Thursday, January 6, 2011

VIGOGO(CCM)WAWATIBUA VIONGOZI WA DINI

  • Krisimasi yatumika kuwaumbua wababaishajiNCHI imegawanyika kuhusu namna inavyoongozwa, viongozi serikalini na ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakitofautiana kwa kiasi kikubwa na viongozi wa dini, pamoja na makundi mengine ya jamii, Raia Mwema, imebaini.

Ni mgawanyo unaotokea katika wakati ambao mtandao wa Wikileaks ukivujisha taarifa za uovu wa viongozi nchini ambao miongoni mwao wameuripoti kwa ofisa balozi wa Marekani.

Kuthibitika kwa taarifa mbaya dhidi ya Tanzania kuhusu viongozi wake kula njama za kununua rada ya kijeshi kwa bei ghali na kisha kugawana fedha, ni kati ya mambo yanayozidi kuitenga Serikali kimtazamo na wananchi, wakiwamo viongozi wa dini.

Ni dhahiri sasa, falsafa zinazounda hoja kongwe za CCM na serikali yake kuhusu ubora wake wa kiuongozi katika kulinda amani na utulivu inaanza kupuuzwa, katikati ya pengo la wenye nacho na wasio nacho kuzidi kupanuka.

Mtazamo wa viongozi wengi wa dini sasa unaashiria kuchoshwa na mwenendo wa mambo, baadhi ya mambo hayo ni kujilimbikizia mali miongoni mwa viongozi wa umma bila kuchukuliwa sheria.

Wimbi la ukosoaji limeonekana kupamba moto zaidi wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Krisimasi, viongozi wa madhehebu ya kikristo wakinguruma kuashiria kutoridhishwa na mwenendo wa uongozi nchini.

Safu ya ukosoaji wa nyendo za viongozi serikalini na mamlaka nyingine za dola haikumtenga Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo pamoja na Askofu Dk. Valentino Mokiwa.

Maaskofu wengine katika orodha hiyo ya kutoridhishwa na hali halisi nchini ni pamoja na Dk. Alex Malasusa na Askofu Stephen Mang’ana. Wamo pia mapadri na wachungaji wengine wengi.

Akionekana kutoridhishwa na wimbo unaochosha wa kulinda amani na utulivu ilihali umasikini ukizidi, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, akiongoza misa ya mkesha wa Krisimasi katika Kanisa la Mtakatifu Thomas, Mikocheni Dar es Salaam, aliweka bayana kuwa amani haipatikani kwa kuilazimisha.

“Wengi wanadhani tunaweza kujipatia amani kwa nguvu yetu wenyewe. Tunapofikiria amani itakuja kutokana na wenye uwezo kufanya mipango ya amani au kuilazimisha.

“Malaika wanatupatia picha tofauti na hiyo (mtazamo huo). Amani haiji kwa mabavu bali ni kama paji la Mwenyezi Mungu linalopatikana kama mwanadamu atampa Mungu utukufu,” alisema Askofu Pengo na kuweka bayana kuwa amani ni jambo ambalo Mwenyezi Mungu “anatukirimia.”

“Amani haitategemea wenye mamlaka bali ni kila mmoja wetu kwa kumtukuza Mungu. Tusitegemee kuleta amani kama nasi tutashiriki kuandika mikataba ambayo kabla wino haujakauka mitaa imejaa damu,” alisema.

Katika kile kinachoweza kutafsiriwa kuwa hoja kongwe katika falsafa za kiutawala serikalini na chama tawala zimeanza kupoteza mvuto, Pengo alisema si lazima kupiga kelele za amani ili uoenake mpenda amani bali amani inapaswa kuanzia moyoni mwako.

“Si lazima tupige kelele za amani, ianzie ndani ya mioyo yetu, ienee ndipo tutakuwa na uhakika wa amani. Naweza kuongea sana lakini siwezi kuwa chanzo cha amani kama sina amani moyoni mwangu,” alisema.

Siku iliyofuata akiongoza ibada katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, Kardinali Pengo alikemea matumizi mabaya ya madaraka, ikiwa ni pamoja na kujilimbikizia mali.

“Ustawi hauwezi kupatikana katika Taifa letu kwa kuwa bado kuna wachache wanafurahia tabia ya kujilimbikizia mali, hali hiyo ipo hata katikati ya wakristo, ni vibaya kwa mtu kujilimbikizia mamilioni ya fedha kwa kuwanyonya wengine na kuwaacha wakifa njaa,” alisema Kardinali Pengo.

Ingawa Kardinali Pengo hakuweza kutaja kwa majina au kashfa mahususi inayohusu mtu au watu kujilimbikizia mamilioni ya fedha, lakini mfano halisi ni pamoja na wizi wa bilioni 133 kutoka Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA) Benki Kuu ya Tanzania.

Mifano mingine ya uthibitisho wa kauli hiyo ya Pengo ni hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Uingereza inayothibitisha kuwa Tanzania imenunua rada ya kijeshi kwa fedha nyingi ambazo ziada imegawanywa kama rushwa kwa maofisa wa serikali ya Tanzania.

Vinara wa matukio hayo hasa la rada bado hawajachukuliwa hatua yoyote na serikali ya Tanzania na katika wizi wa mabilioni ya EPA, wezi vigogo hawakufikishwa mahakamani baadhi wakiwa ni wamiliki wa Kampuni ya Kagoda Agriculture wanaotajwa kukwapua mabilioni mengi zaidi ya wengine.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa alisema amani hailetwi na mabadiliko ya taratibu, sheria, uongozi au matendo ya watu wa itikadi fulani bali amani ya kweli itakuja kwa watu kumuogopa Mungu.

Askofu wa Kanisa la Mennonite nchini, Stephen Mang’ana kwa upande wake alisema; “Moyo safi na mikono isiyo na udhalimu itaondoa tatizo la umeme, maji, uhaba wa dawa hospitalini, rushwa, ufisadi, uchakachuaji na matatizo mengine yanayolifanya Taifa kukosa amani na utulivu.”

Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Valentino Mokiwa alikuwa mkali zaidi akikemea taratibu za kuendeleza malumbano ya kisiasa baina ya viongozi.

“Jambo hili la kukemeana vikali na kutoa maneno ya kejeli ni kitu kisichofaa katika jamii yetu, hii ni dalili mbaya ya vyama vya siasa na serikali kushindwa kuongoza nchi.

“Tanzania inapita katika msongo wa mawazo, hili ndilo tunatakiwa kulitazama kwa makini, hivi sasa haki ya mwananchi imewekwa kwenye mabango, watu wanashindwa kupata huduma zao muhimu kutokana na ubinafsi na ubabe,” alisema Askofu Mokiwa.

Lakini katika kanisa la Mtakatifu Martha Manzese jijini Dar es Salaam siku ya Krisimasi kulifanyika ibada iliyoongozwa na Padri wa Kanisa hilo Baptisti Mapunda.

Katika mahubiri yake, tofauti na ilivyokuwa imezoeleka kwa muda mrefu na hasa juu ya ukimya wa Kanisa Katoliki katika kukosoa moja kwa moja uongozi ulioko madarakani, Padri Mapunda alianza kwa kukosoa baadhi ya mambo yaliyojitokeza kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita.

Katika hilo hakusita kuwaleza waumini wa Kanisa Katoliki baadhi yao kuwa ni sehemu ya waliopiga kura baada ya kuhongwa kwa fedha, fulana na hata pombe na hongo nyingine. Aliwaambia hayo kwa kuwahoji na baadhi walisikika wakipaza sauti ya kuonyesha kukubaliana na madai yake hayo.

“Uchaguzi umekwisha hivi baadhi yenu hamkupewa pombe, fulana na hata rushwa? Wengine wamesema hata uongo wakati wa Uchaguzi,” alisema.

Katika hali ya kuonesha kuanza kunusa dalili mbaya kwa Taifa, Padri Mapunda alishangazwa na ujasiri wa viongozi kuvumiliana katika matendo ya ufisadi akisisitiza kuwa kiwango hicho cha uvumilivu ni kinyume cha mambo yalivyopata kuwa wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Aliwahoji waumini waliohudhuria ibada hiyo akisema; “Je, Nyerere aliacha ufisadi na ubinafsi huu? Viongozi wetu wamejaa uroho wa madaraka na fedha.”

Hata hivyo, katika kuthibitisha kuwa viongozi wameshiba uroho wa madaraka na hata fedha, Padri Mapunda alisema baadhi wamefikia hatua ya kujinasibu kuwa watatawala milele huku wakifanya maovu kinyume cha matarajio ya wananchi.

“Anayetawala milele ni Yesu, si chama chochote cha siasa, labda tu uwe unatumia nafasi ya madaraka uliyonayo kutenda wanayotarajia watu yaani ukubali matakwa yote ya demokrasia.

“Leo hii ukiichambua Tanzania kama karanga utakuta kinachoendelea hapa si demokrasia bali ni domokrasia. Kumekuwa na viongozi wetu kwa ajili ya kudanganya watu ili wabaki madarakani.

“Mimi nasema najiamini siwezi kutumiwa na yeyote. Baadhi yetu raia wamekuwa wanashindwa kuhoji masuala ya msingi kwa nchi, mimi siogopi…nauliza na nitauliza.

“Haiwezekani eti unakwenda kwenye mkutano wa siasa ukiwa na njaa na anayekuhutubia ameshiba na unashindwa kumhoji maswali muhimu. Tunakwenda wapi? Tunapuuza kuwa msingi wa demokrasia ni ukweli.

“Nchi inatawaliwa na polisi, mashushushu, Katiba haifuatwi ni nchi ya kipolisi sasa hii ni hatari. Leo hii tunaadhimisha Krismasi tukubali kuwa Yesu alikuja kuondoa utawala wa mabavu.

“Kama hatutabadilika siku moja tutakuwa kama Kenya anaweza kuja hapa Ocampo na kukamata watu. Mfumo wa kisiasa na uchumi ni vizuri ukaachwa huru kusaidia watu wote kwa usawa, leo wengine tunaombea nchi yetu tukiwa na njaa lakini wengine wameshiba na kusaza.

“Mafisadi wanatazamwa, kwa nini Serikali haiwachukulii hatua, nchi inakwenda hii. Tazama ung’ang’anizi wa madaraka katika umeya Arusha na Mwanza sheria zinashindikana kufuatwa…tunakwenda wapi?

“Katika mazingira magumu kwa wananchi leo hii umeme unapanda bei ni sawa na tunakubaliana kurudi wakati wa matumizi ya koroboi, na gharama hizi zinapanda wakati vigogo mambo yao yakizidi kuwa safi…pato lao linaongezeka.

“Viongozi wetu wengi ni wenye ubinafsi, wanachojali ni madaraka yao si watu wanaowaongoza….nadhani lazima wabadilike. Tunapaswa kujimudu kutumia rasilimali zetu, Serikali lazima iwakilishe na kulinda maslahi ya watu wote,” alisema Padri Mapunda na kushangiliwa na waumini waliokuwa wakimsikiliza katika mwelekeo wa kuwa na hamu ya kusikia neno analotarajia kutamka baada ya kukamilisha kila sentesi.

“Lazima sasa tupate viongozi wanaomjali Mungu. Tunataka Katiba mpya na si maafikiano ya CCM na Chadema au chama kingine chochote. Tunataka pia Tume huru tumechoka kila wakati kusikia kura zimeibiwa.

“Katiba mpya si ombi kwa Rais ni suala la wananchi. Viongozi wa dini tupige kelele za Katiba mpya bila kuruhusu ubabaishaji ili tuwe na nchi ya amani, tupiganie Katiba mpya na tume huru.

“Tumechoka kudanganywa. CCM na Serikali wanatakiwa wakamilishe suala la Katiba mpya si ombi, ni haki ya wananchi…hawa ndio wanaopaswa kuulizwa juu ya Katiba mpya ni wananchi si Rais,” alisema.


RAIA MWEMA

No comments: