Thursday, February 24, 2011

ATCL NAYO YASHTAKIWA MAREKANI
Ramadhan Semtawa

JINAMIZI la taasisi za serikali kushtakiwa nje ya nchi na kudaiwa mabilioni ya shilingi, limehamia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ambalo limeburuzwa kortini na Kampuni ya Celtic Capital Corporation ya Marekani likidaiwa sh 1.6 bilioni huku Shirika la Ndege Afrika Kusini (SAA) likidai Sh6.3 bilioni, kutokana na kuvunja mkataba.


Mpaka Desemba 31, mwaka jana, deni la ATCL lilikuwa Sh 75.99 bilioni, ambazo kati ya hizo, Sh 24.34 bilioni zilikuwa deni la ndani na Sh 51.65 bilioni, deni la nje likiwamo la SAA na Celtic Capital Corporation.

Kati ya madeni hayo, ya nje, zipo dola 24.72 milioni (sawa na Sh 37 bilioni), ambazo ni za Kampuni nyingine ya Wallis Trading Inc, linalotokana na kukodi ndege ya Air Bus A320.

Taarifa ya hali ya utendaji ya ATCL kwenda kwa Kamati ya Bunge ya Miundimbinu, ambayo gazeti hili, imefanikiwa kupata nakala yake jijini Dares Salaam jana, inaonyesha tayari mahakama,nchini Marekani imetoa kibali cha kukamatwa mali za shirika hilo, kwa ajili ya kufidia deni.

Waziri wa Uchukuzi Mhandisi Omar Nundu,alifafanua kwamba hadi sasa, licha ya kupata kibali cha mahakama cha kukamata mali za ATCL, bado wadai hao hawajaweza kukamata mali yoyote ya shirika.

Kwa sasa nchi inatikiswa na kesi ya Dowans ambayo Mahakama ya Usuluhishi ya Kibiashara ya Kimataifa (ICC-Court), imetoa hukumu kwa kuagiza Tanesco kuilipa kampuni hiyo, Sh 94 bilioni, hatua ambayo inapingwa kwa nguvu na Watanzania wengi.

Ukiacha ya ICC dhidi ya Tanesco, tayari pia Kampuni ya City Water, iliwahi kuishataki serikali katika mahakama hiyo ya kimataifa, lakini ilibwagwa, huku pia Kampuni ya Richmond nayo iliishtaki Tanesco na kushindwa.


Kuhusu sakata la ATCL, ripoti hiyo, inaonyesha deni la shirika hilo, hadi kufikia Desemba 31, mwaka jana lilifikia Sh75.99 bilioni, ambazo deni la ndani na Sh24.34 bilioni, Sh 51.65 bilioni ni deni la nje na kati ya madeni hayo ya nje, dola 24.72 milioni (sawa na Sh37 bilioni) ni deni la Kampuni Wallis Trading Inc, litokanalo na kukodi ndege ya Air Bus A320.

Mhandisi Nundu Waziri mwenye dhamana ya usafiri wa anga, alisema madai ya Celtic Capital Corporation yanahusu kukodisha ndege na la SAA linatokana na kuvunjwa mkataba huo, mwaka 2006.

ATCL ilifunga ndoa na SAA Novemba 2002, baada ya kubinafsishwa lililokuwa shirika la Ndege Tanzania, ambalo shirika hilo la kigeni lilinunua hisa asilimia 49 za serikali ndani ya ATC, hata hivyo ubia huo, ulikabiliwa na matatizo ya kiundeshaji na kulazimika kusitishwa Agosti, 2006 na shirika hilo, kurejeshwa serikalini.

Wakati mzigo huo, ukiwa juu ya ATCL ambalo liko taabani, Kampuni ya China Sonongol International Limited (CSIL), imejitoa katika ununuzi wa hisa za ATCL na hivyo, kuondoa ndoto ya shirika hilo kufufuka kwa kupata mtaji wa zaidi ya sh 500 bilioni.

Nundu alifafanua kwamba , Machi 2007 serikali ilifanya mazungumzo na CSIL na kusaini hati ya makubaliano (MoU) ili kuendeleza shirika hilo, na kampuni hiyo, ilikubali kusaidia mpango wa muda mrefu uliopaswa kuanza mwaka 2007/08, kwa kuahidi kutoa kiasi hicho ambacho ni dola 507.7milioni na kwa kuanza ilitoa dola 20 milioni (sh 23bilioni).

"Mpango huo, ungewezesha ATCL kununua ndege tisa za kisasa. Kwa kuanzia utekelezaji CSIL ilitoa zaidi ya dola 20.21 milioni (takribani Sh30 bilioni) kwa ATCL ikiwa ni pamoja na kununua ndege mbili aina ya Bombardier Dash8- Q-300 ambazo ni mali ya ATCL,"alisema. Mhandisi Nundu.

Alisema CSIL ilikubali kununua asilimia 49, ya hisa za serikali ndani ya ATCL na serikali ya Tanzania iwe na hisa asilimia 51.

"Hata hivyo, kwa sasa CSIL imebadili msimamo wake kuhusu ununuzi wa hisa za ATCL. CSIL imeeleza haiko tayari tena kuwa mwanahisa katika Kampuni ya Ndege Tanzania," alifafanua Nundu.

Alisema kutoka na msimamo huo, wizara ilishindwa kuendelea na majadiliano na CSIL na imependekeza kusitisha mazungumzo na kampuni hiyo ya China.


Kuhusu hatua nyingine za kutafuta wawekezaji

Waziri Nundu alisema serikali, imeanza mazungumzo ya awali na Shirika la Ndege la Uturuki (Turkish Airlines) na Kampuni ya Borodino kutoka Urusi.

"Majadiliano ya awali na Turkish Airlines yalifanyika Oktoba 2010, ambayo kimsingi, Uturuki imeonyesha ingependa kuanzisha kampuni mpya kwa ushirikiano na serikali ya Tanzania badala ya kuwekeza kwenye ATCL,"alisema.

"Kimsingi kampuni ya Borodino inapendekeza ianzishe kampuni mpya ya ndege hapa nchini ambayo itamilikiwa kwa asilimia 100 na Borodino. Majadiliano na kampuni mbili, yataendelea,''alisema.

ATC imekuwa ikikabiliwa na hali mbaya kifedha tangu ilipofunga ndoa na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) ambayo ilivunjika katika mazingira tata na kuacha shirika hilo, likiwa taabani.


MWANANCHI