Wednesday, January 26, 2011

KORTI YAAMURU MZUNGU KUCHAPWA VIBOKO 10
MAHAKAMA ya Wilaya ya Bukoba, imemhukumu Robert Maintland (42), raia wa Ugiriki kutumikia kifungo cha miaka miwili jela na kucharazwa viboko kumi, baada ya kupatikana na hatia ya kuingia nchini kinyume cha sheria.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Peter Matete.

Hukumu hiyo inaweza kuwa faraja kwa wananchi wapatao 100 wa kitongoji cha Bujenjeke, Kijiji cha Ruhija, Kata ya Ijumbi mkoani Kagera ambao walikuwa wakivutana na Mgiriki huyo ambaye alikuwa akituhumiwa kuwanyanyasa akishirikiana na polisi.


Polisi mkoani Kagera walikuwa wakilalamikiwa kwamba wanamkingia kifua raia huyo wa kigeni ambaye manyanyaso yake dhidi ya raia yaliwafanya baadhi yao kukimbia nyumba zao na kulala vichakani.


Wakazi wa Bujenjeke waliwahi kuwaambia waandishi wa habari kuwa walikuwa wakilala na kushinda porini, kukwepa kupigwa na askari polisi na mgambo ambao walikuwa wakivaa mavazi ya kufunika nyuso zao maarufu kama mavazi ya kininja.


Lakini , Mahakama ya Bukoba iliridhika na ushahidi uliotolewa dhidi ya mtuhumiwa, hivyo hakimu Matete alimtia hatiani kwa kosa la kuwepo nchini bila kibali na kumhukumu kwenda jela miaka miwili na viboko kumi au kulipa faini ya Sh80,000.


Hata hivyo, Maintland alilipa faini ambayo haikumuondolea adhabu ya kuchapwa viboko ambayo ilikuwa itekelezwe jana.

Mapema hati ya mashtaka iliyowasilishwa mahakamani hapo na mwendesha mashtaka wa Idara ya Uhamiaji, Gerald Mardai ilidai kuwa, raia huyo alikamatwa Februari 23, mwaka jana, akiwa Kituo cha Polisi Bukoba bila kibali halali cha kuingia nchini.

Pia ilidaiwa kuwa, Maintland alikuwa na hati tatu za kusafiria zikiwa na majina tofauti, ambazo alizitumia kuingia nchini isivyo halali.


Katika ushahidi uliowasilishwa mahakamani, hati za Uingereza na Afrika Kusini zilikuwa na jina la Robert John Rubeinstein, huku vielelezo vingine vya Ugiriki vikionyesha kwamba alikuwa akitumia majina ya John Robert Penesis na Robert John Maintland.


Maintland amekuwa na mgogoro wa muda mrefu na wanakijiji wa Ruhija wilayani Muleba, mwaka jana aliripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwachapa viboko wananchi waliodaiwa kuingia katika ardhi yake.


Baadhi ya familia kijijini hapo na Bujenjeke waliondolewa kwa kuvunjiwa nyumba zao kwa madai ya kuvamia eneo la “Buguma Estate” ambalo mzungu huyo alidaiwa kumiliki kihalali kwa shughuli za uwekezaji.


Miongoni mwa wakazi wa Kijiji cha Bujenjeke waliomlalamikia mzungu huyo, ni Leonida Pancras (54), aliyemtuhumu kufukua kaburi la marehemu mume wake na kubomoa nyumba akimshinikiza kuhama eneo hilo.


Pia, miongoni mwa waliomtuhumu mzungu huyo kwa kuwacharaza viboko ni Geniva Romward (30), aliyedai Novemba 2, 2008 alichapwa kwa ushirikiano wa mgambo na polisi wa Muleba.


Mmoja wa walinzi wa mzungu huyo, Joas Kyatuka, anadaiwa kushiriki matukio ya kubomoa nyumba na kufukuza wananchi waliojenga karibu na eneo hilo, Romward ni miongoni mwa wananchi wengi waliofunguliwa mashtaka ya kuvamia eneo la mwekezaji huyo.


Akizungumza mwaka jana kujibu malalamiko ya wananchi hao, Maintland alisisitiza kuwa eneo hilo analimiliki kisheria na kudai kuwa, mgogoro huo ulikuwa unakuzwa na wanasiasa wilayani Muleba.


Kwa mujibu wa wananchi hao, Maintland alifika kijijini hapo mwaka 2003 na kuanza kuweka uzio katika eneo mojawapo la kijiji hicho bila kuishirikisha jamii husika, lakini baadaye aliondoka kurudi kwao.


Mwaka 2008 Maintland alirejea tena nchini na hapo ndipo mgogoro ulipoanza kwani aliwaamuru wananchi hao kuondoka katika eneo hilo, huku akijigamba kwamba alikuwa tayari kuwalipa fidia kati ya Sh100,000 na Sh350,000, malipo ambayo hata hivyo wananchi hao waliyakataa.

No comments: