Tuesday, February 22, 2011

KAMANDA AMESEMA ATABOMOA HADI OFISI ZA CCM ZILIZO BARABARANI

*ASEMA TANESCO, WIZARA YA MAJI WAMEKALIA NAO KUTI KAVU


WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli (pichani) ametangaza msimamo wake mbele ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu kwa kusema, "nitabomoa nyumba zote zilizomo kwenye hifadhi ya barabara hata kama ni mali ya CCM, kwani nimekula kiapo cha utiifu kusimamia sheria za nchi."

Kadhalika, Dk Magufuli amesema ofizi za Makao Makuu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), na Makao Mkuu ya Wizara ya Maji, nazo zipo katika hifadhi ya barabara na kwamba ikiwa kutakuwa na mpango wa upanuzi wa barabara ya Morogoro, nazo zitalazimika kubomolewa kwa mujibu wa sheria.

Dk Magufuli ameshaanza kutekeleza msimamo wake huo baada ya kuagiza ubomoaji wa Ofisi ya Wakala wa Barabara (Tanroads), Mkoa wa Dar es Salaam ambayo iko chini ya wizara yake.

Ofisi hiyo iliyokuwa imejengwa katika eneo la Kituo cha Mabasi ya Abiria Ubungo jijini Dar es Salaam tayari imekwishabomolewa.

Akizungumza wakati na baada ya kikao kati ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Wizara na wadau mbalimbali ikiwamo Polisi na Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA), Dk Magufuli alisema hata ofisi ya Tanesco na Wizara ya Maji na Umwagiliaji, zimo ndani ya hifadhi ya barabara.

"Lazima tuwe wakweli..., mimi nimekula kiapo cha utiifu kwa sheria za Jamhuri ya Muungano. Niliapa mwisho nikasema ewe Mwenyezi Mungu nisaidie..., naamini atanisaidia na ninyi naomba mnisaidie," alisema Dk Magufuli na kuongeza;

"Ile ofisi ya Tanesco na Wizara ya Maji ziko ndani ya hifadhi ya barabara huo ndiyo ukweli. Kama ukifika wakati barabara ikihitaji kupanuliwa, sheria itachukua mkondo wake tu na hakuna jinsi."

Aliendelea "majengo yote yaliyomo ndani ya hifadhi ya barabara yatabomolewa bila kujali ni ya CCM, Chadema au CUF. Katika sheria hakuna ubaguzi. Sheria ni msumeno, haiangalii nani tajiri au masikini."

… asema lazima mabango yaondoke Dar

Katika hatua nyingine, Magufuli ameziwekea ‘mgumu’ Halmashauri za Jiji na manispaa nchini akisema, "mabango yote yaliyomo kwenye barabara zetu tutayang'oa. Haiwezekani nyumba ajenge mwingine halafu aje mtu apangishe bila kukuarifu."

Dk Magufuli alifafanisha kitendo cha halmashauri kuingia mikataba ya kuweka mabango kwenye maeneo ya barabara za Tanroads kwa kisingizio cha kupata kodi, na mtu aliyejenga nyumba yake, lakini akaibuka mtu mwingine na kupangisha bila hata kumpa taarifa mwenye nyumba.

Dk Magufuli alienda mbali zaidi na kusema, "Tutayang'oa mabango yote yaliyomo kwenye barabara zetu. Lakini, huko kwenye barabara zao za halmashauri hata wakiyaweka katikati ni juu yao hatuna shida... hatuwezi kuona msongamano unachangia kuangusha uchumi, kisa kodi za watu ili wakalipane posho za vikao."

Alifafanua kwamba, kama wafanyabiashara wanataka kulipa kodi, ni vema fedha zao ziingizwe kwenye Mfuko wa Barabara ambao hugawa fedha kwa ujenzi na ukarabati wa barabara kuu na za halmashauri, kuliko fedha hizo kwenda katika Serikali za Mitaa na kutumika kuwapa posho watendaji.

Alisema Mfuko wa Barabara kwa mwaka uliopita, kila Mtanzania alichangia na kwamba matarajio ni kukusanya Sh284 bilioni.

Kauli hiyo ya Magufuli imekuja wakati Halmashauri za Manispaa za Jiji la Dar es Salaam zikijipanga kufikisha suala hilo katika ofisi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Hivi karibuni Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Raphael Ndunguru, alinukuliwa akisema kuwa wanajaribu kuangalia suala hilo kisheria ili kuona waliotekeleza hayo wana mamlaka yapi.

Alisema walikutana katika kikao cha pamoja na manispaa za Ilala na Temeke na kuzungumzia chanzo hicho cha mapato kwa halmashauri na yamewekwa kwa kuzingatia kanuni na taratibu.

“Hatukutendewa sawa mabango yale hayawezi kuchangia kutokea kwa ajali wala si uchafu bali yanapendezesha mji …..lakini kitendo cha kuyaweka alama ya x ndicho kilichosababisha uchafu na tumekubaliana kutoyaondoa kabisa,” alisema.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuf Mwenda, alisema wanatarajia kutoa tamko kwa kuwa si kitendo cha kiungwana kilichofanywa cha kuweka alama ya x, kwani mabango hayo ndicho chanzo kikuu cha mapato.

“Kama kulikuwa na tatizo basi sisi ni sehemu ya Idara ya Serikali tungekaa na kujadiliana na si kuweka uchafu kama walivyofanya,” alisema.

Pia Mkurugenzi Mtendaji wa ZEK Group International, Edwin Sannda, wa kampuni zinazojihusisha na uwekaji mabango ya matangazo nchini, amemshauri Waziri Magufuli kusitisha agizo lake la kutaka mabango yaliyoko kandokando ya barabara kuong’olewa badala yake akutane na wadau wote ili kujadiliana juu ya mfumo unaofaa kwa nia ya kuepuka usumbufu na athari ambazo zimeanza kujitokeza.

Mwishoni mwa mwaka jana, Dk. Magufuli alitoa maelekezo kuwa hataki kuona katika hifadhi ya barabara mabango ya matangazo kwa madai kuwa ni chanzo cha ajali.

Agizo hilo lilifuatiwa na uwekaji alama ya X kwenye mabango na mengine kuondolewa au kuharibiwa bila wahusika kupewa notisi au kushirikishwa.

Jana Waziri Magufuli, mwenye msimamo mkali katika usimamizi wa shughuli zilizo chini ya wizara yake, alisema hakuna anayeweza kuzuia mabango hayo yasiondolewe na kusisitiza kuwa “wakati ukifika yataondoka”.

Kauli yake kuhusu msongamano Dar

Kuhusu hatua za kuondoa msongamano, Dk Magufuli alisema Jiji la Dar es Salaam linakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwamo ongezeko la magari binafsi kutoka 231,197 yaliyokuwa yamesajiliwa mwaka 2005 hadi kufikia 805,000 mwaka jana.

Dk Magufuli alitaja hatua za haraka zilizopangwa kuchukuliwa na wizara yake kupunguza msongamano kuwa ni pamoja na kusimamia kwa ukamilifu sheria zinazodhibiti uegeshaji magari, kuzuia uegeshaji ovyo wa magari, kuzuia matumizi mabaya ya barabara na kufufua vituo vya daladala ambavyo sasa vinatumiwa kwa shughuli nyingine.

Magufuli alitaja hatua nyingine kuwa ni kusimamia utaratibu wa malori kuingia mjini na kutafuta maeneo ya maegesho ya magari na malori makubwa, kuweka vituo vya mabasi ya daladala katika maeneo sahihi na salama na kusimamia utaratibu mzuri wa kuegesha malori katika eneo la bandari.

Akichangia hoja hiyo Mbunge Henry Shekifu alihoji kama ripoti za nyuma za maoni ziliwahi kufanyiwa kazi na kuongeza, "nikiwa mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, tuliwahi kutoa ripoti ya kushauri, hivi haya mawazo ya wataalamu huko nyuma yamefanyiwa kazi kweli?"

Hata hivyo, kauli hiyo ilionekana kutomfurahisha mwenyekiti Peter Serukamba, ambaye alisema, "wajumbe naomba tuelewane, kila zama na kitabu chake. Wenzetu walisema acheni na sisi tuseme."

Kauli hiyo ya Serukamba ambayo ilionekana kutoelewa mantiki na umuhimu wa hoja ya Shekifu, ilionekana kutomfurahisha mbunge huyo ambaye alijipanga kuifafanua mchana lakini, hakupewa nafasi.


CHANZO: MWANANCHI

No comments: