Friday, January 7, 2011

WABUNGE WA CHADEMA WASOMEWA SHITAKA NA KUACHIWA KWA DHAMANA






Joseph Ngilisho,Arusha


VIONGOZI na wafuasi 31 wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo {CHADEMA} leo wamefikishwa mahakamani na kusomewa shitaka moja la kufanya mkusanyiko usio halali katika mahakama ya mkoa wa Arusha iliyokuwa na ulinzi mkali wa askari polisi wenye silaha za moto na mabomu ya machozi.

Akisoma mashitaka mbele ya hakimu mkazi,Charles Magesa, Mwendesha mashtaka wa serikali,Haruni Mategara na Zacharia Isalia alisema kuwa washitakiwa wote kwa pamoja walitenda kosa hilo januari 5 mwaka huu, majira ya mchana kwa kufanya makusanyiko na maandamano yaliyopigwa marufuku

Waliopandishwa kizimbani ni pamoja na Mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama hicho Freeman Mbowe{49},Mbunge wa jimbo la Moshi mjini Philimon Ndesamburo{77},Godblles Lema Mbunge wa Arusha mjini{34} na Joseph Selasin{50} mbunge wa jimbo la Rombo mkoani Kilimanjaro.

Viongozi wengine wa Chadema waliosomewa mashitaka mbele ya hakimu Mfawidhi wa mkoa wa Arusha Charles Magesa ni pamoja na katibu mkuu wa Chadema Taifa Willbroad Slaa{62},Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Arusha Derick Magoma ‘’junior’’{30} ambao wote kwa pamoja walikana shitaka hilo.

Washitakiwa sita akiwemo mke wa Slaa Josephine Slaa{40} wamesomewa mashitaka katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru kwani wamelazwa katika hospital hiyo kwa matibabu ya majeraha waliyopata jana.

Wafuasi wengine wa Chadema waliosomewa mashitaka na wanasheria wa serikali Zakaria Elisaria,Robert Roghart na Hamis matagana ni pamoja na Richard Mtui{26},Acquline Chuwa{52},Dady Igogo{26],Juma Wambura{42},Basil Lema {41} na Kennedy Bundara{30}.

Wengine waliosomewa ni pamoja na Proaches Kimario{22}, Nai Stephen{25} ,John Materu{32}, Eusebio Akaro{42}, Bakari Kijuu{32}, Goodluck Kimario {23}, Elisante Noel {23}, Kelvin Onyango{31}, Michael Kimario{30}, Prosper Kimario{26}, Peter Marua{33}, Frank Logath {26}, Mathias Valerian {23}, Walter Mushi{30}, Pancras Kimario{35} Swalehe Salumu{25}, Mevorongori Lukumay{42} na Daniel Taitas.

Washitakiwa wote 31 wameachiwa kwa dhamana ya ahadi ya shilingi milioni mbili kila mmoja, na kesi hiyo itatajwa tena januari 21 mwaka huu,baada ya mwanasheria wa serikali kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Mara baada ya kuachiwa huru Dkt Slaa aliwasihi wananchi waliofurika katika mahakama hiyo kuwa watulivu wakati huu kwani vyombo vyote vya ulinzi na usalama vimeshirikiana na Chadema katika kutafuta haki ya msingi.

Hata hivyo Mbunge wa jimbo la Arusha mjini Godbless Lema yeye aliwataka wananchi kuacha woga na kudai kuwa ili uweze kupata haki yako inayoporwa haina haja ya kuogopa bali ni kupambana mpaka dakika ya mwisho.


WAZIRI WA MAMBO YA NDANI ATOA TAMKO

WAKTI HUOHUO, serikali leo mchana imependekeza pande zinazosigana katika siasia mkoani Arusha zikae meza moja na kutafuta suluhu kwa mazungumzo na sio kwa vurugu. Hayo yamesemwa mchana huu na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mh. Shamsi Vuai Nahodha alipoongea na wanahabari ofisini kwake jijini Dar, akiwa na Inspketa Jenerali wa Polisi, Afande Saidi Mwema, ikiwa ni siku moja baada ya kutokea vurugu baina ya polisi na wafuasi wa CHADEMA baada ya kufanya maandamano yanayodaiwa kuwa si halali. Inasemekana watu wawili wamepoteza maisha na sita wamejeruhiwa vibaya katika vurumai ya jana.
Mh. Nahodha, ambaye amekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibra kwa muda mrefu na mwenye uzoefu wa mambo hayo, amesema serikali imeamua kuingilia kati mgogoro huo kwa kuziweka meza moja pande mbili zinazokinzana ili kuleta amani mpya na kuidumisha jijini Arusha.
Pia Mh. Nahodha amesema askari polisi yeyote ambaye itathibitika alikwenda nje ya mipaka yake ya kazi atachukuliwa hatua kali za kisheria.

No comments: