Friday, January 14, 2011

POLISI WAUA TENA KWA RISASI

Brandy Nelson, Mbeya na Ramadhan Semtawa

POLISI nchini wameendelea kutumia risasi za moto dhidi ya raia na jana wanadaiwa kuwauwa watu wawili kwa kuwapiga risasi katika vurugu zilizotokea katika wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.

Habari kutoka Mbarali zinasema polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi na risasi za moto kuzima vurugu ambazo chanzo chake ni mabishano baina ya raia na polisi hao.

Vurugu hizo zilizotokea jana majira ya saa nane mchana zinadaiwa kusababishwa na baadhi ya wakazi wa kata ya Ubaruku kuzuia kuingia katika eneo lao lori lenye uzito wa zaidi ya tani kumi.

Baadhi ya walioshuhudia tukio hilo walisema hatua ya wananchi kuzuia kwa lori hilo inatokana na kuwepo kwa amri ya serikali wilayani Mbarali itayokataza magari yenye uzito mkubwa wa zaidi ya tani kumi kuingia katika kata ya Ubaruku.

Mmoja wa mashuhuda hao alisema lori hilo lilipokuwa likijaribu kuingie katika eneo hilo wananchi walianza kulizuia huku wakimhoji dereva wake sababu za kuvunja amri iliyopo.

“……walipokuwa wakiendelea kuhojiana na dereva, polisi walifika hapo na hapo wananchi wakaanza kuwauliza polisi sababu za kuruhusu gari kuingie katika eneo lao wakati serikali imeishakataza..,” alisema shuhuda huyo na kuongeza:

“ ni kama polisi na wananchi walishindwa kuelewana lugha hapo tukaanza kusikia mabomu ya machozi na risasi…”.

Alisema hatua ya polisi iliwafanya wananchi kutawanyika na wengine kuanza kuyavamia magari yaliyokuwa kwenye kituo cha mafuta likiwemo gari lililosababisha mvutano huo.

Katika tafrani hiyo magari mawili yaliyokuwa kwenye kituo cha mafuta yalichomwa moto. Magari hayo yanasadikiwa kuwa ni mali ya ndugu wa mwekezaji katika shamba la mpunga la Mbarali.

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Cosmas Kayombo alipohojiwa alikiri kupata taarifa hizo lakini akadai kwamba yuko mbali na tukio hilo na amedai kuwa amewasiliana na mbunge jimbo la Mbarali Dickson Kulufi afike eneo la Tukio.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi alipohojiwa alisema kuwa analifuatilia tukio na mpaka tunakwenda mitamboni tayari gari nne mbili zikiwa zimebeba askari wa kutuliza ghasia (FFU), moja ikiwa imebeba polisi waliovalia kiraia huku wakiongozwa na king`ora kikipiga kelele zikiwa zinaelekea eneo la tukio.

JESHI la Polisi limesema jiji la Arusha sasa liko shwari baada ya vurugu zilizotokea Januari 5 mwaka huu lakini, Kurugenzi ya Makosa ya Jinai inaendelea na uchunguzi kubaini kama kuna makosa mengine ya kijinai dhidi ya viongozi wa Chadema.

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa polisi, Paul Chagonja, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa polisi hawawezi kuzuia haki za watu lakini pia ifahamike kuwa wana wajibu wa kulinda usalama wa wengine.

"Operesheni ya kurejesha amani na utulivu imekamilika na hivi sasa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kwa kushirikiana na timu ya wadau wengine wa Usalama kama vile Haki Jinai, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali bado wanaendelea na uchunguzi,

... ili kuona matukio yoyote ya makosa ya kiutendaji na makosa mengine ya kijinai yaliyotendwa kwa upande wa Chadema na viongozi wao."

Kamishna huyo aliwaonya watu aliowaita wanasiasa wanaojaribu kutumia nguvu ya umma kujipatia umaarufu na kudharau mamlaka zilizopo akisema watashughulikiwa.

"Eti wapo wanaosema nchi haitawaliki,... sisi tunasema sheria zipo na wanaotaka kuingia madarakani wasubiri uchaguzi wa 2015. Watu wanapaswa kutambua mamlaka ya polisi, tuko kulinda mamlaka halali ya Jamhuri ya Muungano. Hata wakiingia wapinzani polisi tutakuwepo na tutalinda mamlaka halali," alisisitiza Chagonja.

Chagonja ambaye alifanya mkutano huo kutoa kile alichokiita ufafanuzi wa upande wa polisi baada ya kuwepo taarifa za upande mmoja, alitumia picha hizo zilizorekodiwa katika vurugu kuonyesha chanzo cha mauaji hayo na kwamba viongozi wa Chadema wanapaswa kulaumiwa na sasa wanajibaraguza baada ya kumwaga damu.

"Kufuatia hamasa hiyo wafuasi wa Chadema wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 3,000 waliitikia wito wa viongozi hao na kuanza kuelekea kituo kikuu cha polisi Arusha, ili kwenda kuwatoa kwa nguvu watuhumiwa waliowekwa mahabusu kama walivyoazimia mkutanoni, lakini hili halisemwi... watu wanazungumza ya upande mmoja tu," alifafanua Chagonja huku akiwaonyesha waandishi wa habari picha kupitia kwenye kompyuta.

Akirejea mchakato mzima wa maombi ya kibali cha mkutano, Chagonji alisema jeshi hilo wilayani Arusha lilipokea barua ya Chadema kuomba kibali cha maandamano hayo mnamo Desemba 31 mwaka jana, yenye kumbukumbu namba CDM/AR/W/20/10, ikitoa taarifa ya dhamira hiyo kufanya maandamano Januari 5, 2011.

Kamishna huyo alianisha maeneo ambayo Chadema iliomba kupita maandamano hayo kwamba ni kuanzia Philips, kuelekea Sanawari, Mianzini, Kituo Kikuu cha mabasi kuelekea mnara wa Azimio, kupitia polisi, Manispaa, Clock Tower kushukia barabara ya Sokoine kisha Friends corner na kuingia viwanja vya NMC.

"Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha mjini baada ya kupokea barua hiyo, aliwajibu Chadema kwa barua Kumb Na AR/B.5/Vol11/63 ya tarehe 4 Januari 2011, akiwaruhusu kufanya maandamano na mkutano tarehe 5 Januari, 2011, lakini akiwataka warejee mazungumzo ya ana kwa ana yaliyofanyika tarehe 3 Januari 2011 ofisini kwa kamanda wa polisi mkoa yakihusisha viongozi wa chama hicho na polisi," alifafanua.

Aliongeza kwamba, pamoja na mambo mengine mazungumzo hayo yalibainisha umuhimu wa kuchagua njia moja itakayotumika katika maandamano hayo kati ya njia zilizotajwa kwa ajili ya kuwezesha polisi kuangalia usalama wa mali na raia huku shughuli nyingine za kiuchumi na biashara zikiendelea.

"Njia hizo ni aidha, itumike kuanzia Philips, Sanawari mataa, kushuka na barabara ya AICC, Goloondoi, barabara ya Sokoine, Friends corner na kuingia uwanja wa NMC, au kuanzia Philips, Sanawari mataa, Florida Annex, Kituo cha mabasi, CRDB benki, Friends Corner hadi uwanja wa NMC, " aliweka bayana na kuongeza,

...siku hiyo ya maandamano ilikuwa ni siku ya kazi watu wengine wangekuwa wanaendelea na shughuli zao katika mitaa hiyo, hivyo matumizi ya njia yalipaswa kuzingatia haki za watumiaji wengine ili kuondoa usumbufu usio wa lazima."

Hali ya miundombinu ya barabara kwa njia ya Arusha ni finyu, hivyo matumizi ya njia mbili kwa wakati mmoja ni wazi yangezuia matumizi ya barabara kwa watumiaji wengine kwa muda mrefu."

Lakini, Chagonja lisema Januari 3, 2011 mkuu wa polisi wilaya ya Arusha mjini alipokea barua ya Chadema yenye Kumb Na CDM/AR/W/02.1.11 iliyosainiwa na Magoma Derick mwenyekiti wa chama hicho wilaya, ikimjulisha maandamano yataanzia Philips na msafara wa Dk Slaa utaanzia uwanja mdogo wa ndege wa Kisongo huku pia yangekuwepo Annex hoteli na kisha kuelekea NMC.

Aliongeza, "kwa maana ya barua hiyo siyo tu Chadema hawakuchagua njia mojawapo kama ilivyoelekezwa bali waliongeza njia nyingine ya pili itakayoongozwa na Dk Slaa, kuanzia uwanja wa Kisongo kinyume na maelekezo ya polisi."

Kaminisha huyo wa operesheni alifafanua, " hata hivyo, wakati mawasiliano hayo yakiendelea taarifa za kiintelejensia zilizokusanywa katika kipindi cha wiki moja kuishia Januari 4, 2011, zilionyesha kuna matishio makubwa ya kiusalama. Matishio hayo yalilenga kuharibu sura ya mji wa Arusha katika uso wa dunia ukizingatia Arusha ni mji wa kibiashara."

Alisema Chadema ilijulishwa kusitishwa kwa mandamano hayo Januari 4 na ofisi ya Polisi mkoa kwa barua yenye Kumb NaARR/B.5/1.VOL.V111, iliyopokelewa muda wa mchana na diwani Estomi Mala, ambaye alikuwa mjumbe kutoka chama hicho na mgombea nafasi ya umeya wa jiji la Arusha, aliyetumwa kufanya majumuisho na kamanda wa polisi wa mkoa wa Arusha kuhusu maandalizi ya mkutano huo.

Hata hivyo, alisema manmo Januari tano saa 5:00 asubuhi ndipo viongozi na wanachama wa Chadema isivyo halali wakaanza maandamano kuanzia Mount Meru hoteli kwenda viwanja vya NMC na hapo kutawanywa na polisi kwa amani, kabla ya kauli za kichochezi za Dk Slaa alizotoa kwenye mkutano akiagiza waliokamatwa kwenye maandamano hayo wakakombolewe.

Katika sehemu ya picha hizo inamuonyesha Dk Willbroad Slaa, akitangazia umati wa vijana uliokuwepo uwanjani hapo kwamba, kabla ya mkutano kumalizika viongozi waliokamatwa na kushikiliwa kituo cha Polisi Kati akiwemo Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, walipaswa kuachiwa huru na kuwaleta uwanjani hapo.

Sehemu nyingine ya picha za kwenye mkutano zinamuonyesha Mbunge wa Moshi mjini Philemon Ndesamburo, akilalamika kukumbana na mkono wa chuma wa dola huku akitaja jina la Rais Jakaya Kikwete akisema, "Kikwete Ndesa anapigwa mabomu...aloo Ndesa anapigwa Kikwete... Kikwete wewee humjui Ndesa... Kikwete hujui vurugu za Ndesa alooo?"

MWANANCHI

No comments: