Tuesday, January 11, 2011

RAI YA JENERALI


Barua Ndefu na Ya Wazi Kwa Jakaya


Mwaka 2005 siku chache baada ya Jakaya Kikwete kushika madaraka ya Rais wa Tanzania kutokana na uchaguzi uliompa ushindi wa Oktoba mwaka huo, nilimwandikia Barua Ndefu ya Wazi kupitia katika gazeti la Rai. Kwa kuwa mazingira ya wakati huo na ya leo yanashabihiana sana, na kwa kuwa bado Barua ile Ndefu ya Wazi ina hoja ambazo zinatukumbusha yaliyopita na kututabiria yajayo, tunairejea barua hiyo ambayo maudhui yake yanabaki yaleyale hata kama imehaririwa hapa na pale kusahihisha makosa ya chapa.Ifuatayo ni sehemu ya tisa ya barua hiyo.

Mpendwa Jakaya,

Bila shaka utakuwa umeng’amua kwamba yote niliyoyawasilisha kwako hadi hapa yanaashiria kuwapo kwa tatizo la msingi ambalo labda sijalitaja bayana. Sijalitaja bayana, si kwa sababu sijalielewa vyema, ila kwa sababu nilitaka kulieleza kwanza kwa kulitolea mifano maridhawa kabla sijalitaja. Sasa naweza kulitaja.

Ndugu Rais, miongoni mwa mambo mengi uliyorithi siku ile ulipokula kiapo kikuu, pamoja na mambo mengi mazuri niliyoyataja mwanzoni mwa waraka huu, pia umerithi jamii iliyopoteza kiasi kikubwa cha mwelekeo wake. Ni jamii ambayo bado inahangaika, inasumbuka, ikitaka kujua inaelekea wapi.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatuambia kwamba nchi yetu inafuata siasa ya “Ujamaa na Kujitegemea”, na chama chako kimekuwa, angalau mara moja moja, kikidai hivyo. Nasema mara moja moja kwa sababu, hata ndani ya chama tawala, ni viongozi wachache sana wanadiriki kutumia maneno hayo, kwa sababu, nahisi, wanaona haya kuyataja wakati wakijua kwamba hayana maana tena.

Hata hivyo, nililazimika kumsifu Katibu Mkuu wa chama, Philip Mangula, kwa kitendo chake cha kishujaa wakati wa mkutano mkuu uliokuchagua kuwa mgombea urais, pale Chimwaga. Kusema kweli sikutegemea kwamba angewaomba wajumbe wasimame na warudie maneno ya Ahadi Kumi za Mwanachama, maneno ambayo niliamini yalikwisha kusahaulika kabisa katika msamiati wa chama tawala.

Sikuamini kwamba maneno kama “Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja”, “Rushwa ni adui wa haki; sitapokea wala kutoa rushwa,” Nitasema kweli daima; fitina kwangu mwiko,” na kadhalika yangeweza kutamkwa na hadhara ambayo inajua ukweli wa jinsi mambo yanavyoendeshwa ndani ya chama hicho, na jinsi mchakato wote wa uchaguzi huo ulivyokuwa.

Ukweli ni kwamba kuna mkanganyiko mkubwa. Nchi yetu inayo historia ya kisiasa inayotusuta kwa kutukumbusha, bila wenyewe kutaka, kwamba huko nyuma tulikwisha kula yamini kufanya mambo kadhaa kwa ajili ya nchi yetu, Afrika na dunia nzima. Tulikwisha kuapa huko nyuma kwamba tunatambua udugu na usawa wa binadamu wote na umoja wa Afrika, na tukalaani kila aina ya ubaguzi.

Huko nyuma tulikwisha kuapa kupambana na rushwa kwa kutambua kwamba rushwa ni adui wa haki na kwamba palpokosekana haki haimei amani. Tulikwisha kuapa kwamba tutaondokana na fitina na tutasema kweli daima. Huko nyuma tulikwisha kujenga chama cha kimaendeleo (progressive), chama ambacho kilisimika mizizi yake katika utambuzi wa kifalsafa wa misingi imara ya ubinadamu, haki na usawa.

Kati ya misingi hiyo ya kale na matendo tunayoyashuhudia leo, lipo lindi pana mno ambalo halivukiki kwa akili ya kawaida ya binadamu. Huwezi tena kukitambua chama tawala tulicho nacho kama mrithi halali wa chama kilichoandika ahadi zile zilizosomwa katia ukumbi wa Chimwaga. Chama kile kilikuwa chama cha “makabwela”, watu wanyonge na masikini, wasio na kitu isipokuwa umoja wao. Kilikuwa ni chama chenye falsafa inayotambulika, iliyoendana na falsafa ya kihistoria ya ukombozi wa binadamu, tangu Mapinduzi ya Ufaransa ya 1789. Kilikuwa ni chama cha mwelekeo wa kimapinduzi na mtazamo wa kiulimwengu.

Tulicho nacho hivi sasa ni “chama tawala” tu, chama ambacho falsafa yake ni kutawala, basi. Si chama cha uongozi wala chama cha ukombozi, achilia mbali chama cha mapinduzi. Ni chama cha kutawala, ni mkusanyiko wa watu wengi, ambao mara kwa mara wanajumuika pamoja na kuweka utaratibu wa kugawana maeneo ya utawala na kukasimiana madaraka. Jambo kubwa pekee linalowaweka watu hawa wengi pamoja ni mgawanyo wa mamlaka ya dola, na matarajio ya wakuu wa makundi mbali mbali kuambulia cho chote katika mgawanyo huo.

Ni dhahiri kwamba kutokana na mkusanyiko kama huo hakuna matumaini ya kupata uongozi isipokuwa kwa bahati tu. Wakipatikana viongozi wazuri kutokana na mchakato ndani ya mkusanyiko kama huo haina maana kwamba chama hicho ni kizuri au utaratibu wake ni mzuri bali maana yake ni kwamba pamoja na ubovu uliomo ndani ya chama hicho na utaratibu usioridhisha, bado ndani yake wanaweza kupatikana viongozi wachache wazuri.

Lakini ukweli unabaki pale pale, kwamba hiyo inakuwa ni bahati tu, na ambayo haiwezi kutegemewa kuzaa matunda mema kila wakati. Ulipoanza mchujo ambao hatimaye ulikuibua wewe, Jakaya, kama mgombea wa chama chako, wataraji mlikuwa zaidi ya kumi, na mkachujwa hadi ukashinda wewe. Lakini katika hatua za mwanzo kabisa, kutokana na jinsi watu walivyokuwa wamejipanga, angalau wagombea watano walikuwa na nafasi ya kuchaguliwa, na baadhi yao wanatisha.

Sasa, inaelekea mwezi Juni utakabidhiwa pia madaraka ya kukiongoza chama chako kama mwenyekiti. Binafsi mimi sijui kama kimsingi hili ni jambo jema, lakini hivyo ndivyo imekuwa tangu Mwalimu Julius Nyerere alipomwachia kiti Rais Ali Hassan Mwinyi kabla ya mwisho wa kipindi chake na Mwinyi akamwachia Rais Benjamin Mkapa vile vile kabla ya kipindi chake kuisha.

Nasema sijui kama kimsingi ni jambo jema kwa sababu naamini linachangia kushadidia dhana ya chama-dola, chama-tawala, hususan kwa kuwa inaelekea kwamba ukiisha kukamata dola, basi unaongezewa na chama pia. Wakati mwingine huwa najiuliza itakuwaje iwapo siku moja mkuu wa dola atatoka chama kingine.Mwenyekiti wa CCM atatoka wapi? Lakini bado hatujafika huko. Tunalojua ni kwamba ifikapo mwezi Juni, insha Allah, utavikwa pia joho la uenyekiti wa chama chako. Ni matumaini ya wengi ambao nabadilishana mawazo nao kwamba hiyo itakuwa ni fursa ya dhahabu utakayopata kutoa mchango mkubwa na wa kihistoria katika kurekebisha siasa za nchi hii. Ni fursa ambayo hajawahi kupata mwanachama mwingine aliyepata madaraka kama uliyopata wewe.

Kabla hajawa mkuu wa dola Mwalimu Nyerere alifanya kazi ya uongozi wa chama cha ukombozi wa kitaifa, TANU, kwa muda wa miaka saba. Baada ya hapo alikuwa bado ni Rais wa TANU, na baadaye Mwenyekiti wa TANU na CCM, lakini wakati huo alikuwa ni Rais wa Jamhuri zaidi kuliko mwenyekiti wa chama. Alipong’atuka urais mwaka 1985 alijipa miaka miwili ya mradi maalumu wa kukijenga upya chama chake. Kati ya mwaka 1986 na 1987 alitembea nchini kote, akapita kila mkoa na kila wilaya, akakutana na viongozi wa chama chake.

Alichokiona huko, kwa kauli yake mwenyewe, kilimvunja moyo. Alikuta chama kilichojaa wababaishaji waliojiita viongozi, watu waliozama katika rushwa na ulaghai, ambao nguvu zao zilikuwa zimebakia katika ule ukweli kwamba chama chao ndicho chenye madaraka serikalini, chama-tawala, siyo chama-kiongozi. Wakati mmoja alisema, “Niliwakuta viongozi wa chama ambao baada ya kuwaangalia na kuwasikiliza, nikajiuliza, ‘Hivi mimi na huyu hapa tuko chama kimoja?’

Wenyeviti wawili waliomfuata Mwalimu hawakuwa na historia ya kufanya kazi ya chama. Walijikuta ni wenyeviti baada ya kuwa wamepata ukuu wa dola. Katika vipindi vyao vya uongozi wa chama hawakufanya kazi kubwa ya kuimarisha chama isipokuw aile ya kikatiba ya kuendesha vikao mbali mbali vinavyopasa. Udhaifu aliokuwa ameuona Mwalimu katika kipindi cha miaka miwili ya mradi kuimarisha chama ukaendelea kujijenga hadi leo, na ni udhaifu huo huo, ukiwa sasa umekubuhu, utakaourithi pindi utakapochaguliwa kuwa mwenyekiti mwezi Juni.

Nasema ahii itakuwa fursa ya dhahabu kwa sababu wewe umekulia ndani ya chama chako. Maisha yako yote tangu uhitimu Chuo Kikuu umekuwa ama mtendaji ama kiongozi wa kuchaguliwa ndani ya chama hicho. Umekiangalia, umekisoma, umekielewa, kutoka ndani yake. Hakuna mtu wa kukudanganya kuhusu chama hicho. Naamini kwamba unaweza kukibadilisha na kukirudisha katika msitari.

Haiwezi kuwa kazi rahisi. Ni watu wengi mno walioingia na kujichimbia katika chama hicho kwa maslahi wanayopata zaidi kuliko kwa utashi wa kuongoza nchi na kuwasaidia wananchi. Ndani ya chama ndiko kunakopatikana vyeo vya kila aina na zawadi kwa “makada wazuri”, hii ikiwa na maana ya wale wanaokubali kupokea uongo wakaufanya uwe ndio ukweli.

Michakato mingi ndani ya chama-tawala imekuwa ni ya kupiga majungu, kueneza fitina, kuchafua majina na kuuuza na kunua nafasi za “uongozi.” Hakuna nafasi tena ya kujadili ni vipi tutaboresha maisha ya mwananchi wa kawaida; kilicho muhimu ni vipi huyu atapata nafasi hii na yule atapata nafasi ile. Chama kimekuwa ni gulio, bazaar, ambamo bidhaa kuu inayoadiwa ni dhamana ya “uongozi” wa nchi.

Pasi na shaka bado wamo watu ndani ya chama chako ambao, kama wakipata uongozi madhubuti watafurahi kufanya kazi ya kukirekebisha chama chao. Hao ni wachache mno, na watahitaji kutiwa shime na mkuu wao mpya kwa njia ambayo hawajaishuhudia kwa muda mrefu. Wewe, Jakaya, unaweza kuwatia shime na chama kikabadilika.

Ni kwa nini nadhani kazi ya kukirekebisha chama chako ni muhimu? Chama hicho ndicho kinachoamua agenda ya kisiasa ya nchi hii. Viko vyama vingine, lakini kwa ushahidi tulio nao chama cako bado kina nguvu kubwa mno ya kisiasa kiasi kwamba vyama vingine vinayo nafasi ndogo sana ya kubadilisha mwenendo wa kisiasa nchini.

Ni kweli pia kwamba vyama vingine vingine vinajifunza na kuiga kutokana na jinsi chama kikongwe kilichomo madarakani kinavyofanya mambo yake. Mifano mizuri itaigwa, na mibaya pia. Iwapo chama-tawala kitaendelea kuhalalisha rushwa kwa kuibandika jina la “takrima” na vyama vingine navyo vitajifunza nyendo za “takrima.” Iwapo kitapiga marufuku vitendo vya rushwa kwa dhati vyama vingine vitajifunza pia.

Chama-tawala ndichi kinachounda serikali, na serikali ndilo chimbuko kuu la sheria za nchi. Chama tawala ambacho ndani yake kina taratibu zinazokaidi maadili ya msingi hakiwezi kuwa chanzo cha sheria zitakazovibana vyama vya siasa katika shughuli zake. Hakiwezi kupeleka miswada Bungeni ili zitungwe sheria zitakazokibana.

Siasa za ushindani bado ni changa nchini mwetu, na zinahitaji kuelekezwa na wale wanaoweza kuona mbali. Aidha hatuna budi kufanya kila jitihada kuhakikisha kwamba ushindani wa kisiasa, ndani ya kila chama na baina ya vyama, unalenga kujenga Taifa lenye mshikamano mkubwa zaidi, utajiri mkubwa zaidi, mgawanyo wa haki zaidi wa utajiri huo na kadhalika.

Iwapo chama chako kitaweza kujisafisha na kukumbatia maadili ya msingi ya awali, kinaweza kuwa ni chachu katika mjadala wa kitaifa wa kutafuta mwafaka kuhusu mustakabali wa Taifa letu na watu wake na kuweka upya mwelekeo ambao hivi sasa, tunaelekea tumeupoteza.

ItaendeleaRAIA MWEMA

No comments: