Wednesday, January 5, 2011

RAI YA JENERALIBarua Ndefu Na Ya Wazi Kwa Jakaya


Mwaka 2005 siku chache baada ya Jakaya Kikwete kushika madaraka ya Rais wa Tanzania kutokana na uchaguzi uliompa ushindi wa Oktoba mwaka huo, nilimwandikia Barua Ndefu ya Wazi kupitia katika gazeti la Rai. Kwa kuwa mazingira ya wakati huo na ya leo yanashabihiana sana, na kwa kuwa bado Barua ile Ndefu ya Wazi ina hoja ambazo zinatukumbusha yaliyopita na kututabiria yajayo, tunairejea barua hiyo ambayo maudhui yake yanabaki yaleyale hata kama imehaririwa hapa na pale kusahihisha makosa ya chapa.Ifuatayo ni sehemu ya saba ya barua hiyo.

Ndugu Rais,

Ununuzi wa magari ya kifahari na matumizi mabaya ya magari ya Serikali kama yalivyoainishwa katika maelezo yangu hapo juu ni eneo moja tu la ubadhirifu unaofanywa ndani ya Serikali. Yako mengine mengi. Ni imani yangu kwamba iwapo maeneo haya yote yatadhibitiwa ipasavyo, Serikali inaweza kuokoa fedha nyingi mno ambazo zinahitajika katika huduma muhimu zinazowahusu moja kwa moja wananchi wetu.

Zipo safari za nje zinazofanywa na wakuu wa Serikali ambazo hazina sababu kabisa isipokuwa tu kwamba wakuu hao wamepata kisingizio cha kwenda kufanya “shopping”. Ingawaje zipo safari za kikazi zinazowahusu wakuu hao, baadhi ya safari hazina maana yo yote na nyingine zingeweza kufanywa na watendaji badala ya viongozi wa kisiasa.

Lakini liko jambo la ajabu ambalo limekuwa likitendeka katika awamu iliyopita kuhusiana na safari hizi. Sina uhakika kama lilitendeka hata katika awamu nyingine mbili zilizotangulia, lakini nina uhakika juu ya kutendeka kwake katika awamu iliyopita.

Waziri, mathalan, au katibu mkuu anafunga safari kwenda kuhudhuria mkutano, ambao unaweza kuwa wa manufaa kwa Taifa hili au la. Kama kawaida ya safari za kikazi, analipwa na wizara yake masurufu anayostahili, ikiwa ni posho na stahili zake nyingine. Kisha unatoka ujumbe wizarani kwenda kwa mkuu wa shirika lililo chini ya wizara husika kumtaka naye achangie safari ya waziri kwa kumlipa posho.

Baadhi ya wakuu wa mashirika hayo wamewahi kuidhinisha posho za kufikia zaidi ya dola za Kimarekani mia tano ($500=) kwa siku, na wakati mwingine kuzidisha kiasi hicho mara idadi ya siku mara mbili ya idadi halisi ya siku za safari za mkuu huyo. Katika mfano mmoja baada ya kuwa mkuu mmoja amechukua posho kutoka katika wizara yake na kupewa ziada ya posho hiyo niliyoitaja kutoka shirika hilo, bado shirika lilihaulisha fedha ya kulipia hoteli yake huko alikokuwa anakwenda.

Isitoshe, katika baadhi ya safari mkuu ambaye ana mashirika mawili au matatu chini ya wizara yake amedai posho hiyo ya ziada kutoka mashirika yote. Matokeo yake ni kwamba mkuu huyo ameweza kuondoka akiwa na zaidi ya $ 15, 000 au $20, 000 kwa safari moja mahali ambapo labda angehitaji kuondoka na dola $ 2, 500 au $ 3, 000.

Haya si majungu na wala si matokeo ya wivu, kama tulivyozoea kuambiwa. Taarifa hizi zinatolewa na watendaji, ama wizarani ama katika mashirika, ambao hawafurahishwi na mtindo huu na ambao wana uchungu na jinsi fedha za umma zinavyotumika hovyo.

Ni dhahiri kwamba kwa mtindo huu safari zinaweza kugeuka kuwa ni kiwanda cha kuchapisha fedha kwa ajili ya mkuu asiyekuwa na huruma na fedha za wananchi. Haishangazi, basi, kwamba safari kama hizo hazina mwisho hata pale ambapo mkuu hahitajiki kusafiri, kwa sababu tu ni chanzo cha utajiri usio na mipaka wala jasho.

Kama unavyosema, Ndugu Rais, jukumu la kwanza kabisa la wakuu waliokabidhiwa madaraka na wananchi ni kufanya kazi ndani ya nchi, na kusafiri nje ya nchi pale tu inapokuwa lazima kwao kusafiri. Hatuwezi kuwa na Serikali ambayo mawaziri wote wanafanya kazi ya Asha-Rose Migiro, ukiondoa wizara mbili au tatu, ambazo mwelekeo wake ni wa “nje-nje.”

Mimi si mmoja wa wale wanaotaka mawaziri na makatibu wakuu wasafiri “Economy” wanaposafiri kwenda nchi za mbali. Naamini kwamba, wanapolazimika kusafiri, ni muhimu kuwasafirisha kwa njia ambayo inawapunguzia uchovu ili wanapofika waendako waweze kufanya kazi vizuri kwa akili iliyotulia. Lakini kusafiri “First Class” kwa viongozi wa nchi kama yetu ni anasa isiyo kubalika, ispokuwa tu kwa viongozi watatu au wane wa juu kabisa nchini. Naamini “Business” linatosha.

Sina taarifa ni nini kinatendeka sasa, lakini tulikotoka mawaziri na makatibu wakuu walikuwa wamezoea kusafiri katika “First Class”, na wakati mwingine katika ndege moja ambayo mumo mumo wamo mawaziri wa nchi “wafadhili”, ambao ndio wanaotoa hizo fedha zinazowasafirisha wakubwa wa nchi yetu, na “wafadhili” hao wanasafiri “Business”.

Huu ni ukwasi wa kuazima, ukwasi bandia ambao hata hao wanaotusaidia wanaushangaa. Serikali yetu, kwa bahati mbaya sana, bado ni “omba omba”, na sala yangu ni kwamba siku moja tuondokane na hali hii ya “Yallah Masikini”. Lakini ni “omba omba” gani anakwenda “kujichana” Movenpick wakati mfadhili wake anakula gengeni?

Pia ziko safari za humu humu ndani ambazo baadhi yake hazina maelezo ya kuridhisha. Hivi karibuni waziri mmoja amesakamawa kwa kutumia ndege ya JW kama vile ni taxi. Inawezekana ni kweli, kama alivyosema, kwamba waliomtangulia walikuwa wakifanya hivyo hivyo. Inawezekana hii ni kweli.

Lakini hata wasiotumia ndege wanao ubadhirifu wao ambao ungetakiwa kuangaliwa. Katika mpangilio wa Katiba ya nchi yetu, ili kuwa waziri ni lazima mtu awe mbunge kwanza. Katika marekebisho ya kikatiba chini ya awamu ya tatu, Rais alipewa madaraka ya kuwateua watu kuwa wabunge kwa maelezo kwamba anaweza kutaka kuwatumia katika serikali yake watu ambao hawakutaka kugombea ubunge ingawa wana uwezo wa kufanya kazi kama mawaziri.

Nimeona umefanya hivyo, na wale uliowateua wengi wamepewa uwaziri, ingawaje katika awamu ya tatu wengi walioteuliwa walipewa zawadi tu ya kuketi Bungeni, kwa sababu moja au nyingine. Ukitoa hao uliowateua kuwa wabunge, pamoja na wale waliopitia viti maalumu, mawaziri wako wengine wote ni wabunge waliotoka kwenye majimbo ya uchaguzi.

Hawa wanajua kwamba ili waweze kuwa mawaziri baada ya miaka mitano, ni lazima wewe uridhike na kazi waliyokufanyia. Lakini kabla hujawateua kuwa mawaziri, watatakiwa kwanza warejeshwe na wananchi wao kama wabunge. Kwa hiyo wana wajibu mara mbili: kwanza wawaridhishe wapiga kura wao; pili wakuridhishe wewe.

Katika uzoefu tulioupata mawaziri ambao ni wabunge wa majimbo wamekuwa wakifanya safari nyingi kwenda katika majimbo yao. Hili linaeleweka, kwa sababu kutembelea jimbo na kujifunza kuhusu ya matatizo ya wananchi na kutafuta utatuzi wake ndiyo kazi ya mbunge.

Lakini wanafanya safari hizo kwa gharama ya nani? Majuzi, wakati wabunge wachache walipolalamika kuhusu maslahi yao, ingawaje walikuwa ni wachache tu waliofanya hivyo, tulikuwa wepesi kuwalaani. Binafsi naamini kwamba kwa wabunge ambao si mawaziri safari za jimboni ni mojawapo ya gharama kubwa zinazowakabili wabunge wetu. Tukichunguza gharama za mafuta na matengenezo ya magari, tutaelewa kwamba kile wanacholipwa ni kidogo sana.

Sasa, tukiwaangalia wabunge ambao ni mawaziri tutaona tofauti kubwa. Waziri ambaye ni mbunge wa jimbo anaposafiri kwenda jimboni mara nyingi, kama siyo zote, anatumia gari lake la uwaziri, mafuta anayotumia ni ya Serikali, dereva anayemwendesha analipwa na Serikali, na msaidizi anayeambatana naye ni ofisa wa Serikali. Gharama zake, pamoja na posho za wote hawa, waziri pamoja na walio naye katika msafara, zinabebwa na Serikali.

Tungetaka kuwatendea haki wanunge wanaosema kwamba maslahi yao hayaridhishi, tungefanya mambo mawili: kwanza, kupitia utaratibu nje ya semina, haya maslahi yatazamwe upya, wajibu wa wabunge uthaminiwe upya kwa maana ya gharama zake, kisha pale inapobidi wapewe wanachostahili. Pili, baada ya kuwa wabunge wote wa majimbo wameboreshewa maslahi yao, mawaziri na naibu mawaziri wasiruhusiwe kuitwisha Serikali gharama za kutembelea majimbo yao.

Ama kwa hakika, hizi safari za jimboni zina gharama kubwa sana, na baadhi ya gharama hizo ni zile zilizojificha. Hata kama waziri atatumia kisingizio cha kukagua miradi inayohusika na wizara yake iliyomo jimboni mwake, tunaweza kufanya hesabu na kujua ni mara ngapi amekwenda kukagua miradi kama hiyo katika maeneo yasiyoko jimboni mwake na tuhesabu ni mara ngapi amekwenda katika jimbo lake kwa miradi kama hiyo hiyo.

Tukiacha gharama za moja kwa moja nilizozitaja hapo juu, iko gharama inayotokana na ukweli kwamba muda wa waziri hautumiki wote katika kazi ya uwaziri. Kwa kweli, kwa baadhi ya mawaziri, tunaweza kujiuliza iwapo wanatumia hata theluthi mbili ya muda wao katika kazi ya uwaziri, kwa jinsi wanavyohangaika na majimbo yao.

Ndugu Rais, inawezekana barua hii si mahali mwafaka pa kutoa maoni yangu juu ya Katiba yetu, lakini ingefaa tukajiuliza iwapo utaratibu wa kuwateua mawaziri kutokana na Bunge bado unatufaa, tukiangalia gharama tunazoingia kutokana na mfumo tulio nao, na ambao inawezekana tunaendelea nao kwa sababu tu tumeuzoea.

Rai yangu ni kwamba sisi bado ni nchi ya watu masikini, tena sana. Kila jitihada lazima ifanywe ili kuwapunguzia wananachi wetu umasikini kwa kufanya yale tunayoweza kuyafanya. Mojawapo ni kupunguza sana gharama za uendeshaji wa Serikali, ili Serikali yetu iache kuwa kile kinachoitwa Treni la Michuzi (Gravy Train). Hili umelisemea, nami sina shaka utalifanyia kazi.

Itaendelea


RAIA MWEMA

No comments: