wa Mahakama kuhodhi hatima; nani afanye nini au aadhibiwe kwa kiwango gani.

Waliamini harakati za ki-utu na ki-maadili, mbali ya kuwa na fursa za kisheria katika kusimamia, lazima zipate ulinzi na utetezi wa ki-mazingira. Yaani wasaliti wawajibishwe kwa ushahidi wa mazingira.

Mwalimu na wenzake waliamini kwa dhati kuwa mazingira ya ki-mahakama si pekee yanayojenga mustakabali wa utawala bora wa utu na maadili (hata baadhi ya majaji, wanasheria hawana utu wala maadili).

Mfano wa Mwalimu kususia chakula cha Gentleman Jim unatofautiana kabisa na dhana mbovu ya CCM inayoshindwa kuwawajibisha watu wachafu (mafisadi), kwa ushahidi wa mazingira.

Ilikuwa Agosti 13, mwaka 1977, CCM ikiwa na umri wa miezi saba tu (mwaka huu imefikisha miaka 34), Rais Nyerere alipokataa kuhudhuria chakula cha mchana mji wa Chequers, jirani na London, kilichoandaliwa na Gentleman Jim.

Alikataa si kwa sababu chakula hicho kingemdhuru afya. Bila shaka alikataa kama ishara ya Tanzania kupigania msimamo wa ki-utu na ki-maadili.

Nyerere alikataa kuhudhuria chakula hicho kwa sababu tu Callaghan pia alimwalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya makaburu ya Afrika Kusini, Pik Botha.

Mbali na kula, ilitarajiwa pia Mwalimu azungumze na Callaghan kuhusu Zimbabwe iliyokuwa iking’ang’aniwa na mlowezi Ian Smith.

Balozi Nsekela ndiye aliyetumwa kumtaarifu Callaghan kwamba; Nyerere amekataa kuhudhuria lakini yuko tayari kukutana naye (Callaghan) Airport kuzungumzia suala la Zimbabwe.

Nyerere alikuwa amekwenda Uingereza kukutana na Callaghan akitokea katika ziara ya Marekani, Canada na Jamaica. Ususiaji huo wa chakula ulikuwa ni uamuzi uliotokana na dhamiri ya ki-utu na ki-maadili.

Ujasiri wa namna hii wa Nyerere na viongozi wenzake kwa wakati huo, akiwamo Balozi Nsekela, ndicho kinachokosekana ndani ya CCM kongwe ya miaka 34. Tujadili kwa mwelekeo ufuatao.

Undani wa Nyerere kususa

Ingawa sababu kuu ni kutokubali ‘kukaa meza’ moja na Waziri Pik Botha, kuna mengi yanaibuka.

Kwanza ni Tanzania kujivunia kuwa upande wa kutetea utu na maadili. Pili, kupigania utu na maadili. Tatu; kulinda na hata kuratibu misimamo ya ki-utu na ki-maadili.

Mwalimu na wenzake walijivunia kuwa upande wa watetezi wa utu na maadili bila hofu. Walipigania utu na maadili si ndani ya nchi bali hata nje.

Walilinda misimamo ndani na nje ya mipaka kwa gharama yoyote, hata kuhatarisha uhusiano wa kidiplomasia.

Walihatarisha uhusiano wa kidiplomasia wa Tanzania kwa maslahi ya wanaopuuzwa ki-utu na ki-maadili, bila kujali mipaka ya nchi iliyowekwa na mkoloni.

Viongozi wajifunze nini?

Katika tukio hilo, hakuna kibali cha mahakama eti Nyerere asusie chakula kama ishara ya kupigania utu na maadili. Dhamiri ya ki-utu na ki-maadili ndiyo iliyowasukuma viongozi wa wakati huo.

Kwa kawaida, dhamiri safi haihitaji uamuzi wa mahakama kwa sababu hata mahakama wakati mwingine haina dhamiri safi.

Dhamiri safi ki-utu na ki-maadili ndiyo inayojenga mazingira safi yanayopinga ufisadi. Mazingira safi ndiyo yanayoibua ushahidi wa mazingira dhidi ya fisadi au hujuma za kifisadi.

Dhamiri safi, mazingira safi ndivyo vinavyokosekana au kupuuzwa na CCM kongwe, tofauti na ilivyokuwa CCM ile changa iliyokuwa na miezi saba tu!

Rais Jakaya Kikwete amehutubia miaka 34 ya kuzaliwa CCM, akisema watu wamekichoka chama ingawa kinatekeleza Ilani yake kwa asilimia zaidi ya 90.

Kinachoshindwa kuzungumzwa ni kuwa; hata kundi la wezi au mafisadi wanaweza kutunga Ilani, wakajenga barabara za juu na chini au miundombinu ya kila aina.

Lakini pamoja na kufanya hivyo, wananchi wengi werevu hawatawaamini. Watakapojenga barabara ya Kilomita 200, wananchi wataamini ilipaswa kujengwa ya Kilomita 400.

Hawataaminika kwa sababu hawana msingi wa maadili wala utu. Ufisadi umeua utu na maadili yao. Hawataaminika kwa kuwa hawana uhalali ki-utu wala ki-maadili.

Hawataaminika bila hata ushahidi wa kimahakama, ushahidi wa mazingira hasa kuporomoka kwa utu na maadili yao vinatosha kuwaondolea imani ya umma.

Kitendo cha wenye utu na maadili (wachache) ndani ya CCM, kwa mfano, kuridhia wasio na utu wala maadili kinyume cha mantiki ya hatua ya Mwalimu Nyerere kususia chakula, ndicho kiini cha CCM au taasisi yoyote kutogusa nyoyo za watu hata kama wataleta maendeleo ya vitu.

Kwa hiyo, katika mazingira ya tukio lile la Nyerere viongozi wasafi wajirejee kupigania utu na maadili wakiamini ndiyo njia ya kufikia kilele cha utawala bora.

Nyerere alisusia chakula si kwa sababu mahakama ilimtaka afanye hivyo, au eti alisubiri uamuzi wa mahakama. Alisusia kutokana na nguvu ya dhamiri ya ki-utu na ki-maadili.

Je, tunaweza kujirudi kitaifa?

Dhamiri safi inaweza kuongoza harakati za ki-utu na ki-maadili katika sehemu mbili.

Mosi, mahakamani. Pili; nje ya mahakama. Si lazima kumwondoa mtu aliyeyumba ki-utu na ki-maadili kusubiri hukumu ya mahakama. Ushahidi wa mazingira unatosha.

Ifahamike, wanaoshindwa kuwajibishana kwa ushahidi wa mazingira hawana dhamiri safi katika juhudi za kurejesha Taifa bora zaidi ki-utu na ki-maadili. Tuanze kuwatia alama, tukisubiri uchaguzi ujao.

Wadau wa sheria wakiwamo wa serikali wanaotutia katika mikataba kichaa na wengine, wafunguliwe milango ya kuadhibiwa ki-mahakama.

Kwa upande mwingine; CCM hasa vyombo vyake - Kamati Kuu na Halmashauri Kuu na vyama vingine au taasisi nyingine nchini vianze kujivika dhamiri (spirit) mpya chini ya mwongozo wa dhamiri ya Mwalimu Nyerere na wenzake kwamba; utu na maadili si lazima vipiganiwe mahakamani pekee.

Kama Nyerere alisusia chakula ili kulinda dhamiri safi ki-utu na ki-maadili, kwa nini leo CCM, vyama au taasisi nyingine viendelee kujadili mustakabali wa nchi na wasio na dhamiri safi, wenye dhamiri za kifisadi.

Kwa pamoja, katika miaka mitano hii tupambane na dhamira za kifisadi, kizandiki na kinafiki katika kila taasisi, vyama vya siasa, vyombo vya dola, vyuoni, shule za sekondari na msingi, mashambani na viwandani.

Viongozi wenye dhamiri safi ki-utu na ki-maadili wanapaswa kumuenzi Mwalimu Nyerere aliyesusia chakula, akihatarisha uhusiano wa kidiplomasia nchini kwake, kwa sababu ya kupigania dhamiri safi ndani na nje ya nchi.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

Simu:
0787-643151RAIA MWEMA

No comments: