Friday, January 21, 2011

UVCCM WAWASHA MOTO


Fredy Azzah na Elias Msuya


KATIKA hali inayoashiria kuwa ndani ya CCM sasa kila mtu na lake, Umoja wa Vijana wa CCM jana umetoa matamshi makali huku ukiwanyooshea vidole baadhi ya watendaji ndani ya CCM, Baraza la Mawaziri na Serikalini.Kadhalika UVCCM kupitia katika tamko lake la jana wamesema iwapo serikali na chama chao hawatachukua hatua kuhusu yale waliyobainisha, basi wao “watakutana na kuamua cha kufanya”.

Jopo la wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la umoja huo katika mkutano wake na Jukwaa la Wahariri jana, liliweka bayana kutofurahishwa na uhusiano baina ya viongozi ndani ya CCM pia ndani ya Serikali, huku likionyesha kuipinga serikali katika mambo kadha wa kadha.

“Hatukuja hapa kwa bahati mbaya, tumedhamiria na tunaomba msipunguze makali ya maneno tutakayoyatumia katika kuwaeleza yale tunayokusudia..,” alisema Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Benno Malisa alipokuwa akitoa maeneo ya utangulizi kabla ya kuanza kwa mkutano huo na kuongeza: “Tunaomba kauli zetu ziende hivyo hivyo kama tutakavyozungumza”.

Katika mkutano huo kamati hiyo ya UVCCM ilieleza kuwa kabla ya kukutana na Jukwaa hilo la Wahariri ilifanya kikao chake juzi Januari 19 na kufikia makubaliano ya kuzunguza na vyombo vya habari jana.

Hatua hiyo ya UVCCM ni kama mwendelezo wa kauli zinazokinzana miongoni mwa viongozi waandamizi wa serikali na ndani ya CCM juu ya masuala mbalimbali ya kitaifa hususani mwelekeo wa kisiasa na suala zima la kampuni ya kufua umeme ya Dowans.

Katika mkutano wao na wahariri jana, kamatihiyo ya utekelezaji iliwatumia wajumbe wake zaidi ya saba kukamilisha tamko lake ambapo kila kipengele kilisomwa na mmoja wa wajumbe hao.

Vijana wa CCM na Mapinduzi
Mbali na kuwanyoshea vidole watendaji na Baraza la Mawaziri UVCCM imewataka vijana na viongozi wote wa chama hicho, kufanya mambo kimapinduzi kama lilivo jina la chama hicho (Chama cha Mapinduzi ), ili viongozi hao waendane na maana halisi ya jina hilo.

Akisoma sehemu ya tamko hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo mkoani Mara ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo ya utekelezaji, Marwa William Mathayo alisema kitendo cha baadhi ya viongozi kutopendana na kujenga uhasama na chuki ni aibu kwa CCM na si urithi mzuri kwa vijana wa leo.
“Wakumbuke kuwa wao walipokuwa vijana hawakuridhi chuki na uhasama miongoni mwao, vitendo hivi haviwezi kuvumika na UVCCM,” alisema Marwa.

Tamko hilo, liliwataka viongozi hao ambao hata hivyo hawakutajwa kwa majina, kuacha mara moja uhasama na chuki lililosema kuwa umejengeka katika msingi wa ubinafsi. “UVCCM unawataka sasa wale wote wanaoendekeza uhasama na chuki uliojengeka katika msingi wa ubinafsi waache mara moja. Vinginevyo utawataja kwa majina na kuwataka vijana kote nchini kuandamana na kuwalaani, maana uhasama na chuki zao zinaleta mipasuko katika jamii na chama kwa ujumla,” alisema Marwa.

Mwaka 2009 , CCM kiliwahi kuunda kamati chini ya Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, kuchunguza kiini cha chuki miongoni mwa wabunge wake ndani ya bunge.

Hata hivyo kamati hiyo ambayo ilikuwa na wajumbe wengine wawiliambao ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa na Spika wa zamani wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdulrahman Kinana ni kama haikuweza kuponya majeraha kwani hadi sasa yanadaiwa kuwepo.

Bodi ya mikopo ivunjwe
Kuhusu migomo inayoendelea katika vyuo mbalimbali nchini, UVCCM mjumbe mwingine wa kamati hiyo, Zainab Kawawa alisema hali hiyo inatokana na ukiritimba wa bodi ya mikopo. Alikwenda mbali zadi na kuitaka CCM ambacho ndicho kinachounda serikali, kuipindua rasmi Bodi ya Mikopo kwa kuwa ndio chanzo cha migogoro ya wanafunzi.

“UVCCM umebaini kwamba, kuna urasimu unaofanywa na watendaji na haiingii akilini, Mkwawa University wagome kwa kutolipwa posho zao na baada ya siku moja walipo posho zao baada ya kugoma. Jambo hili si utamaduni wa vijana wa kitanzania, wale wote wanaohusika CCM ichukue hatua,” alisema Zainab kwa niaba ya kamati hiyo.

Alisema kitendo hicho kinathibitisha kwamba tatizo siyo fedha bali ni uvivu wa watendaji walioko serikalini na “wanapenda kuwanyanyasa watanzania wenzao”.

Alisema UVCCM hawako tayari kuona vijana wakiendelea kugoma na kuwa, wale wote wanaotaka kuanzisha utamaduni mpya wa utawala ambao mpaka watu wagome ndipo ufumbuzi upatikane, wapishe. “Ofisi za Umma wawajibike mara moja na serikali iwafikishe mahakamani kwa kuisababishia hasara serikali,” ilisema sehemu nyingine ya taarifa hiyo.
Malipo ya Dowans
Katika tamko lake UVCCM pia imepinga mpango wa serikali kuilipa kampuni ya Dowans Sh 94 bilioni kama hukumu ya mahakama ya Usuluhishi wa kibiashara (ICC) ilivyoagiza.

Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji wa Baraza Kuu la umoja huo ambaye pia ni Mwenyekit wa Jumuiya hiyo mkoani Arusha, James Millya alisema pesa hizo ni nyingi kwa hali ya maisha ya Watanzania.

Hivi karibuni Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alitangaza nia ya serikali kulilipa deni hilo na kutaja kiasi hicho cha fedha tofauti na taarifa ya awali iliyoonyesha kuwa Tanesco ilitakiwa ilipe Sh 185 bilioni. Naye Mwanasheria mkuu, Jaji Frederick Werema alikaririwa mara kadhaa akiridhia serikali kulipa deni hilo kwa kile alichosema kuwa haiwezekani kukata rufaa kwenye kesi hiyo.

Lakini, jambo hilo lilipingwa wazi wazi na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta aliyekuwa pia Spika katika Bunge la tisa pamoja na Naibu Waziri wa Miundombinu Dk Harrison Mwakyembe aliyehusika kwenye kamati ya Bunge iliyochunguza mkataba wa kampuni hewa ya Richmond huku wanaharakati wa Kituo cha Sheria na Haki za binadamu wakifungua kesi Mahakama Kuu kupinga deni hilo.

Katika taarifa hiyo, UVCCM imetaka hoja hiyo irudishwe Bungeni ili Watanzania wajue nani aliyeifikisha mahali ilipo sasa.

“Kama ni Tume ya Dk Mwakyembe, ieleze kama ilishiriki kulidanga Bunge na iwajibike. Kama ni serikali basi imtaje huyo Richmond ambaye ndiye aliyehamisha mali zake kwa Dowans na atakiwe kulipa badala ya pesa za walipa kodi wa Tanzania ambazo zingesaida shughuli za maendeleo,” alisema Millya.

Alisema haiwezekani Richmond itajwe kuwa ni kampuni hewa hali kukiwa na taarifa kwamba kampuni hiyo ndiyo ilihamishia kazi zake kwa Dowans.

“Hao Dowans waliotajwa na serikali ambao ndiyo walionunua mali za Richmond waisaidie serikali yetu kuwataja wamiliki halali wa Richmond, ili wao ndiyo wawajibike kuzilipa pesa hizo badala ya serikali,” taarifa hiyo ilisema.

UVCCM pia imelaani kitendo cha mawaziri kupingana hadharani ikieleza ni kukosa uwajibikaji wa pamoja, na kwamba iwapo mawaziri wamechoka kuziongoza Wizara zao waachie ngazi, wawapishe vijana wenye nia njema ya kuongoza na kufuata maadili ya Taifa.

Katika mkutano huo na Jukwaa la Wahariri UVCCM pia ulieleza kutofurahishwa kwake na viongozi wa dini kushabikia baadhi ya vyama vya siasa na kusema kwa kufanya hivyo wanawagawa waumini wao.

“UVCCM unawaomba viongozi wa dini, waheshimu imani za waumini wao na wasijiingize katika kuwachagulia vyama vya siasa au itikadi,” alisema Malisa.

MWANANCHI

No comments: