Friday, January 7, 2011

UDINI WA KIJINGA NA CHUPA YA POMBE


Na M.M Mwanakijiji

TANZANIA upo udini; tena udini wa kijinga. Udini na ujinga unaendana kama mlevi na chupa ya pombe. Huwezi kumkuta mdini asiye mjinga kama vile huwezi kumkuta mlevi asiyelewa. Naam, kuna wakati unaweza kumkuta mlevi akiwa timamu na akizungumza na kutenda kama mtu timamu lakini haitakuchukua muda mrefu kuweza kumshangaa anavyokuwa pindi anapolewa.

Vile vile mdini. Mdini ukikutana naye unaweza kabisa kufikiri ni mtu timamu au ni mwenye elimu hadi pale atakapoanza kuzungumzia mambo ya udini na ndipo utajua ni ujinga gani uliomkumba. Narudia tena ili kusiwe na utata wa kile ninachokisema kuwa Tanzania upo udini, tena wa kijinga.

Kwa vile nilitoa tafsiri ndefu ya udini kuwa ni kitu gani hasa baada ya kuitofautisha na kile kinachodhaniwa ni udini leo nataka niende mbele zaidi. Nilionesha wiki mbili zilizopita kuwa udini siyo idadi, udini siyo majina, udini siyo kuwa na imani au kutangaza imani yako na kuwa udini siyo tofauti ya kidini. Nilionyesha kuwa udini ni mtazamo na hisia zinazojengwa au kujengeka ndani ya mtu na kumfanya mtu huyo aamini mambo fulani hasa aidha ya kustahili zaidi kuliko watu wengine wenye tofauti ya dini naye au kujiona duni kwa sababu hiyo hiyo. Nilisema kuwa ni mtazamo wa hatari zaidi tofauti na mitazamo ya ukabila au ubaguzi wa rangi kwani katika udini jambo hili linagusa maisha ya milele.

Leo nataka nidokeze kidogo na kufafanua kwa nini mitazamo hii katika Tanzania msingi wake na inavyoendelezwa inategemea sana ujinga kuliko ukweli au kitu kingine chochote. Lakini kwanza nifafanue ujinga ni kitu gani ili tusije tukatofautiana maana wapo ambao hadi hivi sasa wanaweza kuwa wanafikiria nimewatukana.

Ndugu zangu, ujinga ni hali ya kiakili ya mtu kutokujua jambo fulani ambalo anaweza kujulishwa na akalijua na hivyo kuondokana na hali hiyo. Hivyo ujinga si hali ya kudumu bali ni hali ya muda ya kutokujua; japo kwa upande mwingine ni hali ya kudumu ya kila mwanadamu kwani kila mtu ana ujinga juu ya kitu fulani au jambo fulani.

Ni kutokana na ukweli huo wanadamu hujifunza na kufundishwa mambo fulani fulani na katika kufanya hivyo huanza kujiondolea hali hiyo ya ujinga kuhusu jambo hilo. Tuliposema kuwa maadui wetu wakubwa ilikuwa ni ujinga, umaskini na maradhi ukweli ni kuwa adui mkubwa kati ya hao alikuwa ni ujinga. Inasikitisha kuwa miaka karibu hamsini sasa bado kuna watu kati yetu ambao wanakumbatia ujinga kama rafiki wa kudumu.

Tunawapeleka watoto chekechea, shule ya msingi, sekondari, vyuoni na hata baadaye watu wanapata mafunzo ya juu kuhusu mambo mbalimbali. Katika kufanya hivyo tunawapatia watu na sisi wenyewe nafasi ya kujifunza juu ya mambo ambayo vinginevyo tusingeweza kuyajua.

Hivyo, jukumu kubwa la mwanadamu katika maisha yake ni kujifunza ili kuzidi kujua; hili linawezekana kufanyika kwa kupitia elimu rasmi au elimu isyo rasmi. Ni wazi kuna mambo ambayo watu wengine hujifunza rasmi kwa sababu yameshafanyiwa utafiti wa kutosha na kujulikana vya kutosha kiasi kwamba mtu mmoja hana sababu ya kuanza sifuri kujifunza.

Ndio maana basi hatuwezi kumuacha mtu aanze kujifanyia upasuaji wa mtu mwingine au kuanza utibabu wa mifugo kwa kutumia utaalamu wa miaka 100 iliyopita wakati kuna sehemu ambapo utaalamu huo umehifadhiwa na unapitishwa kutoka kundi moja kwenda jingine. Sehemu hii inaitwa vyuo. Hivyo, ujinga huondolewa kwa kiasi fulani fulani kwa kupatiwa uelewa na ujuzi wa mambo fulani.

Sasa ukikutana na mtu ambaye ni mjinga na ambaye hataki kujulishwa ili aondokane na ujinga huo ili awe miongoni mwa wajuao basi hujakutana na mjinga wa kweli; kwani mjinga wa kweli (kama mimi) yuko tayari kujulishwa ili aondokane na ujinga wake.

Mjinga ambaye hataki kuondokana nao amevuka mpaka wa ujinga na huwa katika kundi la wapumbavu. Sasa haya yote si matusi msije kunijia juu. Tofauti kubwa ya ujinga na upumbavu ni kuwa ujinga huweza kuondolewa.

Nimesema udini uliopo Tanzania ni wa kijinga. Maana yake kama kweli tunataka kuondokana nao ni lazima tujulishwe mambo fulani fulani ambayo pasipo kujulishwa kwake tutaendelea kuwa na hizi hisia au mitazamo ya ubora au uduni kwa misingi ya tofauti za kidini. Ni makusudio yangu katika sehemu hii ya pili kudokeza mambo kadhaa ya udini ili tuyajue na tujijue sisi wenyewe na katika kufanya hivyo tuweze kufanya jitihada ya makusudi ya kuondokana na hisia hizi kati yetu na ndani yetu.

Watanzania wana dini tofauti

Jambo la kwanza ambalo siyo geni na sote tunalijua kiakili ni kuwa Watanzania wana dini tofauti. Kabla ya kuja kwa waeneza dini wa Kikristu na Kiislamu waafrika wa ukanda wetu walikuwa na dini tofauti tofauti. Hata taratibu zao za kusali au kufanya ibada zao za jadi zilikuwa ni tofauti tofauti kulingana na makabila na hata ndani ya makabila uliweza kukuta tofauti fulani fulani za ukoo na ukoo. Wangoni walivyotolea sadaka mahoka wao ilikuwa ni tofauti na Wahaya walivyofanya ibada zao na Wasukuma na imani zao walikuwa ni tofauti na Wachagga na imani yao.

Lakini sijui ni katika historia gani uliwahi kusoma wazee wetu wa jadi wakipigana kwa sababu ya tofauti za kidini? Ni wapi ulisikia Wahehe na Wabena waligombana ati kwa sababu mmoja alikuiwa hasali kama mwingine au alikuwa haamini kama mwingine. Lakini zaidi ni wapi katika historia yetu uliwahi kuona wazee wetu wa jadi wakishindana juu ya ubora wa dini moja ya jadi kuliko dini nyingine.

Yawezekana zilikuwepo tofauti nyingi za kiutawala na maisha lakini migogoro karibu yote (sijaona hata mmoja nitakuwa tayari kusahihishwa) haukuwepo uliojengwa kwa msingi wa tofauti za kidini za jadi. Lakini leo hii sisi wajukuu na vitukuu vyao ati tunapata shida kutofautiana bila kufanyana duni au kupingana bila kutishiana kupigana! Wenyewe tunajiona tumeendelea au tumepiga hatua au tuna imani sana! Kweli tuna imani kuwashinda kina MwanaMalundi? Tuna imani sisi kuliko kina Kinjekitile Ngwale? Ni ujinga tu.

Kumbe leo hii bado sisi tuna tofauti mbalimbali za kidini; tofauti hizi hazikuanza na Uislamu au Ukristo; ni tofauti za asili kabisa dini hizi mbili zimeingia na kuleta tofauti ambazo tayari zilikuwepo. Hivi mmesikia lini wapagani wa Tanzania wakilalamika kuwa dini zao hazipati hadhi inayostahili?

Hivi, mmesikia lini wapagani wa Tanzania wakitaka kitu fulani kifanywe kwa ajili yao? Tena ukifikiria sana utaona kuwa hawa wenzetu wenye imani za jadi wana haki ya kudai zaidi kutoka kwa watawala wetu kuliko sisi wengine tuliokumbatia dini za kigeni! Lakini wao wanaenda kulima kama kawaida, wanaendelea na shughuli zao za kulijenga taifa lao na wala hawajioni duni mbele ya mtu yeyote.

Uchaguzi ulifunua udini wetu wa kijinga

Uchaguzi huu uliopita ulifunua hisia hizi za kidini kwa kiasi cha kutufanya sote tuone aibu. Hata watu ambao tuliamini ni watu wenye hekima wote walijionesha wazi wanavyoguswa na udini huu. Na ukweli huu umetokana na jambo moja kubwa kwamba wagombea wawili wakuu wa vyama vyetu vilivyokuwa vimeshikana pembe walikuwa wanatoka dini mbili tofauti. Kikwete akiwa ni Muislamu na Dk. Slaa akiwa ni Mkristo.

Wote wawili hawa walinufaika kwa namna moja au nyingine na hisia hizi za udini na hakuna hata mmoja kati yao ambaye aliweza kweli kushughulikia watu wa dini yake vizuri ili asinufaike na udini wao. Mgombea wa CCM Kikwete alijua kabisa kulikuwa na hisia za Waislamu kuona kuwa anachaguliwa kwani baadhi yao waliona kuwa anaonewa au kushutumiwa kwa sababu ni Muislamu na si kwa sababu ya uongozi wake na hivyo walijitokeza watu ambao walitumia hili la dini kumtetea Kikwete. Hakuna wakati hata mmoja ambapo Kikwete aliwakemea Waislamu hawa kwamba wasimuingize kwenye masuala ya udini; alikemea 'udini' bila kusema ni upi!

Vile vile Dk. Slaa naye alijua wapo watu ambao walikuwa wanaona kuwa yeye ni bora zaidi kwa sababu ya dini yake na kundi hilo la Wakristo ambao walikuwa wanaona wasingependa kuongozwa tena na Muislamu kwani walikuwa wamechoka. Kundi hili yawezekana lilikuwa na tatizo na uongozi wa Rais Kikwete lakini kwao tatizo kubwa lilikuwa ni kwa vile ni Muislamu.

Makundi yote haya mawili yaliachwa yakafanya shughuli zao wengine kwa uwazi kabisa wengine kwa kutumia majukwaa mbalimbali. Katika kuachwa hivyo wakapenyeza sumu yao ya udini kwa watu wengine. Lakini haitoshi kusema tu hivi hivi ipo haja ya kutoa mifano miwili ya kuonesha jinsi gani hisia au mtazamo huu wa kidini ulijitokeza katika uchaguzi, ukavumiliwa, ukakumbatiwa na ukaachwa kuchanua.

Makanisa na viongozi wake dhidi ya JK

Mojawapo ya mambo ambayo yametokea wakati huu wa uchaguzi ni majibizano ya kiana kati ya viongozi wa kanisa na uongozi wa Rais Kikwete. Haijawahi kutokea wakati wowote ambapo viongozi wa kanisa wamekuwa na nguvu na uwezo wa kusema mambo dhidi ya serikali iliyoko madarakani kama wakati huu.

Kwa juu juu tunaweza kuona kuwa kanisa linafanya kazi yake ya 'kinabii'; lakini huu unabii ambao unaonekana kuwa na nguvu wakati wa uongozi wa Muislamu ni unabii wenye mashaka. Viongozi wa Kanisa wamekuwa wakali na wakati mwingine hata kuonyesha mgongano wa wazi dhidi ya Rais Kikwete; ni nani amesahau yaliyotokea Mwanza au yale yaliyotokea Mbeya wakati wa kampeni?

Lakini viongozi hawa hawa hawajahi kutoa tamko lolote dhidi ya yale yaliyofanywa wakati wa utawala wa Rais Mkapa ambaye ni Mkristu. Kashfa za EPA, Meremeta, manunuzi ya Rada na ndege ya Rais vyote vilifanyika wakati wa Mkapa. Lakini hadi hivi sasa haya yanapozungumzwa inakuwa kama yalifanyika chini ya Serikali ya Kikwete.

Hakuna viongozi wa dini ya Kikristo ambao wamekuwa na ujasiri wa kutaka Mkapa na watendaji wake wawajibishwe (hata kama wametoka madarakani). Sasa huu unabii wao unachagua? Sasa Muislamu aelewe nini katika hili? Inakuwaje viongozi hao hao wanajionyesha kuwa ni wakali wakati wa Richmonds/Dowans lakini walikuwa kimya wakati wa ITPL? Kwa nini inaonekana Mkapa alikuwa na nafuu wakati yeye naye ni mtu wa kutoka chama kile kile anachotoka Kikwete wakiwa na sera zile zile za kichama na wakitumia kimsingi watu wale wale?

Lakini safari hii makanisa na viongozi wake walienda mbali zaidi vile vile. Walikuwepo viongozi ambao walizungumza na umma na kufanya mambo ambayo mtu yeyote mwenye akili timamu alijua walikuwa wanamaanisha nini. Wapo ambao ati kwa mara ya kwanza walisitisha ibaza za Jumapili ili waumini wakapige kura; wapo ambao walishindwa kabisa kujizuia na siku ile ya uchaguzi wakizungumza kwa nyuso zenye matabasamu waliwaharikisha waumini wao waende kupiga kura na kufanya 'uamuzi sahihi'.

Dk. Slaa hakuwakemea viongozi wa Kikristo au makundi ya Wakristo yaliyokuwa yanaonekana kumpigia debe wazi.

Misikiti na viongozi wa dini ya Kiislamu

Lilikuwepo hata hivyo kundi jingine nalo ambalo lilikuwa limeapa kabisa kuwa haijalishi itakuwaje lakini 'Mkristo hamuondoi Muislamu'
. Kundi hili nalo halikufanya kazi yake kwa kificho; hawa walikuwaja na lengo moja tu nalo ni kumtetea Muislamu 'mwenzao'dhidi ya mbinu chafu dhidi ya makanisa. Ingetosha kama wangekuwa wanajibu uongo au mbinu mbaya dhidi ya Kikwete; lakini wao walienda mbali kwani na wao wakaanzisha mashambulizi dhidi ya Dk. Slaa kwa sababu ya dini yake.

Kwanza walishambulia Ukatoliki wake na vile vile walishambulia upadri wake. Mtu yeyote ambaye alikuwa anafuatilia siasa za Tanzania alikuwa anajua mapema kabisa kuwa Dk. Slaa aliwahi kuwa Padre wa Kikatoliki. Hili halikuwa jambo geni hata kidogo. Lakini lilivyoletwa kwenye kampeni liligeuzwa kuwa Ukatoliki dhidi ya Uislamu; kwamba 'Padri Slaa' ametumwa na Kanisa na hivyo akitawala atatekeleza matakwa ya Kanisa. Na wapo ambao waliamini kabisa hilo kwani lilitoka kwenye magazeti na radio ambazo waliziamini.

Wengine walienda mbele na kusambaza nyaraka kwenye misikiti wakitaka waislamu wajitokeze kwa wingi kupiga kura ili 'makafiri' wasije kumuingiza mtu wao. Mambo yaliyofanywa na baadhi ya wachungaji na mapadri makanisani ili kumuinua Slaa yalifanywa na baadhi ya mashehe na maimamu misikitini ili kumuinua Kikwete. Na kinachoshangaza hayakuwa siri! Haya wala hayakuhitaji 'deep cover' ili mtu aweze kuyafichua. Yalifanywa na mengine bado yanafanyika mchana kweupe.

Kikwete hakuwakemea viongozi wa Kiislamu au makundi ya Waislamu ambayo yalionekana kumpigia debe wazi wazi.

Ningeweza kwenda mbele zaidi lakini hapa itoshe kudokeza kuwa udini huu bado upo na msingi wake kama nilivyosema ni ujinga. Udini huu hautaondolewa kwa kunuia au kwa kusema 'tuachane na udini'. Ingekuwa ni rahisi hivyo, ubaguzi wa rangi ungetokomezwa kwa kusema 'tuachane na ubaguzi wa rangi'. Kama vile kauli za 'uzembe haufai' haziwezi kuondoa uzembe vivyo hivyo kauli tunazosikia kuwa 'Watanzania waachane na udini' haziwezi kuuondoa udini.

Kumbuka kama nilivyosema udini msingi wake ni ujinga. Hadi hivi sasa hakuna hatua zozote za makusudi na za kijasiri zilizochukuliwa ili kushughulikia udini. Unaweza kufikiria kwamba ukiwakamata wenye kupandikiza udini basi unakomesha udini. Hili si kweli hata kidogo. Udini hauwezi kuondolewa kwa kuwakemea wahusika au kwa kuwatia pingu watu - sijui kama tuna magereza ya kutosha labda siku hizi chache baada ya msamaha wa Rais!

Tusipoamua kwa dhati kushughulikia huu udini tunaliandaa taifa letu kuendelea kuwa katika mpasuko wa kudumu utakaokuwa unajirudia rudia kila baada ya miaka mitano au kila wakati ambapo wagombea wawili watakuwa wanatoka dini tofauti.

Na ukiangalia vizuri utaona kuwa hisia hizi sasa zimetoka kwenye siasa tu na kuanza kugusa ajira na mahusiano ya karibu. Wakati wananchi wa kawaida wanashirikiana bila kuulizana dini au kujali dini ya mtu mwingine wasomi wetu na watawala wetu wanazidi kusukumiza hii sumu taratibu.

Ndugu zangu, udini hauwezi kutoka hivi hivi; na kwa kadiri ya kwamba watawala wetu hawataki kuuita udini kwa jina lake halisi (ubaguzi wa kidini) wataendelea kujaribu kuficha vichwa vyao mchangani kama mbuni. Lakini hali ilipo sasa ni mbaya kwani yawezekana kuna mtu kaingia madarakani tena kwa sababu ya dini yake au kuna mtu kakataliwa kwa sababu ya dini yake. Vyovyote vile ilivyo, tunajenga msingi mbaya sana wa siasa zetu huko mbeleni maana tusipoangalia itabidi tuanze kuulizana dini kabla mtu hajaajiriwa ili watu wa dini fulani wasiwe wengi mahali fulani. Tutafikia mwisho tutakuwa tayari kupewe kiongozi ambaye hana uwezo alimradi tu ni wa dini yetu.

Nimesema kwa kirefu kuwa udini wetu Tanzania ni wa kijinga; lakini, jambo linaloendana na hilo ni kuwa udini uliopo Tanzania ni wa viongozi. Wadini halisi wa nchi hii siyo Wamachinga, vijana mitaani, kina mama na baba sokoni na wananchi vijijini! La hasha, wadini wa nchi hii wamehitimu katika vyuo mbalimbali, wanavaa tai na suti na wanaheshimiwa kama viongozi wa kada mbalimbali. Wadini wa Tanzania kundi la viongozi wa kisiasa, viongozi wa kidini na watendaji wa taasisi mbalimbali. Ndio hawa walioanzisha udini, ndio wanaupalilia, na ndio hawa hawa wanaotarajia kuvuna matunda yake. Na wao wenyewe wanaamini kabisa kuwa wanasema vitu vya 'kisomi' kumbe wanathibitisha tu kile kilicho wazi; ujinga unaohitaji kuondolewa kwa haraka.

Wakati umefika tuanze kuwakataa, kuwapinga na kuwabeza wanapomwaga sumu yao huku wakichanganya na kimombo ili kuonekana wanasema jambo la maana. Kama mabadu zetu waliondoa tofauti zao za kilugha, kikabila na kidini wakaunganishwa na imani ya kuukataa utawala wa Mjerumaini kwenye vita ya majimaji, zimefika zama sasa Watanzania wenye kujali Utanzania wao hasa kuwakataa na kuwapinga viongozi wadini ambao wanazungumza lugha za kidini, wanaovumilia udini na ambao wanaendelea kuchochea udini kiana. Ukitaka kumjua ni nani mdini - waulize wanaposema 'udini' wanamzungumzia nani! - Utaona kama watawataja watu wa dini zao! Ndio alama ya wadini wetu, kwamba udini uko kwa watu wa dini nyingine tu siyo kwao wenyewe na siyo kwa watu wa dini yao! Ni Udini wa Kijinga.

TANZANIA DAIMA

1 comment:

mtwangio said...

Mwana kijiji hakika umeweka vidole vya tiba katika donda ndugu kwa makala hii ambayo sidhani kwa wananchi wengi wa Tanzania wanaweza kufaidika nayo, na sababu ya kutofaidika nayo ni kutokana na kile ulichokiita(UJINGA WA KIDINI.
Kwa kuongezea maoni yangu mimi naona ujinga huu unatokana na sisi waafrika au sema mataifa ya kiafrika ambayo yaliyoletewa hizi dini kuu mbili za kigeni UISILAMU NA UKRISTO na kuzikumbatia kwa ujinga hii ukiongezea pia ajenda za nje za waleta dini zenyewe ambazo pia wanachangia kutufarikisha na kutuongezea ujinga mpaka kufikia kuwa na akili au mawazo mgando, kwa hoja au madai kwamba ni dini gani ya kweli na sahii na dini gani si ya kweli na potovu.
kuna ukweli mwingine wa wazi na usiojificha kwamba kanisa kuu la katoliki ni dola juu ya wakristo wote duniani na linakua na ajenda mbalimbali kwa waumini wao na hasa kuhakikisha kuwapandikiza wakatoliki katika nafasi zote za ngazi za juu ikiwemo urais na kwa vile waislamu hawana utaratibu wa Msikiti mkuu wa kuwatawala waislamu wote duniani,kama wakatoliki utakuta mataifa haya mawali ya kislamu Saudi Arabia na Irani hujenga na kueneza mtafaruko wa waislamu wenyewe kwa wenyewe kimadhebu na kisiasa mafano wa swala ya Eddi daima uswaliwa kwa udini wa kisiasa badala ya kusali kitaifa kwa wana dini moja hiyo.Hii hukiongezea kwamba wakati huohuo mataifa hayo huwa yanapigania kuhakisha waislamu wanashika nafasi za ngazi za juu kimadaraka ikiwemo urais.
Sasa kwa tatizo kuu la ujinga wa kidini ambalo umelichambua kwa kirefu wataalamu au viongozi wa dini hizi mbili kuu aidha kwa ujinga wao wa kidini au kwa kutekeleza ajenda za kanisa kuu la katoliki au ajenda ya Saudi Arabia au Irani tunajikuta nchi zetu daima tunaukumbatia huu ujinga wa kidini.
Kama ujuavyo daima wanasiasa wanatumia mbinu zote zile za halali na zisizo za kihalali ili wafike madarakani na daima huitumia dini au waumini wa dini zao ziwafikishe madarakani.
Utakumbuka Mwalimu Nyerere,baba wa taifa letu alieipenda nchi yake na wananchi wake alituhumiwa kwamba anawapendelea wakristo eti kwa sababu tu yeye ni mkristo tena wa mkatoliki huo ulikuwa ni ujinga wa kidini wa wafuasi wa kiislamu na kutulia moyo kwa wana dini ya kikristo.Na kwa kusisitizia zaidi ujinga wa wataalamu wetu wa dini hizo mbili pale mwalimu aliposema moja ya tamko lake mashuhuri kwamba''TANZANIA HAINA DINI,BALI WANANCHI WAKE NDIE WENYE DINI''Masikini,wafuasi na viongozi wa dini zote mbili hawakumuelewa mpaka alipowahutubia tena mapadri na masheikh kuwafafanulia msemo huo. kwa maana hiyo basi si wafuasi tu ni wajinga bali mpaka viongozi wao wa kidini ni wajinga wa udini.
Ebu mwangalie mwanasiasa kiongozi Rais wa awamu ya pili Hassani Mwinyi alikua msatari wa mbele kuuonyesha udini wake wakati yeye hakupaswa kufanya hivyo kwa vile alikuwa ni Rais wa nchi lakini amebaki kama ni Rais mwenye kuheshimiwa sana na waislamu kwa vile walimuona kma ni mkombozi wao kutokana na kukandamizwa kwa waislamu(kama wanavyodai)wakati wa utawala wa Baba yetu wa taifa Mwalimu Nyerere ambaye hakuwa kamwe mjinga wa udini wala kuitumia dini kwa masilahi yake kama mwanasiasa.
Mchango wangu katika tiba ya ujinga huu wa udini ni lazima kwanza viongozi wa kisiasa wawe msatari wa mbele na kuwa wakali na wenye kukemea ujinga huu wa udini na kutoitumia dini kwa masilahi yao ya kisiasa au kutumikia ajenda za nje za kanisa katoliki,saudi arabia au Irani.ushahidi wa wazi wa kulipuana mabomu na kuuana kila siku kwa wakareketwa wa ujinga huo wa udini hususa waislamu tunaziona na kuishi nazo duniani kuanzia pakistani,lebanoni,─▒raq na irani kumalizia tukio la kigaidi la kimataifa la Septemba 11 Amerika.Wanasiasa hao wachukue msemo wa Mwalimu Nyerere baba wa taifa ndio mongozo na dira ya kwamba''Tanzania haina dini bali watanzania ndio wenye dini''kwa maana dini yako ni ya kwako wewe mwenyewe na Mungu wako una uhuru wa kuabudu unavyotaka bila kuingilia,kudharau na kukebehi dini au itikadi ya mtu mwingine hata kama anaabudu jiwe au mizimu.