Saturday, January 8, 2011

WANASHERIA WAJIANDAA KUIPINGA DOWANSNa John Daniel

SAKATA ya malipo ya mabilioni ya walipa kodi kwa Kampuni ya Dowans limeingia katika hatua mpya baada ya jopo la wanasheria kuungana na kuanza kupitia vifungu vya sheria kwa lengo la kupinga hukumu hiyo iwapo itasajiliwa katika
Mahakama Kuu ya Tanzania.

Hoja ya wanasheria hao ni ya nne katika kupinga kile kinachotwa kuwa ni hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara ICC tangu kuibuka kwa madai hayo.

Hoja nyingine zilizowahi kutolewa ni uhalali wa kampuni husika ambayo inaelezwa kuwa ni hewa na wamiliki wake hawajulikani, uhalali wa kiasi kilichotajwa kuwa ni sh. bilioni 185 huku taarifa nyingine zikionesha kuwa ni dola milioni 64.2 karibu sawa na sh. bilioni 90 za Tanzania.

Hoja nyingine ni uhalali wa madai hayo kutangazwa kabla ya hukumu ya usuluhishi kusajiliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania kama inavyotakiwa kisheria, hali iliyosababsiha wananchi kuhusisha madai hayo na mbinu chafu za kifisadi.

Wakizungumza na Majira jana kwa sharti ya kutotajwa wala ofisi zao kwa madai kuwa itavuruga maandalizi yao, wanasehria hao walisema serikali ina nafasi kubwa kisheria kukwepa kulipa madai hayo kupitia Mahakama Kuu."Tayari kazi ya kupitia vifungu kadhaa vya sheria kuokoa nchi yetu na malipo haramu ya Dowans imeanza, tunasubiri tu wasajili tu maamuzi ya usuluhishi ili tuanze kazi.

Hadi sasa hatuna anayegharamia lakini tutajitolea kuonesha uzalendo wetu," alisema mtoa habari wetu.Wanasheria hao walisema hadi sasa kuna mambo makubwa manne yanayowapa uhakika kuwa suala hilo bado ni nyepesi kusitishwa kupitia Mahakama Kuu ya Tanzania.

Walitaja mambo hayo kuwa ni pamoja na uhalali wa Kampuni iliyouzwa kwa Dowans ya Richmond ambayo Kamati ya Bunge ilithibitisha pasipo shaka kuwa ni feki na haipo, hivyo kulazimu kuvunjwa kwa mkataba huo.

Sababu ya pili kwa mujibu wa wanasheria hao ni kifungu cha sheria kinachooruhusu madai dhidi ya mdai, (Counter Claim) inayohusisha Dowans na madai mbalimbali ya kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).Walisema kwa mujibu wa sheria hiyo, bado serikali inaweza kuomba tuzo hiyo kusikilizwa upya kwa kuwa kilichofanyika ni usuluhishi na si maamuzi ya Mahakama ya Rufaa.

Sababu nyingine ni kifungu cha 15 ya sheria za usuluhishi wa migogoro ya kibiashara za Tanzania kutoa haki kwa Mahakama Kuu kusitisha tuzo hiyo iwapo upande wowote utakuwa umekosea taratibu zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyingine wanasheria hao wamezidi kumkalia kohoni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, na kuhoji jinsi alivyoweza kupitia na kutoa maamuzi ya haraka kuhusu malipo ya Dowans.Walisema yapo majalada mengi yanayosubiri maoni au maamuzi ya Jaji Werema lakini bado hajafanyiwa kazi.

"Lakini pia tuna shaka ni kwa nini Mwanasheria Mkuu wa Serikali apitie jalada hilo haraka na kutoa jibu kwa muda mfupi hata kabla ya tuzo kusajiliwa Mahakama Kuu."Yeye mwanasheria Mkuu ana majalada mengi yanayosubiri ushauri au maamuzi yake lakini hayajafanyiwa kazi, inakuwaje hii akaishughulikia haraka na kutoa jibu jepesi kiasi hicho?" alihoji mwansheria mwingine.Kwa mujibu wa sheria namba 15 ya usuluhishi wa migogoro ya kibiashara nchini ambayo Majira inayo nakala yake Mahakama Kuu ina mamlaka ya kusitisha malipo ya tuzo hiyo na kutoa nafasi kwa mdaiwa kuendelea na utaratibu mwingine wa kisheria.

Majira ilipofika Mahakama Kuu kujua iwapo Dowans imesajili hukumu hiyo ya ICC ili kutoa nafasi kwa hatua nyingine, Msajili wa Mahakama Kuu, Bw. Ignas Kitusi alisema hawajapokea tuzo hiyo.Alipoulizwa iwapo taratibu za Mahakama Kuu zinaruhusu mwanya kwa hukumu hiyo kusikilizwa upya alisema hawezi kuzungumzia suala la kisheria ambalo halipo na kuweka wazi kuwa wanashangaa wanaojadili kitu ambacho hakipo.

"Sisi kisheria bado hatuna hata habari na hiyo tuzo ya Dowans maana hautujaipata, hatuwezi kuzungumza kitu ambacho hakipo, sheria haibahatishi," alisema.

No comments: