Friday, January 28, 2011

MAKALA YA MBWAMBO
TUMEKUWA DAMPO TWAMWAGIWA VYA DAMPO


MALUMBANO ya hivi karibu kati ya Makamu Mkuu wa Chuo Huria cha Tanzania, Profesa Torry Mbwete na Shirika la Viwango (TBS) kuhusu ubora wa maji ya chupa na ya kwenye vipaketi yanayotengenezwa na kuuzwa nchini, yanafikirisha.

Profesa Mbwete ameutangazia umma wa Tanzania kwamba si maji yote ya chupa na ya kwenye vipaketi, yanayouzwa nchini, ni salama kunywa. TBS inapinga na kudai kuwa maji yote yenye nembo yake ya ubora ni salama kunywa.

Kwa hakika, malumbano hayo yalinikumbusha kitu kimoja nilichokishuhudia mimi na waandishi wenzangu wa Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), mjini Morogoro, mwaka 2006.

Ilikuwa hivi: Tulikwenda Bwawa la Mindu (nje kidogo ya mji wa Morogoro) kwa ziara ya kikazi, na huko kila mmoja wetu alinunua ndoo moja ya samaki wabichi wakubwa aina ya perege.

Tatizo likawa ni namna ya kuwasafirisha samaki hao hadi Dar es Salaam bila wao kuharibika. Tukashauriwa kwenda nyumba fulani karibu na stendi ya zamani ya mabasi, mjini Morogoro, kununua mapande ya barafu ili tuyaweke juu ya samaki hao wasiharibike.

Tulipofika katika nyumba hiyo tukaelekezwa kupita hadi uwani ambako mapande hayo ya barafu yanauzwa. Huko uwani ndiko tukashuhudia kioja:Tulimkuta kijana mmoja yuko bize akijaza maji ya bomba kwenye vipaketi vidogo vya plastiki, na kisha kuvishona vyema na kuvipanga kwenye kasha la barafu (ice cooler).

Kioja chenyewe ni kwamba bomba lenyewe lilikuwa karibu mno na choo kichafu chenye inzi kibao. Pia kulikuwa na karo chafu linalotoa harufu mbaya karibu na bomba hilo. Lakini kijana yule alikuwa hayachemshi wala kuyaweka dawa yoyote maji yale kabla ya kuyajaza katika vipaketi hivyo!

Mmoja wetu (John Chikomo) alipomuuliza ni kwa nini alikuwa akiwauzia wateja maji ambayo hayakuchemshwa wala kuwekwa dawa yoyote jibu lake lilikuwa kwamba angeyachemshwa au kuyaweka dawa asingeyauza maji yale kwa bei ndogo kiasi kile ya Sh. 100 kwa paketi!

Kichwani mwangu nilijenga picha ya mwananchi masikini aliyeshikwa na kiu ya kupita kiasi kwenye maeneo ya stendi. Masikini huyo atakimbilia kununua maji hayo baridi ya Sh. 100 ya kwenye vipaketi, na yenye nembo feki ili akate kiu yake.

Masikini huyu atakuwa hajui kama maji hayo si salama hata kidogo. Hakika umasikini ndiyo unaomponza kuwa mwathirika wa kwanza wa biashara hiyo hatari ya maji ya kijana huyo.

Kwa sababu ya tukio hilo la Morogoro, niliapa kwamba sitanunua tena maji ya kunywa ya kwenye vipaketi bali ya chupa tu. Hata hivyo, kauli ya hivi karibuni ya Profesa Mbwete kwamba hata maji ya kwenye chupa si yote ni salama, imenifanya nifikiri upya kuhusu kiapo changu hicho cha Morogoro.

Lakini pia malumbano hayo kati ya TBS na Profesa Mbwete yalinikumbusha documentary moja ya BBC niliyopata kuiangalia miaka sita iliyopita iliyohusu uchunguzi wa kishushushu ambao waandishi wa shirika hilo walifanya kuhusu utengenezaji wa madawa feki (counterfeit drugs) nchini India.

Utafiti huo wa BBC ulichochewa na tukio moja huko Lagos, Nigeria ambako mgonjwa mmoja wa kisukari alifariki kwenye zahanati moja baada ya kuchomwa sindano za insulin.

Kifo hicho kiliwashangaza madaktari kwa sababu sindano ya insulin ilipaswa impe nafuu mgonjwa huyo na si kumuua, na ndipo ilipoamuliwa uchunguzi wa kimaabara ufanyike kuhusu hiyo ‘insulin’.

Matokeo ya uchunguzi huyo yaliitikisa Nigeria nzima; kwani ilibainika kwamba dawa hiyo ya insulin haikuwa insulin bali maji yaliyochanganywa na kemikali nyingine! Kwa maneno mengine; mgonjwa yule alifariki kwa kuwa sindano aliyochomwa haikuwa na dawa ya insulin; bali maji yaliyochanganywa na kemikali nyingine.

Uchunguzi zaidi ulipofanyika wa wapi ambako zahanati hiyo ilinunua dawa hizo, uliwezesha kugunduliwa kwa shehena kwa shehena ya makasha ya dawa feki (counterfeit drugs) kutoka India.

Na ndipo BBC ilipoamua kwenda huko India kufanya uchunguzi wa kikachero (under cover investigation). Matokeo ya uchunguzi huo wa BBC ni documentary hiyo kabambe inayoonyesha jinsi madawa hayo yanavyotengenezwa katika viwanda vidogo vya uani vilivyopo katika majumba ya wafanyabiashara waovu wa India.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa BBC, ni vigumu mno kwa macho ya kawaida ya binadamu kung’amua tofauti kati ya dawa halisi na dawa feki kutoka katika viwanda hivyo; kwani hufanana mno kuanzia kwenye mwonekano wa dawa yenyewe hadi kwenye muundo wa paketi zake na hata maandishi kwenye lebo.

BBC iliweza kuonyesha, kwenye documentary hiyo, namna chaki ya kawaida kabisa inavyoweza kutengenezwa na kuwa kidonge cha paracetamol na kuwekwa kwenye paketi ya kawaida kabisa ya dawa hiyo!

Hiyo maana yake ni kwamba mgonjwa kule Lagos, Nigeria anaweza kununua na kumeza dawa hiyo akidhani amemeza kidonge cha paracetamol; kumbe amemeza kidonge cha chaki!

Ndugu zangu, nimetoa mifano ya maji na dawa; lakini ukweli ni kwamba bidhaa feki ni nyingi mno katika mitaa ya dunia yetu hii.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka jana inaonyesha kwamba biashara ya madawa feki duniani inaongeza kila mwaka kwa watani wa asilimia saba.

Ni dhahiri soko kuu la bidhaa hizo ni nchi masikini duniani likiwemo Bara la Afrika. Bidhaa hizo zina mvuto kwa mtu masikini, kwa sababu ya bei zake rahisi.

Kwa mfano, masikini kule Morogoro hawezi kumudu chupa ya maji aina ya Kilimanjaro ya Sh. 700, na badala yake atakimbilia kipaketi cha Sh. 100 kilichotengenezwa katika mazingira yale niliyoyasimulia awali asitambue kwamba anakimbilia kifo.

Vivyo hivyo masikini kule Lagos, Nigeria atakimbilia insulin yenye maji kwa sababu ya unafuu wa bei na pia paracetamol ya chaki kwa sababu hiyo hiyo ya bei nafuu. Bei nafuu ndiyo inayowafanya masikini wawe waathirika wa kwanza na wakubwa wa bidhaa feki.

Katika Tanzania hali ni hiyo hiyo. Wiki iliyopita Mamlaka ya Kudhibiti Vyakula na Madawa (TFDA) ilitangaza majina ya aina saba za madawa ambayo imeyapiga marufuku, kwa sababu ni feki.

Sina hakika madawa hayo yamekaa sokoni kwa muda gani kabla TFDA haijayapiga marufuku, lakini nina hakika ya kitu kimoja; nacho ni kwamba kuna wagonjwa waliyanunua na kuyatumia wakiamini ni madawa orijino yanayoweza kuwatibu; kumbe ni feki! Tuombe tu Mungu kwamba hakuna waliokufa kutokana na uchu wa pesa wa wenzetu hao wanaoyatengeneza na wanaoyaingiza nchini mwetu na kuyauza.

Kwa ufupi, serikali yetu ina wajibu wa kuwalinda na kuwatetea wananchi (hususan masikini) dhidi ya biashara hii haramu na ya hatari ya bidhaa feki ambayo imeshamiri nchini.

Wenzetu Marekani (kwa mfano) wana vyombo imara vya kulinda walaji, na ndiyo maana Wachina walipoingiza midoli na maziwa ya watoto yenye kemikali za sumu, ilikuwa haraka kwao kung’amua na kusimamisha uingizaji wa bidhaa hizo.

Je sisi tunavyo? Je, TBS yetu ni imara na ina matawi ya kudhibiti biashara hiyo haramu nchi nzima, na hasa miji ya mipakani ambako kuna njia kibao za panya zinazotumiwa kuingiza nchini bidhaa hizo feki?

Je, TBS, katika udogo wake wa sasa, inaweza kweli ikawahakikishia Watanzania kwamba inawalinda dhidi ya utitiri wa bidhaa feki za Kichina zinazoingizwa nchini kila siku na kuuzwa bei rahisi?

Hivi kweli baada ya nchi yetu kugeuka dampo la bidhaa za kigeni (matokeo ya sera ya Serikali ya CCM ya soko huria) TBS ina capacity ya kupima kila bidhaa inayoingizwa na kuuzwa nchini?

Hivi kweli vyombo vyetu vyote vyenye dhamana ya kuwalinda wananchi dhidi ya bidhaa hizi hatari feki, havijaathirika na utamaduni huu wa sasa wa ufisadi ulioenea kote nchini?

Kama hata magari ya Rais yanawekewa mafuta yaliyochakachuliwa, Mtanzania masikini ataponaje kuuziwa kwenye duka la dawa paracetamol ambayo ni chaki!?

Vyovyote vile; Profesa Mbwete ameanzisha mjadala fikirishi, na TBS haina sababu yoyote ya msingi ya kuukasirikia. Natuujadili; maana unahusu maisha yetu sote hususan wananchi masikini ambao ndiyo wengi wanaokimbilia bidhaa hizo feki kwa sababu ya bei zake nafuu.

Profesa amegusia maji ya chupa tu, lakini orodha ya bidhaa feki ni ndefu. Natuijadili na kuangalia ni vipi tunaweza kuyanusuru maisha yetu; maana tumeridhia nchi yetu kugeuzwa dampo la bidhaa za nje, na sasa tunatupiwa vya dampo!

Tafakari.


RAIA MWEMA

No comments: