Sunday, January 30, 2011

TAARIFA YA MAFANIKIO YA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI MKOA WA MTWARAKutokana na athari zilizojitokeza katika misimu ya nyuma ya ununuzi wa korosho hasa msimu wa 2006/2007, ambapo wakulima hawakuwa na soko la uhakika na linaloaminika kwa zao la korosho, jambo lililosababisha wakulima wa korosho kuyumbishwa sana juu ya bei na hatimaye kuuza zao hilo la korosho kwa bei ya hasara na ya kutupa. Msimu wa 2007/2008 mfumo wa uuzaji wa zao la korosho kupitia stakabadhi za maghala ulibuniwa ili kutatua matatizo yaliyojitokeza nyuma.

Ilikuwa ni juhudi binafsi za mhe. Rais Jakaya Kikwete na serikali yake kulitafutia ufumbuzi swala hili na hivyo kuamua serikali ivilipie madeni vyama vya ushirika viweze kuaminika na kukopesheka. Mfumo wa stakabadhi ghalani ukaanzishwa kisheria (sheria Na. 10 ya 2005), kwa kutumia mazao kwenye maghala kama dhamana ya kupata mkopo kutoka kwenye benki na asasi zingine za fedha.

Tangu msimu huu ulipoanza kumekuwa na mafanikio makubwa kwa wakulima, vyama vya msingi na kwa halmashauri ya wilaya kwa ujumla. Baadhi ya mafanikio hayo ni pamoja na;

1. Mkulima anapata bei nzuri na ya uhakika na inayoongezeka kila msimu.Mfano(2007/2008-Tshs610/=,2008/2009-Tshs675/=, 2009/2010- Tshs 700/= , 2010/2011- Tshs 800/=). Hizi ni takwimu za bei dira, kuna malipo ya majaliwa ”BONUS” ambayo hutofautiana kutoka chama kimoja kwenda kingine, ambayo nayo yamekuwa yakiongezeka kila msimu.Malipo ya majaliwa hua kati ya Tshs 110 mpaka Tshs 340 kutegemea ubora wa korosho na bei ya mnada kwa kilo.

2. Ubora na thamani ya korosho imeongezeka.(Kutoka - Tshs 5,250,000,000/= mwaka 2009/2010, hadi Tshs 13,600,000,000 msimu wa 2010/2011) kwa wilaya ya Masasi.

3. Ununuzi holela (kangomba) umepungua kwa kiasi kikubwa.Ununuzi holela uliyumbisha bei na soko kiasi cha kukatisha tamaa uzalishaji wa korosho kupunguza ushuru.

4. Vyama vya msingi vya mazao na masoko vimeaminika na kukopesheka na vyombo vya fedha.(msimu wa 2010/2011- Tshs 13,600,000,000/=)

5. Ushuru wa korosho na michango mingine inakusanywa kwa urahisi zaidi na kwa uaminifu. Ushuru wa korosho na michango mingine kwa mfumo huu hukatwa na vyama vya msingi toka kwenye malipo ya korosho moja kwa moja na kuwakilishwa kwa Halmashauri.

6. Mapato ya Halmashauri yameongezeka kila msimu.(Mapato kwa msimu 2009/2010 ilikuwa Tshs 487,500,000, msimu wa 2010/2011 inatarajiwa kufikia Tshs 1,190,000,000/=)

7. Mfumo umeongeza ajira wilayani. Hapa zipo ajira za kwenye vyama vya msingi,lakini pia zipo ajira zilizotokana na watu kujiajiri kwenye kilimo cha korosho kutokana na kuvutiwa na soko/bei.

Pamoja na mafanikio haya yote, changamoto kubwa kwa misimu ya nyuma karibu yote kumekuwa na malalamiko ya hapa na pale juu ya malipo ya pili na ya tatu. Kuna baadhi ya maeneo walikuwa wanachelewa sana kulipa au hata kutolipwa kabisa malipo ya tatu, ikiwa ni pamoja na kukatwa pesa za ushuru na michango ya maendeleo.

Kwa msimu wa 2010/2011 kwa wilaya ya Masasi mpaka sasa tunapomalizia msimu wa ununuzi wa korosho mkulima ameshalipwa bei dira pamoja na malipo ya pili bila makato yeyote hivyo kufikia jumla ya Tshs 800/= kwa kilo. Amepata malipo haya bila usumbufu na bila kukatwa senti tano, tunajiandaa kulipa malipo ya tatu hivi karibuni,tunategemea yatakuwa mazuri na bila usumbufu pia.

Kuondoka kwa usumbufu kwa malipo ya pili kwa wilaya nzima na bila kukatwa pesa yeyote kwa malipo haya ya pili ndio msingi wa shukurani za wakulima wa korosho Masasi, ambao mpaka sasa wengi wameandika barua na wengine kufika ofisini kwa mkuu wa wilaya au kutuma wawakilishi wao kutoa shukrani zao kwa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa umahiri wake kuhakikisha anawakomboa wakulima wa korosho Masasi. Wanamtakia afya njema na maisha marefu.

Lakini pia shukurani zao wanazielekeza kwa Mkuu wa mkoa wa Mtwara Mhe. Anatory Tarimo kwa kupambana bila kuchoka kuhakikisha kuwa mfumo unasimama licha ya vikwazo vingi alivyopambana navyo kutoka kwa wasioutakia mema mfumo na wakulima wa korosho kwa ujumla.

Bila kusahau “Task Force” ya mkoa wa Mtwara chini ya katibu tawala wa mkoa wa Mtwara Ndg.Yusuf Matumbo kwa kazi nzuri wakishirikiana na viongozi wa wilaya kuhakikisha wanapambana na wahujumu wa mfumo wa stakabadhi ghalani. Hatimaye leo wakulima wanafurahia matunda ya kazi nzuri hiyo.

Aidha uongozi wa wilaya unawashukuru wananchi kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha hadi kufikia mafanikio haya.Tunawaomba waendelee na moyo huo na wazidishe uzalishaji kwa msimu ujao.

KOROSHO NI DHAHABU NA MKOMBOZI KWA MIKOA YA KUSINI!

Imetolewa na;

Mkuu wa Wilaya Masasi

Nape Moses Nnauye

Kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Masasi


My Take:

Mfumo wa stakabadhi ghalani bado haujaeleweka na unalalamikiwa mno na wananchi. Mfumo huu hauendani na dhana nzima ya soko huria, unamnyima mkulima maamuzi ya kujiamulia katika kile anachokizalisha.

Mfumo wa stakabadhi ghalani utaonekana mkombozi kwa watu wa Mtwara pale mkulima atakapopata fursa nafuu ya kuweza kupata mbolea, pembejeo, mikopo nafuu, pamoja na masoko ya uhakika kwa mazao yake. Vile vile SIDO pamoja na asasi nyingine zije na wazo la kuweza kuwawezesha wakulima kuwa na viwanda vidogo vinavyotokana na zao la korosho. Mwisho ianzishwe benki ambayo itakuwa ni mahsusi kwa ajili ya wakulima wadogo wadogo kwa ajili ya kuweza kupata mikopo pamoja na fursa mbalimbali ningependa benki hiyo iitwe "Korosho Bank".

Fursa nyingine ni huduma mbalimbali za kijamii ambazo nadhani bado ni tatizo kwa mkoa wa Mtwara. Mafanikio ya kweli sio namba mafanikio ya kweli ni kwa namna ipi serikali imewezeshwa na wananchi wake katika kupunguza kiwango cha umaskini kupitia zao lao. Hapa itakuwa ni kama tunapiga porojo tu ili ionekane kwamba kuongezeka kwa namba fulani ya kipato imetokana na mtu fulani. Sio kweli.

No comments: